Download as docx, pdf, or txt
Download as docx, pdf, or txt
You are on page 1of 7

MADA: Fasihi Elektroniki: Matokeo ya Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia1

Majina ya Mwasilishaji: Wallace Mlaga BA.ED. (UDSM), MA. (UDOM), Mwanafunzi

Shahada ya Uzamivu (PhD), OUT

Cheo: Mhadhiri, Koleji ya Elimu, Chuo Kikuu cha Rwanda

Anwani: P.O.BOX 5039, Kigali

Barua pepe: wmlaga@ur.ac.rw

Simu ya Kiganjani: +250730584970

1
Makala haya yamewasilishwa katika makongamano mawili tofauti: Kongamano la Chama cha Lugha na Fasihi
Tanzania (CHALUFAKITA) lililofanyika Zanzibari Chuo Kikuu cha SUMAIT kuanzia tarehe 3 – 5, Agosti 2017 na
iliwasilishwa katika Kongamano la Kamisheni ya Kiswahili Afrika Mashariki (KAKAMA) lililofanyika Zanzibar kuanzia
tarehe 6 – 8, Septemba 2017

1
1.0. Utangulizi

Tungependa kuanza kwa kuuliza maswali yafuatayo: Je, unakubaliana kwamba kugunduliwa kwa

maandishi na teknolojia ya uchapishaji kulileta sio tu utanzu mpya wa fasihi andishi bali pia vipera na

tanzu mpya za fasihi ambazo hazikuwahi kuwepo hapo kabla? Je, umewahi kujiuliza kwamba maendeleo

ya sayansi na teknolojia hususani katika uga wa elektroniki umesababisha kuibuka sio tu kwa utanzu

mpya wa fasihi?

Uanishaji wa fasihi ya Kiswahili umeshughulikiwa na wataalamu wengi. Miongoni mwao ni pamoja na

Mulokozi (1996) na Wamitila (2003). Wataalamu hawa wamefanya uanishaji wa fasihi ya Kiswahili

na kubainisha mgawanyo tanzu kuu mbili: fasihi simulizi na fasihi andishi. Ijapokuwa

wataalamu wote hawa wanakiri kuwa fasihi ni moja tu bila kujali kuwa ni andishi au simulizi.

Uainishaji unaofanywa na wataalamu hawa haushughulikii tanzu mbalimbali mpya zilizoibuka

kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kutokana na kutozingatia uvumbuzi

uliotokana na sayansi na teknolojia, wataalamu hawa hawabainishi kazi ambazo tukiziangalia

zina sifa zote za kuitwa kuwa ni kazi za kifasihi. Kazi hizi za kifasihi ni pamoja na filamu,

maigizo ya runinga, vibonzo jongefu, futuhi au komedi za runingani, nyimbo za bongofleva, na

michezo ya redioni. Kwa mtazamo wetu, kazi hizi zinapaswa kuangaliwa kama sehemu ya kazi

za fasihi ambazo namna zilivyo leo hii ni matokeo ya maendeleo ya sayansi na teknolojia

hususani katika uga wa elektroniki.

Wapo wataalamu walioangalia athari za sayansi na teknolojia katika fasihi simulizi (Mutembei,
2006; Mrikaria, 2007). Wataalamu hawa wanishia kuangalia zaidi athari iliyoletwa na maendeleo
ya sayansi na teknolojia katika fasihi simulizi. Athari hizo ni pamoja na njia za uhifadhi na
mabadiliko yaliyojitokeza katika uwasikishaji ambapo fanani na hadhira hawalazimika kuwa ana
kwa ana katika eneo moja. Hivyo basi, wataalamu hawa hawapigi hatua zaidi kubainisha tanzu

2
na vipera vipya vilivyoibuka na ambavyo haviingii katika fasihi simulizi wala fasihi andishi,
licha ya kutambuliwa kuwa ni kazi za kifasihi. Tanzu na vipera hivyo ambavyo haviingii katika
fasihi simulizi wala fasihi andishi tunaona vinaangukia katika utanzu mpya ambao tunauita fasihi
elektroniki. Hivyo makala haya yanajikita kubainisha ni kwa nini tunapaswa kuwa na tawi jipya
la fasihi nje ya fasihi simulizi na fasihi andishi.

2.0. Uhalali wa kuwepo kwa Fasihi Elektroniki

Tuna mtazamo wa kwamba fasihi elekroniki inapaswa kutazamwa kama tawi la tatu la fasihi
linalojitegemea kutokana na sababu mbalimbali zinazohalalisha kuwepo kwa tawi hili la fasihi
linalojitegemea. Miongoni mwa sababu hizoni hizi zifuatazo:

Mosi ni kurejelea namna ambavyo fasihi andishi ilivyoibuka. Fasihi andishi iliibuka kutokana na
uvumbuzi na ugunduzi uliofanikisha kuwepo kwa maandishi na teknolojia ya uchapishaji. Hii
ilifanikisha kuibuka kwa fasihi andishi. Kuibuka kwa fasihi andishi kulikuja kusababisha
wanazuoni wa kikoloni kufikia hatua ya kutoikubali fasihi simulizi. Kwao wao, fasihi ilikuwa ni
ile tu iliyoandikwa (Castle, 2007). Hii inadhihirika hata namna ambavyo ilikuwa ni changamoto
katika kuipata istilahi ya Kiingereza inayorejelea fasihi simulizi (Okpewho, 1992). Hivyo
tukijaribu kutaka kukataa kuwepo kwa fasihi elektroniki tutakuwa tumefanya hivyo kwa
kuongozwa na mazoea lakini pia tutakuwa tumefanya kosa lilelile lililofanywa na wakoloni
kutoikubali fasihi simulizi kama utanzu wa fasihi. Hata Madumulla (2009) anabainisha kuwa
riwaya kama kipera cha nathari kiliibuka kutokana na kuvumbuliwa kwa teknolojia ya
uchapishaji. Hivyo tunapaswa kuangalia tanzu na vipera ambavyo vimeibuka kutokana na
maendeleo yaliyofikiwa ya sayansi na teknolojia, hususani katika uga wa elektroniki.

Pili ni mtazamo wetu wa kwamba kuna baadhi ya tanzu au vipera vilivyoibuka kutokana na
maendeleo ya sayansi na teknolojia vinaangukia katika fasihi simulizi au fasihi andishi kwa
upande mmoja, na kwa upande mwingine, kuna tanzu au vipera ambavyo havipaswi kuwekwa
katika fasihi simulizi wala fasihi andishi. Vipera na tanzu hizi zinapaswa kuwekwa katika tawi
au utanzu wa fasihi elektroniki. Hii itasababisha kuwa na tanzu kuu tatu za fasihi: fasihi simulizi,
fasihi andishi, na fasihi elektroniki. Tuchukulie kwa mfano filamu pamoja na vibonzo jongefu,
Je, kuna sababu gani ya kuwekwa katika fasihi simulizi? Au kutotazamwa kuwa fasihi licha ya
kudhihirisha hadithi au simulio ndani yake? Ifahamike vema kuwa vyote hivi vimekuja

3
kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia tu. Hata baadhi ya sifa za msingi za fasihi
simulizi hazijitokezi katika tanzu hizi mbili za fasihi elektroniki. Sifa hizo ni pamoja na kuwepo
ana kwa ana kati ya fanani na hadhira, ushiriki ulio hai wa hadhira, kuruhusu mabadiliko ya papo
kwa papo, kuwa ni mali ya jamii, na kuwasilishwa kwa mdomo. Tunatambua kuwa fasihi
simulizi inaweza kuhifadhiwa katika nyenzo mbalimbali na ikabaki kuwa fasihi simulizi. Kwa
mfano, fasihi simulizi inaweza kuhifadhiwa katika maandishi au nyenzo mbalimbali za
kiteknolojia na badoikabaki kuwa fasihi simulizi. Suala tunalolijadili hapa linavuka mipaka ya
uhifadhi. Hivyo mjadala umeegemea katika kuibuka kwa kazi mpya kabisa za kifasihi ambazo si
matokeo ya mchakato tu wa uhifadhi. Hivyo vipera na tanzu zinazopaswa kuwekwa katika
utanzu wa fasihi elektroniki ni zile tu ambazo ni matokeo ya kuibuka kwa maendeleo ya sayansi
na teknolojia hususani katika uga wa elektroniki. Hii ina maana kwamba pasipokuwepo kwa uga
wa elektroniki hatuwezi kuwa na vipera au tanzu hizi.

Tatu ni mtazamo wetu wa kwamba kuwepo na namna fulani ya mfanano haipaswi kuwa kigezo
cha kuamua fasihi elektroniki iwekwe katika fasihi simulizi au fasihi andishi. Hii ni kwa kuwa
licha ya kuwepo kwa mfanano wa namna fulani baini ya tanzu za fasihi simulizi na fasihi andishi
bado tanzu hizo zinawekwa katika tanzu mbili tofauti za fasihi. Tunaweza kutoa mfano wa
tamthiliya, ambayo ni kipera cha utanzu wa nathari katika fasihi andishi kwa upande mmoja, na
matambiko yanayoangukia katika utanzu wa maigizo wa fasihi simulizi kwa upande mwingine.
Vipera vyote hivi viwili vina sifa ya utamthiliya lakini bado vinawekwa katika tanzu
mbilitofauti. Hatusemi kwamba kufanya hivyo ni kosa. Hiyo imefanyika kwa kuzingatia sifa za
msingi za fasihi simulizi na fasihi andishi. Hivyo licha ya filamu kuwa na sifa ya utamthiliya
haipaswi kuwekwa katika utanzu wa fasihi simulizi wala fasihi andishi. Filamu inapaswa
kuwekwa katika utanzu wa fasihi elektroniki. Hali hii inajitokeza pia kwa utanzu wa maigizo ya
runingani kama utanzu mmojawapo wa fasihi elektroniki. Pia tunaweza kulinganisha kuwepo
kwa kufanana kati ya ushairi simulizi na ushairi andishi. Licha ya kufanana huko, bado
tumeweza kuwa na ushairi andishi na ushairi simulizi. Hivyo basi, hoja yoyote ya kupinga
kuwepo kwa fasihi elektroniki haipaswi kuegemezwa katika kufanana peke yake.

Nne ni kutokana na vipera na tanzu zinazopatikana katika utanzu wa fasihi elektroniki kukidhi
sifa ya kutazamwa kama fasihi. Wamtila (2010:13) anaielezea fasihi kuwa ni “sanaa inayotumia
lugha na ambayo hujishughulisha na binadamu pamoja na maisha yake na huathiri, hugusa, na

4
huacha athari fulani na hupatikana katika umbo linalotambuliwa na jamii”. Kwa kuegemea
katika fasili hii, tunaona kuwa hata vibonzo jongefu vinakidhi sifa zote ambazo zimebainishwa.
Vibonzo hivi jongefu vinadhihirisha kuwa na hadithi ndani yake pamoja na wahusika. Tofauti
yake na hadithi nyingine za fasihi simulizi na fasihi andishi ni katika uwasilishaji wake ambao ni
wa kutumia nyenzo za kielektroniki. Tuna mtazamo pia kwamba hata nyimbo za bongofleva
zinapaswa kutazamwa kama utanzu unaoangukia katika utanzu wa fasihi elektroniki. Hivyo sio
sahihi kuzitazama nyimbo za bongofleva kama kipera tu cha fasihi simulizi. Tunapaswa
kuangalia kama ni utanzu kabisa ulio na vipera vyake na unaoangukia katika fasihi elektroniki.

Hoja ya mwisho lakini sio kwa umuhimu, inahusiana na kuzitazama tanzu za fasihi elektroniki
zenye uhadithi kuwazinazojitokeza katika muundo mahsusi unaoendana na utanzu husika.
Hadithi husika inaweza kuwa imetolewa katika riwaya, pamoja na hayo, itafanyiwa mabadiliko
makubwa ili iwe filamu au maigizo ya runingani. Hivyo, huwezi ukasema kuwa riwaya husika
imehifadhiwa tu katika filamu au maigizo ya runingani. Hali hiyo ndiyo inatufanya tufikirie
kuwa na utanzu wa tatu wa fasihi, tofauti na mgawanyo wa kimapokeo ambao tumekuwa nao
kwa muda mrefu. Mgawanyo wa kimapokeo unakuwa kikwazo katika kuyaona maendeleo ya
fasihi ya Kiswahili na fasihi kwa jumla. Hii ndio sababu tumesema kwamba tusipotambua fasihi
elektroniki tutakuwa tumeingia katika mwelekeo uleule uliofanywa na wasomi wa kikoloni
wakuwa na kigugumizi katika kutambua fasihi simulizi kama ni sehemu ya fasihi. Hivyo kama
ni kupinga tujiegemeze katika kuonesha ni kwa namna gani tunadhania kuwa fasihi elektroniki
sio fasihi.

3.0. Tanzu za Fasihi Elektroniki

Licha ya kwamba sio madhumuni ya makala haya kujadili tanzu na vipera vya fasihi elektroniki,
kuna haja ya kubainisha kwamba fasihi elektroniki inaundwa na vipera na tanzu kadhaa.
Tunafanya hivi kwa ajili tu ya kuanzisha mjadala wa kubainisha tanzu na vipera vya fasihi
elektroniki.Kwa mtazamo wetu tunaonamaoni kwamba kazi zifuatazo za kifasihi ni miongoni
mwa tanzu za fasihi elektroniki: filamu, vibonzo jongefu, bongofleva, maigizo ya runingani, na
michezo ya redioni. Tanzu hizi pia huweza kuwa na vipera vyake. Vipera vya tanzu hizi
hutokana na kuwepo kwa aina mbalimbali za miundo katika utanzu husika. Kwa mfano, kuna
aina mbalimbali za filamu. Aina hizi za filamu ndizo zinapaswa kutazamwa kama vipera vya
filamu. Pia kuna aina mbalimbali za maigizo ya runingani. Hivyo aina hizi mbalimbali za

5
maigizo ya runingani ndiyo inapaswa kutazamwa kama vipera vya maigizo ya runingani. Vivyo
hivyo kuna aina mbalimbali za bongofleva, aina hizi ndio zinapaswa kutazamwa kama vipera
vya bongofleva.

4.0. Hitimisho

Baada ya kuona hoja mbalimbali zinazoonesha uhalali wa kuwepo kwa tawi la tatu la fasihi,
yaani utanzu wa fasihi elektroniki, kazi iliyobakia ni kuweza kuzibainisha kwa kina tanzu na
vipera mbalimbali vya utanzu huu wa fasihi elektroniki. Pamoja na hayo, ni muhimu kubainisha
kwamba kutambuliwa kwa utanzu huu utakuwa na manufaa makubwa sio tu katika uga wa
fasihi, bali pia ni kuwafungulia milango ya kujiajiri wanafunzi wa fasihi ya Kiswahili. Zaidi ya
hivyo, itachangia kuinua ubora zaidi hususani katika tasnia ya filamu. Hivyo tunamtazamo wa
kwamba wakati sasa umefika wa kuitazama upya fasihi ya Kiswahili kwa kuendana na
maendeleo ya sayansi na teknolojia yaliyofikiwa. Hili linawezekana tu iwapo tutaimulika vema
fasihi ya kielektroniki.

MAREJELEO

Castle, G. (2007). The Blackwell Guide to Literary Theory. Blackwell Publishing: USA.

Earnshaw, S. (Ed.) (2007). The Hand Book of Creative Writing. Edinburgh University Press:

Edinburgh.

Madumulla.J.S (2009). Riwaya ya Kiswahili: Nadharia, Historia na Misingi ya

Uchambuzi.Mture Educational Publishers Ltd. Dar es salaam.

Mrikaria, E. S. (2007). Fasihi Simulizi na Teknolojia Mpya katika Swahili Forum, Juz. 14, Kur.

197 – 206.

Mulokozi, M. M. (1996). Utangulizi wa fasihi ya Kiswahili: OSW 105. Chuo Kikuu Huria

cha Tanzania. Dar es salaam.

6
Mutembei, A. K. (2006). Nadharia ya Fasihi Simulizi na Maendeleo Katika Sayansi na

Teknolojia katika Mulika, JUZ. 27, Kur. 1 – 17.

Okpewho, I. (1992). African Oral Literature.Indiana University Press. USA.

Wamitila, K. W. (2010). Kichocheo cha Fasihi: Simulizi na Andishi (Chapa ya tano). Focus

Publication. Nairobi.

You might also like