Download as pdf or txt
Download as pdf or txt
You are on page 1of 20

TAASISI YA WAHANDISI TANZANIA

(The Institution of Engineers Tanzania)

MAONI YA BARAZA LA KATIBA LA


TAASISI YA WAHANDISI TANZANIA KUHUSU RASIMU YA
KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA 2013

Maoni haya ya wadau wa Baraza la Katiba la Taasisi ya Wahandisi Tanzania


kuhusu Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 2013
yamegawanywa katika sehemu mbili. Sehemu ya kwanza inawasilisha maoni ya
jumla na sehemu ya pili inawasilisha maoni mahsusi kwenye vipengele vya
Rasimu.
1. SEHEMU YA KWANZA:
MAONI YA JUMLA.
Katiba ya nchi huweka na/au kuelekeza kuwekwa kwa utaratibu na sheria mama
za kusimamia haki za watu/viumbe na uendeshaji wa shughuli na maendeleo ya
Taifa kijamii, kiuchumi na kiteknolojia.
(a) Katika Rasimu hii, miongozo ya kina imejikita zaidi kwenye masuala ya
utawala na haki za binadamu. Masuala ya uchumi na Rasilimali za Taifa
havikupewa uzito unaostahili. Hali hii inaweza kutoa mwanya wa
migongano kwenye utayarishaji wa sera na sheria katika masuala ya
utendaji, usimamizi na umiliki.

(b)

Masuala ya ukaguzi na udhibiti yanaelekezwa zaidi kwenye mambo


yaliyokwishatokea badala ya kujumuisha vile vile ukaguzi na udhibiti
unaozuia madhara kutokea.

(c)

Rasimu haitoi miongozo ya kuiwezesha serikali kuibua sera za


kusimamia huduma za uchumi na mambo ya kijamii na kuelekeza
mwenendo wa maendeleo ya Taifa. Huduma hizo ni pamoja na; utumiaji
wa Sayansi na Teknolojia, ubora wa mitambo/vyombo vya utoaji wa
huduma na uzalishaji wa mali, majengo na majenzi, vyakula na madawa
na masuala ya uwekezaji kwa ajili ya maendeleo ya Taifa. Kukosekana
kwa miongozo ya Kikatiba katika maeneo haya kunatoa mwanya kwa
watu waliopewa madaraka kufanya watakavyo na kusababisha, siyo tu
usumbufu na hasara kwa wananchi na Taifa, bali pia kukosa mwelekeo
wa maendeleo ya Taifa. Misuguano baina ya wawekezaji na wananchi
kwenye sekta ya Nishati na Madini ni mifano hai.

(d)

Angalizo:
Kwa kuwa wajumbe wa Bunge la kutunga Katiba wana
uwezekano mkubwa wa kuweka vifungu vinavyopendelea watu
au makundi ya watu fulani, Sheria ya mabadiliko ya Katiba
ingerejewa ili kiwekwe kifungu kitakachozuia wajumbe hao
kugombea nafasi za kuchaguliwa mwanzoni mwa matumizi ya
Katiba mpya. Hatua hii itawafanya wajumbe hao kuachana na
ubinafsi.
Iwapo angalizo la hapo juu halitapendeza, basi sheria irejewe ili
kulifanya Bunge la kutunga sheria lisijumuishe wanasiasa wengi
kama ilivyo kwenye sheria ya sasa. Ikumbukwe kwamba suala la
kuwa na wabunge wote na wawakilishi wote na wajumbe
wachache wa kuchaguliwa na Rais litaelekea zaidi kwenye
maamuzi ya kisiasa badala ya kitaifa.

2.

SEHEMU YA PILI:
MAONI KWENYE RASIMU.

2.1

Sura ya (1): Jamhuri ya Muungano.


(a) Ibara ya (1): Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Maoni:
Ibara hii inataja Hati ya makubaliano ya muungano ya mwaka
1964 kuwa ndio msingi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Katiba hii. Kwa kuwa yaliyomo kwenye Hati hiyo
hayakuandikwa, uwezekano wa watu kudadisi na kuongeza
chumvi unaleta kutoaminiana na hivyo kuzaa kero zisizoisha.
Mapendekezo:
Hati ya makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 iwekwe
kwenye Katiba hii kama "Nyongeza"
(b)

Ibara ya 5: Tunu za Taifa.


Kwenye Tunu za Taifa iongezwe UBUNIFU.

(c)

Ibara ya 6: Mamlaka ya wananchi.


Maoni:
Ibara ya 1(1) inataja Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ni
shirikisho. Ibara hii ya 6 inataja Jamhuri ya Muungano kama
nchi. Hali hii inaleta mkanganyiko kwani Shirikisho ni tofauti na
Muungano na ni totauti na nchi.
Mapendekezo:
i)

ii)

Katiba inatakiwa kutofautisha na kueleza bayana maana ya


Shirikisho, Muungano, Nchi na Serikali ili kuondoa
utata wa tafsiri.
Aidha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itambulike kama
ni nchi inayotokana na Muungano wa Jamhuri ya
Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar. Waasisi wa
Muungano walichanganya udongo wa Tanganyika na
Zanzibar kuashiria kwamba muungano inakuwa nchi na
wala siyo shirikisho.
3

(d)

Ibara ya 7: Watu na Serikali.


Maoni:
i) Ingawa suala la Ardhi limetajwa kwenye kifungu 2(d),
mwongozo unaotolewa haulingani na umuhimu wa ARDHI
kama rasilimali kuu na msingi wa Taifa. Ardhi inabeba
mambo mengi ikiwa ni pamoja na madini, nishati na mbuga
za wanyama, kilimo, mifugo na mengine mengi.
ii) Maneno "mwenye uwezo" yaliyopo kwenye kifungu 2(f)
yanaweza kuleta taabu ya tafsiri.
Mapendekezo:
i) Inapendekezwa kwamba katiba iwe na SURA KAMILI
kuhusu miongozo ya masuala ya Ardhi hususan:
Umiliki na ugawaji ; (Ardhi imilikiwe na raia wa
Tanzania tu)
Matumizi, Kilimo, ufungaji, uchimbaji madini
Miundombinu; kama reli, barabara, usambazaji wa
maji, nishati n.k.
Mipango miji; makazi na shughuli za ujenzi.
Ili kufanikisha yote haya inapendekezwa iundwe
TUME ya kudumu ya Ardhi kwa kutumia sheria ya
Bunge.
ii) Maneno mwenye uwezo wa kufanya kazi kwenye
kifungu 2(f) yafutwe.

2.2

SURA YA PILI.
(a) Ibara ya 11: Malengo makuu.
Maoni:
i) Kifungu (2) kinaainisha nyanja zitakazotumika kuendeleza
na kuimarisha lengo kuu la katiba bila kutaja Sayansi na
Teknolojia.
4

ii) Aidha kifungu (3) kinataja namna ya kutekeleza malengo


ya Taifa bila kujumuisha uendelezaji wa Sayansi na
Teknolojia pamoja na kuimarisha uwezo wa rasilimali watu
isipokuwa wakulima, wavuvi na wafugaji.
Mapendekezo:
i) Malengo makuu ya Taifa yajumuishe
Kuimarishwa na kuendelezwa kwa Sayansi na
Teknolojia.
Kujenga na kuendeleza rasilimali watu katika nyanja
zote.
ii) Katika kifungu 3(c)(xi), suala la ubora wa elimu lizingatiwe
kwa kutoa mwongozo kwamba sifa za mhitimu
zitathibitishwa kisheria.
2.3

SURA YA TATU.
(a) Ibara ya 17: Mgongano wa kimaslahi.
Maoni:
Katika kifungu (1), rafiki na ndugu wa karibu hawako bayana.
Mapendekezo:
Katiba itamke kwamba Bunge litatunga sheria ya kuondoa utata
huo.
(b) Ibara ya 19: Matumizi ya masharti ya maadili kwa watumishi wa
umma.
Maoni:
Ibara hii inasema kwamba masharti yaliyoainishwa katika ibara za
13 mpaka 18 yatatumika pia kwa watumishi wa umma baada ya
kufanyiwa marekebisho stahiki.
Je marekebisho haya yatafanywa na nani na lini?
Je marekebisho stahiki ni yapi?
Mapendekezo:
Katiba iweke jambo hili wazi.
5

(c) Ibara ya 20: Utii wa miiko ya uongozi wa umma.


Maoni:
Kifungu 2(v) kinakataza kiongozi wa umma kutoa siri za Serikali
kinyume na Sheria. Kutotajwa kwa Siri za Serikali kunatoa
mwanya kwa taarifa za muhimu kwa matumizi ya umma
kufichwa kwa kisingizio cha kifungu hiki. Aidha kifungu
kinakinzana na ibara za 30(i)(a) na 30(3) za Rasimu hii.
Mapendekezo:
Kifungu hiki kiboreshwe kwa kulipa Bunge uwezo wa kutunga
Sheria inayoainisha Siri za Serikali.

2.4

SURA YA NNE.
(a) Ibara ya 34: Haki ya kufanya kazi.
Mapendekezo:
Kifungu (2), kiboreshwe kwa kuongeza mwishoni mwake maneno
yafuatayo; kulingana na utaratibu uliyowekwa na Bunge
kisheria
(b) Ibara ya 39: Haki ya watu waliyo chini ya ulinzi
Maoni:
Kifungu (3) kinazuia Raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kupelekwa nje kwa mashtaka au mahojiano bila ridhaa yake.
Kifungu hiki kinaonekana kukinzana na kifungu 12(d) cha
Rasimu hii.
Mapendekezo:
Kifungu hiki kibadilishwe kwa kuweka maneno ridhaa ya
serikali badala ya maneno ridhaa yake.

(c) Ibara ya 41: Haki ya Elimu na kujifunza.


Maoni:
Katika ibara hii, haki ya kujitambulisha kielimu au kitaaluma
haijatajwa. Kukosekana kwa haki hiyo kunaleta vurugu na
kuzorotesha ubora wa elimu kwa watu kujipachika sifa
wasizostahili. Aidha kukosekana kwa haki hiyo kunadumaza
ubunifu.
Mapendekezo:
i) Kwenye Ibara hii, kifungu (1) kiongezwe kifungu kidogo
cha (e) na kisomeke kama ifuatavyo;
(e) Kujitambulisha kielimu na kitaaluma kulingana na
taratibu na sheria za nchi.

(d)

UBUNIFU (ibara mpya)


Maoni:
Masuala ya kuhimiza na kutumia ubunifu wa aina zote unatumika
kote ulimwenguni kuleta maendeleo. Hapa Tanzania wabunifu
hawajapewa umuhimu wa kutosha na mara nyingine hukamatwa
na kunyanganywa mali au vitu walivyobuni kwa visingizio vya
kuhatarisha usalama.
Mapendekezo:
Iongezwe ibara mpya baada ya ibara ya 41 kuhusu Haki na
matumizi ya ubunifu na isomeke kama ifuatavyo;
42 mpya (1) Kila mtu atakuwa na haki ya kubuni na
kutengeneza kitu chochote kulingana na sheria za
nchi.
(2) Serikali itahakikisha wabunifu wanalindwa na
ubunifu wao unatumika katika kuliletea Taifa
maendeleo.

2.5

SURA YA SITA.
(a)

Ibara ya 57: Muundo wa Muungano.


Maoni:
Katika kifungu (1)(b) na (c) kunatajwa serikali za Mapinduzi
Zanzibar na Serikali ya Tanzania Bara. Hapa kuna mkanganyiko
kwa sababu neno Tanzania linatokana na maneno Tanganyika na
Zanzibar (yaani Tan na Zan)
Kwa hiyo kama tunasema Tanzania Bara lazima tuseme
vile vile Tanzania Visiwani.
Vinginevyo, tukisema Zanzibar lazima vile vile tuseme
Tanganyika jambo ambalo linaonekana ni kurudi nyuma.
Mapendekezo:
i) Mfumo wa serikali tatu (ingawa wengi wa wadau wetu
wanapendelea serikali moja) unakubalika kulingana na
mazingira yaliyopo.
ii) Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iitwe serikali ya Tanzania
Visiwani.

(b)

Ibara ya 59: Mamlaka ya Serikali ya Muungano.


Maoni:
Ibara hii inasema Serikali ya Jamhuri ya Muungano inaweza
kutekeleza mambo yasiyokuwa ya Muungano kwa makubaliano
na masharti maalum baina yake na serikali za washirika.
i)

Je haya makubaliano yatafanywaje ? wakati gani na kwa


mazingira yapi ?

ii)

Kama Katiba haitoi mwongozo usiotegemea matakwa, hisia


au uelekeo wa watu, ni nani atakayezuia uwezekano wa
kuwepo wakorofi kwa manufaa yao au wafadhili wao?

iii)

Mwongozo huu unaonyesha wazi udhaifu wa Muungano au


kutokuwepo kwa dhamira ya Muungano.
8

Mapendekezo:
i) Katika ibara hii itamkwe wazi kwamba Katiba ya Jamhuri
ya Muungano ndiyo Katiba mama na kwamba Katiba za
washirika wa Muungano zitakuwa sehemu ya Katiba hiyo.
ii) Kuhusu utekelezaji wa mambo ambayo siyo ya Muungano
Katiba ielekeze Bunge kutunga sheria na taratibu za
kushughulikia masuala hayo kwa kuzingatia maudhui ya
Katiba mama. Utaratibu uliyo rahisi ni kuliweka suala hili
katika ofisi ya Makamu wa Rais.

(c)

Ibara ya 60: Mambo ya Muungano.


Maoni:
i) Kama mambo ya Muungano yatakuwa kama
ilivyooneshwa, Je, ibara za 7, 11, 29 na 104(2) zilizoko
kwenye Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano
zitatekelezwaje?
ii) Kulingana na mpangilio huu serikali zote tatu zitatengwa
kwa muda katika masuala ya mawasiliano ambayo
huratibiwa kimataifa kwa kupewa namba za kikanda (code
numbers). Maombi ya namba za mawasiliano huchukua
muda mrefu kupatikana.
iii) Kwa kuwa siyo rahisi ndani ya nchi moja kuweka mipaka
katika masuala ya usafiri wa anga na baharini na mazingira
na hali ya hewa mambo haya yakiachwa kwa washirika
utekelezaji wake, unaweza kusababisha misuguano kiasi
cha kuhatarisha ustawi wa muungano.
iv) Serikali ya Jamhuri ya Muungano haina rasilimali ikiwemo
ardhi.
v) Kwa kuwa mambo ya Muungano yaliyotajwa hayazalishi
isipokuwa ushuru uliotajwa, kuna uwezekano wa Serikali
ya Muungano kuhitaji michango kutoka kwenye serikali za
Washirika. Hali ikiwa hivyo serikali ya Muungano siyo tu
9

itakosa nguvu, bali pia itakufa kutokana na dhana ya


kuongezeka kwa gharama na/au washirika kutegeana katika
utoaji wa michango.
Mapendekezo:
i) Mambo ya Muungano yawe kama ifuatayo;
1. Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
2. Ulinzi na Usalama.
3. Uraia na Uhamiaji.
4. Sarafu na Benki Kuu.
5. Mambo ya Nje.
6. Usajili wa Vyama vya Siasa.
7. Mawasiliano na Uchukuzi Baharini na Angani.
8. Hali ya Hewa na Mazingira

(d)

ii)

Serikali ya Muungano ijiendeshe kwa mapato yake kutokana


na mambo ya Muungano. Pale itakapowezekana Serikali ya
Muungano ndiyo iwe na uwezo wa kutoa ruzuku kwa
Serikali washirika kwa kuzingatia uwiano wa idadi ya watu.

iii)

Kwenye masuala yasiyokuwa ya Muungano (ibara za 7, 11,


29 na 104(2)), Katiba itamke hivyo na ielekeze namna
mambo haya yatakavyoshughulikiwa na serikali washirika
ili kuonesha kiungo kati ya Serikali ya Muungano na zile za
washirika.

Ibara ya 64: Mawaziri Wakaazi.


Maoni:
Katika ibara hii kunatajwa Mawaziri Wakaazi na majukumu yao.
Kitu ambacho hakiko bayana ni uwajibikaji wao pamoja na ulipaji
wa gharama za kuendesha ofisi zao. Watakuwa na ofisi kwenye
Makao Makuu ya serikali ya muungano lakini watapangiwa kazi
na serikali za washirika. Je wanawajibika kwa nani na uendeshaji
wao wa ofisi unahudumiwa vipi na kwa gharama za nani?
10

Mapendekezo:
Majukumu yanayofanywa na mawaziri hawa ni majukumu ya
ofisi ya Makamu wa Rais. Kuwepo kwao ni kuonesha udhaifu au
kutokuwepo kwa dhamira ya muungano.
(e)

Ibara ya 65: Wajibu wa kulinda Muungano.


Maoni:
Katika kifungu (2), Rasimu inaelekeza serikali za washirika wa
Muungano kuandika Katiba zinazozingatia ustawishaji wa
mamlaka ya wananchi kwa kugatua madaraka kwa serikali za
mitaa. Uzoefu unaonesha kwamba kuwepo kwa Serikali Kuu na
Serikali za Mtaa, siyo tu kunaongeza wingi wa viongozi kwa kazi
zile zile, bali pia kunaleta misuguano inayoathiri ufanisi na
kuongeza gharama zisizokuwa za lazima.
Mapendekezo:
Kifungu hiki kieleze kwamba Katiba za Washirika wa Muungano
zizingatie ustawishaji wa Mamlaka ya wananchi kwa kuhakikisha
kwamba viongozi watendaji wa mikoa na wilaya wanachaguliwa
na wananchi. Hawa ni pamoja na Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa
Wilaya, Mtendaji wa Kata na Watendaji wa Mitaa na Vitongoji.

(f)

Ibara ya 66: Wajibu wa kulinda Muungano.


Maoni:
Ingawa hivi sasa tunao marais wawili, hali hiyo inaweza
kuchukuliwa kwamba wakati tunaanzisha Muungano tulikuwa
tunajifunza na hivyo kulazimika kubadilika pole pole. Baada ya
miaka 40 sasa hatuna budi kuelewa kwamba jambo la msingi ni
mamlaka ya kiongozi na wala siyo jina la cheo chake. Aidha
ukiacha vyeo vya Rais kwenye mashirika na Taasisi mbalimbali
ambazo hazina itifaki ya kimataifa, ni Tanzania peke yake iliyo na
marais wawili. Pendekezo la kutaka Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kuwa na Marais watatu na Makamu wa Rais siyo sifa
nzuri kwa watu waliodhamiria kudumisha muungano.
11

Mapendekezo
Katiba itamke kwamba kutakuwa na Rais wa Jamhuri wa
Muungano na Makamu wake. Viongozi wa Serikali za washirika
waitwe Mawaziri Mkuu.

2.6

SURA YA SABA : SERIKALI YA JAMHURI YA MUUNGANO WA


TANZANIA.
(a)

Ibara ya 69 : Madaraka na majukumu ya Rais.


Maoni:
Katika ibara hii madaraka na majukumu ya Rais yanatajwa.
Ingawa kifungu (4) kinamtaka Rais kuepuka kujinasibisha kwa
namna yoyote ile na chama cha siasa au kundi lolote, bado
madaraka ya uamuzi yanaonekana kuwa ya mtu mmoja, yaani
Rais.
Mapendekezo:
Ibara hii na hususan kifungu (4) kitamke wazi kwamba Rais
atazingatia uteuzi wa Tume mbalimbali za kudumu
zitakazoundwa kwa ajili ya majukumu husika.

(b)

Ibara ya 73 : Utekelezaji wa majukumu ya Rais akiwa hayupo.


Maoni:
Kifungu (1)(b) cha ibara hii kinaeleza kwamba mmojawapo wa
kutekeleza majukumu ya Rais kama hayupo ni Waziri
Mwandamizi. Katika Rasimu hii hakuna anapotajwa Waziri wa
namna hiyo wala nafasi hiyo.
Mapendekezo:
Kifungu (b) ama kifafanuliwe au kifutwe na kifungu (c) kielekeze
kwamba Baraza la Mawaziri litateua mmojawapo miongoni mwao
kwa kuzingatia uandamizi (Seniority).

12

(c)

Ibara ya 75: Sifa za Rais.


Maoni:
i. Kifungu (d) kinatoa umri wa mwanzo wa mgombea nafasi ya
Rais lakini hakitaji umri wa mwisho.
ii. Kifungu (e) kinaeleza kwamba mojawapo ya sifa za
kumwezesha mtu kugombea nafasi ya urais ni kuwa na sifa za
kumwezesha kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano kwa mujibu wa Katiba hii.
Katika ibara ya 117 (2) (a) ya Rasimu inaelekeza kwamba mtu
hatakuwa na sifa za kugombea kuchaguliwa kuwa Mbunge ikiwa
mtu huyo aliwahi kuwa Mbunge kwa vipindi vitatu vya miaka
mitano. Kwa kuwa kazi ya Rais na Mbunge ni tofauti, kifungu
hiki kinawabana waliowahi kuwa wabunge kwa vipindi vitatu
kuwania nafasi ya urais.
Mapendekezo:
i. Kifungu (d) kiboreshwe kwa kuweka ukomo wa kugombea
nafasi ya Urais kwa kuongeza maneno; au umri usiozidi
miaka sabini (70).
ii.

Kifungu 75(e) kifutwe.

(d) Ibara ya 93 : Uteuzi wa Mawaziri na Naibu Mawaziri.


Maoni:
Idadi ya mawaziri wanaotajwa katika kifungu 93(2) inakubalika.
Kutaja idadi peke yake kunatoa mwanya wa kumwachia mteuzi
kuamua maeneo ya kuundiwa Wizara kama anavyotaka. Uhuru wa
namna hii unaweza kusababisha maeneo muhimu kwa maendeleo
ya taifa kutopewa uzito unaostahiki.
Mapendekezo:
Katiba ielekeze kwamba miongoni mwa Wizara hizo iwepo
Wizara ya Elimu na Ufundi.

13

2.7

SURA YA NANE: URATIBU WA MAHUSIANO YA WASHIRIKA


WA MUUNGANO.
(a) Ibara za 102 na 103: Tume ya mahusiano ya uratibu wa serikali.
Maoni:
Kama ilivyoelezwa kwenye maoni ya ibara ya 64, kuwepo kwa
Mawaziri Wakazi kwa mtindo uliopendekezwa siyo tu kunaleta
mkanganyiko wa uwajibikaji na uendeshaji bali pia kunaonesha
kutoaminiana na mashaka ya dhamira ya kudumisha Muungano.
Mapendekezo:
Badala ya kuwa na mawaziri wakaazi wenye ofisi kwenye serikali
ya Muungano, katiba itamke kwamba kila mshirika wa muungano
atakuwa na wizara inayoshughulikia mahusiano ya muungano na
kwamba waziri mwenye dhamana hiyo atakuwa mjumbe wa Tume
inayopendekezwa.

2.8

SURA YA TISA: BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO.


(a) Ibara ya 105: Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Maoni.
Ibara hii inaeleza jinsi Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano watakavyopatikana na kutoa upendeleo kwa watu wenye
ulemavu.
Mambo yafuatayo yanahitaji kufikiriwa:
Kufanya mikoa (Tanzania Bara) na wilaya (Zanzibar) kuwa
majimbo ya uchaguzi kunaweza kuleta matatizo baadaye kwa
sababu kugawa mikoa au wilaya siyo suala la Muungano.
Bunge ni muhimili muhimu kama ilivyo mihimili mingine
katika maendeleo ya Taifa. Kuna haja ya kulifanya Bunge la
Muungano kuwa la weledi zaidi ili kuweza kuisimamia serikali
ambayo inaendeshwa kitaalam na wala sio kisiasa.
Kuingiza siasa kwenye Bunge la Muungano kunaweza
kupunguza ufanisi wa serikali ya Jamhuri ya Muungano
kutokana na ushabiki wa vyama. Hebu tufikirie serikali zote
tatu zikichukuliwa na vyama tofauti kwa kila serikali, kitatokea
nini?
14

Kuwafanya wananchi wapige kura kuchagua wabunge wa


Bunge la Muungano kuwachosha na mambo ya uchaguzi kwani
ni wale wale wanaochagua Wabunge wa Mabunge ya
washirika wa Muungano. Aidha kupiga kura moja, nyingi kiasi
hicho huongeza mzigo usiokuwa wa lazima kwa Taifa.
Mapendekezo:
Badala ya kuwa na Majimbo ya uchaguzi kama ilivyoainishwa
kwenye Rasimu, Katiba itaje makundi yanayostahili uwakilishi
Bungeni na kuainisha sifa na namna ya kupata wawakilishi stahili.
Makundi haya yanaweza kuwa miongoni mwa yafuatayo;
i. Vyama vya siasa (kila kimoja kinateua Mbunge 1)
ii. Serikali za washirika (kila moja mbunge 1)
iii. Wadau wa Maliasili na Utalii.
iv. Wadau wa Kilimo, Umwagiliaji na Maji.
v. Wadau wa Ardhi na Mazingira.
vi. Wadau wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.
vii. Wadau wa Elimu ya Juu.
viii. Wadau wa Elimu ya Msingi na Kati.
ix. Wadau wa Wataalam mbalimbali.
x. Wadau wa Viwanda.
xi. Wadau wa Biashara.
xii. Wadau wa Ufugaji.
xiii. Wadau wa Uvuvi.
xiv. Vijana.
xv. Wanawake.
xvi. Walemavu.
n.k.
(b) Ibara ya 115: kupitishwa kwa Hoja za serikali.
Maoni.
Kifungu (2) kinaeleza kwamba endapo Bunge litakataa kwa mara
ya pili hoja kuhusu Bajeti ya Serikali, basi hoja hiyo itahesabika
kuwa imepitishwa na Bunge.
15

Kifungu hiki kinahitaji ufafanuzi kwa sababu kikitafsiriwa kama


kinavyosomeka, Serikali inaweza ikakaidi kufanya marekebisho
yaliyopendekezwa na Bunge wakati hoja ilipowasilishwa kwa mara
ya kwanza.
Mapendekezo.
Maudhui yaliyokusudiwa katika kifungu hiki yaonekane bayana na
yalenge kuimarisha Bunge kusimamia serikali.

2.9

KUONGEZA SURA MPYA.


Maoni.
Kama ilivyoelezwa kwenye maoni ya jumla, Katiba inatakiwa
kutoa miongozo ya kusimamia, kuchochea na kuongoza maendeleo
ya Taifa kwa sababu zilizoelezwa kwenye maoni hayo.
Mapendekezo.
Inapendekezwa kwamba, baada ya SURA YA KUMI NA MOJA,
iingizwe sura mpya ya KUMI NA MBILI. Sura ya Kumi na Mbili
ya sasa ipewe namba 13 na kuendelea. SURA mpya ya KUMI NA
MBILI isomeke kama ifuatavyo:
SURA YA KUMI NA MBILI
HUDUMA ZA KUSIMAMIA UCHUMI NA KUCHOCHEA
MAENDELEO YA TAIFA
SEHEMU YA KWANZA
USIMAMIZI WA HUDUMA ZA UCHUMI

180. Huduma za Uchumi


Huduma za uchumi zinajumuisha maeneo yafuatayo:
a) Miundombinu
b) Vitendea kazi vya utoaji huduma na uzalishaji wa mali
c) Majengo na majenzi
d) Rasilimali watu
16

181.

Majukumu ya usimamizi
(1) Serikali itahakikisha kwamba inajenga na kusimamia miundombinu
stahiki na ya kutosha kwa mahitaji ya wananchi na ukuaji wa uchumi
wa Taifa.
(2) Bunge litatunga sheria inayoweka utaratibu wa kuhakikisha kwamba
vitendea kazi vya utoaji wa huduma au uzalishaji mali vina ubora
unaotakiwa kwa kazi husika pamoja na teknolojia stahiki inayozingatia
usalama wa watu na utunzaji wa mazingira.
(3) Mamlaka ya nchi itaweka utaratibu wa sheria kuhakikisha kwamba
majengo na majenzi yanawekewa viwango na usimamizi ili kuboresha
mipango miji na kulinda matumizi ya ardhi na usalama wa watu na mali
zao.
(4) Wakati wote serikali itahakikisha kwamba raia wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania wanajengewa uwezo wa kushiriki kwenye
shughuli za uchumi na maendeleo ya Taifa kivitendo kwa kuweka
mazingira na mipango ya makusudi ya kufikia lengo hilo.

SEHEMU YA PILI
UWEKEZAJI
182. Misingi ya uwekezaji
1) Serikali itahakikisha kwamba kila uwekezaji unaofanyika nchini;
(a) Unazingatia mpango mahsusi uliowekwa na Taifa kwa
madhumuni stahili.
(b) Unaongeza fursa za kuwaendeleza raia wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
(c) Unaliongezea Taifa fursa za kuuza mali zilizokamilika nje ya
nchi.
183. Masharti ya uwekezaji
1) Kila anayewekeza nchini atalazimika kuingia ubia na raia wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa kiwango kitakachowekwa kila inapobidi na
mamlaka ya nchi au Bunge.
17

2) Serikali itahakikisha kwamba;


(a) Wawekezaji wanatumia mitambo na malighafi`stahiki kwa
kuzingatia ubora wa vitu hivyo na utunzaji wa mazingira.
(b) Wawekezaji wanatumia rasilimali zilizopo nchini kikamilifu.
(c) Wananchi wanahusika kikamilifu katika mipango na shughuli za
uwekezaji kwenye maeneo yao.

SEHEMU YA TATU
UTAYARISHAJI NA USIMAMIZI WA VIWANGO
184. Maeneo ya viwango
1) Maeneo yanayotakiwa kuwekewa viwango ni haya yafuatayo;
(a) Vyakula, dawa, vipodozi na vitu vinginevyo vinavyotumiwa na
watu na wanyama.
(b) Matumizi ya viwandani na makazi ya watu
(c) Vitendea kazi mbalimbali
(d) Melighafi kwa matumizi mbalimbali
(e) Mengineyo kama yatakavyoainishwa na sheria ya Bunge.
185. Majukumu ya utayarishaji na usimamizi
1) Bunge litatunga sheria inayoweka utaratibu wa kutayarisha na kusimamia
viwango katika maeneo yaliyotajwa kwenye ibara 184.
2) Utayarishaji wa viwango vya taifa utazigatia viwango vya kimataifa na
mazingira ya ndani ya nchi.

SEHEMU YA NNE
UTUNZAJI WA MAZINGIRA
186. Maana ya mzingira
Mazingira kwa maana ya Katiba hii yanajumuisha mambo yafuatayo;
(a) Hewa na tabia ya nchi
(b) Maji katika hali mbalimbali
(c) Ardhi
18

187. Majukumu ya utunzaji


1) Bunge litatunga sheria inayoweka utaratibu wa namna ya kusimamia na
kutunza ubora na viwango katika maeneo yaliyotajwa katika ibara ya 186.
2) Serikali itahakikisha kwamba inazingatia mambo yafuatayo;
(a) Maeneo ya ardhi yenye vyanzo vya maji yanaainishwa na
kutunzwa.
(b) Maeneo yanayofaa kwa kilimo yatumike hivyo bila kuchanganywa
na ufugaji wa nje ya mabanda.
(c) Maeneo ya ardhi yatengwe na kuendelezwa kwa ajili ya ufugaji wa
nje ya mabanda.

SEHEMU YA TANO
UENDELEZAJI WA SAYANSI NA TEKNOLOJIA
188. Tume ya Sayansi na Teknolojia
Kutakuwa na Tume ya kuendeleza Sayansi na Teknolojia kwa manufaa na
maendeleo ya ustawi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watu wake.
Tume hiyo itateuliwa kwa sheria na utaratibu utakaotungwa na Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

189. Majukumu ya Tume


1) Majukumu ya tume hiyo yatakuwa ni pamoja na haya yafuatayo.
(a) Kuweka, kusimamia na kuratibu malengo ya Taifa kwenye
Sayansi na Teknolojia
(b) Kukusanya, kuhifadhi na kusambaza kwa wananchi aina na
viwango vya maendeleo katika nyanja za Sayansi na Teknolojia
ulimwenguni.
(c) Kuhimiza, kuratibu na kuongoza shughuli za utafiti na
uendelezaji wa Sayansi na Teknolojia nchini, ikiwa ni pamoja
na kuendeleza mitaala stahiki kwenye shule zote na vyuo vya
elimu ya juu.
19

(d)

(e)

Kusimamia na kufuatilia mabadiliko na mienendo ya utunzaji


wa mazingira, na tabia ya nchi kulingana na maendeleo ya
Sayansi na Teknolojia.
Kutekeleza majukumu mengine ambayo tume itapewa na
mamlaka au sheria iliyotungwa.

2) Tume ya Sayansi na Teknolojia itakuwa na wajumbe wasiopungua saba


na wasiozidi kumi na mmoja ikiwa ni pamoja na Mkurugenzi Mkuu
ambaye atakuwa Mtendaji Mkuu wa tume hiyo. Wajumbe watateuliwa
kwa kuzingatia uwiano wa fani zinazojumuisha masuala ya Sayansi na
Teknolojia.

MWISHO

KAMATI YA BARAZA LA KATIBA.


(KWA NIABA YA BARAZA)

20

You might also like