Download as pdf or txt
Download as pdf or txt
You are on page 1of 5

SOMO: MEZA YA BWANA (USHIRIKA MTAKATIFU)

MAANDIKO YA SOMO: 1 Wakorintho 11:23-34

“Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule
aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili
wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Na vivi hivi baada ya kula
akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi
kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu. Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea
kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo. Basi kila aulaye mkate huo, au
kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na
damu ya Bwana. Lakini mtu ajihoji mwenyewe, na hivyo aule mkate, na kukinywea kikombe.
Maana alaye na kunywa, hula na kunywa hukumu ya nafsi yake, kwa kutokuupambanua ule
mwili. Kwa sababu hiyo wako wengi kwenu walio hawawezi na dhaifu, na watu kadha wa
kadha wamelala. Lakini kama tungejipambanua nafsi zetu, tusingehukumiwa. Ila
tuhukumiwapo, twarudiwa na Bwana, isije ikatupasa adhabu pamoja na dunia. Kwa hiyo,
ndugu zangu, mkutanikapo mpate kula, mngojaneni; mtu akiwa na njaa, na ale nyumbani
kwake; msipate kukutanika kwa hukumu. Na hayo yaliyosalia nijapo nitayatengeneza.”

UTANGULIZI

Katika Kanisa la Agano Jipya sawa sawa na kanisa la siku hizi, MEZA YA BWANA
inajulikana kwa majina mbalimbali. Mtume Paulo aliita “chakula cha Bwana” kwa sababu
Wakristo walitekeleza karamu hiyo kwa kufuatana na agizo la Bwana Yesu na kwa heshima
yake.

1 Wakorintho 11:20 “Basi mkutanikapo pamoja haiwezekani kula chakula cha Bwana”

Meza ya Bwana pia inaitwa “ushirika” kwa sababu ni tendo la kushirikiana, baina ya waamini
pamoja na kristo.

1 Wakorintho 10:16 “Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, je! Si ushirika wa damu ya
Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo?”

Pia katika kitabu cha matendo ya Mitume ibada nzima ya Meza ya Bwana inaitwa “kumega
mkate”.

Matendo 2:46 “Na siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, wakimega mkate
nyumba kwa nyumba, na kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa moyo mweupe,”

Matendo 20:7 “Hata siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo
akawahutubu, akiazimu kusafiri siku ya pili yake, naye akafuliza maneno yake hata usiku wa
manane”
Bwana Yesu alianzisha na kuagiza Chakula cha Bwana au Ushirika mtakatifu alipokula karamu
ya Pasaka pamoja na wanafunzi wake usiku ule kabla ya kusulibiwa kwake.

Luka 22:8-20 “Akawatuma Petro na Yohana, akisema, Nendeni, mkatuandalie pasaka tupate
kuila. Wakamwambia, Wataka tuandae wapi? Akawaambia, Tazama, mtakapoingia mjini
mtakutana na mwanamume akichukua mtungi wa maji; mfuateni mkaingie katika nyumba
atakayoingia yeye. Na mtamwambia mwenye nyumba, Mwalimu akuambia, Ki wapi chumba
cha wageni, nipate kula pasaka humo pamoja na wanafunzi wangu? Naye atawaonyesha
chumba kikubwa orofani, kimekwisha andikwa; andaeni humo. Wakaenda, wakaona kama
alivyowaambia, wakaiandaa pasaka. Hata saa ilipofika aliketi chakulani, yeye na wale mitume
pamoja naye. Akawaambia, Nimetamani sana kuila pasaka hii pamoja nanyi kabla ya
kuteswa kwangu; kwa maana nawaambia ya kwamba siili tena hata itakapotimizwa katika
ufalme wa Mungu. Akapokea kikombe, akashukuru, akasema, Twaeni hiki, mgawanye ninyi
kwa ninyi; Maana nawaambia ya kwamba tangu sasa sinywi mazao ya mzabibu hata ufalme
wa Mungu utakapokuja. Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, Huu
ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Kikombe
nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu,
inayomwagika kwa ajili yenu.”

Kila mwaka tangu wakati wa kitabu cha kutoka hadi wakati wa kusulibiwa kwa Yesu, wayahudi
walikuwa wanasherehekea pasaka ili kukumbuka juu ya usiku ule ambapo malaika wa kifo
alipita juu ya milango iliyokuwa imetiwa damu katika misri. Katika Agano Jipya Mwanakondoo
wa Mungu Mwenyewe yaani Yesu kristo alikuwa achinjwe kwa ajili ya kutimiliza yote ya
sikukuu hiyo.

1 Wakorintho 5:7 “Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya,
kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa
sadaka, yaani, Kristo”

MEZA YA BWANA NI IBADA YA KUMBUKUMBU YA KIFO CHA YESU

Meza ya Bwana ni ibada ambayo Yesu aliliagiza Kanisa liendelee kuitekeleza kama ukumbusho
wa mateso na kifo chake msalabani. Luka 22:19 “…Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu”
Tunaposhiriki meza ya Bwana kunatufanya tumkumbuke Yesu kama Mwanakondoo
aliyechinjwa na kwamba maisha yake yote yalikuwa ni sadaka ambayo ilitolewa na Mungu kwa
ajili ya dhambi zetu.
MEZA YA BWANA HUASHIRIA USHIRIKA ULIOPO BAINA YA WAAMINI
PAMOJA NA YESU KRISTO MWENYEWE

Mbali na kuwa sababu ya mafarakano baina ya wakristo kama ilivyotokea kwa Kanisa la
Wakorintho, Meza ya Bwana ni ibada ya kuwaunganisha wakristo kuwa kitu kimoja.
Tunaposhiriki katika kula sehemu ya mkate mmoja na kunywa divai moja tunaonyesha ushirika
wetu kama wakristo pamoja na kristo. Hii huonyesha kuwa tumeunganika sisi kwa sisi pamoja
na kristo katika mwili mmoja (1 Wakorintho 10:17, 1 Wakorintho 11:18-21).

Bwana Yesu alikuwepo mwenyewe kwenye kile chakula cha kwanza na yeye yupo kila mara
wawili au watatu wa watoto wake wanapokutana kwenye meza ya ushirika kwa pamoja
(Mathayo 18:20). Hivyo lazima tukumbuke kuwa kila tunaposhiriki meza ya Bwana Yesu
mwenyewe huwa yupo pale pamoja nasi katika ibada hii. Mioyo yetu inatakiwa kuwa wazi
wakati tunaposhiriki Meza ya Bwana ili tuweze kumtambua kristo aliye kati yetu.

Hivyo Meza ya Bwana inatakiwa kuwa mkutano wa ushirika kwa maana ushirika wetu ni
pamoja na Baba na Mwana wake, pamoja na Roho Mtakatifu na washirika wengine wa Kanisa(1
Yohana 1:3).

VIFAA VITUMIKAVYO KATIKA MEZA YA BWANA

Luka 22:19-20 “Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, Huu ndio mwili
wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Kikombe nacho vivyo
hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu,
inayomwagika kwa ajili yenu.”

MKATE (MFANO WA MWILI WA YESU)

Yesu kristo alijifananisha na mkate pale aliposema kuwa yeye ndiye mkate wa uzima. Pia katika
kuagiza utekelezaji wa meza ya Bwana, Yesu alitumia mkate kama mfano wa mwili wake ambao
angeutoa uuawe kama sadaka. Mkate unaotumika katika meza ya Bwana huwa ni kielelezo au
mfano tu wa mwili wa kristo ulioteswa pale msalabani na si mwili halisi wa Yesu.
Tunapochukua ule mkate wa kawaida na kuuombea kwa ajili ya matumizi ya meza ya Bwana,
mkate ule huwa haubadiliki dhahiri kuwa nyama ya mwili wa Yesu bali hubadilika kutoka mkate
wa kawaida wenye kuliwa na mtu yeyote na kuwa mkate uliowekwa wakfu na kujaa Baraka za
kiroho na nguvu za Mungu wenye kuliwa na wale waliomwamini Yesu tu kuwa Bwana na
Mwokozi wa maisha yao na kuendelea kuishi maisha safi yaliyotengwa na dhambi. Hivyo
tunapochukua ule mkate uliovunjwa wakati wa meza ya Bwana na kula huwa ni mfano wa
kutukumbusha juu ya mwili wa Kristo uliotolewa msalabani kama sadaka kwa ajili ya msamaha
wa dhambi.
DIVAI (MFANO WA DAMU YA YESU)

Divai itumikayo wakati wa meza ya Bwana ni mfano wa Damu ya Yesu iliyomwagika msalabani
kwa ajili ya ondoleo la dhambi.

Walawi 17:11 inatuonyesha kuwa uhai wa kitu umo katika damu yake. Damu ya kitu
inapomwagwa, huashiria kutoa uhai wa kitu hicho. Katika Agano la kale Mungu aliwaagiza
wanadamu kutoa uhai wa wanyama kuwa fidia au kipatanisho kwa ajili ya dhambi zao.

Katika Agano Jipya Yesu alitolewa kuwa sadaka ya dhambi za watu wote na hivyo akachukua
nafasi ya wanyama ili kwamba wanadamu wasiendelee kuchinja na kutumia damu ya wanyama
tena.

Nguvu ya kutakasa ya damu ya Yesu inaletwa mbele ya mawazo yetu kila wakati tunaposhiriki
meza ya Bwana. Wakati wa kutoka misri Mungu aliwaambia waisraeli kuwa “wakati
nitakapoona damu, nitapita juu yake”. Leo hii anatazama kuona kama damu ya Yesu ipo katika
mioyo yetu. Wakati tunapokuja kwenye meza ya ushirika tunapaswa kuomba kwamba mioyo
yetu izidi kutakaswa kwa damu ya Yesu.

MEZA YA BWANA HUTUKUMBUSHA KURUDI KWA YESU

Ahadi nyingine ya thamani sana inaletwa mawazoni mwetu kila wakati tunaposhiriki meza ya
Bwana ni ya kurudi kwa Bwana Yesu kuja kutuchukua tukaishi pamoja naye milele.

1Wakorintho 11:26 “…Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki,
mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo”

Yesu ameliagiza Kanisa kuendelea kufanya kumbukumbu ya kufa kwake kupitia meza ya Bwana
mpaka atakaporudi tena. Hii inamaanisha kwamba meza ya Bwana itakoma baada ya Yesu
kurudi kulichukua Kanisa.

MANUFAA YA KIMWILI YA KUSHIRIKI MEZA YA BWANA

kuna manufaa na faida za kimwili vile vile licha ya kiroho, kama tutaelewa ukweli kwamba
mwili wa kristo ulivunjwa kwa ajili ya kuponywa kwetu. Mkate katika ushirika unazungumzia
mwili ule ulioteseka wa Bwana wetu, ambaye kwa kupigwa kwake tuliponywa. Katika
1Wakorintho 11:30 watu wengine walipata shida ya magonjwa ya kimwili na wengine walikufa
kwa sababu walishindwa kutambua ukweli ule kuhusu maana ya mkate uliovunjwa katika
ushirika.

Kupambanua mwili wa kristo kama inavyoelezwa katika Wakorintho humaanisha kufahamu


kwamba mwili wa Yesu ulikuwa na afya na nguvu, na kwamba Mungu anatutaka tufurahie sifa
ile ile ya afya.
Hivyo basi tunaposhiriki meza ya Bwana, tunapaswa kwa imani kuchukua mkate kama ni mwili
wake Yesu na hivyo tule kwa imani ya kupokea uzima juu ya magonjwa ya kimwili
yatusumbuayo.

HITIMISHO

Ndani ya ushirika wa meza ya Bwana upo uzima, afya na nguvu za Yesu. Hivyo inatubidi tule
kwa imani, tukijitwalia kiasi na ubora wa afya ambao upo ndani ya Yesu kwa ajili yetu.

You might also like