Download as pdf or txt
Download as pdf or txt
You are on page 1of 2

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MFUKO WA FIDIA KWA WAFANYAKAZI (WCF)

UCHANGIAJI NA MAFAO YATAKAYOTOLEWA NA MFUKO WA FIDIA


KWA WAFANYAKAZI
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi ni Taasisi ya Serikali chini ya Wizara ya
Kazi na Ajira iliyoanzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 5 cha Sheria ya
Fidia kwa Wafanyakazi Na. 20 ya mwaka 2008 kwa madhumuni ya kutoa
fidia kwa Wafanyakazi kutokana na ulemavu au vifo vinavyosababishwa na
ajali au magonjwa yatokanayo na kazi sambamba na kukuza mbinu za
kuzuia matukio ya ajali mahali pa kazi.
Mfuko umeanza kazi rasmi tarehe 1 Julai 2015 baada ya kuteuliwa kwa
Mkurugenzi Mkuu na Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini. Mkurugenzi Mkuu
ndiye Mtendaji Mkuu na anafanya kazi chini ya Bodi ya Wadhamini.
Mfuko umeanzishwa kutokana na nia ya Serikali kukabiliana na
changamoto za ulipaji wa fidia kwa Wafanyakazi katika mfumo wa utoaji
fidia uliokuwepo awali. Changamoto hizo ni pamoja na kiwango kidogo cha
malipo ya fidia (kiwango kisichozidi shilingi 108,000 kwa ulemavu wa
kudumu na shilingi 83,000 kwa wategemezi endapo kifo kitatokea kwa
Mfanyakazi husika), uchache wa mafao na urasimu kwa baadhi ya Waajiri
katika utoaji wa fidia.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 2 cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi,
Na.20/2008, Mfuko huu unawahusu Waajiri na Wafanyakazi wote katika
sekta ya Umma na sekta Binafsi, Tanzania Bara.
Uchangiaji katika Mfuko umeanza rasmi tarehe 1 Julai 2015 kama
ilivyoelekezwa katika Tangazo la Serikali Na. 169 la Mei, 2015. Katika
mwaka wa fedha 2015/16, viwango vya uchangiaji kwa kila mwezi ni
asilimia moja (1%) ya mapato ya Wafanyakazi kwa Waajiri wa Sekta
Binafsi na asilimia sifuri nukta tano (0.5%) ya mapato ya Wafanyakazi kwa
Waajiri wa Sekta ya Umma. Aidha michango hii ni gharama ya Mwajiri na
haipaswi kukatwa kwenye mapato ya Mfanyakazi.

Mwajiri ana wajibu wa kuwasilisha michango kupitia akaunti za Mfuko


zilizopo katika benki ya NMB (Akaunti Na. 20110016403, tawi la Bank
House) na CRDB (Akaunti Na. 0150237547300, tawi la Holland House)
kwa njia ya Mtandao (Electronic money transfer), Hundi (Cheque
payments), Fedha Taslimu (Cash payments) au njia nyingine inayokubalika
na Benki Kuu ya Tanzania. Ucheleweshaji wa malipo ni kosa linalostahili
adhabu kwa mujibu wa vifungu vya 75 (2), (3) na (4) vya Sheria ya Fidia
kwa Wafanyakazi, Na. 20 ya mwaka 2008.
Uwasilishaji wa nyaraka zinazohusu malipo ya michango utazingatia
utaratibu uliowekwa na Mfuko. Mwajiri atawasilisha nakala mbili za fomu
WCP1 zilizojazwa, viambatishi vyake na uthibitisho wa malipo. Fomu na
kiambatishi chake vinapatikana Ofisi za Mfuko na pia katika tovuti ya Mfuko
(www.wcf.go.tz), tovuti ya Wizara ya Kazi na Ajira (www.kazi.go.tz) na Ofisi
za Kazi zilizopo mikoani na wilayani.
Mafao yatakayotolewa na Mfuko huu ni huduma ya matibabu, malipo ya
ulemavu wa muda, malipo ya ulemavu wa kudumu, malipo kwa
anayemhudumia mgonjwa, huduma za ukarabati na ushauri nasaha,
gharama za mazishi na malipo kwa wategemezi wa marehemu.
Kipindi kati ya Julai 2015 na Juni 2016 ni cha mpito na Waajiri wataendelea
kushughulikia malipo ya fidia kwa Wafanyakazi kwa taratibu zilizopo.
Mfuko utaanza kupokea madai ya fidia kwa Wafanyakazi tarehe 1 Julai
2016.
Mfuko wa Fidia utasaidia kuboresha mazingira ya kazi, kulinda nguvu kazi
ya Taifa, kuimarisha ustawi wa Wafanyakazi, kuwaongezea ari ya
utekelezaji wa majukumu na hivyo kuwezesha ongezeko la tija na kukua
kwa uchumi wa Taifa.
Imetolewa na Mkurugenzi Mkuu,
MFUKO WA FIDIA KWA WAFANYAKAZI (WCF)
GEPF House, Barabara ya Bagamoyo, Regent Estate
Tafadhali uliza mapokezi, Ghorofa ya 9.

Simu Na.: +255 22 2110877


Simu Na.: +255 22 2926107
16 Agosti, 2015

You might also like