Download as doc, pdf, or txt
Download as doc, pdf, or txt
You are on page 1of 4

TAARIFA KUTOKA KWA MBUNGE WA BUNGE LA AFRIKA LA

AFRIKA
MASHARIKI
(EALA-TZ)
SHY-ROSE
BHANJI
09/11/2014
Kwa siku kadhaa sasa, mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari
- ndani na nje ya Tanzania vimekuwa vikiandika na kutangaza habari za
kile kinachodaiwa kuwa tuhuma dhidi yangu zilizotolewa na baadhi ya
Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA).
Tuhuma hizo ambazo kimsingi ni mkakati wenye ajenda ya siri nyuma
yake, umekuzwa na hata kufikia hatua ya baadhi ya Waheshimiwa
Wabunge kukwamisha baadhi ya shughuli za Bunge hilo mjini Kigali,
Rwanda.
Kuvunjika kwa kikao hicho kulitokana na madai ya baadhi ya wabunge
waliokuwa wakishinikiza Bunge linichukulie hatua kwa kuniondoa kwenye
Ujumbe wa Kamati ya Uongozi ya EALA.
Madai yao ni pamoja na lugha mbaya kwa baadhi ya wabunge, kuwatukana
baadhi ya marais wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, ulevi wa
kupindukia na kufanya fujo, kuvunja chupa ndani ya ndege na hatimaye
kufungwa pingu wakati wa ziara ya baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wa
EALA nchini Ubelgiji.
Madai yote haya hayana ukweli wowote na yanalenga kuniharibia jina na
sifa yangu ya utendaji kazi wangu katika Bunge la Afrika Mashariki. Lengo
kuu la shutuma hizi ni kunivunja nguvu na ari ya kutetea maslahi ya nchi
yangu na Afrika Mashariki kwa ujumla. Shutuma hizi zinadhihirisha
waziwazi chuki kubwa walioyonayo maadui zangu kwa vile daima
nilisimama kidete kuhakikisha Spika wa Eala Dr. Margaret Zziwa
haondolewi madarakani kwani hoja hiyo haikuwa na maslahi ya Tanzania
na ilikuwa ni kinyume na malengo ya EAC.
Kwa tuhuma nzito kama hizo nilitarajia kupata mawasiliano rasmi ya
kimaandishi kutoka kwa uongozi wa bunge kutaja shutuma zote dhidi
yangu na ni nani anayelalamika. Hilo halikufanyika
Kwa mfano madai ya ulevi wa kupindukia, kufanya fujo na kuvunja chupa
ndani ya ndege ni kosa kubwa la jinai (ugaidi). Madai haya yalipaswa kuwa
na ushahidi kwa sababu si rahisi abiria afanye fujo ndani ya ndege, halafu

aachwe hivi hivi bila kuchukuliwa hatua za kisheria. Safari yetu ya Ubelgiji
tulitumia usafiri wa Shirika la Ndege la KLM. Iwapo tuhuma hizi zingekuwa
na ukweli shirika hilo lisingesita kunichukulia hatua za kisheria.
Tuhuma kama hizi zinapashwa kupelekwa kwenye Kamati ya Uongozi ya
Bunge (EALA Commission) ambayo ina mamlaka ya kushughulikia jambo
hilo. Spika aliitisha kikao cha kamati hiyo lakini kilikosa akidi kwa
makusudi kabisa kutoka kwa baadhi ya wajumbe.
Lengo na makusudi ya kutohudhuria kikao hicho ilikuwa ni kupeleka hoja
hiyo moja kwa moja bungeni ili nichukuliwe hatua za kinidhamu bila ya
mimi kama mtuhumiwa kusikilizwa.
Baada ya kikao cha Kamati ya Uongozi kukosa akidi, hatua iliyofuata ni kwa
Mbunge kutoka Uganda, Dora Byamukama, (aliyeshindwa kwenye
uchaguzi wa uspika 2012 Juni mwaka 2012 dhidi ya Dr. Zziwa) kuwasilisha
hoja kwenye kikao cha Bunge, akipendekeza niadhibiwe kwa kuvuliwa
Ujumbe wa Kamati ya Uongozi.
Katika hilo, hekima ilitawala kuwa sikutendewa haki kwani sikupewa
malalamiko kimaandishi; badala yake hoja hiyo ililetwa jumla. Kwa hilo la
kukosa kunipa mashitaka kimaandishi, wabunge wengi wa Tanzania
waliamua kutoka nje ya Bunge kuonyesha msimamo wao dhidi ya
upungufu wa ukiukwaji wa mtuhumiwa kutopewa kimaaandishi mashtaka
dhidi yake na fursa ya kujitetea (Natural Justice).
Baada ya kukwama kwa hoja hiyo, baadhi ya wenyeviti wa Kamati na
baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Uongozi walitangaza kujiuzulu nafasi
zao. Walifanya hivyo ili kushinikiza Bunge linivue Ujumbe katika Kamati ya
Uongozi.
Hata hivyo, katika hatua ya kushangaza, Wenyeviti wawili kati ya
waliotangaza kujiuzulu wameonekana wakiendesha vikao vya kamati zao
katika miji ya Kigali, Rwanda na Nairobi, Kenya. Ni Mhe. Dora Byamukama
(kamati ya sheria) na Mhe. Martin Nduwimana (Kamati ya Maendeleo ya
Jamii) ambaye alishiriki kama mwenyekiti katika mkutano wa EAC
iliofanyika Nairobi kuanzia tarehe 5-7 Novemba. (Hii nimeshuhudia kwa
macho yangu maana nilihudhuria mkutano huo)

Wakati viongozi hawa walitangaza hatua ya kujiuzulu baada ya tuhuma za


uzushi dhidi yangu kukosa mashiko, inashagaza kuwaona wakiendelea na
nyadhifa zao kana kwamba hawakuutangazia umma juu ya uamuzi wao.
Ikumbukwe kwamba umebaki mwezi mmoja tu wa kipindi cha viongozi
wote wa Kamati ya Uongozi na Kamati zote za bunge la Eala kumaliza
kipindi cha uongozi ili wachaguliwe wengine baada ya kutumikia nafasi
hiyo kwa miaka miwili na nusu (kuanzia Juni 2012). Kwa lugha nyingine
viongozi hawa wameamua kujiuzulu ikiwa zimebaki wiki chache tu kabla ya
timu mpya kuchaguliwa.
MIGOMO
Ukweli ni kwamba migomo kama hii ni mwendelezo wa migomo iliyodumu
kwa makusudi baada ya azma yao ya kumngoa Spika wa Bunge, Dr. Zziwa
kushindwa. Hawakupata sahihi za kutosha kutoka kwa wabunge wa
Tanzania. Kwa sababu hiyo, katika Kikao cha Bunge kilichofanyika Agosti,
mwaka huu jijini Dar es Salaam wabunge wengi kutoka Rwanda na Burundi
walisusia na hivyo kusababisha akidi kutotimia.
Hapa anayetafutwa si Shy-Rose Bhanji, bali Spika Dr. Zziwa kwani
wabunge kadhaa wameshupaa ili angolewe kwenye kiti hicho. Wabunge
hao wanajua mimi siungi mkono jambo hilo, na kwa sababu hiyo
wameamua kunizushia uongo ili wana Afrika Mashariki waone sina uhalali
wa kumtetea Mheshimiwa Spika Zziwa. Msimamo wangu ni kwamba bado
sioni sababu za msingi zinazowasukuma wabunge kadhaa kutaka kumngoa
Spika Zziwa.
Si mimi pekee ninayemtetea Spika Zziwa. Wapo wengine. Tofauti yangu ni
kwamba nilisimama kidete muda wote kumtetea; ndani ya Kamati ya
Uongozi ya Bunge, ndani ya vikao vya bunge na nje ya Bunge; hatua
ambayo sina shaka ndio iliyowakasirisha na kuamua kunizushia uongo.
Wabunge wa EALA tumepewa dhamana kubwa kwa ajili ya kuimarisha
utangamano wa wananchi wa Afrika Mashariki; lengo kuu likiwa kuinua
hali zao za maisha. Ni kwa sababu hiyo, chombo hiki kinapaswa kuwa na
watu wenye weledi na wenye kujua kutumia vema muda na rasilimali
ambazo zinatokana na jasho la walipakodi wa Afrika Mashariki.
Haiingii akilini, na kwa kweli si kuwatendea haki wananchi wa Afrika
Mashariki kwa Wabunge wa EALA kutumia muda na fedha za walipakodi

kujadili uzushi, kugomea vikao na kupoteza muda wakitaka kumngoa


Spika na kuendekeza mivutano isiyokoma. Haya siyo tuliyotumwa na wana
Afrika Mashariki.
Rai yangu kwa wabunge wenzangu ni kurejea kwenye maudhui ya
kuanzishwa kwa EAC na kuwapo kwa Bunge la EALA kuanzia kwenye kikao
cha bunge kinachotarajiwa kufanyika jijini Nairobi, Kenya.
Kwa kufanya hivyo, tutajua tuna deni kubwa la kuwaletea wananchi wetu
maendeleo.
Migongano ya kisiasa au tofauti zetu za kimtazamo zisiwe chanzo cha
kuvurugika kwa utangamano ambao umeonyesha kuwa tukiwajibika vizuri,
wananchi zaidi ya milioni 140 wa EAC watapata mafanikio makubwa.
HITIMISHO
Makusudio ya tuhuma hizi ni kunidhalilisha na kunipunguzia nguvu, ari na
kasi ya utendaji kazi wangu kama Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki.
Lakini pia ni kutaka kunivunja nguvu ili nisiendelee kumtetea Spika
Mheshimiwa Dk. Zziwa na pia kujenga hofu na woga mkubwa kwa wabunge
wengine ambao wana mtazamo na msimamo kama wangu.
Kuna ushahidi tosha kwamba mchango wangu ni kwa Tanzania kwanza na
Afrika Mashariki kwa jumla. Ninawaomba wananchi waendelee kuwa na
imani katika juhudi na mchango wangu; na kupuuza uzushi na tuhuma
ambazo hadi sasa wazushi wameshindwa kuzithibitisha.
Kwa kuwa tuhuma hizi si tu kuwa ni mbaya kwangu, bali hata kwa nchi
yangu; iwapo wabunge hawa watashindwa kuthibitisha madai yao, sitosita
hata kidogo kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.
Shy-Rose
Bhanji
Mbunge wa Afrika Mashariki-Tanzania

You might also like