Rasimu Ya Tamko Tahadhari Ya Ebola Agosti 2018

You might also like

Download as pdf or txt
Download as pdf or txt
You are on page 1of 7

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA


WATOTO

TAMKO KUHUSU UGONJWA WA EBOLA ULIOTOKEA KATIKA


NCHI JIRANI YA JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA KONGO

Utangulizi
Ndugu wanahabari,
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
inaendelea kutoa taarifa kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika
nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Nchi hiyo ya
DRC imetangaza tena kuwa na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola mnamo
tarehe 1 mwezi Agosti, 2018, ambapo jumla ya wagonjwa 26 na vifo 10
vilitolewa taarifa na wagonjwa 4 kati yao walithibitishwa kimaabara kuwa
na ugonjwa wa Ebola. Wagonjwa hawa wametokea katika vijiji/Maeneo
ya Mangina ikiwa ni kama km 30 tu magharibi mwa mji wa Beni kwenye
jimbo la Kivu Kaskazini linalopakana na nchi ya Uganda ikiwa ni kama
km 100 tu, na pia likiwa karibu sana na nchi ya Rwanda.
1
Huu ni mlipuko wa 10 wa ugonjwa wa Ebola kutokea nchini DRC, na
umetokea wiki moja baada ya nchi hiyo kutangaza kuisha kwa mlipuko
mwingine uliotokea mwezi Mei mwaka huu ambao ulikuwa katika jimbo
la Equator, Magharibi mwa DRC, umbali wa zaidi ya km 2,000 kutoka
eneo la huu mlipuko mpya uliotokea.

Ndugu wanahabari,

HADI SASA HAPA NCHINI TANZANIA HAKUNA MGONJWA


YOYOTE ALIYEHISIWA AU KUTHIBITISHWA KUWA NA VIRUSI VYA
EBOLA. Hata hivyo, kugunduliwa kwa ugonjwa huu kwenye jimbo la
Kivu Kaskazini linalopakana na nchi za Uganda na Rwanda ni jambo la
kutuweka kwenye wasi wasi kwani eneo hili liko karibu sana na nchi
yetu kuliko eneo lingine lolote ambako ugonjwa huu umeshawahi
kutokea kwenye nchi ya DRC. Hivyo nchi yetu ipo hatarini kuambukizwa
ugonjwa huu kutokana na ukaribu na muingiliano wa watu, hasa
kuhusiana na wasafiri wanaotoka na kuingia hapa nchini.

Kwa sababu hizi, watanzania hatuna budi kuchukua tahadhari ya hali ya


juu ili kujikinga na kudhibiti na ugonjwa wa Ebola. Hivyo Wizara
inapenda kutoa tahadhari ya ugonjwa huu kwa wananchi wote katika
Mikoa yote ya Tanzania, lakini hasa ile inayopakana na nchi jirani za
DRC, Uganda na Rwanda. Mikoa hiyo ni pamoja na Mwanza, Kagera,
Kigoma, Katavi, Rukwa na Songwe. Aidha tahadhari na hatua stahiki
zichukuliwe katika maeneo yote ya mipakani ambapo abiria wanaingia
nchini kutoka nchi jirani.

2
Ugonjwa wa Ebola

Ugonjwa wa Ebola husababishwa na virusi vya Ebola ambavyo


huambukiza kwa njia zifuatazo;

• Kugusa Damu au majimaji kutoka kwa mtu aliyeambukizwa


ugonjwa huo,

• Kugusa maiti ya mtu aliyekufa kwa ugonjwa huo,

• Kugusa wanyama (Mizoga na wanyama wazima) walioambukizwa


kama vile Sokwe na Swala wa msituni.

Dalili za Ugonjwa

Dalili za Ugonjwa huanza kuonekana kwa mtu aliyeambukizwa baada


ya siku 2 hadi 21 tangu kupata maambukizi. Dalili hizo ni pamoja na;

1. Homa kali ya ghafla,


2. Kulegea kwa mwili,
3. Maumivu ya misuli,
4. Kuumwa kichwa na vidonda kooni.
5. Mara nyingi dalili hizo hufuatiwa na kutapika, kuharisha, vipele vya
ngozi na pia figo na Ini kushindwa kufanya kazi.
6. Kwa baadhi ya wagonjwa kutokwa na damu ndani na nje ya mwili.

3
Namna ya Kujikinga na ugonjwa wa Ebola:

Ugonjwa wa Ebola unaweza kuzuilika. Njia kuu za kujikinga na ugonjwa


huu ni:-

Kuepuka kugusa au kuingiwa na mate, damu, mkojo, jasho, kinyesi,


machozi na majimaji mengine yanayotoka mwilini mwa mgonjwa
mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola

o Kuepuka kushughulikia maiti ya mtu aliyefariki akiwa na dalili za


Ebola; badala yake watoe taarifa kwa uongozi wa kituo cha
huduma za Afya kwa ushauri.
o Kuepuka kula nyama za Wanyama wa porini kama sokwe, swala
na popo na pia kugusa mizoga ya Wanyama hao
o Kuepuke mila na desturi zinazoweza kuchelewesha kupata
huduma muhimu na kuzidi kueneza ugonjwa wa Ebola.
o Kuzingatia usafi wa mwili
o Kutoa taarifa mapema kwa viongozi wa Serikali na wa huduma za
Afya katika ngazi zote pale anapotokea mtu mwenye dalili za
Ebola.
o Kuwahi katika vituo vya huduma za Afya pale mtu anapoona dalili
za ugonjwa huu.

4
Hatua zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na Wizara
kufuatia kupatikana kwa taarifa ya Ugonjwa huu huko DRC

Kufuatia kuwepo kwa taarifa hizi tangu mwezi Mei 2018, hatua zifuatazo
zinaendelea/zimechukuliwa na Wizara ili kujiandaa kukabiliana na
mlipuko huo:
1. Kufanya tathmini ya utayari wa kukabiliana na ugonjwa wa Ebola
nchini (Operational readiness assessment) kwa nchi nzima kwa
kushirikiana na WHO na kuainisha mapungufu ambayo
yanapaswa kufanyiwa kazi. Mapungufu hayo yanaendelea
kuyafanyiwa kazi ili kujenga uwezo na utayari katika nchi yetu.

2. Tumetengeneza mpango mkakati wa kujiandaa na kupambana na


mlipuko wa Ebola endapo utatokea nchini (Costed Ebola
Contingency Plan). Mpango huu umeandaliwa kwa kushirikiana
na WHO. Mpango umeainisha maeneo ya kujenga uwezo kwa
wakati huu wa kujiandaa, pamoja na hatua za kuchukua endapo
ugonjwa utaingia ikiwa ni pamoja na gharama zake.

3. Tumefanya mafunzo ya Timu za dharura (Rapid Response


Teams) ngazi ya Taifa na katika Mikoa ya Dar es Salaam,
Songwe, Rukwa, Katavi, Kigoma na Kagera

4. Tumeimarisha ufuatiliaji wa wasafiri mipakani (travellers entry


screening) kwa kutumia vifaa vya kupima joto la mwili (thermo
scanners) na fomu maalum za wasafiri

5
5. Wizara imepokea vifaa vya kukabiliana na Ebola kutoka WHO
vikiwemo; Thermo scanners, Vifaa Kinga, au PPE, kama vile
gloves, body bags, vifaa vya ufungashaji wa sampuli nk. Vifaa
hivyo vimeanza kusambazwa mikoani kupitia MSD

6. Uelimishaji wa umma umefanyika na unaendelea kufanyika kwa


kupitia vyombo vya habari vya kitaifa na kijamii, na mitandao ya
kijamii. Vile vile vipeperushi na mabango vinaendelea kuandaliwa

7. Vikao vya uratibu vimefanyika katika ngazi ya taifa na mikoa


ambayo ipo katika hatari zaidi. Pia ufuatiliaji wa karibu
unaendelea kupitia Kituo cha ufuatiliaji wa magonjwa ya dharura
cha Wizara (Public Health Emergency Operation Centre is on
“ High Alert” )

8. Wataalam kutoka ngazi ya Taifa kwa sasa wako katika mikoa ya


Kigoma Katavi Rukwa Kagera Kilimanjaro Mwanza Songwe na
Mbeya kufanya tathmini ya utayari katika ngazi ya mikoa na
Wilaya (Readiness Assessment)

9. Maandalizi yanaendelea kwa ajili ya kutekeleza kazi nyingine


kama ifuatavyo:

a. Kufanya mafunzo katika mikoa iliyo salia ikiwemo Mwanza,


Kilimanjaro na Mbeya ambayo imesalia katika ile mikoa nane
iliyo katika hatari zaidi

b. Mafunzo ya waandishi wa habari 30 (media orientation)

6
c. Zoezi la udhibiti wa matukio ya dharura (simulation exercise)
katika ngazi ya Taifa

d. Mafunzo kwa wasfirishaji wa sampuli kwenda katika maabara

Hitimisho

Nawaomba Wakuu wa Mikoa na Waganga Wakuu wa Mikoa na


Halmashauri wote nchini kuchukua Tahadhari na kuendelea kuelimisha
wananchi wote juu ya ugonjwa huu na kuwataka kutokuwa na hofu ila
kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huu kwani
mpaka sasa hakuna mtu aliyethibitishwa kuugua ugonjwa huu
hapa nchini.

Aidha Wizara itaendelea kushirikiana na sekta mbalimbali katika


kuimarisha ufuatiliaji na kuendelea kutekeleza mikakati ya kudhibiti ili
ugonjwa huu usiingie nchini. Vilevile Wizara itaendelea kutoa taarifa
pamoja na Elimu kwa Jamii kadri itakavyohitajika.
Imetolewa na

Ummy A. Mwalimu (Mb)


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto
10/08/2018

You might also like