You are on page 1of 6

CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)

KAMATI YA WABUNGE WA CHAMA CHA


MAPINDUZI (CAUCUS)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


____________________

Ndugu wana habari, mnamo tarehe 8 Januari, 2019, Spika wa


Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Job
Yustino Ndugai (Mb) kwa mamlaka aliyopewa kwa mujibu wa
Kanuni ya 4 fasili ya (1) (a) ya Nyongeza ya Nane ya Kanuni za
Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016 aliagiza Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad
afike mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili
ahojiwe. Wito huo unatokana na kauli zake za kudharau na
kudhalilisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika
maelezo yake akiwa nchini Marekani alipohojiwa na Idhaa ya
Kiswahili ya Sauti ya Umoja wa Mataifa (UN).

Ndugu wana habari, baada ya maelekezo hayo ya Mheshimiwa


Spika yapo mambo kadha wa kadha yaliyojitokeza ambayo tuko
hapa mbele yenu nasi tuweze kuyazungumzia ili wananchi wapate
kuyaelewa kutokana na upotoshaji mkubwa wa jambo hili.

1. Jambo la kwanza ni kuhusu wito wa Spika kwa CAG.


Ndugu wana habari, kama tulivyoeleza hapo juu, kwa mujibu
wa Kanuni ya 4 (1) (a) ya Nyongeza ya Nane ya Kanuni za
Kudumu za Bunge, Mheshimiwa Spika anayo mamlaka ya
kumwita mtu yeyote kufika mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na
Madaraka ya Bunge kwa kwa ajili ya kuhojiwa kuhusu masuala
yanayohusu haki, kinga na madaraka ya Bunge.

1
Baada ya agizo la Mheshimiwa Spika, Katibu wa Bunge
alielekezwa kuandaa hati ya kumuita CAG ili afike mbele ya
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge tarehe 21
Januari, 2019. Wito huo ulitolewa chini ya kifungu cha 15 cha
Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za Bunge, Sura ya 296 [The
Parliamentary Immunities, Powers and Privileges Act, CAP. 296
R.E. 2015] ambacho kinaeleza kuwa Kamati inayo mamlaka ya
kumwita mtu yeyote kufika mbele yake na kutoa maelezo au
ushahidi wa jambo lolote lililotokea.

Ndugu wana habari, sisi Wabunge wa Chama cha Mapinduzi


(CCM) tunampongeza sana Prof. Mussa Assad (CAG) kwa
kuitikia wito wa Kamati licha ya kuwepo propaganda za watu
mbalimbali zilizoenezwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari
na mitandao ya kijamii zilizolenga kupotosha suala hili.
Upotoshaji huo ulieleza maneno mengi kwamba CAG anayo
kinga na hivyo hawezi kuitwa mbele ya Kamati ya Maadili ya
Bunge. Kwa kutambua kwamba hakuna mtu yeyote aliye juu ya
sheria, CAG amepuuza propaganda hizo na kuamua kutii sheria
na mamlaka ya Bunge kwa kuitikia wito wa kuhojiwa na Kamati
ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.

Tunapenda kutumia fursa hii kumpongeza sana kwa uungwana


wake na nia ya kutii wito wa mamlaka ya Mheshimiwa Spika na
Bunge. Sisi Wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ndani ya
Bunge la Jamhuri ya Muungano tuna imani kuwa hatua hii
itaendelea kudumisha na kuboresha mahusiano mazuri ya Ofisi
ya CAG na Ofisi ya Bunge katika kutumikia umma wa

2
Watanzania, kama CAG mwenyewe alivyoeleza kwenye taarifa
yake kwa vyombo vya habari tarehe 17 Januari, 2019.
Aidha, tunapenda kutumia fursa hii kumpongeza Mheshimiwa
Spika kwa jitihada zake za kulinda heshima ya Mhimili wa
Bunge kwa kusimamia Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki za
Bunge.

2. Jambo la pili linahusu hatua alizochukua Mhe. Zitto


Kabwe Ruyagwa (Mb) kuzuia mamlaka ya Mheshimiwa
Spika kutekelezwa
Ndugu wana habari, katika hatua ya kushangaza na iliyo
kinyume cha sheria tajwa, Mhe. Zitto Kabwe (Mb) akishirikiana
na baadhi ya wanasheria, walifanya jitihada za kuzuia mamlaka
ya Spika kutekelezwa. Moja ya jambo walilofanya ni kufungua
kesi katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam ili kuzuia
CAG asihojiwe na Bunge. Kesi hiyo ilitupiliwa mbali kwa kukosa
vigezo vya kusikilizwa mahakamani.

Vilevile Mbunge huyo aliandika barua kwa Katibu Mkuu wa


Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA) na pia, Mhe. Zitto
alituma nakala kwa Maspika wa Mabunge yote ya Afrika kwa
nchi wanachama wa Jumuiya ya madola na Maendeleo ya Nchi
za Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC) pamoja na Wadhibiti
na Wakaguzi Wakuu wa Hesabu za Serikali wa Jumuiya ya
Madola.

Ndugu wana habari, kitendo hicho cha Mhe. Zitto ambaye ni


Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mbali
na kwamba ni kinyume cha sheria za nchi na Kanuni za Bunge,
pia ni kitendo cha kudharau mamlaka ya Mheshimiwa Spika.
3
Mhe. Zitto Kabwe kama Mbunge wa Kambi ya Upinzani
Bungeni, anayo nafasi kupitia Kiongozi wa Kambi hiyo
kumshauri Mheshimiwa Spika katika Kamati ya Uongozi kuhusu
uendeshaji wa shughuli za Bunge kama inavyoelekeza Kanuni
ya 2 (3) ya Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge.
Kitendo cha Mhe. Zitto kukimbilia mahakamani kupinga
mamlaka ya Spika, au kuandika barua kwa Mabunge ya nchi
nyingine akipinga uamuzi wa Mheshimiwa Spika, au kujadili
mamlaka yake kwenye vyombo vya habari na mitandao ya
kijamii ni dharau kubwa kwa Mamlaka ya Spika na Mhimili wa
Bunge kwa ujumla.
Ndugu wana habari, Kanuni ya 5 (4) na (5) ya Kanuni za
Kudumu za Bunge imeweka utaratibu ambao Mbunge ambaye
hakuridhishwa na uamuzi wa Spika anaweza kupinga uamuzi
huo. Mbunge atawasilisha sababu za kutoridhiswa kwake kwa
Katibu wa Bunge na malalamiko hayo yatafanyiwa kazi na
Kamati ya Kanuni za Bunge na baade Bunge litajulishwa kuhusu
uamuzi utakaotolewa.

Mhe. Zitto Kabwe ni Mbunge mkongwe ambaye anazielewa


taratibu za Kikanuni zinazosimamia shughuli za Bunge. Kama
hakuridhika na uamuzi wa Spika wa kumuita CAG kwenye
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge alitakiwa
kuzingatia utaratibu huo.

Ndugu wana habari, si mara ya kwanza kwa Mhe. Zitto


kkufanya upotoshaji wa aina hii kwa umma. Hivi karibuni, kwa
kushirikiana na baadhi ya wanasiasa walipeleka mahakamani
kesi Namba 31 ya mwaka 2018 katika Mahakama Kanda ya Dar
es Salaam, kupinga Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya
4
Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018, kesi ambayo nayo ilitupiliwa
mbali kwa kukosa uhalali wa kisheria. Kama tulivyoeleza, huyu
ni Mbunge mkongwe ambaye anazijua vyema taratibu za Bunge
za kujadili na kupitisha Miswada kuwa Sheria. Anajua anayo
fursa ya kulishawishi Bunge lisipitishe Muswada wowote kuwa
Sheria pale ambapo anaona Muswada husika una mapungufu.

Mhe. Zitto Kabwe anajua kuwa Muswada uliosomwa kwa Mara


ya Kwanza Bungeni unapelekwa kwenye Kamati ili kujadiliwa
(Kanuni ya 84 (1) na (2). Na kwamba kwa mujibu wa Kanuni ya
84 (3) Kamati inao uwezo wa kufanya marekebisho katika
Muswada wa Sheria kabla ya kuletwa Bungeni Kusomwa Mara
ya Pili. Na pia Muswada unaposomwa Mara ya Pili Mbunge
anayo nafasi ya kuleta Jedwali la Mabadiliko (Kanuni ya 88 [3]
na kuwashawishi Wabunge wamuunge mkono katika kupitisha
mabadiliko hayo.

Ndugu wana habari, kitendo cha Mhe. Zitto Kabwe kukimbilia


mahakamani wakati anayo fursa kama Mbunge ya kuujadili
Muswada na kuufanyia marekebisho, ni kitendo kinachoonesha
kwamba ana uelewa mdogo wa Kanuni za uendeshaji wa
shughuli za Bunge.

3. Jambo la tatu ni kuhusu taarifa zilizotolewa na baadhi


ya Waheshimiwa Wabunge kuwa Mheshimiwa Spika
amevunja Kamati za PAC na LAAC
Ndugu wana habari, kuna taarifa zilizotolewa na Wabunge
wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwamba, Mheshimiwa
Spika amezivunja Kamati za Bunge zinazosimamia matumizi ya
fedha za umma ambazo ni Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC)
5
na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC). Taarifa hizi
pia zimekuwa zikitolewa na watu mbalimbali na kusambazwa
katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Mhe Zitto
Kabwe amekuwa ni mmoja wa waliopotosha jambo hili katika
mitandao ya kijamii.

Ndugu wana habari, taarifa hizi hazina ukweli wowote.


Tunamshukuru Mheshimiwa Spika kwa kulitolea ufafanuzi
jambo hili kwani ni jambo la kawaida katika utekelezaji wa
shughuli za Bunge na ni la muda tu.

Hivyo basi, tunapenda kuwataarifu kuwa Kamati za PAC na


LAAC hazijafutwa, bali Wajumbe wake wametawanywa katika
Kamati nyingine za Bunge hadi hapo wito wa Mheshimiwa Spika
kwa CAG utakapotekelezwa kwa mujibu wa masharti ya Kanuni
za Bunge.
Hata hivyo, katika utaratibu huu bado hakutakuwa na madhara
yatakayotokana na uamuzi wa Mheshimiwa Spika.
Ndugu wana habari, huo ndio mwisho wa taarifa yetu,
tunawashukuru sana kwa kutusikiliza.

-------------------------------
Jasson Samson Rweikiza (Mb)
KATIBU WA WABUNGE WA CCM
19 Januari 2019

You might also like