Download as pdf or txt
Download as pdf or txt
You are on page 1of 19

TAFAKARI JUU YA MAENDELEO KATIKA

ELIMU YA TANZANIA KABLA NA BAADA


YA UHURU

Kalafunja M. Osaki, PhD

PROFESA
WA MITAALA NA SAYANSI-ELIMU
CHUO KIKUU CHA DODOMA

Mchango katika kongamano kuhusu Miaka 50 ya Uhuru Tanzania


Dodoma Hotel

1 Agosti 2011

1
Utangulizi
Mjadala wowote kuhusu elimu katika Tanzania inabidi utafakari juu ya maswala
muhimu ya: malengo ya elimu katika vipindi mbalimbali vya historia yetu, fursa
ya wadau mbalimbali kupata elimu na kushiriki katika shughuli za elimu, ubora
wa elimu iliyotolewa na umahiri wa uongozi katika taasisi za elimu. Hapa
napitia mada nikizingatia maswala haya na kuchambua vipindi vifuatavyo: -
(i) Kabla ya ukoloni
(ii) Wakati wa ukoloni
(iii) Baada ya Uhuru na hadi Azimio la Arusha
(iv) Tangu Azimio la Arusha hadi kuanza kwa mfumo soko huria
(v) Kipindi hiki cha soko huria.
Mwisho naorodhesha changamoto tisa zinazolikabili taifa katika nyanja ya elimu
wakati huu wa ushindani mwingi na utandawazi. Ijulikane kuwa siku zote sera
za elimu hubuniwa ili kuridhisha mfumo wa uchumi na siasa uliopo katika
jamii, uwe wa ujima, utumwa, ukabaila, ubepari au ujamaa. Sera mbovu za
elimu huathiri kila sekta ya nchi. Kama alivyosema Mwalimu, Kupanga ni
kuchagua, na ukichagua uchafu utavuna uchafu huo huo. Amesema pia
mtaalamu mmoja wa Kichina:

Ukitaka kuweka mpango wa mwaka mmoja, panda mahindi;


Ukitaka kuweka pango wa miaka kumi, panda miti;
Ila ukitaka kuweka mpango wa miaka 100, elimisha watu.
[Confusius]

Kabla ya ukoloni
Kipindi hiki kinajulikana kwa kuwepo mifumo mbalimbali ya Elimu ya Jadi
ikiiitwa majina mbalimbali
- Jando, Unyago, rika
- Malezi ya Jadi
- Ngasi na Shigha

2
- Omuteko nk.
Mkazo ulikuwa, sehemu ya kwanza elimu isiyo rasmi iliyotolewa na wazazi na
majirani, pili elimu rasmi baada ya kuvunja ungo na kupitia mafunzo ya rika,
jando au unyago. Lengo la jando na unyago ilikuwa ni kumuandaa kijana aweze
kutambua wajibu wake katika jamii kama mtu mzima. Wajibu katika familia
kiuchumi na ujuzi mbalimbali vilifundishwa katika utaratibu uliowekwa na
jamii, na vijana walipelekwa mahali maalum kwa ajili ya jando na unyago.
Mifano iko pwani katika mikoa ya Tanzga, Pwani, LIndi na Mtwara, (unyago)
miongoni mwa wafugaji kama vile Wamasai, Wambugwe, Wakurya, na
Omuteko (Kanda ya Ziwa), ngasi , na shigha (Kilimanjaro).

Sehemu hii ya Elimu haikuisha kabisa baada ya ujio wa wageni lakini iliathiriwa
sana na mambo makuu mawili: -
- Dini za kigeni ambazo zilifundisha kuwa imani, mila na desturi za kijadi
za Mwafrika zilikuwa mbaya na kinyume na dini ya kweli
- Utamaduni wa kigeni (Kiarabu, Kizungu) ambao uliingizwa kupitia shule
za misheni au kiislamu na kubeza utamaduni wa kiafrika.

Hata hivyo hadi leo baadhi ya jamii (kama wafugaji wa Kimasai, Wambulu,
Wasonjo, Wakurya nk) na watu wa pwani (Wamakonde, Wazaramo na
wengineo) bado huendesha elimu ya jando na unyago pale watoto wafikiapo
umri unaokubalika. Sasa hivi utoaji wa elimu hii una changamoto kubwa kwa
sababu ya upinzani toka vikundi shinikizo mbalimbali vya kitaifa (wanaharakati
wa jinsia na hata kimataifa (UNESCO nk) kwamba elimu hii inaendekeza
ukeketaji wa wanawake na udhalilishaji wa kijinsia. Inafahamika wazi kuwa
wengi wanaoshabikia upinzani huu hawaelewi undani wa jando na unyago na
wanatazama tu tendo la tohara na kufundisha watoto mambo ya ngono. Kuna
mengi zaidi katika mtaala huu na utafiti unahitajika ili kuuboresha uende na
wakati badala ya kuutokomeza. Lakini pia mfumo wetu wa elimu haujatoa
nafasi ya watoto kupata mafunzo yatolewayo katika jando na unyago, ingawa

3
sasa yameingizwa katika somo la Uraia na kwenginepo na yanafundishwa na
watu wasio na mafunzo ya kutosha. Jamii za pwani bado huwatoa watoto wao
shuleni pindi wafikiapo umri wa jando na unyago ili wakapate kuhudhuria
mafunzo hayo, na hii huathiri sana mahudhurio yao shule wakiitwa sasa watoro.

Kipindi cha Ukoloni


Kipindi hiki cha utawala wa kigeni kiligubikwa na harakati za kudhoofisha
elimu za jadi zilizokuwepo na kusimamisha mifumo mipya yenye sura kubwa
mbili.
- Elimu ya dini za kigeni-Kiislamu na Kikristo na Kisabato, hii ikiendeshwa
na taasisi za kidini, za misheni na za kiislamu.
- Elimu rasmi (formal education) iliyopangwa tangu Elimu ya Msingi,
Elimu ya kati (Middle School), Elimu ya Sekondari na Elimu ya Juu
ikifuata mtindo wa elimu wa nchi iliyotutawala.
Baadhi ya taasisi zilizoendesha elimu ya dini zilipewa pia ruhusa na serikali ya
mkoloni kuendesha elimu rasmi ya msingi na sekondari na vyuo na nyingi
zimebaki na mfumo huo hadi leo.

Lengo kuu la elimu ya ukoloni ilikuwa kubomoa elimu ya jadi na mila na desturi
zake ili kupandikiza elimu, mila na desturi za kigeni ziandae waafrika kuwa
watumishi waaminifu wa serikali ya kikoloni na wazipende mila na desturi za
hao wakoloni. Mtaala ulikuwa na mfumo ufuatao: -
Elimu ya Msingi:
Kipindi cha ukoloni wa Mjerumani kilikuwa kifupi ila kilitoa elimu ya darasa
la 1 hadi la 6, na kufundisha kwa Kiswahili, na dini na utii ilikaziwa sana.

Kipindi cha Ukoloni wa Mwingereza, Darasa la 1 hadi la 4: Kiswahili


kilifundishwa pamoja na kusoma na kuandika maarifa, usafi, hesabu na dini.

4
Sehemu kubwa ilikuwa pia inafundisha adabu ya kula, mavazi, na lugha ya
heshima, ilitilia mkazo mila za wakoloni. Darasa la 5 hadi 8 lilifundishwa
kwa kiingereza na masomo yalikuwa Civics, General Knowledge,
Agriculture, Health Sciences, Maths. Kulikuwa na mtihani darasa la 4
kuingia Middle school. Baada ya darasa la 8 wengi walipata kusomea ajira za
ualimu Grade C, ukarani na uafisa kilimo au mifugo wakifanya kazi kijijini.
Darasa la 8 kulikuwa na mtihani wa kuingia sekondari, na huko walifuata
mtaala wa sekondari hadi darasa la 10 na kwenda Makerere kusomea
diploma ya ualimu au udaktari. Cha muhimu ni kuwa baada ya darasa la 8
wengi walikuwa wanamudu lugha tatu, kwanza, lugha ya mama, pili
Kiswahili na tatu kiingereza, na walikuwa na stadi moja ya kazi (kilimo,
ufundi, mapishi) wanayoimudu.

Elimu ya Sekondari
Ilitolewa tangu darasa la 9 hadi la 10 na kabla ya kipindi Fulani std 10
ilikuwa ni mwisho wa sekondari na waliofaulu wakaenda chuo kikuu
kusomea diploma. Baada ye sekondari iliendelea hadi kidato cha 4 ambapo
walifanya mtihani wa Cambridge O Level. Masomo ya lazima yalikuwa
Kiingereza, Jiografia, Hesabu, Health Sciences, Kiswahili, Biology.
Mengine yalikuwa ya kuchagua yakiwa ni Physics, Chemistry, Bible
knowledge, Islamic knowledge, Needle work and Dress making, Cookery,
Agriculture na masomo ya ufundi kwa shule za ufundi. Mfumo wa
sekondari uliiga ule wa Uingereza ulioanzishwa 1944 (Tripartile Education
System) wa shule za Grammar (Academic) kwa wenye uwezo kufaulu zaidi
mtihani wa Msingi, secondary modern (za kawaida) kwa wanaofuata na sec
technical (trade schools) kwa wale wapendao zaidi ufundi. Hapa Ufundi
ulidharauliwa kwa kufanya mtu achafuke hapa Tanzania miongoni mwa
shule za Grammar zilikuwa Tabora School na Malangali, Alliance (Mazengo)
Minaki, Umbwe, Pugu, Marian (Kilakala) Msalato, Ashira, Weruweru Girls.
Mtihani wa Cambridge uliendelea. Trade School zilikuwa Ifunda na Moshi.

5
Sera ya sekondari ilikuwa mtaala wa wote kidato cha 1 & 2 na baada ya
kidato cha 3 wanafunzi wanachagua sayansi au sanaa, na wa ufundi
wanachagua aina ya ufundi. Kiingereza kilikuwa lazima na ndio lugha ya
kufundishia. Walimu wengi walikuwa wageni-waingereza, hivyo wanafunzi
walifundishwa kiingereza na watu ambao kiingereza kilikuwa lugha yao ya
mama.

Kidato cha 5-6 waliingia wachache tu waliofaulu O level ya Cambridge na


shule zilikokuwa na A level zilikuwa chache. Mwanzo ilikuwa St Michael
and St George (baadaye ikaitwa Mkwawa) na Pugu, Minaki, baadaye
zilipanuliwa na kuongeza nyingine.

Kwa ujumla sekondari ilikuwa ni ngazi ya juu na ya wachache maana nafasi


zilikuwa finyu. Wengi walipata ajira baada ya kidato cha 4 hasa za ukarani
wa mahakama, reli, forodha, serikali nk. Baadhi walipata fursa kuendelea na
mafunzo ya nurse, medical assistant, ualimu Grade A, kilimo nk. Ni
wachache tu waliingia A level na kufanya mtihani wa Cambridge `A` level.
A level ilikuwa uchaguzi wa masomo matatu na General Paper kwa wote, na
subsidiary maths kwa wale wa sayansi. Shule zilikuwa na ubaguzi wa rangi,
na ziligawanywa za wazungu, waasia na waafrika.

Baada ya Uhuru
Wizara ya Elimu iliundwa kama chombo kilichojitegemea mwaka 1960, Mhe.
Oscar Kambona akiwa waziri anayehusika na elimu. Katika kipindi chake
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilianzishwa na usawa ukaanza kuzingatiwa
katika kuchagua wanafunzi kuingia sekondari bila kujali rangi. Kabla ya
hapo kulikuwa na shule za wazungu k.m (St. Michael na St George) wahindi
(Aga khan, Alliance Sea nk) na za waafrika (Malangali, Tabora School nk).
Mh Solomon Eliufoo alichukua wizara 1962-65 na wakati huo ada
ikaondolewa sekondari na kupanua elimu kwa daraja la A na C. Kiswahili

6
kilianza kutumiwa kufundisha elimu ya msingi hadi darasala 5 na
kupanuliwa hadi la 8 mwaka 1968. Ubaguzi katika elimu ya msingi
uliondolewa pia na darasa la nane likafutwa kuanzia 1967. Eliufoo
alipokelewa na Mhe. Chediel Mgonja 1965-1970. Katika kipindi hiki mfumo
wa elimu haukubadilika, ulibakia ule wa kikoloni na mitihani ya kidato cah 4
na 6 ilitoka Cambridge na London.

Azimio la Arusha
Elimu ya Kujitegemea
Mwaka 1967 kulipitishwa Azimio la Arusha na mfumo wa Elimu ya
Kujitegemea. Mfumo huu ulilenga kuimarisha mambo makuu manne: -
(i) Kujenga dhana ya udadisi,
(ii) Kujenga uwezo wa kujifunza kutoka wengine na kutathmini ya
wengine,
(iii) Kujifunza kufikiri na kuchambua mambo,
(iv) Kujenga uwezo wa kujiamini na kujikomboa kimawazo; na
kujitegemea Kuthubutu , kuweza, kusonga mbele.. (Tazama
Nyerere, 1967).

Makala ya ESR (Nyerere 1967) ilitafsiriwa kwa namna mbalimbali na


watekelezaji na wadau mbalimbali. Baadhi ya wakuu wa taasisi na walimu
walidhani kujitegemea ni kujilisha na kufanya kazi za mikono ili kuondoa dhana
kuwa msomi hachafuki, shule zilifungua mashamba, mifugo, maduka,
mitumbwi ya kuvua na kukawekwa kumbukumbu za uzalishaji mali za kila
taasisi (Taz. Komba 2006).

Wizara pia iliazima mitaala kutoka nje yenye kulenga kudadisi na ifuatayo
ililetwa: -

7
(i) Elimu ya kufikiri- toka Marekani ili kuandaa watoto kufikiri wakifuata
mfano wa Mwulize fukufuku. Shule za msingi, kuanzia 1967 mtaala
huu ulijaribiwa shule za msingi.
(ii) School Science Project of East Africa, mtaala wa Sayansi Physics,
Chemistry na Biology wa sekondari uliotolewa toka Nuffied Sciences,
Uingereza.
(iii) School Maths Project SMP of East Africa na baadaye Entebbe
Mathematics ambayo ilitolewa pia toka Uingereza kwa ajili ya shule za
sekondari Afrika Mashariki.
Bahati mbaya mitaala hii ilijaribiwa tu katika mashule na kama Osaki, (2008)
anavyoeleza kwa kirefu iliondolewa baada ya malalamiko na upinzani toka
kwa wadau wasioelewa, kwa kuwa mitihani tofauti ilifungwa kwa shule
tarajali bila kulenga sayansi kwa kufikiri na vitendo (wakatunga ya nadharia-
Alternative T ya sayansi), wanafunzi wakafeli mitihani hiyo na mitaala ya
SSP ikandolewa mashuleni miaka ya 1972-75. Wakati huo, Taasisi ya Elimu
pia ilianzishwa mwaka 1970 na kuanza kusimamia uboreshaji na utungaji wa
mitaala mipya. Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima pia iliundwa 1969. Baraza
la Mitihani lilianzishwa 1971. Mwaka 1968 Jeshi la Kujenga Taifa
lilianzishwa na wahitimu wote wa kidato cha sita na kuendelea walilazimika
kwenda JKT kwa mujibu wa sheria. Hii ilijenga ukakamavu, stadi za kazi na
nidhamu.

Wakati wa Mhe. Simon Chiwanga anateuliwa kuwa Waziri wa Elimu 1971-74


elimu ya msingi ilitangazwa kuwa miaka 7 kwa Tanzania nzima (badala ya 8)
na ada zikaondolewa. Ujenzi wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi
ulianzishwa pia katika kipindi hiki. Mhe Elinewinga alichukua uwaziri wa
Elimu 1975-77 na taasisi ya ukuzaji mitaala ya Elimu watu wazima
ukaimarishwa. Mwaka 1977, shule za sekondari zilifanywa michepuo ya
kilimo, sayansi kimu nk. Mhe Nikolas Kuhanga alipokea Wizara ya Elimu
mwaka 1978, akifuatiwa na Mama Thabitha Siwale, 1979-1982 kama

8
mwanamke wa kwanza kuongoza wizara hiyo ambapo MANTEP ilianzishwa
kipindi hicho; na Tume ya Elimu iliyoongozwa na Mhe. Makweta ilitoa ripoti
yake mwaka 1982 ikiainisha udhaifu kadhaa katika elimu hasa: -
(i) Kupungua kwa uwezo wa kusoma, kuandika na kuhesabu,
(ii) kutowahudumia walemavu,
(iii) Kutoimarisha ufundishaji wa lugha ya kiingereza.
Ikumbukwe kuwa 1977 UPE ilianzishwa na kuajiri walimu wengi wasio na sifa,
wakapewa mafunzo ya miezi mitatu chini ya waratibu wa kata, yaliyofadhiliwa
na kuongozwa na UNESCO-UNICEF, na kusimamiwa na waratibu wa kata.
Katika uandaaji wa Mpango kamambe wa Mafunzo ya Ualimu, [Teacher
Education Masterpan (2000)], walimu hawa walionekana kuwa na tatizo kubwa
na kwa kuwa hawakuwa na uwezo, waliathiri sana ufundishaji hasa wa lugha ya
kiingereza na hisabati. Mhe. Makweta alliongoza Wizara ya Elimu 1983-85
akaanzisha ujenzi wa shule za umma. Kuondolewa kwa mitihani ya vitendo
katika sayansi (Practical) kulifanya walimu wengi waache kufundisha kwa
vitendo.

Uchumi Huria 1985


Mhe. Kighoma Malima aliongoza wizara 1986-89 na kipindi hicho Chuo Kikuu
SUA kilianzishwa. Baada ya hapa kulipitishwa Azimilo la Zanzibar ambalo
pamoja na mambo mengine kilipunguza msukumo wa sera ya Azimio la Arusha
na Elimu ya Kujitegemea na kuruhusu uanzishaji wa shule za binafsi, zikiwamo
za `Academic` na nyingi za msingi zinazofundisha kwa lugha ya kiingereza.
Tangu hapo, ukuaji wa shule za sekondari za binafsi umeendelea sana.

Mwaka 1995 Mhe Mayagila aliongoza wizara ya Elimu na kipindi hicho


kukaundwa Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu chini ya waziri Mhe.
Benjamin Mkapa. Charles Kabeho alipokea Wizara ya Elimu 1991-1994 akafuata
Prof Philemon Sarungi 1995. Sera mpya ya Elimu na Mafunzo ilizinduliwa 1995
na kutoka 1995 hadi 1999 wizara iliitwa Wizara ya Elimu, Utamaduni na

9
Michezo ikiongozwa na Prof Kapuya. Prof Kapuya atakumbukwa kwa kuhimiza
sana michezo. Mwaka 2000 -2005 michezo iliondolewa katika wizara na ikabaki
ya Elimu na Utamaduni chini ya Mhe Joseph Mungai. Katika kipindi hiki
mpango muhimu katika sekta ya Elimu ilianzishwa baada ya ufadhili wa benki
ya Dunia nayo ni:

i) Mpango wa maendeleo ya Elimu ya msingi [MMEM]


ii) Mpango wa maendeleo ya Elimu ya Sekondari [MMES]
iii) Mpango Mkakati wa Elimu ya ualimu [Teacher Education Master plan]
iv) Muda wa Mafunzo ya ualimu ukapunguzwa, na mtaala ukabadilishwa
v) Michezo ikaondolewa katika mtaala wa Elimu.

Mhe. Mungai anakumbukwa kwa kusukuma sana maandalizi ya MMEM na


MMES na pia kuanzishwa vyuo vikuu vishiriki vya DUCE na MUCE, pampja na
kuondoa elimu kwa michezo mashuleni, na kufuta masomo ya biashara katika
kidato cha 1 hadi 4.

Mama Sitta aliongoza Wizara 2005-8 na kipindi hiki ikabadilishwa kuwa Wizara
ya Elimu na Ufundi. Katika kipindi hiki shule za sekondari za Kata zilijengwa
kwa kasi kwa msaada wa Benki ya Dunia pamoja na nguvu za wananchi kwa
uhamasishaji wa aliyekuwa Waziri Mkuu Mhe. Edward Lowasa.. Profesa
Jumanne Maghembe alipokea uwaziri mwaka 2008-2010 na akatangaza kufutwa
kwa ada ya mitihani ya kidato cha 4. Pia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Juu
ulianzishwa. Mwaka 2010 Dr. Shukuru Kawambwa alipokea na anaongoza
wizara hadi sasa, kipindi hiki kimeshuhudia upanuzi wa vyuo vikuu katika
wakati mgumu kibajeti na wanafunzi wa vyuo vikuu wameleta matatizo mengi
ya migomo.

10
Changamoto zinazolikabili taifa katika katika Sekta ya Elimu
Kuna changamoto kadhaa zitokanazo na sera za huko nyuma na zinazochangia
zana kurudisha nyuma maendeleo ya Elimu hapa Tanzania, na kuathiri
ushindani wa Watanzania. Baadhi ni habari njema, baadhi ni matatizo
yanayohitaji kutatuliwa haraka iwezekanavyo. Changamoto ni hizi:

i) Sera kuhusu kufundisha lugha mashuleni na lugha ya kufundishia. Tanzania


ilirithi lugha zaidi ya 120 za makabila yake zikiwa lugha mama za
watu wake mbalimbali. Lugha hizi zina utajiri mwingi wa elimu ya
mimea na wanyama, fasihi simulizi, mambo ya utamaduni na taaluma
mbalimbali. Wakati wa ukoloni wa Mjerumani Kiswahili kikatiliwa
mkazo kufundishwa mashuleni lakini waliosoma walikuwa wachache.
Mwingereza hakuimarisha sana Kiswahili lakini Sera ya Phelps Stokes
Commission Report ya Education for adaptation na indirect rule ya
Gavana Donald Cameron ziliimarisha Serikali za Mitaa katika kila
kabila. Nakumbuka Moshi tulikuwa na daftari na vitabu vimeandikwa
Kilimanjaro Native Education Authority na nembo ya chui iliyoandikwa
Lukuwawie na Ruwa (tumemkumbatia Mungu) na vilitosheleza kabisa.
Ingawa Kiswahili kilifundishwa, lugha mama zilitumika nyumbani na
hata shuleni. Tofauti na nchi jirani Kenya, Uganda, Zambia, Malawi,
lugha za makabila hazikufundishwa shuleni ila mkazo uliwekwa
kwenye Kiswahili, kikifundishwa na walimu waliotokea vyuo vya
ualimu daraja la C. Cha muhimu kusema hapa ni kuwa walimu wengi
wa Kiswahili si wazaliwa waliokua na lugha hiyo kama lugha mama.
Kwa ajili hii ingawa Kiswahili kinatumika nchi nzima, na
kimeunganisha taifa, uandishi wa vitabu umepungua sana karibuni
baada ya kazi za kutukuka za waandishi wa mwanzo kama vile
Shaaban Robert, Mathias Mnyampala, na Salehe Farsi na wengine.
Majirani zetu Kenya wana machapisho mengi ya Kiswahili kutushinda
ingawa tuna Taasisi kubwa ya Taaluma za Kiswahili. Vile vile lugha

11
mama zinapotea na vijana wengi sasa wa kitanzania wanajua lugha ya
Kiswahili pekee na kiingereza kidogo, huku wakisahau Kigogo,
Kisukuma, Kipare chao. . . (Osaki, 2005). Uwezo wa Kiingereza ni
mdogo kuliko nchi za jirani hasa baada ya kuruhusu walimu wasio na
sifa kufundisha lugha za Kiswahili na Kiingereza. Utafiti kuhusu
lugha unaonesha kuwa msingi wa lugha hujengeka kichwani kabla ya umri
wa miaka miwili na kuwa mtoto akiweza kusikia lugha mbili zikizungumzwa
kabla hajatimia miaka miwili ataweza kujenga misingi hiyo miwili na
itansaidia sana kujifunza lugha mpya hapo baadaye. Pia mwalimu wa lugha
akiwa dhaifu anampotosha mtoto katika kujenga uwezo wa kufahamu
na kutumia lugha kikamilifu. Kwa kufundisha watoto lugha moja tu
wakiwa wadogo tunawalemaza kama walivyofanya Waingereza na
Wamarekani ambao wanapata tabu sana kujifunza lugha ya pili. Kwa
kutumia walimu dhaifu tunaharibu pia. Baada ya muda watoto wetu
wengi watakuwa wanaongea mchanganyiko (pidgin) wa Swanglish
(Kiswahili na kiingereza), na hili litatugharimu sana.
ii) Umoja wa Kitaifa: Katika kipindi cha baada ya uhuru hadi 2000 wanafunzi
waliweza kusoma popote Tanzania hasa sekondari na kuchanganyika
na wenzao wa makabia mbalimbali. Pia katika kuhudhuria mafunzo
ya Jeshi la Kujenga Taifa, walifanya kazi nyingi pamoja na wenzao na
wakachanganyika makabila, dini na tabaka zote, hii imeimarisha sana
umoja wa kitaifa. Kwa kufungua shule za kata na watoto kusoma
huko walikokulia mpaka kidato cha sita, umoja wa kitaifa unaweza
ukaathirika na vijana wakawa finyu kwa namna mbalimbali. Tuna
habari kuwa mpango wa kufufua Jeshi la kujenga taifa kwa mujibu wa
sheria unarejeshwa na ukiongozwa vema, labda itasaidia. Pia watoto
wasisome shule moja tangia kidato cha kwanza hadi sita, wahame
kidato cha tano na kuwe na kuchanganya watoto wa wilaya
mbalimbali ili kuongeza upeo wao.

12
iii) Masomo ya Kidato cha 1-4 na 5-6. Hadi sasa vijana wengi wanapoingia
sekondari wanahimizwa kujifunza masomo mengi ya sayansi, lugha,
sanaa, kidato cha 1-4. Baadhi hukimbia sayansi mapema mno, tangu
kidato cha pili. Wengi hawafanyi kazi za mikono maana ziliondolewa
baada ya kufuta Elimu ya Kujitegemea. Hawatoki shule wakiwa na
ujuzi wowote mbali na kukariri machache kwa ajili ya mitihani. Kuna
haja ya kurudisha dhana ya Elimu ya Kujitegemea na kuhimiza zaidi
maswala ya udadisi, na uchambuzi katika mijadala mbaimbali ili
kujenga uwezo wa kufikiri na ubunifu. Hii inahitaji mafunzo imara
zaidi kwa walimu. Kidato cja 5-6 kinakazia sana masomo yale matatu
na ingefaa kutoa mwanya kwa wale wanaotaka kuongeza masomo
wakachukua manne au zaidi sio tu somo la Divinity au Islamic
Knowledge bali pia Kiingereza, Sayansi, nk.
iv) Ujasiriamali na Stadi za kazi: Hizi ni stadi muhimu sana katika ulimwengu
wa leo na Tanzania tumezipuuza katika sera muda mrefu. Kuingizwa
kwa somo la Stadi za Kazi hakujafanyiwa maandalizi ya kutosha ya
mitaala, vifaa na walimu wa kufundisha somo hili vema. Masomo
kama vile Elimu ya Michezo na Elimu kwa Michezo, sanaa, muziki,
ufundi, na ujasiriamali havina walimu hodari na vyuo haviyatilii
mkazo, na wasanii wengi hujifunza tu mitaani (0saki, 2009). Nyanja hii
yaweza kuwapatia ajira watu wengi sana ikikuzwa vizuri, na wakati
wa kuikuza ni sasa. Katika nchi jirani ujasiriamali hufundishwa kwa
dhati na watoto wa sekondari humaliza wakiwa na maarifa ya kutosha
juu ya kuanzisha biashara, kutafuta soko la bidhaa, kupatana kazi
(negotiation skills) na kuandaa mikataba ya biashara kwa busara,
kujitangaza na kutangaza biashara, kutunza hesabu za biashara nk.
Hapa Tanzania bado sana na hili linatugharimu katika mikataba na
biashara na watu wa nchi nyingine.
v) Elimu ya kufikiri, udadisi, kujiamini nk Hapa hatuna budi kurejea mitaala
yetu na kuiboresha, lakini muhimu zaidi ni kufundisha walimu jinsi

13
ya kuwapa vijana fursa ya kufikiri na kugundua, kujituma, kudadisi
na kufatiti kabla ya kukurupukia jambo lolote (Osaki, 2007). Hii ina
umuhimu sana katika ufundishaji wa sayansi na mambo ya uchumi.
Watanzania wengi bado hawana ujasiri kuanzisha shughuli mpya ila
kuiga tu kwa wengine.
vi) Sayansi, Teknolojia na Hesabu [Science, Mathematics and Technology
Education STEM]. Hili linahusiana na la kufikiri, lakini ni muhimu
zaidi kuhimiza vijana kusomea masomo ya sayansi Hesabu na
Teknolojia maana nchi zote zilizosonga mbele ni zile zilizokazia
masomo haya. Tangu Mapinduzi ya Viwanda ya Ulaya, Marekani,
Asia ya Kusini Mashariki (Japan, Korea, Malaysia, Singapore. . . ),
Israeli na Afrika ya Kusini, sayansi imeleta maendeleo makubwa
duniani. Mtaalamu mmoja. Harry Kroto, aliyewahi kushinda medali
ya Nobeli ya Kemia 1996 amesema,
`Elimu ya sayansi ni suala la kimaadili maana ndiyo tu
iwezayo kufundisha mtu namna ya kufikiri, kutafuta ukweli
na kupima kama ni kweli au si kweli, kwa majaribio na
uchunguzi. Taifa lisilowafundisha watu wake namna ya
kutafuta ukweli linapotosha watu, litaangamia` (Krotto,
2011).

Tatizo la nishati tunalokabiliwa nalo sasa ni kielelezo tosha kuwa


hatuna vipaumbele vinavyozingatia raslimali yetu na mali ghafi zetu
za gesi asilia, makaa ya mawe, upepo, nk licha ya kuwa na vyuo vikuu na
wataalamu waliosomeshwa tangu miaka hii 50 baada ya uhuru. Ijulikane pia
kuwa kuanzisha vyuo vikuu peke yake bila kuwekeza katika utafiti na
kuwaamini wataalamu wetu haitoshi. Wataalamu wengi wa sayansi
na teknolojia hapa Tanzania wameacha kuchangia kwenye taaluma
zao na kuwa wanasiasa, bila kuonesha kutumia huo utaalamu
kuboresha sera na uwekezaji katika sayansi na teknolojia walizosoma.
Inabidi hapa chama chochote cha siasa kinachotawala kiweke

14
kipambele katika hili pamoja na kukuza uhusiano na watanzania
walio nchi za nje.
vii) Uongozi katika taasisi za Elimu: Hapa pana kazi pia. Baada ya Uhuru,
Mwalimu aliwaondoa walimu wengi waliokuwa bora katika elimu na
kuwapa madaraka ya kiutawala na kisiasa. Shule zilikuwa chache,
lakini iliathiri uongozi wa elimu kiasi. Sasa shule na taasisi za elimu ni
nyingi na katika ushindani yabidi ziongozwe na watu wenye taaluma
na uzoefu. Kumezuka mtindo wa kuteua watu wasio na sifa kuongoza
taasisi muhimu za elimu na hili litatugharimu sana. Chuo cha
Madaktari ingefaa kiongozwe na mwenye taaluma ya Udaktari; vivyo
hivyo na chuo cha Uhandisi kiongozwe na Mhandisi, Cha Elimu na
Mwalimu mwenye uzoefu. Shule ya sayansi ingeongozwa na mwenye
utaalamu na uelewa wa sayansi pia, na shule yoyote katika dunia ya
leo isiongozwe na mtu asiye mwalimu mwenye utaalamu na uzoefu.
viii) Uwekezaji katika Elimu: Serikali iliongeza bajeti ya Elimu kufikia 20%
tangia 2005. Hii imesaidia kufungua shule nyingi mpya na kupanua
vyuo vikuu, na pia kuongeza idadi ya walimu wenye shahada na
diploma. Lakini upanuzi unapozidi uwezo taasisi zinaendeshwa bila
fedha na zinaporomoka haraka. Pia upanuzi unafanyika bila ushauri
wa kitaalamu ni hasara kwa taifa. Mfano, uwekezaji mkubwa katika
Vyuo Vikuu vipya kama Dodoma umejenga majengo mengi lakini
umesahau vipaumbele kama kuandaa maabara ya sayansi na lugha
mapema, fedha za uendeshaji wa programu ni chache na mafunzo
yanaendeshwa bila zana, na bila kutoa nafasi ya kutosha kuandaa
wafanyakazi bora. Somo la mafunzo kazini limeathirika sana kwa
kukosa fedha za kuendesha na kulisimamia na wahitimu wanaweza
kujikuta wana uwezo mdogo wa kiutendaji wanapoenda makazini
hapo baadaye (Taz Osaki, 2008). Katika mahojiano hivi karibuni
kutafuta wafanyakazi na walimu wapya UDOM, tumegundua kuwa
vijana wengi hawana ujuzi wala hawawezi kujieleza licha ya kuwa na

15
vyeti vya First Class toka Vyuo mashuhuri vya hapa nchini. Pengine
kwa sababu ya mtaala wa mtindo wa semester na course unit system wao
husahau kila kitu baadaya kumaliza mtihani. Hili linatakiwa lifanyiwe
uchunguzi wa kina na lipatiwe ufumbuzi.
ix) Elimu ya jadi na utamaduni wa Mwafrika: Hapa nakumbusha tu kuwa kuna
elimu nyingi ya jadi ambayo tumeipuuza katika nchi yetu. Kupuuzwa
huku kulianza wakati wa ukoloni ingawa wageni huichangamkia
katika utafiti na kutumia maarifa ya wataalamu wetu wa jadi kama
vile madawa ya mitishamba, elimu ya wanyama, utatuzi wa migogoro
kimila, mambo ya kifamilia na malezi ya watoto kiafrika, fasihi
simulizi, kilimo cha jadi kama vile ngoro, vinyungu, nk kuendeleza
sayansi huko kwao. Hivi vingefaa vitafutiwe nafasi maana ingawa
tunavidharau, vina nafasi ya pekee katika ulimwengu wa utandawazi;
ndio nguvu yetu tusiipoteze kwa kutoirithisha kwa vizazi vijavyo.
Makala ya (Osaki, 2004) imeeleza kwa kirefu juu ya swala hili.

Hitimisho
Katika uchambuzi huu wa Elimu kabla na baada ya uhuru, tumetazama mkazo
uliokuweo katika elimu za jadi na ambao uliporomoshwa na utamaduni wa
wageni na ukoloni, lakini tumeona umuhimu wa kuurudisha na kuurithisha kwa
vizazi vijavyo. Tumeona pia kuwa maendeleo ya elimu yetu baada ya uhuru ni
makubwa kiasi, hasa ikikumbukwa kuwa Tanzania ndio nchi ya kwanza Afrika
kubadili siasa Elimu kuwa ya Ujamaa na kujitegemea. Pamoja na sera nzuri
timeona sera hizi zikirudi nyuma na katika kupanua Elimu, shule nyingi na
vyuo sasa zinakazia kuongeza idadi ya wanafunzi na kuhubiri nadharia zaidi ya
kufikiri, maadili na vitendo. Kwa ajili hiyo tunazo changamoto mbalimbali ili
kuboresha elimu yetu na kuhimili ushindani katika ulimwengu wa leo na siku za
usoni. Zaidi tunayo changamoto ya kuimarisha udadisi, kujiamini, sayansi,
hesabu na teknolojia, na kutafakari juu ya sera ya kufundisha lugha, kujenga
dhana za ujasiriamali na stadi za kazi katika ngazi mbalimbali. Tusisahau pia

16
kuweka viongozi imara katika shule na taasisi za elimu na kuimarisha uandaaji
wa walimu bora katika ngazi zote. Kama alivyosema mwalimu, Kupanga ni
kuchagua. Tuchague ubora na hekima, maana Hekima ni Uhuru. Na
tunaponukuu busara ya wenzetu wachina, tukumbuke kuwa tukitaka kupanga
mipango mizuri ya miaka 50 hadi 100 ijayo, tuelimishe watu wetu wapate
maarifa na uwezo wa kufikiri, kujiamini na kupenda kazi.

Marejeo
Komba, D. (2006). Reflections on Mwalimu Nyereres Philosophy of Education for Self
Reliance. A paper read at the International Seminar to Commemorate the
7th Anniversary of Mwalimu Nyerere. Dar es Salaam. Faculty of
Education. University of Dar es Salaam.

Krotto, Harry: Why science education is an ethical issue; The Independent


newspaper, (UK) 12 May, 2011

Ministry of Education and Culture, Tanzania (2000). Teacher Education Master


Plan. Dar es Salaam. MOEC.

Ministry of Planning and Development, (2005). Government Projections. Dar es


Salaam. Govt Printer. Ministry of Planning Statistics (2006)

Odhiambo, T R (1981). Understanding science: The influence of African


traditional view of nature. In P.D.G. Gilbert & M.N. Lovegrove. (Eds.)
Science education in Africa. Heinemann.

O-saki, K. M. (2000). The Science Education in Secondary Schools. Internal project


evaluation. Dar es Salaam: Ministry of Education and GTZ.

O-saki, K. M. (2005). Reflections on the medium of instruction and interaction: A


focus on science teaching and learning. In B. Brock-Utne, Z. Desai, & M.
Qorro LOITASA (Language of Instruction in Tanzania and South Africa)
Research in progress. Dar es Salaam: KAD Associates.

Osaki, K. M (2004). Reflection on the state of science education in Tanzania. In:


O-saki, K. M., Hosea, K., & Ottevanger, W. (2004). Reforming science and

17
mathematics education in Tanzania: Obstacles and opportunities. Dar es
Salaam: TEAMS project.

Osaki, K. M (2007). Science and Mathematics teacher preparation in Tanzania: 1966-


2006: Lessons from teacher improvement projects in Tanzania, 1965-2006. In:
International Journal of Education, Naruto University, Japan. Vol 2, 51-64.

Osaki, K. M (2008). Science Teacher Education in Tanzania: The changing content and
form of science teaching and teacher education. In: Richard Coll and Neil
Taylor (eds) (2007). Science Education in Context. An international
Examination of the influence of context on science curriculum development
and implementation. Rotterdam & Taipei. Sense Publishers.

Osaki, K, M (2009). The Challenges of science and mathematics education in


Tanzania. Paper presented at the Annual INSET workshop for science and
maths educators. Dar es Salaam, 2009.

Ottevanger, W.J.W., Feiter, L., O-saki, K. M., & van de Akker, J. (2005). The
TEAMS project in Tanzania: From intervention to capacity building,
Journal of International Co-operation in Education, 8(1), 111-128.
.
Tanzania Government (1967). The Arusha Declaration and the Philosophy of
Socialism and Self Reliance. Dar es Salaam. Government Printer.

Tanzania Government. (1967). The Arusha Declaration and TANUs policy of


socialism and self reliance. Dar es Salaam: Government printer.

Tanzania Government. (2005). Secondary education Development programme


(SEDP). Dar es Salaam: Ministry of Education and Culture.

Tanzania Government. (2006). Hotuba ya Waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi


kuhusu makadirio ya matumizi ya fedha kwa mwaka 2006/7. Dar es Salaam.
Ministry of Education and Vocational Training.

Tanzania Government (2006). Basic education statistics (BEST), 2002-2006. National


Data. Dar es Salaam. Ministry of Education and Vocational Training.

Tanzania Government (1995). Tanzania. Education and Training Policy. Dar es


Salaam. MOEVT
Tanzania Government (2005). Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya SEkondari
MMES. . Dar es Salaam. Mpiga chapa wa Serilali.
Tanzania Government (2000). Mpango wa Maendeneo Elimu ya msingi [MMEM]
. Dar es Salaam. Mpiga chapa wa Serikali.

18
19

You might also like