Download as pdf or txt
Download as pdf or txt
You are on page 1of 6

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI

TAARIFA KWA UMMA TAARIFA YA UCHAGUZI WA WANAFUNZI WA KUINGIA KIDATO CHA TANO KATIKA SHULE ZA SEKONDARI ZA SERIKALI NA VYUO VYA UFUNDI MWAKA 2013

1.0 Utangulizi Uchaguzi wa wanafunzi wa kuingia Kidato cha Tano katika shule za serikali, Vyuo vya Ufundi na Taasisi ya Menejimenti ya Maendeleo ya Maji mwaka 2013 umekamilika. Uchaguzi umefanyika kwa kuzingatia takwimu za matokeo ya watahiniwa waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012. 2.0 Watahiniwa waliofanya mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012 Jumla ya watahiniwa waliofanya mtihani wa kidato cha Nne mwaka 2012 ni 431,650 wakiwemo watahiniwa wa shule 370,837 na watahiniwa wa kujitegemea 60,813 . Waliofaulu wote (daraja la I IV) walikuwa 185,940 wakiwemo watahiniwa wa shule 159,747 na watahiniwa wa kujitegemea 26,193, sawa na asilimia 43.08. Kati ya hao, wanafunzi waliopata ufaulu wenye ubora (Daraja la I III) walikuwa 35,357, wakiwemo wavulana 24,433, na wasichana 10,924. Kati yao, wa Tanzania Bara ni 34,599 (wavulana 24,046 na wasichana 10,553). Kati ya watahiniwa wa Tanzania Bara 34,599 waliofaulu Daraja la I III, waliokuwa na sifa za kuchaguliwa kuingia Kidato cha Tano na vyuo vya ufundi kwa mujibu wa vigezo vilivyopo walikuwa 34,482 wakiwemo
1

wavulana 23,976 na wasichana 10,506. Kati yao watahiniwa wa shule walikuwa 34,289 na watahiniwa wa kujitegemea walikuwa 193. 3.0 Taratibu za Uchaguzi

Mwanafunzi aliyefikiriwa kuchaguliwa kuendelea na masomo ni yule aliyejaza SelForm, ambayo ndiyo Fomu rasmi ya Maombi ya kila mwanafunzi anayetaka kufikiriwa kujiunga na Kidato cha Tano, Vyuo vya Ufundi au Taasisi ya Menejimenti ya Maendeleo ya Maji. Katika maombi hayo, mwanafunzi huchagua maombi Matano ya Combinations za masomo anayotaka kusoma na shule anayotaka kujiunga nayo kwa kila chaguo. Kamati ya uchaguzi humpanga mwanafunzi katika machaguo yake ya masomo na shule kuanzia chaguo la kwanza. Kama machaguo yote aliyoomba mwanafunzi yatakuwa yamejaa, mwanafunzi husika hupangiwa chaguo la somo alilofaulu zaidi na katika shule iliyopo karibu zaidi na wilaya yake ya makazi kulingana na combination zilizopo katika shule husika. 4.0 Nafasi za Kidato cha Tano na Vyuo vya Ufundi mwaka 2013 Kulikuwa nafasi za Kidato cha Tano 43,757 zikiwemo za masomo ya sayansi 18,564 na za masomo ya Sayansi za Jamii 25,193. Hilo ni ongezeko la nafasi 3,757 ikilinganishwa na nafasi 41,000 zilizokuwepo mwaka 2012. Nafasi zilizojazwa ni 33,683. Aidha, nafasi zote za masomo ya sayansi zimepangiwa wanafunzi na baadhi ya tahasusi (combination) waliopangwa ni wengi kuliko nafasi zilizopo. Kwa mfano katika tahasusi ya PCB kulikuwa na nafasi 6,188 na waliopangwa ni 6,400. Kwa masomo ya tahasusi za sayansi za Jamii (Arts subjects) nafasi nyingi zimebaki wazi. Kwa mfano, tahasusi ya HKL kulikuwa na nafasi 5,300 lakini zilizopangiwa wanafunzi ni 1,527 tu. 5.0 Idadi ya shule zilizopangiwa wanafunzi wa kidato cha Tano mwaka 2013 Wanafunzi wamepangwa kujiunga Kidato cha Tano katika jumla ya shule 207, zikiwemo shule 02 zilizopangiwa wanafunzi wa Kidato cha Tano kwa mara ya kwanza mwaka 2013. Shule hizo ni Tandahimba na shule ya sekondari mpya Miono.

Kutokana na uchache wa wanafunzi wenye sifa za kujiunga kidato cha Tano, hasa kwa masomo ya Sayansi za Jamii, hatukuweza kuongeza zaidi shule mpya za kidato cha Tano mwaka 2013. Ninawahamasisha wadau wote katika Halmashauri mbalimbali kuimarisha miundombinu, ikiwemo ya maabara katika shule za Kidato cha Tano na Sita zilizopo na zinazotarajiwa kuanza kidato cha Tano badala ya kujenga mpya. 6.0 Idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kuingia Kidato cha Tano na Vyuo vya Ufundi mwaka 2013

Jumla ya Wanafunzi waliochaguliwa kuingia Kidato cha Tano na vyuo vya Ufundi pamoja na Taasisi ya Menejimenti ya Maendeleo ya Maji mwaka 2013 ni 34,213, wakiwemo wa Kidato cha Tano 33,683 na ufundi 530. Hilo ni ongezeko la wanafunzi 2,790 sawa na asilimia 8.9 ikilinganishwa na wanafunzi 31,423 waliochaguliwa mwaka 2012. 7.0 Wanafunzi Waliochaguliwa kuingia Kidato cha Tano mwaka 2013 Jumla ya wanafunzi 33,683 wakiwemo wavulana 23,383 na wasichana 10,300 wamechaguliwa kujiunga Kidato cha Tano katika shule za serikali mwaka 2013. Idadi hiyo ni ongezeko la wanafunzi 2,824, sawa na asilimia 9.15 ikilinganishwa na wanafunzi 30,859 waliochaguliwa mwaka 2012. Wanafunzi waliochaguliwa ni kutoka shule za serikali na zisizo za serikali. Kati ya wavulana 23,383 waliochaguliwa kujiunga Kidato cha Tano, 13,708 sawa na asilimia 58.62 wamechaguliwa kusoma masomo ya sayansi, na 9,675 sawa na asilimia 41.38 wamechaguliwa kusoma masomo ya sayansi za Jamii. Aidha, kati ya wasichana 10,300 waliochaguliwa kujiunga Kidato cha Tano , 5,038 sawa na asilimia 48.91 wamechaguliwa kusoma masomo ya sayansi na 5,262 sawa na asilimia 51.09 wamepangwa kusoma masomo ya Sayansi za Jamii. Kwa ulinganisho kijinsi, takwimu za wanafunzi waliopangwa zinaonesha kuwa wasichana ni wachache zaidi ikilinganishwa na wavulana. Hali hiyo inaonesha kuwa wasichana waliofaulu kwa ubora wa alama walikuwa wachache sana. Aidha, wanafunzi waliopangwa kusoma masomo ya sayansi ni wengi kuliko waliopangwa kusoma masomo ya Sayansi za Jamii.
3

Ninawapongeza walimu kwa kuzingatia mbinu za ufundishaji sayansi walizopata kupitia mpango wa mafunzo kazini kwa walimu wa sayansi unaosimamiwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Pia hali hiyo inaonesha kuwa jitihada za Serikali za kuhamasisha vijana kusoma masomo ya Sayansi zimeanza kuzaaa matunda. Vile vile takwimu za wanafunzi waliopangwa zinaonesha kuwa asilimia kubwa ya wavulana waliochaguliwa watasoma masomo ya Sayansi ikilinganishwa na wasichana. Ninatoa wito kwa wanafunzi wa jinsi zote kujisomea kwa bidii masomo yote, yakiwemo ya sayansi na sayansi za jamii, kwani yanategemeana. Aidha, walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati wanakumbushwa kutumia mbinu rafiki za kitaalam na kisaikolojia katika kufundisha ili kuwavutia wanafunzi wengi zaidi kusoma masomo ya sayansi, wakiwemo wanafunzi wa kike. Aidha, wanafunzi wa kike wanapaswa kujiamini kuwa wanaweza masomo yote yakiwemo ya Sayansi, kwani siri ya kujifunza ni utayari. Aidha wizara yangu itafanya utafiti kubaini sababu za wanafunzi wa masomo ya Sayansi za Jamii kufaulu wachache, na hivyo kusababisha nafasi nyingi za masomo hayo kubaki wazi. 8.0 Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Vyuo vya Ufundi na Taasisi ya Menejimenti ya Maendeleo ya Maji mwaka 2013 Jumla ya wanafunzi 530, wakiwemo wavulana 416 na wasichana 114 wamechaguliwa kujiunga na Vyuo vya Ufundi na Taasisi ya Menejimenti ya Maendeleo ya Maji. Idadi ya wanafunzi wote waliojiunga na vyuo vya ufundi imepungua kutoka 564 mwaka 2012 hadi 530 mwaka 2013. Aidha, idadi ya wanafunzi wa kike waliochaguliwa kujiunga na vyuo vya ufundi imeongezeka kutoka wanafunzi 47 mwaka 2012 hadi wanafunzi 114 mwaka 2013 ambalo ni ongezeko la wanafunzi 67 sawa asilimia 142. 55 Ninatoa wito kwa wanafunzi wa kike waliopo shuleni kusoma kwa bidii masomo ya sayansi ili mwakani idadi ya wasichana wanaojiunga na Vyuo vya Ufundi iongezeke zaidi ikilinganishwa na wavulana. 9.0 Mambo ya kuzingatia: Shule za Kidato cha Tano na Sita kuwa na mahitaji yote ya msingi
4

Shule za Kidato cha Tano na Sita zinatakiwa kuwa na mahitaji yote ya msingi, ikiwemo miundombinu yenye uwiano sahihi wa vyoo, mabafu, madarasa, hosteli/bweni, jiko, ukumbi/bwalo, maktaba, maabara na chumba cha Jiografia; pamoja na samani za kutosha. Aidha shule zenye Kidato cha Kwanza mpaka cha Nne zinatakiwa kuwa na miundombinu na mahitaji yote kamilifu kabla ya kuanza kujenga miundombinu ya Kidato cha Tano na Sita. Wanafunzi kuwa na malengo katika masomo yao Jumla ya wanafunzi 76 waliokuwa na sifa za msingi hawakuchaguliwa kwa sababu mbalimbali zikiwemo zifuatazo: Kukosa combination (wanafunzi 70), watatu (03) kuwa na umri mkubwa wa zaidi ya miaka 25, (wanafunzi hao walikuwa na umri wa miaka 28, 32 na 35); na mmoja (01) hakuwa raia wa Tanzania, ambaye hakujaza selform Kukosa combination kwa wanafunzi wenye sifa za msingi ilisababishwa na wanafunzi husika kufaulu vizuri zaidi masomo yasiyounda combination yoyote. Ninachukua fursa hii kuwakumbusha Wakuu wa Shule, walimu wa taaluma, walimu wa madarasa, walimu wote, pamoja na wazazi/walezi kutimiza wajibu wao wa kuwaelekeza wanafunzi kuwa na dira, na kuwasaidia kusoma vizuri kwa malengo. Wanafunzi Kuripoti katika shule walizopangwa: Muhula wa kwanza kwa wanafunzi wa Kidato cha Tano kuanzia mwaka huu 2013 itaanza mwezi Julai. Wanafunzi wamepangwa katika shule zenye miundombinu na walimu kwa masomo husika. Aidha, kama baadae upungufu utajitokeza, wakuu wa shule wameelekezwa kufanya taratibu za kuazima walimu wa muda na kutoa taarifa kwa uongozi wa halmashauri husika kuhusu upungufu wa walimu uliopo. Kwa nafasi hii, ninaagiza wanafunzi wote kuripoti katika shule walizopangwa tarehe 29 Julai, 2013. Kama kutakuwa na sababu yoyote ya msingi ya kuhamia shule nyingine, uhamisho wa kawaida utafanywa baada ya kuripoti shuleni kupitia kwa mkuu wa shule husika, Mkurugenzi wa Halmashuri/Manispaa na Katibu Tawala wa Mkoa. (Wizara haitabadilisha shule walizopangwa wanafunzi).
5

10.0

Hitimisho Mwisho ninachukua nafasi hii kuwapongeza wanafunzi waliochaguliwa kujiunga Kidato cha Tano na Vyuo vya Ufundi mwaka 2013, walimu, wazazi, Bodi za Shule, viongozi, jamii na wadau wote wa shule husika kwa jitihada za kuwaandaa wanafunzi, hata kufanikiwa kuingia Kidato cha Tano. Ushirikiano wa wadau wote unatakiwa ili kuboresha elimu hapa nchini. Wataalam wa elimu kuanzia ngazi ya shule wawe na utaratibu endelevu wa kuelimisha wadau katika utekelezaji wa malengo yanayopimika. Katika utaratibu wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now), kila mmoja anatakiwa kuacha utendaji wa mazoea; kufanya kazi kwa malengo, kuwa na mipango inayotekelezeka ya muda mfupi na muda mrefu; na kuwa na vipindi vya tathmini kwa kila lengo kabla, kati na mwisho wa utekelezaji. Ni matumaini yangu kuwa wakuu wa shule na viongozi wote wa elimu wakizingatia taratibu hizi tutaboresha elimu hapa nchini. Orodha za waliochaguliwa zinapatikana katika tovuti zifuatazo:
1. www.moe.go.tz 2. www.tamisemi.go.tz 3. www.necta.go.tz

Ahsanteni kwa kunisikiliza, PHILIPO A. MULUGO (MB) NAIBU WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI 10 Julai, 2013

You might also like