Download as pdf or txt
Download as pdf or txt
You are on page 1of 36

BIBLIA

YA
WATOTO

Toleo la kwanza Magulya Meja


BIBLIA YA WATOTO

Mafundisho Matakatifu Ya Hadithi Za Biblia Kwa Watoto.

JC-RECORDS STUDIO.

Picha zote kwa hisani ya SweetPublishing.com , FreeBibleImages.org na


BibleArtLibrary.com

Haki zote zimehifadhiwa. Hairuhusiwi kupiga chapa, kunakili au kutumia kitabu


hiki kwa namna nyingine yoyote zaidi ya kujifunza. Matumizi mengine yoyote
ni lazima yaambatane na ridhaa ya mwandishi wa kitabu hiki.
BIBLIA YA WATOTO, Toleo la kwanza 2017.

Wasiliana na mwandishi wa kitabu hiki kwa anuani zifuatazo:

P.O BOX 46037, Dar es salaam, Tanzania.

Barua pepe:books@jcrecordsstudio.com

Simu namba: 0712 266865.

ISBN 8181 2219 8720 12

I
SHUKURANI

Kipekee napenda kumshukuru Mungu Baba ambaye ni mtunzi, mhariri mkuu na


pumzi ya uhai ya kila neno katika maandiko matakatifu.

Bila yeye kuwa kiongozi wangu na mshawishi mkuu kwangu basi nisingeweza
kuandika kitabu hiki cha BIBLIA YA WATOTO. Kupitia Roho Mtakatifu
amenitia moyo, amenipa faraja na ameniinua ili nipate kukamilisha vyema wito
wa kuandika kitabu hiki cha BIBLIA YA WATOTO.

Shukurani za dhati ziende kwa wote ambao kwa namna mbalimbali


wamenisaidia kufanikisha toleo la kwanza la kitabu cha BIBLIA YA WATOTO.
Mungu azidi kuwabariki na kuwajaza roho ya upendo.

Kutoka sakafu ya moyo wangu namshukuru mama yangu Dr. Neema Ellah
Kapalata , Marafiki zangu wawili wa karibu sana Amanda Audax Kapalata na
Jayden-Christ Magulya Meja kwakua nami wakati wote, wakinitia moyo na
kunipa nguvu ya kuitikia wito wangu Kiroho.

Nawashukuru sana kwakunipa muda wao tuliostahili kuwa pamoja lakini


wakautoa kwangu ili kuniwezesha kuandika kitabu hiki. Mungu azidi
kuwabariki na kutimiza kusudio lake jema maishani mwenu. Amina.

Mwisho lakini siyo mwisho kwa umuhimu, napenda kuwashukuru


SweetPublishing.com , FreeBibleImages.org na BibleArtLibrary.com kwa kutoa
ruhusa ya michoro yao mbalimbali ya masimulizi ya Biblia kutumika katika kazi
hii ya kitabu cha Biblia ya Watoto.

Mungu awabariki nyote.

II
TABARUKU

Kitabu hiki nakitabaruku kwa rafiki yangu wa karibu sana na mtoto wangu
Jayden-christ Magulya Meja.

Baraka ya uwepo wako imeyapa sura mpya maisha yangu katika namna ya
kipekee sana, hakika Mungu amekutumia kunibadilisha.
Nimeona matendo makuu na upendo mkuu wa Mungu kupitia wewe.

Shauku yako ya kupenda kujifunza neno la Mungu limekua kichocheo changu


katika kuitikia wito wangu wa kuandika kitabu cha masimulizi ya maandiko
matakatifu kwa ajili ya watoto.

Kitabu hiki ni maalumu kwa ajili ya watoto wote na wazazi wote kupitia baraka
niliyopewa na Mungu ya mwanangu mpendwa Jayden-christ Magulya Meja.

Sifa na utukufu naurudisha kwa Mungu aliye mkuu na muweza wa yote.

III
YALIYOMO

HAKI MILIKI - I
SHUKURANI - II
TABARUKU - III
YALIYOMO - IV
UTANGULIZI -V

MUNGU AUMBA ULIMWENGU - Sura ya kwanza, 1-2


ADAMU NA HAWA - Sura ya pili, 3-4
MAJARIBU NA DHAMBI - Sura ya tatu, 5-7
NUHU AJENGA SAFINA - Sura ya nne, 8-10
MNARA WA BABELI - Sura ya tano, 11-13
KUZALIWA KWA ISAKA - Sura ya sita, 14-17
NDOTO YA YUSUFU - Sura ya saba, 18-20
YUSUFU AKIWA MISRI - Sura ya nane, 21-24
MUSA AFANYWA MWANA MFALME - Sura ya tisa, 25-26
MUSA AONGEA NA MUNGU - Sura ya kumi, 27-29

IV
UTANGULIZI

Jukumu la malezi mema kwa watoto wetu ni msingi mkuu na wajibu wa kila
mzazi.
Hakuna njia sahihi zaidi kama kutumia nyenzo bora kabisa katika malezi, yani
mafundisho matakatifu ya neno la Mungu.
Kitabu hiki cha BIBLIA YA WATOTO kinatoa fursa nzuri kwa wazazi au
walezi kufafanua kiurahisi hadithi za mafundisho matakatifu kutoka katika
Biblia.
Kitabu hiki pia kimelenga kuwajengea watoto ufahamu wa matendo makuu ya
Mungu.
Ufahamu huu utawasaidia watoto kukua katika mazingira ya kumfahamu na
kumtumikia Mungu.
Sote tunatambua kuwa neno la Mungu ni chanzo kikuu cha maarifa, hivyo
maarifa haya ya neno la Mungu yatawajenga watoto wetu kuwa wanajamii bora.
Kitabu hiki kimesheheni picha za kuvutia zenye kuakisi simulizi kutoka katika
Biblia.
Nimatumaini yangu kuwa kitabu hiki cha BIBLIA YA WATOTO kitaboresha
malezi bora na mema kwa watoto wetu na kujenga misingi imara ya familia zetu
katika kumtumikia na kumuabudu Mungu.
Mungu awabariki wazazi wote na kuwatumia kama vyombo vyake katika
kusimamia malezi bora ya watoto. Amina.

V
MUNGU AUMBA ULIMWENGU-Sura ya kwanza

Mungu alipoanza kuumba Mbingu na Dunia, Dunia ilikua haina umbo, hivyo
alisema ufanyike mwanga, nao ukafanyika.
Kisha akagawanya giza na nuru, giza akaita usiku na nuru akaita mchana, kwa
pamoja vikafanya siku moja.
Mungu akasema maji yajigawanye, yalipojigawa basi juu ikafanyika anga na
chini ikafanyika bahari. Yote haya yalifanyika siku ya pili ya uumbaji.
Mungu akasema maji yote yajikusanye yafanyike bahari ili ipatikane nchi kavu,
na hivyo ndivyo ilivyofanyika.
Kisha Mungu aliumba mimea ya aina mbalimbali, haya yote yalifanyika siku ya
tatu ya uumbaji.
Mungu akaumba Jua ili litoe mwanga wakati wa mchana, kisha akaumba Mwezi
ili utoe nuru wakati wa usiku, pia akaumba Nyota za angani. Haya yote
yalitendeka siku ya nne ya uumbaji.
Mungu akasema vifanyike viumbe ndani ya Bahari, Mito na Maziwa.
Wakafanyika Samaki na viumbe hai wengine wengi wa aina mbalimbali wa
majini.
Mungu akasema anga ifanyike kuwa na Ndege wa kila aina, navyo ndivyo
ilivyofanyika.
Mungu akaubariki uumbaji wote, haya yote yalifanyika siku ya tano ya uumbaji.
Mungu akasema Dunia ijazwe wanyama wa kila aina watambaao, watembeao na
pia wadudu wa aina mbalimbali.
Kisha Mungu akamuumba Mwanadamu kwa taswira yake, akamuona ni kiumbe
bora kuliko viumbe vyake vyote, hivyo akapewa utawala juu ya viumbe vingine
vyote katika uso wa Dunia, kuanzia katika Bahari, Nchi kavu na Angani.
Mungu alimuumba kwanza mwanaume ambaye jina lake alimuita Adamu na
kisha akamuumba mwanamke kwa kutumia ubavu wa Adamu, naye jina lake
aliitwa Hawa.
Akawabariki wote na kisha akawambia wazae na kuujaza ulimwengu. Haya yote
yalifanyika katika siku ya sita ya uumbaji.
Siku ya saba Mungu alipumzika na hakufanya kazi yoyote . Mungu aliibariki
siku ya saba na kuifanya kuwa siku takatifu ya Mungu.
Uumbaji wa Mungu kama unavyoonekana katika picha. Ndege, wanyama,
mimea, mito na anga.

1
MUNGU AUMBA ULIMWENGU-Sura ya kwanza

Viumbe hai vyote viliishi kwa amani na furaha, hapakua na tabu, dhiki wala
magonjwa.

Somo la kujifunza:
Je, ni somo gani la kimaadili ambalo tunaweza kujifunza kupitia uumbaji
wa Mungu?

Tunajifunza kuwa Mungu ndiyo muumbaji wa kila kitu.


Tunapaswa kumshukuru Mungu kwavitu vyote tulivyonavyo, vinavyotuzunguka
na zaidi tunapaswa kumshukuru Mungu kwa kutuumba na kutupatia uhai.

2
ADAMU NA HAWA-Sura ya pili

Mungu alitengeneza bustani ya Edeni. Bustani hii aliita Paradiso.


Katika bustani hii Mungu aliweka miti ya matunda mazuri na maua ya kuvutia.
Katikati ya bustani ya Edeni Mungu aliweka mti ulioitwa mti wa uhai.
Mungu akamuweka mwanadamu wa kwanza aliyeitwa Adamu katika bustani ya
Edeni ili aitunze na kuilinda.
Kulikua na vyakula na matunda ya kila aina katika bustani hiyo.
Mungu alimpa ruhusa Adamu ya kula matunda katika miti yote iliyopo katika
bustani ya Edeni isipokuwa mti ule wa katikati ambao ni mti wa uhai.

3
ADAMU NA HAWA-Sura ya pili

Mungu akaleta wanyama na ndege wote katika bustani ya Edeni, kisha


akamwambia Adamu awape majina Wanyama na Ndege wote, naye Adamu
akawapa majina viumbe hai wote.
Mungu akaona Adamu ni mpweke, hivyo akasema atamuumba msaidizi wake
wa kumfaa.
Mungu akampa usingizi mzito Adamu, akatoa mbavu yake moja na kumuumba
mwanamke, naye akafanywa kuwa msaidizi wake, mwanamke huyu aliitwa
Hawa.
Adamu akamfurahia sana Hawa na kusema huyu ni ubavu wangu na mwili
wangu.

Somo la kujifunza:
Je, ni somo gani la kimaadili ambalo tunaweza kujifunza kupitia uumbwaji
wa Adamu na Hawa?

Tunajifunza kuwa Mungu anatupenda sana Wanadamu ndiyo maana akatuumba


kwa mfano wake.
Mungu aliona kila alichoumba ni chema machoni mwake lakini alipomuumba
Adamu na Hawa akaona ni wema zaidi na ni bora kuliko viumbe wengine wote.
Ndiyo maana akatufanya Wanadamu kuwa watawala wa kila kitu kilichopo
duniani.
Tunajifunza kuwa Mwanaume na Mwanamke wote wana hadhi na haki sawa
machoni mwa Mungu kwa kuwa wote wawili ni mfano wake.
Tunajifunza kuwa asili ya uumbaji wa Mwanadamu ni kupendeza kwa usafi wa
moyo, roho na uhai wa milele.
Iliwapasa Adamu na Hawa kutii kila Mungu alichowaamuru bila kujiamulia
wenyewe watakavyo.
Tunajifunza kuwa tunapaswa kuwa na utii mbele ya maamrisho yote ya Mungu.
Tusipokua watii kwa Mungu tutakua tumefanya dhambi na mwisho wa dhambi
ni anguko la Mwanadamu na mauti.
Mungu aliwataka Adamu na Hawa wapendane, washirikiane na kusaidiana
kwakuwa wao ni mwili mmoja kama ilivyo kwa Yesu Kristo na Kanisa.

4
MAJARIBU NA DHAMBI Sura ya tatu

Miongoni mwa viumbe alivyoviumba Mungu, Nyoka aliumbwa kama kiumbe


mjanja sana na mwerevu.
Hivyo Shetani kwakutambua werevu na ujanja wa Nyoka, akaamua kumtumia
Nyoka kumrubuni Hawa.
Nyoka alimuuliza Hawa, Hivi ni kweli Mungu amekataza msile tunda la mti
ulio katikati ya bustani?
Hawa akamjibu, Ndiyo tunaweza kula matunda ya miti yote, isipokua ule mti
ulio katikati ya bustani, tukifanya hivyo tutakufa.
Nyoka kwa kutumia werevu na ujanja wake akamshawishi Hawa kwa
kumwambia, Hapana hamuwezi kufa, ila mkila tunda hilo mtafunguka macho
ya ufahamu na kuwa kama Mungu, mtayajua mema na mabaya.

5
MAJARIBU NA DHAMBI Sura ya tatu

Basi Hawa akatamani kula tunda lile, hivyo akaamua kulichuma na kula,
akaenda pia kumpa mume wake Adamu, naye akaingia katika mtego wa Shetani
kwa kula tunda alilopewa na Hawa.
Baada ya kukiuka amri ya Mungu ya kutokula tunda la mti wa katikati ya
bustani, macho yao yakafunguka na kujiona kuwa wako watupu.
Wakaingiwa na aibu na kutafuta majani na magome ya miti ili wapate kujistiri.
Ilipofika jioni wakasikia sauti ya Mungu ikiita Uko wapi Adamu?
Adam akajibu, Nimesikia sauti yako lakini naogopa niko mtupu.
Mungu akamuuliza, Ni nani amekwambia kwamba uko mtupu?
Adam akajibu, Huyu mwanamke uliyenipa kama msaidizi wangu, kanipa tunda
la mti uliotukataza nami nikala.
Mungu akamuuliza Hawa, Kwa nini umefanya hivyo?

Hawa akajibu, Ni Nyoka ndiyo amenirubuni kula tunda la mti uliotukataza.


Mungu akamwambia Nyoka ya kwamba umelaaniwa kuliko viumbe vyote na
utatambaa kwa tumbo siku zote za uhai wako.
Kisha Mungu akamwambia Hawa, Utazaa kwa uchungu na mume wako
atakutawala.
Halafu Mungu akamwambia Adamu, Utakula kwa jasho lako siku zote za
maisha yako mpaka utakapozikwa ardhini.
Mungu akawapa mavazi ya ngozi ya wanyama ili wajistiri, hii ina maana
wanyama walikufa kama mbadala wa Adamu na Hawa baada ya kuvunja amri
ya kutokula tunda la mti wa katikati ya bustani.
Mungu akawafukuza Adamu na Hawa kutoka katika bustani ya Edeni na kuanza
maisha ya kujitegemea duniani.

Somo la kujifunza:
Je, ni somo gani la kimaadili ambalo tunaweza kujifunza kupitia majaribu
ya dhambi ya Adamu na Hawa?

Katika masimulizi ya anguko la dhambi kutoka kwa Adamu na Hawa


tunajifunza kuwa tunapaswa kuwa watii na wanyenyekevu mbele za Mungu.
Utii hutulinda hivyo kila wakati ni vizuri kufanya kile ambacho Mungu
amesema na kutuamrisha.

6
MAJARIBU NA DHAMBI Sura ya tatu

Tunapo mtii Mungu tunaonyesha kuwa tunampenda na tunamtumikia yeye hivyo


hatuwezi kumkosea Mungu.
Maisha yetu yanategemea utii kwa Yehova, yaani Mungu aliye mkuu.
Adamu na Hawa walipaswa kuonyesha utii kwa Mungu nao wangeishi katika
paradiso milele.

Je, ni kweli nyoka anaweza kuzungumza?


Hapana, Nyoka alitumika tu katika kutimiza lengo la ulaghai wa Shetani.
Malaika aliyeasi Mbinguni yaani Shetani ndiye aliyekua akizungumza na Hawa
kwa kutumia muonekano wa Nyoka.

Alimtumia Nyoka kwasababu Nyoka ni mnyama mjanja na mwerevu.


Anguko la Adamu na Hawa linatufundisha kuwa tusipomtii Mungu matokeo
yake ni kupoteza ukamilifu wetu, kupoteza baraka zetu na neema za Mungu juu
yetu.
Pia somo hili la anguko la dhambi kupitia wasifu wa Nyoka tunajifunza kuwa
sote tunapaswa kuwa wajanja na werevu ili kuepuka ulaghai wa Shetani pale
anapopanga kuturubuni kwa njia mbalimbali za kumuasi na kutomtii Mungu.

7
NUHU AJENGA SAFINA-Sura ya nne

Kadiri watu wa ulimwengu walivyozidi kuongezeka uovu nao ukazidi. Mion-


goni mwa wote Mungu alimuona Nuhu kuwa mtu pekee aliye mwema machoni
pake.
Mungu akamwambia Nuhu atengeneze Safina kubwa, kwakuwa anataka kuun-
gamiza ulimwengu kwasababu maovu yamekithiri.
Nuhu akaanza kujenga Safina, ilimchukua miaka mia moja kuikamilisha Safina
hiyo.
Nuhu alikuwa na umri wa miaka mia sita alipokua anaingia ndani ya Safina.
Ndani ya Safina aliingia yeye, mke wake na watoto wake watatu walioitwa
Shemu, Hamu na Yafeti. Nao pia walikua pamoja na wake zao.

8
NUHU AJENGA SAFINA-Sura ya nne

Mungu pia alimuagiza Nuhu kubeba hifadhi ya chakula kwa ajili ya kukidhi
mahitaji ya chakula katika kipindi chote cha gharika kubwa.
Baada ya siku saba Mungu mwenyewe alifunga mlango wa Safina.
Mvua ikaanza kunyesha usiku na mchana kwa siku arobaini bila kukoma.
Mungu akafungulia chemuchemu zote za ardhini. Mafuriko makubwa
yakatokea.
Maji yalikua mita saba juu ya kilele cha mlima mrefu kuliko yote Duniani.
Mungu akamuelekeza Nuhu aingize ndani ya safina Wanyama wawili wawili wa
kila aina ili wasidhurike.

Viumbe vyote vikateketea, isipokuwa vile vilivyokuwa ndani ya Safina tu.


Mafuriko yalidumu katika Dunia kwa siku mia moja na hamsini.
Mungu akamkumbuka Nuhu, hivyo akaamuru upepo mkali ukayakaushe maji.
Kina cha maji kilishuka katika ardhi.
Safina ikaweza kusimama juu ya milima ya Ararati.
Baada ya muda Nuhu alimtoa Njiwa nje ya Safina ili atambue kama maji yote
yamekauka au la. Njiwa akarudi baada ya muda mfupi tu kwakua alikosa
sehemu ya kutua.
Baada ya siku saba Nuhu akamtoa tena Njiwa, baada ya kitambo kidogo njiwa
alirudi na jani la mmea wa mzeituni.
Nuhu akaamua kusubiri kwa siku saba kisha akamtoa tena Njiwa lakini mara hii
Njiwa hakurudi tena katika Safina.

Nuhu akajua ya kwamba maji yamekauka katika ardhi.


Maji ya gharika yalikaa katika uso wa dunia kwa zaidi ya mwaka mzima.
Nuhu akatoka nje ya Safina, akajenga Madhabahu na kumtolea Mungu sadaka.
Mungu akaweka agano na Nuhu akimwambia Sitaangamiza tena ulimwengu
kwa sababu ya wanadamu.
Mungu akambariki Nuhu na wanawe na kuwambia zaeni na mkaongezeke, na
kila kiumbe mkakitawale.

9
NUHU AJENGA SAFINA-Sura ya nne

Somo la kujifunza:
Je, ni somo gani la kimaadili ambalo tunaweza kujifunza kupitia masimulizi
ya maandiko matakatifu kuhusu Nuhu na Safina?

Tunajifunza kuwa Mungu anachukizwa sana na dhambi za wanadamu.


Hivyo ilimpasa kuondoa uovu wote na waovu wote Duniani ili Dunia impendeze
Yeye kama alivyokusudia alipoiumba.
Pia tunajifunza kuwa tunapaswa kuwa wasikivu juu ya mafundisho na maonyo
ya Mungu, ndiyo maana Mungu alimsalimisha Nuhu na familia yake kwakuwa
walikua waadilifu mbele za Mungu.Kabla ya gharika Nuhu aliwahubiria watu na
kuwaonya waache maasi na kutenda mema lakini hakuna aliyesikiliza isipokua
familia yake tu.

10
MNARA WA BABELI-Sura ya tano

Baada ya kipindi cha gharika kupita, idadi ya watu ikaanza kuongezeka tena.
Wengi wakaweka makazi katika mji ulio mashariki mwa ardhi ya Babiloni.
Mungu aliamrisha watu kujiwekea viongozi miongoni mwa jamii zao.
Katika kipindi hicho alikuwepo muwindaji mmoja hodari aliyeitwa Nimrodi,
alikua ni mtu mwenye haiba ya kiungozi na mwenye ushawishi mkubwa.
Lakini Nimrodi hakua mwaminifu kwa Mungu, alitumia kipawa chake kikubwa
alichopewa na Mungu kuwashawishi watu wajenge jamii ambayo haikumuabudu
na kumtumikia Mungu.

Baada ya ushawishi mkubwa wa Nimrodi watu wote wakakubaliana kujenga


mnara mrefu utakaofika hadi mbinguni.Dhumuni lao likiwa ni kujijengea
umaarufu mkubwa, huku wakiamini kuwa itakua alama yao katika kujenga
ufalme mkubwa utakaowawezesha kutokutawanyika na kutambulika Duniani
kote. Haya yote walipanga kuyafanya kwa ajili ya utukufu wao.

11
MNARA WA BABELI-Sura ya tano

Mji wa Babeli ulikua alama ya umoja wa watu katika jamii ambayo ililenga
kutotii maamrisho ya Mungu.
Pia mnara wa Babeli ulikua ni alama ya umoja wa kidini ambao ulikua na
dhumuni la kupingana na mamlaka kuu ya Mungu.
Watu wale wakaanza kuujenga mnara wa Babeli huku wakishirikiana kwa
kugawana kazi mbalimbali kufanikisha adhima yao.
Kwakuwa wote walikua wakiongea lugha moja Mungu aliona ni rahisi kwao
kukubaliana kufanya kila jambo walitakalo.
Hivyo Mungu akawachanganya lugha yao, wakashindwa kuelewana tena.
Watu wote wakatawanyika sehemu mbalimbali Duniani kote, wengine wakaenda
Mashariki, wengine Magharibi, Kusini na Kaskazini.
Mahali hapo paliitwa Babeli ikimaanisha mchanganyiko au kuchanganyika.

Somo la kujifunza:
Je, ni somo gani la kimaadili ambalo tunaweza kujifunza kupitia watu wa
mnara wa Babeli?

Tunajifunza kuwa watu wa Babeli walipoamua kujenga jamii moja mahali


pamoja walipingana na maagizo ya Mungu kuwa watu watawanyike na kuujaza
Ulimwengu.
Lakini tunajifunza kuwa ni chukizo mbele za Mungu kujenga jamii ambayo
haimuabudu wala kumtumikia Mungu.
Tunajifunza kuwa jambo lolote tunalofanya ambalo halirudishi sifa na utukufu
kwa Mungu haliwezi kusimama na kufanikiwa.
Kila tunalofanya lazima liwe katika njia sahihi na lirudishe sifa na utukufu kwa
Mungu.
Tunajifunza kuwa kiburi na dhambi hufanya watu watengane na kutokuelewana
lakini palipo na upendo na utii wa Mungu hata tofauti za lugha na utamaduni
bado huunganisha watu.

Mungu alimtokea Abramu na kumuahidi kuwa uzao wake utakua mkumbwa na


mwingi kama Nyota za angani.
Lakini Abramu na Sarai walikua wazee sana na hawakubarikiwa kupata mtoto
kwa kipindi hicho chote.

12
MNARA WA BABELI-Sura ya tano

Abramu alikua na miaka Mia moja na Sarai alikua na miaka Tisini.


Hata hivyo Abramu akawa ni mwenye imani na kumtumainia Mungu juu ya
ahadi yake.
Kutokana na imani yake kubwa kwa Mungu, Mungu akambadili jina Abramu
lenye maana ya Baba na kuwa Ibrahimu, ikiwa ina maana ya Baba wa wengi.
Pia akambadili jina Sarai lenye maana ya Mama na kuwa Sara lenye maana ya
Mama wa wengi.

13
KUZALIWA KWA ISAKA-Sura ya sita

Mungu alimtokea Abramu na kumuahidi kuwa uzao wake utakua mkumbwa na


mwingi kama Nyota za angani.
Lakini Abramu na Sarai walikua wazee sana na hawakubarikiwa kupata mtoto
kwa kipindi hicho chote.
Abramu alikua na miaka Mia moja na Sarai alikua na miaka Tisini.
Hata hivyo Abramu akawa ni mwenye imani na kumtumainia Mungu juu ya
ahadi yake.
Kutokana na imani yake kubwa kwa Mungu, Mungu akambadili jina Abramu
lenye maana ya Baba na kuwa Ibrahimu, ikiwa ina maana ya Baba wa wengi.
Pia akambadili jina Sarai lenye maana ya Mama na kuwa Sara lenye maana ya
Mama wa wengi.

Siku moja Ibrahimu alikua pembezoni mwa nyumba yake, akaona watu watatu,
akawasalimu kwa kuwasujudia, kisha akawambia wasipite bila yeye
kuwakarimu kwa chakula.

14
KUZALIWA KWA ISAKA-Sura ya sita

Ibrahimu aliwachinjia Mwanakondoo na Sara akawatayarishia mkate mzuri wa


kuoka.
Wote wakamshukuru Ibrahimu kwa ukarimu wake.
Mmoja wa wageni wale akamuuliza Ibrahimu, Mke wako Sara yuko wapi?,
Ibrahimu akamjibu, Yuko ndani ya nyumba.
Mmoja kati ya wageni wale watatu alikua ni Mungu aliyejivisha umbo la
Mwanadamu. Mgeni huyu akamwambia Ibrahimu, Baada ya mwaka mmoja
nitarejea tena, na katika kipindi hicho mke wako Sara atakua na mtoto wa
kiume.
Sara akiwa pembeni alisikia, akaanza kucheka kwakuwa hakuamini maneno
hayo.
Yeye aliamini umri wa kuzaa umeshampita na ni mzee sana, hivyo
isingewezekana kwake kushika mimba na kuzaa mtoto.

Baada ya mwaka Mungu alitimiza ahadi yake, aliwabariki Ibrahimu na Sara


mtoto wa kiume, nao walimuita jina lake Isaka.
Baada ya mtoto kukua, siku moja Mungu alimuamuru Ibrahimu amtoe sadaka ya
kuchinja mtoto wake wapekee Isaka.
Ibrahimu kwakuwa alikua na imani iliyojengeka ndani yake alitii sauti ya
Mungu.
Akamchukua mwanae Isaka huku akiwa na mzigo wa kuni wakielekea sehemu
ambayo Ibrahimu alikua akiitumia kutolea sadaka ya kuchinja. Walipofika
mahali hapo Ibrahimu aliandaa kuni na kisha kumlaza mwanae Isaka ili amtoe
sadaka kwa Mungu.
Kabla ya Ibrahimu kuchukua kisu chake muda uleule Mungu alimshusha kondoo
katika kichaka na kumwambia Ibrahimu amchinje Kondoo yule kama sadaka na
amuache mtoto wake wa pekee Isaka.
Mungu aliijaribu imani ya Ibrahimu na akapendezwa na imani aliyoinyesha
Ibrahimu.
Kwa imani hii kubwa aliyokuwa nayo Ibrahimu kwa Mungu, mpaka leo hii
Ibrahimu anatambulika kama Baba wa imani.

15
KUZALIWA KWA ISAKA-Sura ya sita

Somo la kujifunza:
Je, ni somo gani la kimaadili ambalo tunaweza kujifunza kupitia
mafundisho matakatifu juu ya kuzaliwa kwa Isaka?

Kupitia kuzaliwa kwa Isaka tunajifunza kuwa Mungu hutimiza ahadi zake kwa
wakati alioupanga Yeye. Tunapaswa kumuamini na kumtegemea Mungu.
Kupitia Ibrahimu tunajifunza kuishika imani katika mazuri tunayobarikiwa na
Mungu na hata kipindi ambacho tunapitia magumu katika maisha yetu.

Ibrahimu alisadiki juu ya ahadi ya Mungu hata pale ilipoonekana kibinadamu


yeye na Sara hawawezi kupata mtoto kutokana na uzee. Ibrahimu alimtii Mungu
pale alipoijaribiwa imani yake kwa kupewa agizo la kumtoa mwanae sadaka.
Ibrahimu bado aliishika imani na kusadiki maneno ya Mungu bila chembe ya
shaka.

16
KUZALIWA KWA ISAKA-Sura ya sita

Kupitia ibrahimu pia tunajifunza kuwa wakarimu kwa wageni


wanapotutembelea.
Pia Ibrahimu anatufundisha kuwa imani huonyeshwa kwa matendo hasa pale
aliporidhia kumtoa mtoto wake Isaka kama matoleo ya sadaka kwa Mungu.
Kupitia maisha ya Ibrahimu tunajifunza kuwa kutoa sadaka ni kuiishi imani na
ni njia ya kubarikiwa zaidi na Mungu katika maisha yetu.

17
NDOTO YA YUSUFU-Sura ya saba

Mtoto wa Isaka aliitwa Yakobo. Yakobo alikua na watoto kumi na mbili.


Mtoto aliyependwa sana na Yakobo alikuwa anaitwa Yusufu.
Yusufu alikua akifanya kazi ya kuchunga mifugo ya familia akiwa pamoja na
kaka zake.
Mara kadhaa Yusufu alitoa taarifa kwa baba yake juu ya mwenendo mbaya wa
kaka zake, hivyo baba yake alimpenda zaidi lakini kaka zake walimchukia na
kumuonea wivu.
Usiku mmoja Yusufu aliota ndoto kuwa atakuwa na mamlaka ya ukuu juu ya
kaka zake, na pia juu ya baba na mama yake.
Alipowaeleza ndugu zake juu ya ndoto hiyo, walipatwa na hasira na
wakamchukia sana mdogo wao.

18
NDOTO YA YUSUFU-Sura ya saba

Baba yake aliamua kumzawadia Yusufu koti zuri lenye rangi mchanganyiko,
lilikuwa ni koti la heshima na kimamlaka.
Kaka zake kwakuwa walimchukia Yusufu, siku moja walipanga njama ya
kumuua lakini mmoja kati ya kaka zake aliyeitwa Reubeni akawashauri
wasimuue lakini wamtupe katika shimo kubwa la kisima kilichokauka.
Walipomtupa katika shimo hilo ghafla wakaona wafanyabiashara Waishmaeli
kadhaa wakitoka Gileadi wakielekea Misri.
Mmoja wa kaka yake Yusufu aliyeitwa Yuda akawashauri wenzake wamtoe
shimoni na kuumuza kama mtumwa kwa wafanyabiashara wale Waishmaeli.
Hivyo walimuuza Yusufu kwa mfanyabiashara Muishmaeli kama mtumwa kwa
thamani ya vipande ishirini vya fedha.

19
NDOTO YA YUSUFU-Sura ya saba

Walipomaliza makabidhiano ya kumuuza mdogo wao walipanga njama kuuficha


uovu wao, hivyo wakachinja Mwanambuzi na kisha kuchukua nguo aliyovaa
Yusufu na kuichovya katika damu ili ionekanae kana kwamba Yusufu aliuwawa
na mnyama akiwa machungoni.
Walipofika nyumbani waliomuonyesha Baba yao nguo aliyokua ameivaa Yusufu
ikiwa imeloa damu.
Yakobo alilia kwa uchungu na huzuni kubwa, aliomboleza kwa kipindi kirefu
sana kutoweka kwa mtoto wake aliyempenda sana Yusufu.

Somo la kujifunza:
Ni somo gani la kimaadili tunalojifunza kupitia simulizi za mandiko
matakatifu juu ya ndoto ya Yusufu?

Masimulizi haya yanatufundisha juu ya mahusiano baina ya ndugu, kuwa


upendeleo na wivu miongoni mwa watoto wa Yakobo ulizaa chuki miongoni
mwao.
Wivu mbaya huzaa chuki, na chuki hupelekea anguko la dhambi.
Chuki iliwafanya kaka zake Yusufu hata watamani kuumua ndugu yao.
Ingawa hawakumuua laikini walimtendea maovu, waliamua kumuuza kama
mtumwa lakini bado mpango wa Mungu juu ya maisha ya Yusufu ulibaki
vilevile kumfanya kuwa mtawala mkuu wa Misri.
Mungu anaweza kuutumia uovu na kuubadili kuwa neema ya mazuri ili kutimiza
kusudio lake.

20
YUSUFU AKIWA MISRI-Sura ya nane

Wafanyabiashara Wakieshmaeli wakampeleka Yusufu Misri na kumuuza kama


mtumwa.
Wafanyabiashara wale walimuuza Yusufu kwa Potifa ambaye alikua kiongozi
mkuu wa wasaidizi wa Farao.
Farao alikua ni Mfalme wa nchi ya Misri.
Kutokana na tabia nzuri,uaminifu na imani ya Yusufu, Mungu alimbariki na
akafanywa kuwa msaidizi wa nyumba ya Potifa.
Mungu akaibariki nyumba ya Potifa kwasababu ya uwepo wa Yusufu.
Mungu alizidi kumbariki Yusufu na hatimaye kuwa msaidizi wa Mfalme.

Yusufu aliaminiwa sana na Farao lakini mke wa Farao alimuweka majaribuni


Yusufu kwa kumtaka kimapenzi.

21
YUSUFU AKIWA MISRI-Sura ya nane

Kutokana imani yake iliyo imara, Yusufu alikataa kufanya dhambi hiyo.
Baada ya kushindwa kumrubuni Yusufu mke wa Farao akamsingizia Yusufu
kuwa alijaribu kumbaka. Farao akaamuru Yusufu akamatwe na kufungwa
gerezani.
Lakini kamwe Mungu hakumuacha Yusufu, akaendelea kusimama naye hata
alipokua gerezani, huko nako akafanywa kuwa kiongozi wa wafungwa wote.
Yusufu alibarikiwa kipawa cha kutafsiri ndoto.
Siku moja Farao aliota ndoto ambayo watu wote wenye elimu ya kutafsiri ndoto
pamoja na waganga wa jadi katika nchi ya Misri walishindwa kutafsiri ndoto ile.

Waganga wale wa jadi wakapewa adhabu ya kifungo gerezani baada ya


kushindwa kutafsiri ndoto ya Farao.
Wakiwa gerezani waganga wale wa jadi, walimueleza Yusufu juu ya ndoto ya
Farao na ndoto zao nyingine, naye akawapa tafsiri sahihi ya ndoto hizo.
Baada ya miaka miwili msaidizi mmoja wa Farao ambaye alitolewa gerezani
alimkumbuka Yusufu juu ya uwezo wake katika kutafsiri ndoto, hivyo
akamwambia Farao juu ya kipawa cha Yusufu katika kutafsiri ndoto.

Ndoto ya Farao ilikua hivi, ndotoni aliona ngombe saba walionona wakiwa
kando ya mto, wakatokea ngombe saba wengine walio dhaifu na wamekonda
sana. Ngombe hao saba waliodhoofika wakawala wale ngombe wazuri
walionona.
Kisha akaota ndoto nyingine, katika ndoto hii aliona masuke membamba saba
yametokeza katika bua moja. Masuke hayo saba yakakaushwa na upepo mkali
wa Mashariki, kisha yakajitokeza masuke mengine saba makubwa yaliyojaa.
Masuke yale membamba yaliyo kauka yakameza yale masuke mema yaliyojaa.

Baada ya Farao kusikia juu ya kipawa cha Yusufu kutafsiri ndoto akaamuru
Yusufu atolewe gerezani.
Yusufu akapelekwa mbele ya Farao, naye akaitafsiri ndoto ya Farao kwa
utimilifu mkubwa. Akamwambia Farao kutakua na kipindi cha neema kwa
miaka saba hivyo ni bora kuwa na hifadhi kubwa ya chakula kwakuwa baada ya
kipindi hicho kutatokea kipindi cha ukame mkubwa kwa miaka saba hivyo
hifadhi ya chakula itakayokuwepo itasaidia taifa la Misri na hata watu wengine
katika kipindi hicho cha njaa kali.

22
YUSUFU AKIWA MISRI-Sura ya nane

Farao akafurahishwa na kipawa kikubwa cha Yusufu hivyo akamfanya Yusufu


kuwa mtawala wa Misri.
Chini ya uongozi wa Yusufu Misri ikawa taifa kubwa na lenye ustawi mkubwa.
Baada ya muda wa neema kupita ukame ukatanda sehemu kubwa ya Dunia,
lakini Misri ilikua na hifadhi kubwa ya chakula cha kutosheleza hata Mataifa
mengine yenye uhitaji wa chakula kwa kipindi hicho.
Katika kipindi cha ukame na dhiki kubwa ya chakula Duniani, siku moja kaka
zake Yusufu walienda Misri ili kutafuta chakula, hawakujua kuwa mdogo wao
waliyemuuza kama mtumwa ndiye mtawala wa Misri katika kipindi hicho.

23
YUSUFU AKIWA MISRI-Sura ya nane

Yusufu alipowaona aliingiwa na huzuni kubwa na kulia, akajitambulisha kwao


na kuwaomba wamlete Baba yake na ndugu wote ili wapate kuhamia Misri.
Kaka zake waliingiwa na simanzi kwa ubaya walioutenda dhidi ya mdogo wao
lakini Yusufu akawambia, Msihuzunike Mungu alinipeleka mbele zenu ili
kuwahifadhia masazo katika Nchi, na kuwaokoa nyinyi kwa wokovu mkuu.
Hivyo si nyinyi mlionileta huku ila ni Mungu, naye amenifanya mtawala katika
nchi yote ya Misri.
Kaka zake wakamleta Baba na ndugu zake wote nchini Misri, nao wakaishi
huko.

Somo la kujifunza:
Je, ni somo gani la kimaadili ambalo tunaweza kujifunza kupitia maisha ya
Yusufu akiwa Misri?

Kupitia maisha ya Yusufu tunajifunza kuwa, utii na imani ya Yusufu kwa


Mungu ilimsaidia kuweza kuvuka vikwazo vyote na majaribu yaliyomkabili.
Imani na hofu ya Mungu ulimsaidia Yusufu kutokulipiza kisasi kwa ndugu zake
hata kwa mabaya yote waliyomfanyia.
Masimulizi ya Yusufu yanatufundisha kuwa mwenye kusamehe na mwenye hofu
na utii kwa Mungu daima hutembea katika uangalizi wa Mungu na kufunikwa na
neema na baraka zake.
Kupitia tabia nzuri aliyoionyesha Yusufu tunajifunza kuwa pamoja na kufanyiwa
mambo mabaya na kusingiziwa uovu bado yatupasa kulipa yaliyo mema kwa
kila mabaya tunayotendewa.
Masimulizi ya Yusufu yanatufundisha kutokusahau ahadi ya Mungu, Yusufu
aliishika ahadi ya Mungu juu ya nchi ya ahadi, kabla ya kifo chake alisema
mifupa yake ifukuliwe na kusafirishwa mpaka nchi ya ahadi, na mifupa yake
izikwe huko kwakuwa aliamini juu ya siku ya utimilifu wa ahadi ya Mungu.
Maisha ya Yusufu yanatufundisha kuwa hata pale tunapoona uwepo wa Mungu
hauonekani katika ya mapito tunayopitia lakini tuamini ya kwamba Mungu
yupamoja nasi na anatupigania. Daima mipango ya Mungu ni mikubwa kuliko
tunavyoweza kuona au kufikiri.
Tunajifunza pia Mungu anaweza kutumia mapito yetu magumu kabisa katika
kuleta ushindi ili kusudi lake lipate kutimia hivyo tunapaswa kuwa wavumilivu
na wenye imani kwake.

24
MUSA AFANYWA MWANA MFALME-Sura ya tisa

Wanaisraeli waliishi Misri kwa miaka mingi, wakaongezeka na kuwa wengi sana
kwa idadi.
Mfalme mpya aliyekuwa mtawala wa Misri hakujua vyema juu ya msaada
mkubwa alioutoa Yusufu katika ustawi wa Misri na kuiepusha na janga kubwa la
ukame lililoikumba Misri kwa miaka saba.
Hakupendezwa kabisa na ongezeko kubwa la idadi ya Waisraeli nchini Misri.
Alihofia kuwa idadi yao itawapa nguvu na hata kuamua kuupinga utawala wa
Misri.
Hivyo mfalme akawapa wakati mgumu sana Wanaisraeli wote, aliwapa kazi
ngumu kupita kiasi, zenye mateso na unyanyasaji mkubwa.
Lakini Waisraeli walizidi kuzaliana na kuongezeka.
Baada ya Mfalme kuona Waisraeli wanaendelea kuongezeka, Mfalme akatoa
amri ya kuuwawa kwa kila mtoto wa kiume atakayezaliwa na Mama yeyote wa
Kiisraeli.

25
MUSA AFANYWA MWANA MFALME-Sura ya tisa

Mama mmoja wa kabila la Lawi alizaa mtoto mzuri wa kiume, alimficha kwa
miezi mitatu lakini hakuweza kuendelea kumficha tena.
Hivyo akaamua kumficha katika kikapu kilichotengenezwa kwa majani makavu
na kisha kupakwa lami.
Akamuweka mtoto wake katika kikapu hicho na kukificha katika majani marefu
pembezoni mwa mto Nile.
Katika muda wote huo Dada yake alikua akitazama kikapu hicho na kumlinda
mtoto. Baada ya muda akatokea binti Mfalme wa Misri, aliyeenda kuoga
pembezoni mwa mto Nile.
Akaona kikapu kile huku akisikia sauti ya Mtoto mchanga, aliingiwa na huruma
sana, naye akamwambia Dada yule ampeleke kwa Mama yoyote ili
amunyonyeshe na atakapokua basi atamchukua Mtoto huyo na kuishi naye
katika jumba la Mfalme.

Basi Dada yule akamchukua Musa na kumpeleka kwa Mama yake mzazi ili
aendelee kumtunza na kumnyonyesha bila yule binti Mfalme kujua kuwa mama
anayemtunza Musa ndiyo Mama mzazi wa Musa.
Baada ya mtoto kukua, binti Mfalme alimchukua Mtoto na kumuita jina lake
Musa likiwa na maana ya Aliyetwaliwa kutoka katika maji.

Somo la kujifunza:
Je, ni somo gani la kimaadili tunaloweza kujifunza kupitia simulizi za
maandiko matakatifu kuhusu kuzaliwa kwa Musa na kufanywa mwana
Mfalme?

Kuzaliwa kwa Musa kunatufundisha ni namna gani Mungu ana kusudi lake
katika kila jambo liwe baya au zuri.
Kusudio la Mungu hudhihirisha mema yote ambayo ametuandalia hata pale
tunapoona ni mabaya tu yanayotuzunguka.
Musa alizaliwa kipindi ambacho Mfalme alitoa agizo la kuuwawa kila Mtoto wa
kiume wa Kiisraeli lakini tunaona jinsi mipango ya Mungu ilivyojaa neema
kwani Musa hakuuwawa na aliweza hata kulelewa katika jumba la Mfalme kama
Mwanamfalme.

26
MUSA AONGEA NA MUNGU-Sura ya kumi

Musa aliishi Misri mpaka alipokua mtu mzima. Alikuwa ni mcha Mungu na
mwenye huruma sana juu ya mateso wanayopata Wanaisraeli.
Siku moja alimuona Mmisri mmoja akimpiga Muisraeli, alipotazama na kuona
hakuna watu katika eneo lile Musa alienda kuingilia ugomvi huo na kumpiga
Mmisri huyo kwa jiwe, bahati mbaya Mmisri huyo akafariki.
Taarifa zilipomfikia Mfalme akagadhibika na kuamuru Musa akamatwe mara
moja kwa mauaji hayo.
Musa akatoroka kuelekea nchi ya mbali na Misri, alikimbilia mahali palipoitwa
Midiani.
Musa alikaa huko kwa miaka arobaini, akaoa binti aliyeitwa Sipora.
Akiwa huko Midiani alifanya kazi ya kuchunga mifugo.

27
MUSA AONGEA NA MUNGU-Sura ya kumi

Siku moja akiwa anachunga mifugo, Musa akaona kichaka kikiwaka moto katika
mlima Horebu.
Musa alistaajabu kuona moto ule ukiwaka bila kukiteketeza kichaka kile, hivyo
akaamua kukisogelea.
Mara Mungu akamuita kwasauti na kumwambia, Vua viatu vyako kwasababu
mahali unapokanyaga ni patakatifu. Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, Isaka na
Yakobo. Nimeona watu wangu wanavyoteseka. Nitakutuma kwa Farao ili
kuwakomboa watu wangu kutoka misri.
Musa akiwa ni mwenye mashaka akamjibu, Mimi si kitu mbele ya Farao
nitamwambia nini mpaka akanisikiliza?
Mungu akamwambia, Mwambie Mimi niliye Mungu mkuu nimekuagiza.
Lakini Musa bado alionyesha mashaka juu ya uwezo wake katika kumkabili
Farao.

Basi Mungu akampa Musa nguvu za kutenda miujiza ili akamthibitishie Farao
uweza na ukuu wake.
Mungu akamuamuru Musa atupe fimbo chini, naye Musa akafanya hivyo,
hapohapo fimbo ikageuka kuwa nyoka, Musa akashituka na kutaka kukimbia.
Mungu akamwamuru amshike Nyoka yule mkiani, naye Musa akafanya hivyo,
muda huohuo tena Nyoka yule akageuka kuwa fimbo kama ilivyokua awali.
Ingawa Mungu alimuonyesha miujiza yote hiyo lakini bado Musa alikuwa na
wasiwasi wa kwenda kumkabili Farao, hivyo Musa akatoa kisingizio tena kuwa
yeye si muongeaji mzuri, hataweza kumueleza vyema Farao ujumbe uliotoka
kwa Mungu.
Mungu akamwambia atambariki ndugu yake aliyeitwa Haruni ili awe msemaji
wake mbele ya Farao.
Basi Musa akarejea Misri na kuwambia Waisraeli yale yote ambayo Mungu
amemuagiza.

28
MUSA AONGEA NA MUNGU-Sura ya kumi

Somo la kujifunza:
Je, ni somo gani la kimaadili ambalo tunaweza kujifunza kupitia uhusiano
wa karibu wa Musa na Mungu?

Kupitia Musa tunajifunza kuwa hatupaswi kuogopa kuwa na uhusiano wa karibu


na Mungu.
Musa alijenga uhusiano wa karibu sana na Mungu, Mungu akajitokeza kwake na
kuongea naye uso kwa uso.
Kupitia uhusiano wa Musa na Mungu tunajifunza kuwa tunapaswa kuwa watii
kwa sauti ya Mungu kila ituitapo katika wito fulani.
Tunajifunza kuwa utii wetu na imani yetu kwa Mungu hutuwezesha nguvu ya
Mungu kutenda kazi ndani yetu kwa kadiri ya kusudio lake kama ilivyokua kwa
Musa. Mungu alitenda miujiza mingi kupitia kwa Musa.
Tunajifunza pia Mungu huweka karama juu ya watu anaotaka kuwatumia kama
ilivyokuwa kwa Musa na kaka yake Haruni.

29
Kitabu hiki cha BIBLIA YA WATOTO ni barua ya upendo kutoka kwa
Mungu mwenye upendo mkuu kwa Watoto wote.
BIBLIA YA WATOTO ni kitabu kinachowapa Watoto baraka ya kuujua
ukweli kuhusu Mungu.
Ukweli wa matendo makuu yote ambayo Mungu alitufanyia wanadamu na
mambo ambayo tunapaswa kuyafanya ili kumpendeza Yeye aliye mkuu.
Barua hii ya upendo kutoka kwa Mungu inatufundisha namna gani
unavyotakiwa kuishi, inatuonya, inatuasa lakini pia inatueleza habari njema
ya wokovu wa mwanadamu kupitia Yesu Kristo.
Mungu mwenye enzi anataka tuisome barua hii ya upendo kutoka kwake kila
siku ili tumjue vyema, tumuabudu na kumtumikia.
Kitabu cha BIBLIA YA WATOTO kimeichambua barua ya upendo toka kwa
Mungu katika simulizi nyepesi ili zikapate kuwafunza watoto wote matendo
makuu ya Mungu aliye hai.
Kitabu hiki ni baraka ya kipekee kwa wazazi na watoto kwakua ni nyenzo
bora kabisa ya malezi mema yanayompendeza Mungu.
Sifa na utukufu urudi kwa Mungu.

PAGE 36

You might also like