Download as docx, pdf, or txt
Download as docx, pdf, or txt
You are on page 1of 28

KUSUDI LA KUUMBWA KWAKO

A: Lengo la Somo
1. Kukusaidia kuelewa dhana nzima ya kusudi.
2. Kukufanya utambue kwamba umeumbwa na umezaliwa kwa kusudi maalumu.
3. Kukuongoza hatua kwa hatua katika kugundua kusudi la kuumbwa kwako.
4. Kukufundisha ni namna gani unaweza kupiga hatua za kukuwezesha kuishi katika kiini cha
kusudi la kuumbwa kwako.
5. Kukujulisha vikwazo vinavyoweza kukuzuia usiishi katika kusudi la kuumbwa kwako na
namna ya kuvishinda.

B: Maandiko ya Kutuongoza.
Yeremia 1:4-5
Neno la Bwana lilinijia, kusema,
Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa;
nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.

Matendo 13:36
Kwa maana Daudi, akiisha kulitumikia shauri la Mungu katika kizazi chake, alilala, akawekwa
pamoja na baba zake, akaona uharibifu.

C: Utangulizi
Nini maana ya neno Kusudi?
Kusudi maana yake ni
- Sababu iliyofanya kitu kitengenezwe au kiumbwe.
- Sababu ya uwepo wa kitu.
- Kilichohamasisha uumbaji wa kitu fulani.
- Matokeo yaliyotarajiwa na kusababisha kufanyika kwa kitu fulani.
- Mwisho unaoamua mwanzo wa safari.
- Matarajio ya chanzo cha kitu.
Tunapozungumzia kusudi la kitu chochote tunamaanisha sababu iliyofanya kuwepo kwa hicho
kitu. Hakuna jambo linalofanyika pasipo kuwepo kwa sababu ya kulifanya. Isitoshe, kusudi ndilo
huamua kuwepo au kutokuwepo kwa kitu au jambo fulani.

Uumbaji wowote hutanguliwa na kusudi. Pasipo kusudi hapana uumbaji na kama kitu
kimeumbwa au kutengenezwa basi kina kusudi nyuma yake.

Tazama mahali ulipokaa sasa na uangalie vitu vinavyokuzunguka. Je, kuna kitu chochote
unachokiona ambacho unadhani hakina kusudi au sababu ya kuwepo? Naweza kukuambia kwa
uhakika ya kwamba, kila unachokiona kina sababu iliyokifanya kiwepo.

Kwa hiyo, tunapozungumzia kusudi la kuumbwa kwako, tunazungumzia sababu iliyofanya


wewe uumbwe. Sababu iliyomfanya Mungu akuachilie katika dunia hii kwa majira haya tuliyopo
leo.

Jaribu kujiuliza,
- Hivi kwa nini ninaishi?
- Kwa nini Mungu aliamua kuniumba mimi?
- Kuna umuhimu gani wa mimi kuendelea kuishi?
- Hivi kama nisingekuwepo duniani kungekuwa na tofauti yoyote?
- Kwa nini nipo hivi nilivyo?
- Hivi ninahitajika katika hii dunia?

Maswali haya na mengine mengi yanayofanana na haya ni baadhi ya maswali yanayolenga


kutaka kujua kusudi la kuwepo kwa mtu duniani.

Kama binadamu anaumba au kutengeneza kila kitu kwa ajili ya kutimiza kusudi fulani, Je si
zaidi sana Mungu aliyekuumba wewe na mimi?

Ni lazima tujiulize,
- Hivi Mungu alikuwa na mpango wowote wakati ananiumba?
- Hivi kuna sababu yoyote iliyomfanya Mungu aniumbe hivi nilivyo?
- Hivi Mungu hakuwa na kazi nyingine ya maana hadi akaamua kuniumba mimi na
kunileta duniani?
- Kwa nini Mungu aliamua nizaliwe katika familia, jamii na taifa nililozaliwa?
- Hivi wakati Mungu ananiumba, alikuwa na matarajio gani kutoka kwangu?

Kusudi ni sababu ya kuwepo kwa kitu. Kuna sababu ya kuwepo kwako duniani. Tutakwenda
kulithibitisha hili kutoka kwenye maandiko.

D: Kanuni za Kusudi
(Zimenukuliwa kutoka kwenye kitabu cha In Pursuit of Purpose kilichoandikwa na Dr. Myler
Munroe)

Kuna kanuni saba za msingi ambazo zinaeleza tabia ya kusudi kama ilivyoamuriwa na Mungu.

1. Mungu ni Mungu wa Kusudi.


Mungu hafanyi kitu chochote kwa ajili ya kujifurahisha tu

2. Kila kitu katika maisha kina kusudi la kuwepo.


Kutokujua kusudi hakuondoi uwepo wa kusudi

3. Siyo kila kusudi linafahamika.


Kusudi lisilojulikana siku zote hupoteza muda na huleta uwezekano wa maisha ya hatari

4. Kusudi lisipofahamika, matumizi mabaya hayaepukiki.


Matumizi mabaya hutokea pale ambapo hatufahamu malengo ya muumbaji katika kukiumba
kitu fulani

5. Kama unataka kujua kusudi la kitu, usikiulize kitu chenyewe.


Kitu kilichoumbwa hakiwezi kujua nini kilikuwa kwenye mawazo ya muumbaji wakati
anapanga na kukitengeneza

6. Kusudi la kitu hupatikana kwa aliyekiumba tu.


Ni Mungu pekee ndiye anajua kusudi la maisha yako

7. Kusudi ndiyo ufunguo wa maisha ya utoshelevu.


Mungu anataka tujue malengo na makusudi yake kwa ajili ya maisha yetu kwa sababu
anafahamu kwamba nje ya hayo hatuwezi kufahamu tumaini, amani na furaha.

Katika mambo yote, kusudi ndiyo ufunguo wa utoshelevu kwa sababau linaweka msingi ambao
maisha hujengwa juu yake.

E: Uthibitisho kwamba Umeumbwa kwa Kusudi Maalumu

Kama bado huna uhakika na hujashawishika kwamba Mungu alikuumba kwa kusudi maalumu
ninataka kutumia kipengele hiki kukuthibitishia hilo.

Inawezekana umekuwa ukiyaendesha maisha yako kwa namna unavyojua wewe bila kuwa na
fikira zozote kuhusu mpango na makusudi ya Mungu kwako, kupitia kipengele hiki nataka kuleta
katika umakini wako ukweli kwamba kuna kusudi la kuumbwa kwako.

Sote lazima ifike wakati tutambue kwamba maisha haya si yetu, Mungu ndiye aliyetuumba ili
tuishi kwa kufuata mapenzi yake na siyo mapenzi yetu. Mungu anadai tuishi kwa kutimiza
kusudi lake na siyo kutimiza matakwa yetu.

Kuishi nje ya kusudi la Mungu ni kuishi maisha yasiyo na faida. Mafanikio ya kweli ni kutimiza
mapenzi ya Mungu hapa duniani. Kipimo cha mafanikio ya Yesu ilikuwa ni kutangaza habari
njema za ufalme wa Mungu, kufa na kufufuka kwa ajili ya ukombozi wa watu. Mafanikio ya
Yesu hayakuwa katika kujipatia utajiri, au kujipatia umaarufu au kujitengenezea jina katikati ya
watu.

Mambo ambayo wengi tunayasherehekea kama ni mafanikio yanaweza kuwa ni takataka tu


mbele za Mungu, pale ambapo tunaishi nje ya mpango na kusudi lake la kutuumba na kutupa
nafasi ya kuishi.
Kama nilivyosema, lengo la kipengele hiki ni kutaka kukuthibitishia kwamba umezaliwa kwa
kusudi maalumu. Hebu tutazame maandiko yafuatayo.

1. Mungu ni Mungu wa Makusudi.

Kila kitu anachokifanya Mungu hukifanya kwa makusudi maalumu. Mungu hafanyi chochote
bila kuwa na sababu ya kukifanya.

Ukisoma habari ya uumbaji katika Mwanzo sura ya kwanza, utaona ya kwamba kila kitu
alichokuwa anakiumba Mungu alikuwa anakipa kazi ya kufanya au kusudi la kuwepo kwako.
Tutazame baadhi ya maandiko.

Mungu akasema, Na liwe anga katikati ya maji, likayatenge maji na maji. Mwanzo 1:6

Mungu akasema, Maji yaliyo chini ya mbingu na yakusanyike mahali pamoja, ili pakavu
paonekane Mwanzo 1:9

Mungu akasema, Na iwe mianga katika anga la mbingu ili itenge kati ya mchana na usiku; nayo
iwe ndiyo dalili na majira na siku na miaka Mwanzo 1:14

Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa
baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa
kitambaacho juu ya nchi. Mwanzo 1:16

Maandiko haya machache kutoka kwenye habari ya uumbaji yanatuonesha kwamba Mungu
aliumba kila kitu kikiwa na kusudi. Mungu hakuumba ili kujifurahisha tu, aliumba kila kitu kwa
ajili ya kuhakikisha uwepo wa hicho kitu utafanya maisha ya duniani yawe na mwendelezo.

Mbali na maandiko hayo yanayoonesha uwepo wa kusudi kwa kila kiumbe cha Mungu, nataka
nikuthibitishie kwamba, hata kwa mtu mmoja mmoja kuna kusudi la kuwepo kwake.
Kila mtu aliyeumbwa na Mungu ameumbwa kwa kusudi maalumu, siyo wachache tu, bali ni
wote. Mifano kadhaa katika Biblia inatuthibitishia hili.

2. Mfano wa Yeremia

Yeremia 1:4-5
Neno la Bwana lilinijia, kusema, Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka
tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.

Katika kauli hii ya Mungu kwa Yeremia tunajifunza vitu kadhaa;


i. Mungu alimjua kila mmoja wetu kabla hata ya kutungwa kwa mimba yake.
ii. Mungu alimtakasa/alimtenga kila mmoja wetu tangu alipokuwa tumboni.
iii. Mungu amemuweka kila mtu hapa duniani kwa ajili ya kazi fulani.

Kitu alichokiongea Mungu kwa Yeremia hapa hakijafungwa kwa Yeremia tu, bali kwa kila mtu
aliyezaliwa duniani. Ukweli huu tunauona hata kwenye maisha ya Paulo.

3. Mfano wa Paulo

Wagalatia 1:15-16
Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake,
alipoona vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri Mataifa habari zake; mara
sikufanya shauri na watu wenye mwili na damu;

Kupitia andiko hili, Mtume Paulo anatuthibitishia ya kwamba kila mmoja wetu
alitakaswa/alitengwa tangu alipokuwa tumboni mwa mama yake, kila mmoja wetu ana neema ya
Mungu kwa ajili ya kufanya kazi fulani, kila mmoja wetu ana wito wa Mungu kwa ajili ya
kutimiza kusudi fulani lenye kumtukuza Mungu.

Mpendwa, lengo langu ni kwamba kwanza kabisa ushawishike kwamba Mungu ana kusudi na
wewe. Mungu hakukuumba na kukutupa tu duniani ili uhangaike na kuishi maisha ya
kubahatisha.
Hakuna kiumbe cha Mungu ambacho kililetwa duniani kuja kubahatisha. Maisha yako ni ya
thamani sana, hayapaswi kugeuzwa kuwa bahati nasibu.

Kuna kusudi na sababu maalumu ya kuumbwa kwako na kuzaliwa kwako. Endelea kufuatilia
somo hili ili upate kutambua kusudi hilo na uanze kuishi katika kutimiza mapenzi ya Mungu.

F: Maana ya Kuzaliwa

Kila mtu aliyekuja duniani amezaliwa. Hakuna namna nyingine yoyote ya mtu kuja hapa duniani
bila ya kuzaliwa. Watu pekee ambao hawakuzaliwa ni Adamu na Hawa, ambao waliumbwa
moja kwa moja kutoka kwa Mungu.

Je, kuna maana yoyote katika kuzaliwa?


Je, mchakato wa kuzaliwa na mtu una kusudi gani?
Je, kuzaliwa ni mchakato wa kibaiolojia tu au kuna zaidi ya baiolojia mtoto anapokuwa tumboni
mwa mama yake?

Baiolojia imeweza kuelezea mchakato mzima unaoendelea tangu kutungwa kwa mimba hadi
kuzaliwa kwa mtoto. Vitu vingi vimeelezwa na vimekuwa msaada kwa watu kupitia sayansi ya
baiolojia. Lakini kupitia sehemu hii, nataka tufahamu kwamba, kinachoendelea mtoto akiwa
tumboni ni zaidi ya baiolojia.

Kitabu cha Yeremia 1:5 na Wagalatia 1:15 inaeleza kitu kimoja kwa namna inayofanana sana.

Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa;


nimekuweka kuwa nabii wa mataifa. Yer 1:5
Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake Gal
1:15
Kupitia maandiko haya mawili tunajifunza kwamba, tumbo la uzazi ni chombo ambacho Mungu
anakitumia kwa ajili ya kumuandaa, kumtakasa, kumtenga na kumfanya mtu kuwa tayari kwa
ajili ya kutimiza mapenzi ya Mungu hapa duniani.

Tumbo la uzazi ni kama kiwanda cha Mungu kwa ajili ya kumtengeneza mtu na kumuwekea kila
sifa anayoihitaji kwa ajili ya kutimiza kusudi lake la kuishi.

Kukaa miezi tisa katika tumbo la uzazi hakupo kwa ajili ya kupoteza muda tu, au siyo kwa ajili
ya kukamilisha mchakato wa kibaiolojia tu, bali kubwa zaidi ni kwa ajili ya Mungu kukuandaa
na kukuwekea kila unachokihitaji ili kutimiza kusudi lake hapa duniani.

Kwa sababu hiyo, mtu anapozaliwa anazaliwa akiwa na kila kitu anachohitaji ili kuishi maisha
yenye mafanikio. Kila ulichokihitaji kwa ajili ya kuishi hapa duniani Mungu alikuwekea kabla
hata ya kuzaliwa kwako. Ulizaliwa mraba baada tu ya Mungu kumaliza kukusheheneza hazina
zote unazozihitaji.

Vipaji ulivyonavyo, mwonekano wako, rangi yako, kimo chako, haiba yako, shauku zako, vitu
unavyovipenda n.k. ni baadhi ya vitu ambavyo Mungu alikuwekea ukiwa tumboni mwa mama
yako kwa ajili ya maisha yenye ufanisi.

Tukiwa duniani tunachofanya ni kuvigundua tu na kuviboresha ili viweze kutumika kutimiza


mapenzi ya Mungu.

Kwa hiyo ulizaliwa ukiwa tayari kwa ajili ya kazi aliyokuumbia Mungu.
Ulizaliwa ukiwa na kila kitu unachokihitaji kwa ajili ya kuishi.

KWAMBA UMEZALIWA
1Kuzaliwa kwako ni uthibitisho kwamba kuna kusudi la Mungu lililokutangulia.

2Kuzaliwa kwako ni uthibitisho kwamba wewe ni wa muhimu na unahitajika katika dunia hii.

3Kuzaliwa kwako ni uthibitisho kwamba kuna tatizo katika dunia hii ambalo unatakiwa kulitatua.

4Jiulize, ni tatizo gani litakoma kuwepo kwa sababu ya kuishi kwako?


5Kuzaliwa kwako ni uthibitisho kwamba umeandaliwa na kutengwa maalumu kwa ajili ya kazi
fulani hapa duniani.

6Kuzaliwa kwako ni uthibitisho kwamba Mungu amekutuma katika dunia hii kwa ajili ya utukufu
wake.

7Kuzaliwa kwako ni uthibitisho kwamba kuna hazina ndani yako ambayo unatakiwa uiache
duniani kabla hujaondoka.

8Kuzaliwa kwako ni uthibitisho kwamba hakuna mwingine kama wewe duniani, wewe ni wa
kipekee na wa aina yake, hajawahi kuwepo kabla yako na hatakuwepo baada yako.

9Kuzaliwa kwako ni uthibitisho kwamba una maisha yako ya kuishi ambayo ni tofauti na mtu
mwingine yeyote.

10Kuzaliwa kwako ni kielelezo kwamba umepewa fursa moja ya kuishi, itumie vizuri kwani
utapaswa kuitolea hesabu kwa yeye aliyekupa.

11Hukuzaliwa kimakosa.

12Ulikuwa katika mpango wa Mungu kabla hata hujazaliwa.

13Umezaliwa katika kizazi hiki, kwa sababu hiki kizazi kinakuhitaji.

14Usijidharau, ulipitia mchakato wa kuzaliwa na ukatoka kama bidhaa ya kipekee kutoka kwa
Mungu kuja kwa dunia hii.

15Wewe ni zawadi ya Mungu kwa kizazi hiki. Mtumikie Mungu kwa kutimiza kusudi lake katika
kizazi chako.

Nikuulize swali, hivi wewe ulizaliwa? Kama ulizaliwa, basi sifa zote nilizozieleza hapo juu
unazo na zinakuhusu.

Acha kujionea huruma, acha kulalamika, una kila unachohitaji kwa ajili ya kutimiza kusudi la
Mungu na kuishi maisha yenye mafanikio. Tuendelee kujifunza kutoka kwenye Biblia.
G: Mifano ya watu katika Biblia

Kutoka kwenye Biblia tunaweza kujiridhisha kwamba Mungu alimuumba kila mmoja wetu kwa
kusudi maalumu, kwa wakati maalumu na katika kizazi maalumu.

Tutatazama maandiko yanayoonesha mifano ya watu mbalimbali na namna ambavyo kusudi la


kuwepo kwao liliamuriwa kabla hata ya kuzaliwa kwao.

1. Yesu
Unabii wa kuzaliwa kwa Yesu na kazi atakayoifanya ulitoka miaka mingi kabla ya kuzaliwa
kwake.
Isaya 7:14
Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto
mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.

Mathayo 1:21
Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu
wake na dhambi zao.

2. Daudi

Matendo 13:36
Kwa maana Daudi, akiisha kulitumikia shauri la Mungu katika kizazi chake, alilala, akawekwa
pamoja na baba zake, akaona uharibifu.

Kulikuwa na shauri/kusudi la Mungu ambalo lilimfanya Mfalme Daudi azaliwe katika kizazi
chake, naye alipokwisha kulitumikia ilimlazimu aondoke.

3. Yohana Mbatizaji

Isaya 40:3
Sikiliza, ni sauti ya mtu aliaye, Itengenezeni nyikani njia ya Bwana; Nyosheni jangwani njia kuu
kwa Mungu wetu.

Luka 1:13-17
13 Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo
Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yohana.
14 Nawe utakuwa na furaha na shangwe, na watu wengi watakufurahia kuzaliwa kwake.
15 Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana; hatakunywa divai wala kileo; naye atajazwa
Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye.
16 Na wengi katika Waisraeli atawarejeza kwa Bwana Mungu wao.
17 Naye atatangulia mbele zake katika roho ya Eliya, na nguvu zake, ili kuigeuza mioyo ya baba
iwaelekee watoto, na kuwatilia waasi akili za wenye haki, na kumwekea Bwana tayari watu
waliotengenezwa

Unabii wa ujio wa Yohana Mbatizaji ulitolewa miaka mingi kabla ya kuzaliwa kwake, n ahata
malaika alipokuja kumweleza Zakaria habari za kuzaliwa Yohana alieleza hadi jinsi maisha yake
yatakavyokuwa na kazi atakayoifanya.

4. Samsoni

Waamuzi 13:3-5
3 Malaika wa Bwana akamtokea yule mwanamke, akamwambia, Tazama, wewe sasa u tasa,
huzai; lakini utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume.
4 Basi sasa, jihadhari, nakuomba, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi;
5 kwani tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume; na wembe usipite juu ya
kichwa chake; maana mtoto huyo atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye ataanza
kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti.

Kazi ya Samsoni iliamuriwa kabla ya kuzaliwa kwake, n ahata mtindo wake wa maisha
uliwekwa na Mungu kabla Samsoni hajazaliwa. Isitoshe, Samsoni alikuwa mnadhiri wa Bwana
kabla hata ya kuzaliwa kwake.
5. Yeremia

Yeremia 1:4-5
Neno la Bwana lilinijia, kusema, Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka
tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.

Mifano hii michache ni kututhibitishia kwamba, Mungu ni Mungu wa makusudi. Kila mtu
aliyeumbwa na Mungu amebeba kusudi la Mungu.

Kila mtu anahitajika na ana umuhimu hapa duniani kwa sababu kuna ajenda maalumu ya Mungu
ambayo ametumwa kuifanya hapa duniani.

Kabla hujaanza kutafuta kujua kusudi la kuumbwa kwako, ni lazima ushawishike kwamba
umezaliwa kwa kusudi maalumu na ilikuwa ni lengo la somo hili la leo kukushawishi kwamba
hakika kuna kusudi la kuzaliwa kwako.

H: Kujua Kusudi la Kuumbwa Kwako

Mpaka sasa ninaamini kwamba una uhakika kwamba umezaliwa kwa kusudi maalumu. Bila shaka
unafahamu kwamba haupo duniani kupoteza muda tu na kujifurahisha, bali kutimiza kazi
uliyotumwa na muumba wako kuifanya.

Ninafikiri kwa sasa utakuwa unajiuliza, ninawezaje kujua kusudi la kuumbwa kwangu sasa? Ni
swali ambalo kila mmoja wetu anapaswa kujiuliza na kupata majibu yake. Somo la leo litakwenda
kutusaidia na kutupa mwongozo wa nini cha kufanya ili kujua kusudi letu la kuzaliwa.

Nianze kwa kusema kwamba, ni wajibu binafsi wa kila mtu kutafuta kujua sababu ya kuwepo
kwake duniani. Mungu hajaweka hatma yako mikononi mwa mtu mwingine yeyote isipokuwa
wewe. Hakuna mtu anayeweza kukujua vizuri zaidi yako.
Wapo wachungaji, wainjilisti, walimu, manabii na mitume, lakini hao wote hawana wajibu wa
kukutafutia kusudi la kuzaliwa kwako. Wanaweza kukusaidia kwa kukufndisha na kukuonyesha
njia ya kuifuata lakini mwisho wa siku wewe binafi ndiye unapaswa kujua na kushawishika kuhusu
kusudi la uwepo wako duniani.

Kabla hatujaanza kujifunza kuhusu namna ya kutambua kusudi, nitumie kipengele hiki
kukuonesha ni kwa nini unatakiwa kutafuta kujua sababu ya kuzaliwa kwako.

KWA NINI UJUE KUSUDI LA KUUMBWA KWAKO


1. Uliumbwa kwa ajili ya kutimiza kusudi.
2. Bila kuishi katika kusudi la kuumbwa kwako, utakuwa umepoteza muda wako wa kuishi
duniani.
3. Mafanikio ya kweli mbele za Mungu ni pale tunapotumiza kusudi lake la kutuumba.
4. Maisha ya utoshelevu yamefungwa katika kuishi ndani ya kusudi.
5. Kuha hatma za watu zimeambatanishwa na kusudi la kuishi kwako.
6. Mungu anapima maisha yetu kulingana na tunavyotimiza mapenzi yake hapa duniani.
7. Hatuna uchaguzi mwingine zaidi ya kutimiza kusudi la Mungu hapa duniani.
8. Hakuna maisha bora zaidi ya kuishi ndani ya kusudi la kuumbwa kwako.
9. Kitu pekee kinachokufanya uhitajike hapa duniani ni kusudi ulilolibeba.
10. Tunaufurahisha moyo wa Mungu pale tunapomtii kwa kutimiza kusudi lake la kutuweka hapa
duniani.

Nataka ufahamu kwamba, Hatupaswi kuhangaika kukusanya vitu vingi tulivyovikuta duniani,
bali kuachilia vitu vingi tulivyokujanavyo duniani

Japo ulizaliwa uchi, haukuja duniani ukiwa mtupu. Kuna hazina nyingi umekujanazo duniani na
hupaswi kuondoka nazo. Kwa kuishi katika kusudi la kuumbwa kwako, utaweza kumimina na
kuziacha duniani hazina zote ambazo Mungu aliwekeza ndani yako wakati anakuumba.

Sasa tuangalie ni kwa namna gani unaweza kujua kusudi la kuumbwa kwako.
I: MUULIZE ALIYEKUUMBA
Aliyekuumba anajua ni kwa nini alikuumba, kwa hiyo ukitaka kujua sababu ya kuzaliwa kwako
muulize Mungu.

Kazi mojawapo ya maombi ni kutusaidia kuyajua yale tusiyoyajua.

Yeremia 33:3
Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua.

Mungu yupo kwa ajili ya kutujuza yale tusiyoyajua. Mungu anapenda ujue kwa nini alikuumba,
kwa hiyo yupo tayari kukufunulia ili uanze kuishi kwa kutimiza kusudi lake.

Haya ni maombi ya kuuliza, kutaka kujua nini kilikuwa katika moyo wa Mungu wakati
anakuumba.

Unapomuomba Mungu na kumuuliza kuhusu sababu ya kuzaliwa kwako, Mungu anaweza


kukujibu kwa namna mbalimbali, baadhi ya namna hizo ni hizi zifuatazo.

i. Kwa njia ya maono au ndoto.


Maono na ndoto ni njia ambazo Mungu huzitumia kwa ajili ya kufikisha ujumbe wake kwa watu.
Katika maono au ndoto Mungu anaweza kukuonyesha picha halisi ya kile unachopaswa kufanya
katika maisha. Kuna mifano ya watu wengi katika Biblia ambao kupitia maono na ndoto Mungu
aliweza kuwajuza kuhusu nini wanapaswa kufanya.

Mfano wa kwanza ni Yusufu, Mungu alimletea ndoto mbili ambazo zote zilikuwa zinaonesha
hatma yake ni ipi na anatakiwa kutimiza kusudi gani katika maisha. Mwanzo 37:5-10

Yusufu aliota ndoto mbili ambazo zote zilikuwa zinaonesha kwamba atakuwa mtawala na kwamba
ndugu zake wote watakuwa chini ya hifadhi yake. Ndugu zake wote watakuja kumtegemea kwa
sababu Mungu alimuandaa kwa ajili ya kuhifadhi hatma za ndugu zake. Mwanzo 50:20
Mfano wa pili ni nabii Isaya ambaye naye kwa njia ya maono Mungu aliweza kusema naye na
kumtuma kwa ajili ya kazi aliyomkusudia aifanye. Isaya 6:1-13

Pia Mungu anatuonyesha katika Habakuki 2:1-3 kwamba tunaposimama na kuomba Mungu
hutuletea njozi au maono ambayo yanatuonyesha nini tunapswa kufanya. Habakuki 2:1-3

ii. Kwa kutufunulia Neno lake.


Neno la Mungu limebeba dira ya maisha yetu. Kila mmoja wetu habari za maisha yake
zimeandikwa katika neno la Mungu. Kuna mapenzi ya Mungu ambayo umeandikiwa kuyafanya
katika neno lake na kuna wakati unaposoma neno Mungu anakubananisha kwenye baadhi ya
maandiko na kukuonyesha kwamba kuna kitu unapaswa kufanya.

Waebrania 10:7
Ndipo niliposema, Tazama, nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa) Niyafanye mapenzi
yako, Mungu.

Zaburi 119:105
Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.

Isaya 29:11-12
Na maono yote yamekuwa kwenu kama maneno ya chuo kilichotiwa muhuri, ambacho watu
humpa mtu aliye na maarifa, wakisema, Tafadhali ukisome hiki; akasema, Siwezi, kwa kuwa
kimetiwa muhuri; kisha chuo hiki apewa mtu asiye na maarifa, akaambiwa, Kisome hicho
tafadhali, akasema, Sina maarifa mimi.

Biblia ni kitabu cha maono na unapokuwa na Roho wa Mungu ndani yako anakuwezesha kupata
maono na kujua mpango wa Mungu kuhusu maisha yako.

Wakati unasoma Biblia kuwa makini sana, kuna wakati Mungu analeta neno fulani au maandiko
fulani kwa msisitizo sana kwako, maneno hayo yanaweza kuwa yanaonyesha kuhusu kusudi la
kuumbwa kwako na kukuambia ni nini unapaswa kufanya.
Yohana mbatizaji alijua kuhusu kusudi lake kupitia maandiko ya nabii Isaya. (Yohana 1:23). Yesu
pia alijua kusudi lake kwa kusoma chuo cha nabii Isaya na kuona mahali palipoandikwa
kumuhusu. (Luka 4:17-21)

Biblia ni kitabu kinachoeleza kuhusu kusudi la maisha yako. Unaposoma na kumruhusu Roho
Mtakatifu akuongoze, atakuongoza katika kujua ni nini Mungu anataka ufanye kupitia maisha
yako.

Kwa hiyo, unapomuomba Mungu akufunulie kuhusu kusudi la kuumbwa kwako, usiache kusoma
neno na usiache kuwa makini katika roho yako, wakati wowote Mungu anaweza kukufunulia.

Pamoja na njia ya maombi, ambayo inaonekana ni ya kiroho sana, kuna njia za asili ambazo kwa
wengi inaweza kuwa ni rahisi zaidi katika kujua kusudi la kuumbwa kwao.

J: JITAFUTE au JICHUNGUZE

Kila bidhaa imeundwa na features au tabia zote zinazohitajika ili kuiwezesha kutimiza kusudi
lake. Kwa mfano, ukikiona kiti tu unajua hiki ni kwa ajili ya kukaliwa. Kwa sababu muundo wake
unasadifu kazi yake.

Huwezi kuchukua kisu alafu ukataka utumie kula wali, utakuwa na shida wewe. Hii ni kwa sababu
muundo wa kisu unaonyesha kabisa kwamba kazi yake ni kukata. Na hata kisu na kisu
kinatofautiana mahali vinapotumika.

Ninachotaka kusema hapa ni kwamba, hata wewe umeumbwa na umeundwa kwa namna ambayo
una features au tabia zitakazokuwezesha kuishi katika kusudi lako. Kwa hiyo ukijitathimini
vizuri kwa kuangalia jinsi ulivyoumbwa, tabia mbalimbali ulizonazo, shauku mbalimbali
ulizonazo, vitu unavyopenda na kuvichukia, haiba yako, mwonekano wako, uongeaji wako n.k.
vinaweza kukuongoza kujua umeumbwa ili kufanya nini.

Dondoo zifuatazo zinaweza kukupa mwongozo wa kujitathimini ili ujue ni nini hasa unaweza
kufanya na maisha yako. (Zimenukuliwa kutoka kwenye kitabu cha WHO AM I? WHY AM I
HERE? Kilichoandikwa na Dr. Sunday Adelaja)
1. Shauku uliyonayo ndani yako.
Wito na Kusudi letu lipo ndani ya shauku zetu za asili. Tumembwa na kuwekewa shauku katika
vitu fulani. Shauku ni msukumo unaotokea ndani yakow a kutaka ufanye vitu fulani.
Unahamasika kufanya nini?
Unavutiwa kufanya nini?
Unapenda kufanya nini?
Muda ambao huna kazi, unapenda kufanya nini?
Nini kimekuwa kinakuvutia sana tangu utoto wako?

Haya ni baadhi ya maswali yanayoonyesha shauku yako iko wapi.

2. Ni kazi gani ambayo ungependa kuifanya, hata kama hautalipwa kitu chochote?

Ni vitu gani ambavyo vinakufurahisha kufanya kiasi kwamba hata usipolipwa unaridhika?
Kama pesa isingekuwa tatizo kwako, ungependa kufanya kazi gani?

3. Una uwezo mzuri wa kufanya vitu gani?


Hiki ni kielelezo cha vipaji vyako na karama ulizonazo. Zinaweza kukusaidia kuonyesha hatma
yako iko wapi.

4. Ni vitu gani ukifanya vinakupa utoshelevu?


Kazi ambazo ukiwa unafanya zinakupa furaha na kukufanya ujisikie vizuri.

5. Watu wanaona nini kwako?


Je, ni vitu gani ambavyo ukifanya watu hukusifia mara kwa mara?
Tangu utotoni watu wamekuwa wanakusifia katika mambo gani?

6. Ni sifa gani unazo zinawafanya watu wakupende sana?


Angalia ndugu zako, marafiki, wafanyakazi wenzako
Je, wanakupendea nini?
Ni vitu gani hawavipendi kwako?
Ukiwa mtoto, watu walikuwa wanakupendea nini?
Vitu gani vinawafanya watu wakuonee wivu?

7. Nini kinakutofautisha na watu wengine?


Nini kinakufanya uwe wa kipekee na tofauti na wengine?
Watu hukukosoa sana katika mambo gani?
Katika mambo ambayo uko tofauti na wengine, upekee wako umefichwa humo. Tafuta kitu
kinachokutofautisha na wengine.

8. Ni kazi gani unaweza kufanya bila kuhitaji maandalizi yoyote?


Mambo unayoweza kufanya vizuri na kwa ubora bila hata kujiandaa yanaonyesha wito wako uko
wapi.

9. Ni mambo gani unaweza kufanya bila kutazama muda.


Kuna baadhi ya vitu ukianza kufanya unazama kweli na kujitoa kiasi kwamba huwezi hata
kutazama muda.

10. Ni kitu gani kinaweza kukufanya ukae nacho peke yako?


Kama ungefundiwa kwenye chumba kwa siku tatu bila kutoka nje, je ungeomba ukae na nini
kwenye hicho chumba? Je ungependa ukiwa peke yako uwe na kitu gani?
TV? Internet? Peke yako tu? Vitabu? Marafiki?

11. Ni mambo gani au habari gani unapenda kuzisoma, kusikiliza au kuzizungumzia mara kwa
mara?
Kuna baadhi ya mada ambazo unapenda kuzisoma na kuzifuatilia sana. Inawezekana ni hali ya
hewa, watoto, vijana, vitabu, uongozi n.k.

12. Ni mambo gani unayafikiria mara kwa mara?


13. Ni vitu gani ukianza kufanya unaweza kusahau hata kula?

14. Ni mtu gani au watu gani wanakuhamasisha sana?


Andika orodha ya watu wanaokuvutia na kukuhamasisha.
Ni watu gani unatamani kuwa kama wao?
Ni watu gani ambao unatamani kuwa na mafanikio kama yao?

15. Matatizo gani yanakukera na unatamani ungekuwa kwenye nafasi ya kuyatatua?

Ukiweza kupata majibu ya maswali haya yote, utakuwa katika nafasi nzuri ya kujua maisha yako
yanapaswa kuelekea wapi. Vitu ambavyo Mungu amewekeza ndani yako hujidhihirisha sana
kupitia majibu ya maswali yaliyoorodheshwa hapo juu.

Hakikisha unapata muda wa kujiuliza na kutathmini kwa kina. Jibu maswali hayo yote. Angalia
uhusiano uliopo kati ya majibu ya swali moja na maswli mengine. Muunganiko wa majibu yote
utakupa mwelekeo mzuri wa maisha yako.

Mwisho wa yote, unganisha majibu ya maswali hayo na mwongozo wa Neno la Mungu katika
kufanya maamuzi ya namna ya kuendesha maisha yako. Lazima kuna namna ambayo neno la
Mungu na Roho Mtakatifu watakupa mwongozo bora wa kutumia vipawa, karama na uwezo wote
ulionao kwa ajili ya kutimiza kusudi la Mungu hapa duniani.

K: KUTIMIZA KUSUDI LA KUISHI KWAKO

Lengo la kujua kusudi la kuumbwa kwako ni ili uishi sawasawa na hilo kusudi. Hakuna maana ya
wewe kujua kusudi la kuumbwa kwako kama baada ya kujua utaendelea kuishi kwa kufuata
matakwa yako tu. Kuishi kokote kinyume na kusudi uliloligundua ni kujisaliti mwenyewe na
kupuuzia wito wa Mungu juu ya maisha yako.

Tunapaswa kufahamu kwamba, maisha yetu yote yanapaswa kuwa yanahusu kutimiza mapenzi ya
Mungu. Mawazo yetu, mipango yetu na kila tunachofanya vinapaswa kulenga katika kuyatumikia
mapenzi ya Mungu na kuueneza ufalme wake hapa duniani. Tunapowekeza maisha yetu mahali
tofauti na alipokusudia Mungu inakuwa ni hasara kwa maisha yetu.

Kwa hiyo, ni lazima ushawishike moyoni mwako na kuamua kwa dhati kwamba utatoa maisha
yako kwa ajil ya jambo moja tu, kuyatumikia mapenzi ya Mungu.

Wafilipi 3:13
Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau
yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele

Jambo moja linalopaswa kutushughulisha kila siku ni kutumikia wito wa Mungu juu ya maisha
yetu. Hatuna biashara nyingine ya kufanya duniani zaidi ya kumpendeza Mungu. Hakuna mradi
mwingine tulionao duniani zaidi ya kuutumikia ufalme wa Mungu. Hatupaswi kuwa watumwa wa
kitu au mtu mwingine yeyote isipokuwa Bwana Yesu Kristo na Ufalme wake pekee.

Tunapaswa kufahamu kwamba tumenunuliwa kwa damu ya thamani sana, hivyo sisi si mali yetu
tena. Hakuna mwana wa Mungu anayejimiliki, kwa hiyo hatupo hapa duniani kutumikia matakwa
yetu bali matakwa ya Mungu..

Ni lazima tutoe maisha yetu kama dhabihi iliyo hai kwa ajili ya matumizi ya Mungu. Ni wakati
wa kila mmoja wetu kusimama na kusema, MIMI HAPA BWANA, NITUMIE UPENDAVYO.
Maisha yetu ya kila siku yanapaswa kuonyesha ya kwamba tunawajibika kwa Mungu kwa kila
tunalofanya hapa duniani.

Ili uweze kutumika na kutimiza kusudi la Mungu hapa duniani, yafuatayo ni mambo ya Muhimu
kufanya.

1. Kubali Wito
Baada ya kugundua kusudi la kuumbwa kwako, ni muhimu uweze kukubaliana nalo. Ni muhimu
uweze kukubali kwamba hakika nimeumbwa kwa ajili ya kazi hii.

Usicho kubaliana nacho huwezi kukitimiza.


Wito wowote anaokupa Mungu huwezi kuufanyia chochote mpaka uwe umeukubali kwanza. Eneo
lolote la maisha ambalo Mungu amekuita kutumika, lazima moyo wako ukubaliane nalo kama
kweli unataka kutumika na kuwa na mafanikio katika utumishi wako.

Ayubu 36:11
Kama wakisikia na kumtumikia, Watapisha siku zao katika kufanikiwa, Na miaka yao katika
furaha.

Inapokuja kwenye swala la kutimiza kusudi la Mungu, Mungu anachokitaka kutoka kwako ni
kusikia/Kukubali na kumtumikia.

Ni salama kukubaliana na wito wa Mungu. Hakuna faida yoyote ya maana nje ya kusudi la
kuumbwa kwako. Kubali, Tumika!

2. Kubali kwamba Unaweza Kutimiza.


Mbali na kukubali wito, ni lazima ukubali au uamini kwamba unaweza kutimiza jukumu alilokupa
Mungu. Siyo kwa uwezo wako au kwa nguvu zako, bali kwa sababu tu Yeye aliyekuita anajua
kwamba amekuwezesha kutimiza.

Siku zote Mungu atakuita utumike katika eneo ambalo amekupa neema ya kufanya vizuri na
kufanikiwa. Mungu atakuita utumike katika eneo ambalo ana uhakika kwamba msaada wote
unaouhitaji kwa ajili ya kufanikiwa upo kwa ajili yako.

Zaidi ya yote, Mungu anakuhakikishia kwamba yupo nawe popote anapokutuma uende. Nguvu
zake na uwezo wake unakuwa nawe kwa ajili ya kukufanikisha na kukushindia dhidi ya kila
vikwazo vitakavyoibuka njiani. Amini kwamba Unaweza.

Mara nyingi kazi anayokupa Mungu inaweza kuonekana kuwa ni kubwa kuliko uwezo wako, jua
tu kwamba Mungu hahitaji uwezo wako, anao uweza wake ambao upo kwa ajili ya kukufanikisha.

Mungu hakupi kazi inayoendana na uwezo wako bali uweza wake.


Yeremia 1:6-10
6 Ndipo niliposema, Aa, Bwana MUNGU! Tazama, siwezi kusema; maana mimi ni mtoto.
7 Lakini Bwana akaniambia, Usiseme, Mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu
nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru.
8 Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema Bwana.
9 Ndipo Bwana akaunyosha mkono wake, akanigusa kinywa changu; Bwana akaniambia,
Tazama, nimetia maneno yangu kinywani mwako;
10 angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu,
na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.

Hakuna kisingizio cha kufeli katika kazi yoyote anayokupa Mungu, kwa sababu Yeye mwenyewe
ndiye anayekuwezesha.

3. Jiandae (Hesabu Gharama)


Unahitaji maandalizi kwa ajili ya utendaji wenye matokeo mazuri. Hakuna jukumu lolote katika
maisha lisilohitaji maandalizi.

Mungu huwaandaa watu wake kabla hajawatumia. Pata muda wa kujiandaa kabla haujaingia moja
kwa moja katika kumtumikia Mungu kwenye kusudi la kuumbwa kwako.

Kipindi cha kujiandaa kinaweza kuhusisha kujifunza mambo mbalimbali yanayohusiana na wito
wako, kufanya kazi chini ya mtu mwenye utaalamu au ujuzi unaouhitaji, Kuombea kazi iliyopo
mbele yako, kuweka mipango yote inayohitajika kabla hujaanza, pia kuhesabu gharama
utakayopaswa kuingia katika kutumikia mapenzi ya Mungu.

Luka 14:28
Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama,
kwamba anavyo vya kuumalizia?

Maandalizi ya kina ni muhimu sana kabla ya kuanza kufanya kazi yoyote ile. Musa aliandaliwa,
Daudi aliandaliwa, Yoshua Aliandaliwa, Yesu aliandaliwa, Mitume waliandaliwa, wewe pia
unapaswa kujiandaa vizuri kabla hujajiingiza katika kazi unayopaswa kufanya.
Mhubiri 10:10
Iwapo chuma hakipati, wala mtu hakinoi; Ndipo hana budi kutumia nguvu zaidi. Walakini yafaa
kutumia hekima, na kufanikiwa.

Wakati wa maandalizi ni wakati wa kujinoa ili uwe tayari kwa kutimiza kusudi lako kwa ufanisi
mkubwa.
Jiulize,
- Unahitaji kuwa na ujuzi gani?
- Maarifa gani unapaswa kuwa nayo?
- Watu gani unaweza kujifunza kutoka kwao?
- Tabia gani unapaswa kujijengea?

Haya yote yatakusaidia kujipanga vizuri na kupata kila unachohitaji kwa ajili ya kutimiza kusudi
la Mungu.

4. Jitoe Kikamilifu kwa Ajili ya Kutumika katika Wito Wako.

Kuwa mchapa kazi. Hatma inahitaji wachapakazi. Hakuna mvivu mwenye nafasi katika ufalme
wa Mungu.

Kusudi la Mungu linahitaji uwajibikaji binafsi. Usipojibidiisha, maono ya Mungu yatafia


mikononi mwako.

Mambo hufanikiwa mikononi mwa wenye bidii. Hakuna kinachokuja bure katika ufalme wa
Mungu.

Bidii ni hitaji la lazima kwa kila anayetaka kumpendeza Mungu na kutimiza mapenzi ya Mungu
hapa duniani.
Yesu alikuwa mchapa kazi, Paulo alikuwa mchapa kazi, nawe unapaswa kuwa mchapakazi.

Ili chochote kiweze kufanikiwa ni lazima nguvu iwekezwe katika kufanya kazi.

Hakuna maono yanayojitimiza, ni wale wenye bidii tu ndio hutimiza maono yao.

Mithali 22:29
Je! Wamwona mtu mwenye bidii katika kazi zake? Huyo atasimama mbele ya wafalme;
Hatasimama mbele ya watu wasio na cheo.

Destiny demands Dilligence.

5. Kubali Kuongozwa na Mungu

Kubali kuongozwa na Mungu katika kila hatua ya maisha yako.

Mungu anajua vema kuliko wewe. (God knows better than you)

Ishi katika ushirika na Mungu, na jifunze kusikiliza uongozi wake, utajiepusha na makosa mengi.

Siyo kila njia inakupasa kuifuata, Mungu atakuongoza katika njia ikupasayo kuifuata.

Isaya 48:17
Bwana, mkombozi wako, mtakatifu wa Israeli, asema hivi; Mimi ni Bwana, Mungu wako,
nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata.

Katika kuongozwa na Mungu kuna uhakika wa mafanikio na maisha yenye faida. Tafuta
kuongozwa na Mungu.
L: Dhana Potofu Kuhusu Kusudi la Mungu

Kwa watu wengi, tunapozungumzia kusudi la Mungu, wao hudhani kwamba ni lazima liwe
linajihusisha na mambo ya kidini.

Wengi hudhani kwamba, kusudi la Mungu limefungwa kwenye mambo ya kikanisa, kama vile
Uchungaji, Uinjilisti, Ualimu, Unabii, Utume, Uimbaji, Uhudumu Kanisani, Ushemasi, Uongozi
wa Kanisani n.k. Watu wanataka kumfungia Mungu kwenye mipaka ya shughuli za kidini na za
kikanisa pekee.

Lakini ukweli ni kwamba, Kusudi la Mungu ni kubwa kuliko kanisa. Wakati ni kweli kwamba
kuna watu walioitwa kwa ajili ya kutumika katika eneo la kanisa, hasa huduma kuu tano katika
kanisa, tunapaswa kutambua kwamba asilimia kubwa ya watu huduma zao na wito wao ni nje ya
kanisa.

Tunapaswa kutambua kwamba, kuna watu wito wao ni kwenye siasa au uongozi kama akina Musa,
Yusufu, Danieli na Daudi, Kuna watu wito wao ni kwenye biashara kama akina Ayubu, Wengine
ni wafugaji na wakulima kama akina Ibrahim, Isaka na Yakobo. Kusudi la Mungu linabeba kila
Nyanja ya maisha.

Tunapaswa kutambua kwamba Mungu alimpa mwanadamu agizo la kuimiliki na kuitawala dunia.
Kila Nyanja ya maisha inapaswa kuwa na watu waliobeba kusudi la Mungu na wanaotawala kwa
niaba ya Mungu katika eneo husika.

Mwanzo 1:26
Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha;
mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya
nchi

Kazi yetu pekee ni kuhakikisha kwamba, kila mahali ambapo Mungu ametuweka tunatumikia
mapenzi yake, tunatumika kwa ajili ya kueneza ufalme wa Mungu katika hilo eneo na tunakuwa
chanzo cha watu katika hilo eneo kukutana na Mungu.
Kama wewe ni mfanyabiashara, basi Mungu amekupa fursa ya kuuingiza ufalme wake katika
Nyanja za biashara. Kama wewe ni mwalimu, Mungu amekupa fursa ya kuuingiza ufalme wake
katika Nyanja ya elimu. Kila eneo la maisha linahitaji watu walio na Mungu ndani yao ili waweze
kumuwakilisha Mungu huko.

Kwa hiyo, usiifungie karama ya Mungu na wito wa Mungu kwako kwenye mipaka ya kidini, tumia
kila alichokupa Mungu kwa ajili ya kuueneza ufalme wake kila mahali anapokuweka.

M: Vikwazo vya Kutimiza Kusudi Lako.

Kuna sababu nyingi zinazoweza kumfanya mtu ashindwe kutimiza kusudi la kuishi kwake duniani.
Tutaziangalia baadhi kwa ufupi na namna unavyoweza kuziepuka.

1. Kutokulijua kusudi lako


Hakuna namna unaweza kutimiza kusudi usilolijua. Ujinga wa kutojua uwepo wa kusudi au hata
kutotaka kujisumbua kutafuta kusudi la Mungu kwenye maisha unawafanya wengi kuishi maisha
ya kubahatisha tu.
Hapa suluhisho pekee ni kutafuta kulijua kusudi la kuumbwa kwako. Fuata hatua zote
tulizozungumza nwenye somo hili mpaka ujue ni kwa nini unaishi.

2. Kutokujua wapi pa kuanzia.


Kuna ambao inawezekana wanajua wanapaswa kufanya nini katika maisha, ila tatizo moja tu ni
kwamba hawajui waanzie wapi. Kwa sababu ya kutojua pa kuanzia wanaendelea kukaa tu huku
wakitumaini kwamba ipo siku wataanza kufuatilia maono yao.

Mahali sahihi pa kuanzia ni kwa kujipatia maarifa, hasa kwa watu waliotangulia katika eneo lako
la wito. Tafuta watu kadhaa ambao wanafanya vitu vinavyoendana na wito wako, jifunze kutoka
kwao, tafuta kujua wao walianzaje, changamoto walizokutana nazo na namna walivyozishinda.

Wakati huo huo endelea kuwa katika ushirika na Roho Mtakatifu, atakuongoza kuhusu hatua gani
unapaswa kuchukua ili uanze kufuatilia maono yako.

3. Kujiona Huwezi
Mara nyingi maono au wito anaokupa Mungu unaweza kuonekana ni mkubwa kuliko uwezo wako.
Kwa hali ya kawaida utajiona ni mdogo sana kufanya kazi anayokupa Mungu. Pia unaweza kujiona
huna uwezo wa kutimiza kusudi la Mungu. Hii ilimtokea Musa, Ilimtokea Yeremia n ahata Isaya.

Unachopaswa kujua ni kwamba, Mungu anapokuita kufanya kazi yoyote ni kwa sababu msaada
wote utakaouhitaji upo tayari na Yeye mwenyewe atakuwa pamoja nawe kuhakikisha unaweaza.

Pamoja na kumwamini Mungu, jiongezee uwezo. Tafuta maarifa na ujuzi unaohitaji ili kuwa na
ufanisi katika kutimiza majukumu yako. Kumtegemea Mungu hakuondoi uhitaji wa maarifa na
ujuzi.

4. Shinikizo la Maisha
Mahitaji ya maisha yamewafanya wengi kuacha kumtumikia Mungu na kuanza kutumikia
matakwa yao. Udanganyifu wa mali unawafanya watu watoe maisha yao kuitumikia pesa badala
ya kumtumikia Mungu. Mahitaji ya maisha yamekuwa shinikizo kubwa kwa watu kiasi kwamba
wanashindwa kutimiza kusudi la Mungu

Unahitaji kujua kwamba, katika kumtumikia Mungu kuna utimilifu wa mahitaji yako yote.
(Mathayo 6:33)

Pamoja na hayo, unahitaji kujiongezea maarifa yanayohusu fedha ili pesa isiwe kikwazo kwako
katika kumtumikia Mungu. Jiongezee uwezo wa kuitawala pesa, kuzalisha pesa na kuifanya pesa
ikutumikie. Tafuta uhuru wa kifedha ili uwe huru kutumia muda wako kumtumikia Mungu na
mapenzi yake.

5. Kutojitoa Kikamilifu (Lack of Total Commitment)


Kufuatilia kusudi la Mungu kunahitaji ujitoe kikamilifu, Roho, Nafsi na Mwili. Usipojiweka
wakfu kwa ajili ya kulitimiza kusudi la Mungu, utakuwa unafanya mambo nusu nusu na kwa
kubahatisha, na hivyo utakosa ufanisi katika ulifanyalo.

Unapaswa kufahamu kwamba maisha ni kwa ajili ya kutimiza kusudi la Mungu, hivyo tunahitaji
kujitoa kikamilifu kwa ajili ya kulitimiza. Weka bidii katika kumtumikia Mungu, kwani hapo
ndipo kwenye mafanikio ya kweli. Mithali 22:29.
6. Hofu ya Kushindwa.
Hofu ya kushindwa inawafanya wengi washindwe hata kuanza. Ni vigumu kupiga hatua yoyote
kama moyoni mwako umejawa na hofu.

Husisha nguvu ya Roho Mtakatifu kuishinda hofu. Lakini pia angalia mafanikio ya wengine
waliokutangulia ili uone uwezekano wa wewe kufanikiwa pia.

Hizi ni baadhi ya sababu zinazowafanya wengi washindwe kutimiza kusudi la kuumbwa kwao.
Japo zipo sababu nyingine nyingi, lakini kwa namna yoyote usiwe na kisingizio cha kutotaka
kutimiza kusudi la Mungu.

Chukulia kwamba KUISHI KATIKA KUSUDI LA MUNGU NI KITU CHA LAZIMA KWAKO.
IKIWA NI LAZIMA, KWA NAMNA YOYOTE UTAFANIKIWA TU.

Barikiwa Daima.

You might also like