Download as doc, pdf, or txt
Download as doc, pdf, or txt
You are on page 1of 5

HOTUBA YA MHE.

DKT. MOHAMMED GHARIB BILAL, MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA


MUUNGANO WA TANZANIA KATIKA UFUNGUZI WA KONGAMANO
LA UWEKEZAJI UKANDA WA ZIWA TANGANYIKA TAREHE 09 SEPTEMBA 2015
Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mhe. Eng. Cristopher Chiza
Waziri wa Nchi - Uwekezaji na Uwezeshaji;
Waheshimiwa Mawaziri;
Wakuu wa Mikoa ya Katavi, Rukwa na Kigoma;
Waheshimiwa Mabalozi;
Washiriki;
Wageni Waalikwa;
Waandishi wa Habari;
Mabibi na Mabwana;
Awali ya yote napenda kushukuru kupata fursa ya kushiriki nanyi kwenye
Kongamano hili, linaloangazia fursa za uwekezaji na utanuaji maendeleo kwa
ukanda huu wa Ziwa Tanganyika. Nimefurahi kuwa nanyi hapa Kigoma na nafarijika
zaidi kuona namna mlivyojitokeza katika kongamano hili ukilinganisha na lile
lililofanyika mwaka jana mjini Sumbawanga ambapo pia nilipata fursa ya
kuhudhuria.
Pili, napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wenyeji wetu kwa mapokezi mazuri.
Nimefurahishwa na maandalizi mazuri ya Kongamano hili kwenye mazingira mazuri
ambayo yanaonesha umakini katika uandaaji. Nadhani washiriki wote mtakubaliana
nami kwenye hili. Asanteni sana.
Ninawashukuru pia Mabalozi kutoka nchi mbalimbali walioshiriki. Hali kadhalika
nawashukuru wageni wetu kutoka nchi za nje kama vile Marekani, Jumuiya ya Ulaya
na Burundi. Na washiriki wengine kutoka taasisi na sehemu mbalimbali kwa
kushiriki Kongamano letu, hii inadhihirisha umuhimu wa shughuli yenyewe na
inatuhakikishia mafanikio chanya siku zijazo.
Tatu, napenda kuwashukuru Wananchi wa Kigoma na hasa Mkuu wa Mkoa wa
Kigoma Lt. Col. (Mst.) Issa S. Machibya kwa ukarimu wao na kukubali kutupokea
kwenye Kongamano hili. Ni ukweli ulio dhahiri kwamba Kongamano hili kufanyika
katika mkoa wenu ni mafanikio makubwa ya kuutangaza mji wenu Kigoma/Ujiji.

Waheshimiwa,
Mabibi na Mabwana;
Katika msafara wangu nimefuatana na Maafisa kadhaa Waandamizi wa Serikali
ambao wako hapa kusikiliza, kuzungumza na kuchangia hoja mbali mbali kwenye
sekta ya Uwekezaji na Mazingira ya Biashara katika Ukanda huu wa Ziwa
Tanganyika. Ninawaomba washiriki wote kuitumia fursa hiyo ya kupata habari
muhimu wakiwa hapa ili kufanikisha malengo yenu ya Uwekezaji katika Ukanda huu.
Ninaelewa baadaye mtapata fursa ya kufanya mazungumzo ya mtu mmoja mmoja
na wenzenu kutoka Ukanda huu. Mtapata maelezo ya kutosha kuhusu fursa za
Uwekezaji nchini na maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uendelezaji
Maeneo Maalum ya Kiuchumi (EPZA) kuhusu fursa na mazingira ya biashara katika
Ukanda wa Ziwa Tanganyika. Hali hiyo itaifanya kazi yangu iwe rahisi. Nachukua
fursa hii kuwaeleza kwa kifupi kwa nini Ukanda huu ni eneo muhimu la kimkakati
kwa uwekezaji nchini.
Waheshimiwa,
Mabibi na Mabwana;
Ukanda wa Ziwa Tanganyika unajumuisha mikoa mitatu (Rukwa, Kigoma na Katavi),
sina shaka ukanda huu ni mahali muafaka pa kuwekeza katika nchi yetu. Ukanda
huu ulikuwa nyuma kimaendeleo kwa miaka mingi na ukombali na Makao makuu ya
nchi Dodoma na hata kutoka kwenye mji mkuu wa kibiashara wa Dar es Salaam.
Miundombinu ya usafiri wa Barabara, Reli, Maji na Anga ulikuwa hafifu hali ambayo
iliathiri kwa kiasi kikubwa maendelo ya ukanda huu. Lakini kwa sasa Serikali
imewekeza kwa kiwango kikubwa kwenye Barabara, Viwanja vya ndege, Bandari na
Reli, hivyo kuufanya Ukanda huu ufunguke.
Uboreshaji wa miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami unaendelea, ujenzi
wa barabara ya Tunduma hadi Sumbawanga, kutoka Sumbawanga hadi Kasanga
kupitia Matai, kutoka Sumbawanga hadi Tabora kupitia Namanyere na Mpanda, pia
barabara ya Mpanda hadi Tabora kupitia Koga, kutoka daraja la Mto Malagarasi hadi
Tabora kupitia Kaliua na Urambo, kutoka Mpanda kupitia Uvinza hadi Kanyani,
Wilaya ya Kasulu. Barabara kutoka Kigoma hadi mpaka wa Burundi na kutoka
Kigoma kupitia Kidahwe hadi Uvinza.
Ukamilikaji wa barabara hizo unaufanya ukanda huu ufunguke na kuwezesha
kufikika kwa urahisi kutoka kwenye miji mikubwa ya Mbeya, Dar es salaam na
Dodoma, na pia kwa nchi jirani za Afrika ya Kati na Kusini kama vile Malawi,
Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Msumbiji, Rwanda, Burundi na Afrika ya
Kusini. Hali ya maji kwa sasa inaridhisha, umeme upo wa kutosha kwa matumizi ya
nyumbani hata hivyo kuna juhudi mbalimbali kuuongeza ukidhi kwenye shughuli za
viwanda. Sehemu za Mkoa wa Rukwa zimeunganishwa na Shirika la Umeme la
Zambia Zambian Electricity Supply Company (ZESCO). Kwa upande wa Kigoma na
Katavi bado wanatumia umeme wa jenereta hata hivyo kuna juhudi za ujenzi wa
umeme wa jua katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji na kuunganisha na umeme wa gridi
ya Taifa kutokea Tabora.

Waheshimiwa,
Mabibi na Mabwana;
Ninaweza kuendelea tena na tena kuelezea fursa na hatua zilizochukuliwa na
Serikali. Lakini ni vyema kusema tu kuwa kwa sasa mazingira ya biashara
yameboreshwa sana na yameanza kuvutia wawekezaji wengi kiasi kwamba shughuli
za uwekezaji zimeongezeka kwenye sekta za Kilimo, Madini na Umeme katika
kipindi cha miaka mine iliyopita.
Kuna wawekezaji ambao wanasema kuwa ukanda huu ni eneo ambalo wawekezaji
wanaliangalia kwa jicho la kimkakati kwa sasa. Hii inatokana na ukweli kuwa madini
mengi yanapatikana katika Ukanda huu kama vile Dhahabu, Nickel, Makaa ya Mawe,
Chokaa, Shaba na Madini ya Vito. Hivyo mtu anaweza kuchagua eneo lo lote
analopenda katika ukanda huu ambao una watu wapatao 3,697,073 kutokana na
sensa ya mwaka 2012. Kulingana na takwimu za Shirika la Takwimu za mwaka 2013
pato la mkaaji wa ukanda huu anapata wastani wa Tshs. 910,963 kwa mwaka.
Uanzishwaji wa Eneo Maalum la Kiuchumi Kigoma (Kigoma Special Economic Zone
KiSEZ) ni hatua nyingine ya Serikali kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji
katika viwanda, biashara na huduma za kiuchumi katika kuunganisha fursa zilizopo
na masoko ya ndani na nje ya nchi. Hali hiyo imelenga katika kuufanya mji wa
Kigoma/Ujiji kuwa kituo kikuu cha biashara katika eneo la Maziwa Makuu. Kuwekeza
kwenye eneo hili kunamfanya mwekezaji kupata faida ya kiushindani katika
shughuli za viwanda na biashara kwenye eneo lote la Maziwa Makuu.
Waheshimiwa;
Mabibi na Mabwana;
Kwa sasa napenda kuwakaribisha nyote na biashara zenu kuwekeza katika Ukanda
huu wa Ziwa Tanganyika. Kuna fursa nyingi ambazo watoa mada watabainisha na
mtapata fursa ya kuwasiliana mmoja mmoja na kila Mkoa au kila Halmashauri au
kila Mfanyabiashara.
Ukanda unategemea zaidi kilimo na zaidi mazao ya chakula kama vile mpunga,
ndizi, mahindi, viazi, maharage, na karanga ambapo mazao ya biashara ni kahawa,
tumbaku, alizeti, mawese. Mazao hayo ndiyo yanaendesha maisha ya watu wa
ukanda huu shughuli zingine ni uvuvi na biashara. Hata hivyo kilimo ni cha hali ya
chini sambamba na uvuvi. Ninawaalika kuwekeza kwenye eneo hilo kuboresha sekta
ya kilimo ambayo inaajiri watu wengi. Ukanda huu umejaliwa mito na maziwa yenye
maji baridi na safi, hivyo umwagiliaji unaweza kufanyika kwa ufanisi mkubwa.
Nimesikia kuna baadhi yenu mnataka kuwekeza kwenye nishati, ninawakaribisha.
Kama nilivyosema hapo awali Ukanda huu unahitaji umeme mwingi zaidi ili kuweza
kuimarisha sekta ya viwanda hasa viwanda vya usindikaji wa mazao ya kilimo na
uvuvi.
Waheshimiwa;
Mabibi na Mabwana;

4
Ninafahamu kuwa baadhi yenu mnataka kuwekeza kwenye utalii. Ukanda huu bado
haujapiga hatua nzuri kwenye sekta ya utalii, hivyo ni fursa nzuri kwa sasa
kuwekeza kwani hili ni eneo lililojaliwa aina mbali mbali ya wanyamapori
wanaopatikana kwenye mbuga na maeneo mengine ya hifadhi kama vile Hifadhi za
Taifa za Mahale, Gombe na Katavi au pori la Moyowosi na Ugalla. Katika mbuga hizo
kuna wanyama kama vile tembo, twiga, mamba, nyati, kiboko na sokwe mtu. Aidha,
kuna ndege na mimea ya aina yake. Wawekezaji wanaweza kuwekeza kwenye hoteli
na huduma mbali mbali za kitalii.
Kama nilivyosema awali, eneo la viwanda ni muhimu kuangaliwa kwa mapana yake,
ukanda huu una maliasili nyingi kama vile madini na mazao mbali mbali. Hali hiyo
inaufanya Ukanda uwe na mali ghafi ya kusaidia kuanzishwa kwa viwanda vya
uchakataji wa mazao mbali mbali kama vile mazao ya alizeti, mchikichi, mahindi,
mpunga, mazao ya mifugo na madini.
Waheshimiwa;
Mabibi na Mabwana;
Tanzania kwa sasa inatoa huduma bora za kiushindani kupitia sheria mbali mbali
kama vile sheria ya Uwekezaji ya mwaka 1997, sheria ya Maeneo Uchakataji kwa
ajili ya kuuza nje ya mwaka 2002, sheria ya Maeneo Maalum ya Kiuchumi ya mwaka
2006, sheria ya Madini ya mwaka 1998 na sheria ya mafuta ya Nishati ya mwaka
1981.
Serikali imejikita katika kutekeleza Mpango wa Kuboresha na Kuimarisha Mazingira
ya Biashara (Business Environment Strengthening for Tanzania BEST). Lengo
kubwa la mradi huo ambao ulianza Desemba, 2003, ni kupunguza urasimu wa
Serikali na kuboresha huduma kwa sekta binafsi ikiwemo na mashauri ya
kibiashara.
Tanzania ni nchi inayotoa motisha nzuri kwa wawekezaji. Pengine ni moja ya nchi
zinazotoa motisha bora kuliko nchi nyingi katika Afrika. Nina imani kuwa
Wakurugenzi wa Maeneo Maalum ya Kiuchumi (EPZA) na Mkurugenzi wa Kituo cha
Uwekezaji Nchini watakuwa wako hapa pamoja nasi. Nina hakika watazungumza
kwa kina kwenye mawasilisho yao kuhusu jambo hilo.
Ni dhahiri kuwa, Ukanda wa Ziwa Tanganyika ndiyo lango kwa nchi nne
zinazopakana na Ukanda huo. Ukanda huu unatoa njia fupi ambayo ni ya asili kwa
nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda, Burundi, na Zambia. Hivyo
kuwekeza katika Ukanda huu unatoa fursa ya kuyafikia masoko ya nchi hizo kwa
urahisi zaidi.
Waheshimiwa;
Mabibi na Mabwana;
Nimezungumza kwa kirefu kuliko nilivyotarajia. Naomba nihitimishe kwa kusema
yafuatayo. Kwanza, Ukanda wa Ziwa Tanganyika uko tayari kufanya biashara nanyi.
Pili, katika ukanda huu kuna kila kitu kinachohitajika katika uwekezaji: mazingira
mazuri ya biashara, hali ya amani na utulivu, serikali inayojali wawekezaji, mali asili,
wafanyakazi wanaojituma, soko la kutosha, hali nzauri ya kijiografia na kadhalika.

5
Lakini, kitu cha muhimu, kuwepo kwangu na kuwepo kwa Waziri Mkuu na Serikali
yote kwa ujumla ni kuwahakikishia kuwa tuko makini na tumejipanga kikamilifu
kufanya biashara nanyi. Serikali hii ni ya kuwawezesha wadau na imedhamiria
katika kuunganisha fursa zilizopo na masoko ya ndani na nje ya nchi
kama kauli mbiyu ya kongamano inavyosema.
Ninaimani kuwa hakuna sababu ya kusita kuwekeza na kufanya biashara katika
Ukanda huu wa Ziwa Tanganyika.
Ninawashukuru sana na ninawatakia mafanikio katika mazungumzo yenu. Karibuni
sana Ukanda wa Ziwa Tanganyika.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA

You might also like