Je, Matibabu Unayopewa Yanakufanya Kuwa Mgonjwa Zaidi?

You might also like

Download as doc, pdf, or txt
Download as doc, pdf, or txt
You are on page 1of 3

JE, MATIBABU UNAYOPEWA YANAKUFANYA KUWA MGONJWA ZAIDI?

Katika mfumo wa tiba tulizozoeshwa, ni jambo la kawaida kabisa kuugua ugonjwa na katika harakati za
kukutibu ugonjwa huo, ukazaliwa ugonjwa mpya ambao kuna wakati unakuwa mbaya kuliko hata huo wa
awali. Kibaya zaidi ni kwamba inaweza kuchukua muda mrefu sana kabla ya kubainika kuwa matibabu
uliyopewa ndiyo kiini cha maradhi yako mapya.

Historia ya tiba hizi zinazoitwa za kisasa imejaa mifano isiyo na idadi juu ya hali hii. Kwa mfano, tarehe
29, June 2013 Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC, lilinukuu taarifa ya Mamlaka ya dawa ya nchi hiyo,
iliyokuwa inatoa onyo kwa watumiaji wa dawa ya maumivu ya Diclofenac.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watumiaji wa dawa hiyo walikuwa wanajiongezea uwezekano wa kupata
magonjwa ya mfumo wa mzunguko wa damu ikiwa ni pamoja na kiharusi (stroke) na shambulizi la moyo
(heart attack). Diclofenac ni dawa ambayo imekuwa ikitumika kwa miaka mingi sana. Je, ni mamilioni
mangapi ya watu duniani kote ambao katika kipindi kilichotangulia tahadhari hii, wamepata kiharusi au
shambilizi la moyo kwa sababu ya matumizi ya dawa hii?

Mfano mwingine ni dawa inayoitwa Avandia (rosiglitazone). Mtengenezaji wa dawa hii, kampuni ya
GlaxoSmithKline Plc, ya Uingereza amejikuta kwenye matata makubwa baada ya dawa hiyo kubainika
kuwa ina madhara makubwa sana – hasa kwenye moyo – na kwamba kwa kipindi chote ilichotumika
imeua mamilioni ya watu dunia nzima. Mnamo tarehe 11, mwezi wa 5, 2011 ilitangazwa kuwa kampuni
hiyo ilikuwa imekubali kulipa fidia ya kiasi cha dola za kimarekani milioni 700 kwa walalamikaji 12,000
ambao walikuwa wameifungulia mashtaka kampuni hiyo. Na hii ilikuwa ni kwa Marekani pekee.

Hivi tunavyozungumza kampuni hiyo bado inakabiliwa na mashtaka katika nchi nyingine mbalimbali
duniani, na kuna uwezekano mkubwa kuwa katika hizo kesi itabidi ilipe fidia kubwa kwa wahanga
mbalimbali wa dawa hiyo au wawakilishi wao.

Kwa kweli mifano ya dawa ambazo zimetolewa kwa nia njema na madaktari lakini zikaishia
kuwasababishia watumiaji madhara makubwa ni mingi sana. Katika mlolongo huu zinaingia dawa kama
asprin na thalidoamide. Nyingine ni dawa za kupunguza tindikali tumboni (anti acids) zenye madini ya
aluminum, dawa za kupunguza lehemu (cholesterol) zinazoitwa Statins, dawa za kuua vimelea vya
bakteria (anti biotics) zenye kiambata cha fluoride (fluoroquinolones), nakadhalika.
Ilichukua miaka mingi hadi kubainika kuwa asprin ilikuwa inatoboa matumbo ya watumiaji wake na
kuwasababishia vidonda vya tumbo. Hali kadhalika ilichukua miaka mingi pia kubainika kuwa dawa
iliyokuwa inatumiwa na kina mama waja wazito kwa ajili ya kuwakinga na misukosuko ya mimba
(thalidoamide), ndiyo iliyokuwa inapelekea wazae watoto wasio na viungo!

Katika miaka ya hamsini na sitini ambamo dawa hii ilitumika, kina mama wengi wa nchi zilizoendelea
kama Ulaya, Marekani na Japani walikuwa wahanga wakubwa. Kina mama wa nchi masikini walisalimika
siyo kwa sababu nyingine yeyote ile, ila – UMASIKINI, basi! Hii ilikuwa ni dawa ya anasa zaidi, na kwa
wakati huo nchi masikini hazikuwa na uwezo wa kuitafuta anasa hiyo.

Ama kuhusu dawa za kupunguza tindikali zenye viambata vya aluminum, kuna ushahidi unaozidi
kuongezeka kila siku kuwa dawa hizo zinachangia sana katika kuwafanya watumiaji wake kukumbwa na
maradhi ya kupoteza kumbukumbu yanayofanana na maradhi ya Alzheimer ambayo huwakumba zaidi
baadhi ya watu wenye umri mkubwa. Tofauti hapa ni kwamba upotevu wa kumbukumbu unaotokana na
dawa hizi haujali umri.

Wakati dawa za Statins, mathalani Lipitor, nazo zinatuhumiwa sana kuwa zinaleta athari mbaya kama vile
kiwango kikubwa cha kupoteza kumbukumbu na kisukari cha ukubwani, madhara ya anti biotics za
fluoroquinolones yanatajwa kuwa ni ya kutisha.

Madhara ya dawa hizi yanatajwa kuwa ni pamoja uharibifu wa mfumo wa neva, uharibifu kwenye
mfumo wa fahamu, uharibifu kwenye mfumo wa misuli na mifupa, uharibifu kwenye mfumo wa damu,
uharibifu kwenye mfumo wa usagaji chakula, uharibifu kwenye ngozi, nakadhalika. Uharibifu unaotokea
unatajwa kuwa ni wa muda mrefu na wakati mwingine huwa ni wa kudumu. Baadhi ya watu ambao
wameathiriwa na fluoroquinolones wamepoteza uwezo wa kuhifadhi kumbukumbu kwa kiasi kikubwa
kiasi kwamba wanalazimika kuwa na kalamu na daftari muda wote ili yale mambo muhimu katika
mathalani, mazungumzo, wawe wanayaandika!

Ukiondoa dawa hizi na nyingine ambazo aghalabu madaktari wanawapa wagonjwa wao kwa nia njema,
kwa kutojua madhara yake, kuna kundi la dawa ambalo pamoja na kwamba madhara yake yanajulikana
fika, wagonjwa wanapewa kwa kisingizio cha kukosekana dawa mbadala.

Dawa hizi ni pamoja na zile zinazotumiwa kwa wagonjwa wa saratani, maarufu kama Chemotherapy.
Dawa hizi zinaingiza sumu nyingi mno kwa mgonjwa kiasi kwamba inabidi zitolewe kwa kukatishwa
katishwa, la sivyo mgonjwa atakufa kabla hata hiyo dozi yenyewe haijamalizika! Pamoja na kukatisha
katisha huku dawa hizi zinamdhuru mno mtumiaji kiasi kwamba ni kawaida kumkuta amedhofu sana na
nywele zote kichwani zimeng’oka!

Pamoja na mateso anayopata mtumiaji wa dawa hizi, lakini kwa kawaida siyo rahisi mtumiaji kuishi zaidi
ya miaka mitano, tangu aanze dozi! Inasikitisha lakini wenye fani yao wanasema kuwa mgonjwa wa
saratani anayetumia dawa hizi na matibabu ya mionzi, akifanikiwa kuishi hadi akafikia miaka mitano, kwa
wao huyo anahesabika kuwa kapona!

Kundi jingine la dawa zenye madhara makubwa kwa mtumiaji, lakini wanapewa wagonjwa kwa makusudi
ni lile linalojumuisha matibabu ya meno. Hata hivyo Mungu akipenda tutazielezea dawa hizi katika
makala ya peke yake siku nyingine.

Sasa kama hali yenyewe ndiyo hii, je, mtu ukiumwa unapaswa kuchukua hatua gani? Kwa kweli ukiumwa
unapaswa kumuona daktari. Hata hivyo ni muhimu ukajua kuwa una haki ya kumuuliza daktari wako
maswali mengi kadri inavyowezekana ili ujiridhishe kuwa tiba atakayokupatia ni sahihi na haitakuwa na
madhara kwako.

Iwapo daktari atashindwa kujibu maswali yako, muombe radhi na ujaribu kuonana na daktari mwingine.
Kama una uwezo siyo vibaya ukaonana na daktari wa tatu na ukajaribu kupima na kulinganisha ushauri
ulioupata toka kwa kila mmoja. Utashangaa ni kwa kiasi gani maoni ya madaktari utakaowaona
yanavyoweza kuwa na tofauti kubwa.

Ni vizuri pia ukatafuta ushauri wa madaktari wa mifumo mingine ya tiba. Faida kubwa utakayopata hapa
ni kuwa mifumo mingine ya tiba ni yenye kulenga kuondoa kiini cha tatizo, badala ya kuhangaika na
tatizo lenyewe.

Kwa mfano, badala ya mtu mwenye cholesterol nyingi kwenye damu yake kupewa Statins, madaktari wa
mifumo hii watataka kujua ni kwa nini ini lake linazalisha cholesterol nyingi kuliko kawaida, na
wakishaijua sababu watajua ni nini cha kurekebisha, ili ini lako lirejee katika uzalishaji wa cholesterol wa
kiwango cha kawaida. Tafadhali kumbuka kuwa afya ni ya kwako hivyo una wajibu, haki na uhuru wa
kuchagua tiba itakayoiendeleza afya hiyo na siyo kuisambaratisha.

You might also like