Download as pdf or txt
Download as pdf or txt
You are on page 1of 20

MWONGOZO WA

MWEZESHAJI
UZAZI WA MPANGO
Fuata nyota ya kijani, Upate mafanikio
May 2014

1
MWONGOZO
WA
MWEZESHAJI
UZAZI WA MPANGO
Fuata nyota ya kijani,
Upate mafanikio

2
Yaliyomo
Utangulizi 5

Maelezo kuhusu uzazi wa mpango 5

Mchezo namba moja 7

Majadiliano kuhusu mchezo namba moja 8

Majadiliano kuhusu maana ya uzazi wa mpango 9

Faida za uzazi wa mpango 10

Majadiliano kuhusu mchezo wa ugawaji wa


kipato katika familia (vizibo) 12

Njia za uzazi wa mpango 14

Ukweli kuhusu uzazi wa mpango 16

Hitimisho 18

3
4
SEHEMU YA 1:

UTANGULIZI
Mwezeshaji:
Karibisha washiriki, waeleze kuwa:

Hiki ni kipindi kuhusu uzazi wa mpango. Katika kipindi hiki tutajifunza maana,
faida na njia za uzazi wa mpango pamoja na namna uzazi wa mpango
unavyoweza kuwafanya wenza wakawa na maisha mazuri na ya furaha kwa
pamoja.

Suala hili ni muhimu pia ni nyeti na linaweza kuibua mijadala mingi, hivyo basi,
nawasihi kufuatilia kwa makini na kushiriki pamoja na kuwa huru kuchangia
kwa uwazi wakati wote wa mjadala.

SEHEMU YA 2:

MAELEZO KUHUSU UZAZI


WA MPANGO.
Mwezeshaji:
Waulize washiriki wanajua nini kuhusu uzazi wa mpango na andika
pembeni maelezo ya washiriki.

5
6
SEHEMU YA 3:

ANGALIZO: Mwezeshaji hakikisha kuwa umeandaa


punje 40 za mahindi

MCHEZO NAMBA MOJA


(MOJA YA MAANA NA FAIDA ZA UZAZI WA MPANGO)

Mwezeshaji:
Waeleze washiriki kwa kusema:
Tutajifunza mojawapo ya maana na faida za kupanga uzazi. Katika somo hili
tutacheza mchezo wa upandaji wa mahindi yaliyopandwa katika msimu sahihi,
lakini kwa namna mbili tofauti; moja ni mahindi yaliyopandwa kwa mpangilio
na pili ni yaliyopandwa bila mpangilio. Mchezo huu unaonyesha mojawapo ya
namna ya ustawi wa watoto katika familia.

Namuomba mshiriki mmoja ajitokeze mbele.


Nitampatia punje 20 za mahindi na azipande katika mistari miwili na kwa
kufuata vipimo kati ya punje moja hadi nyingine.

Akishamaliza mruhusu arudi kukaa; kisha endelea kwa kusema:


Namuomba tena mshiriki mwingine. Huyu pia nitampatia punje 20 za mahindi,
naye atazipanda karibu karibu bila kufuata mstari wala vipimo.

Akishamaliza mruhusu arudi kukaa; kisha waulize washiriki:


Mmeona au mmejifunza nini katika mchezo huu?

7
SEHEMU YA 4:

MAJADILIANO KUHUSU
MCHEZO NAMBA MOJA
Mwezeshaji uliza maswali yafuatayo hapo chini. Ukishauliza swali, acha
washiriki watoe majibu yao na kisha uyalinganishe na majibu ya swali
husika yaliopo.

1. Je unadhani hali ya mahindi itakuwaje katika upandaji wa kufuata


mpagilio na vipimo?
Majibu.
• Yatastawi vizuri
• Yatatoa mavuno mengi na ya kutosha

2. Je unadhani mahindi yatakuwaje katika upandaji wa kutokufuata


mpangilio na vipimo?
Majibu.
• Hayatastawi vizuri
• Yatashindania rutuba iliyopo ardhini
• Hayataweza kutoa mavuno mengi na ya kutosha.

3. Kipi kitatokea kama mahindi yatapandwa mapema zaidi na kabla ya


msimu wa mvua?
• Jibu: Hayataweza kustawi vizuri, yanaweza kukauka.

4. (A) Katika aina hizi mbili za upandaji wa mahindi, ni aina ipi ambayo
ungependa kuifuata?
Majibu:
• Aina ya kwanza
• Aina ya pili

(B) Kwa nini umechagua aina hiyo?


• Aina ya kwanza-Kwa sababu yalipandwa kwa nafasi hivyo yatakua
vizuri.
• Aina ya pili-kwa sababu yatakuwa yamebanana hivyo hayatakua vizuri
na kuna uwezekano wa kutotoa mazao ya kutosha.

8
SEHEMU YA 5:

MAJADILIANO KUHUSU
MAANA YA UZAZI WA
MPANGO
1. Ni kwa jinsi gani upandaji wa mahindi kama tulivyoona kwenye mchezo
unalingana na ustawi wa watoto katika familia?

2. Kwa nini kuzaa watoto kwa mpangilio na kwa kupishana ni muhimu?

3. Kwa nini upangaji wa lini kuanza kuzaa watoto ni muhimu?

4. Ni athari gani zinazoweza kutokea kwa mtoto na kwa mama endapo


mama atazaa bila mpangilio wa kupishana mtoto mmoja na mwingine ?

Mwezeshaji:
Sasa waeleze au wasomee washiriki maana halisi ya uzazi wa mpango
kama ilivyo tafasiriwa katika Mwongozo wa Kitaifa wa Ujumbe kuhusu
Uzazi wa Mpango na kitendea kazi cha Mtoa Huduma za Uzazi wa
Mpango.

Uzazi wa Mpango ni uamuzi wa hiari unaofanywa na mtu binafsi, mke/mume/


mwenza/kijana katika kupanga ni lini wapate watoto, idadi ya watoto, baada
ya muda gani na njia ipi ya Uzazi wa Mpango wangependa kutumia.

Uamuzi wa kuanza kuzaa ufanyike katika umri wa kuanzia miaka 20 na


watoto wapishane kwa muda wa miaka mitatu na kuendelea.

9
SEHEMU YA 6:

ANGALIZO: Hakikisha umeandaa kadi 4 na vizibo 80

FAIDA ZA UZAZI WA
MPANGO
Mwezeshaji:
Waeleze washiriki watacheza tena mchezo mwingine ili kujua zaidi faida
za uzazi wa mpango.

Mwezeshaji sema maneno yafuatayo:


Naomba washiriki wanne waje mbele.
Kila mmoja nitampatia kadi inayoonyesha idadi ya watoto atakaokuwa nao.
- Mshiriki namba 1 atakuwa na idadi ya watoto 2
- Mshiriki namba 2 atakuwa na idadi ya watoto 3
- Mshiriki namba 3 atakuwa na idadi ya watoto 5 na
- Mshiriki namba 4 atakuwa na idadi ya watoto 7.

Waeleze pia kuwa: Kila mshiriki nitampatia seti ya vizibo 20 ambavyo


atavitumia kama kipato alichonacho katika kukidhi mahitaji muhimu ya familia
kama vile, MAVAZI, CHAKULA, ADA za shule na MATIBABU.

Baada ya maelezo hayo, mwambie mwenye idadi ya watoto wawili agawe


vijiti hivyo kama ifuatavyo:-
• MAVAZI - Vizibo kimoja kimoja kwa kila mtoto.
• CHAKULA vizibo viwili viwili kwa kila mtoto.
• ADA za Shule vizibo viwili viwili.
• Mshiriki akae na vizibo vinavyobaki

Baada ya mshiriki wa kwanza kumaliza kugawa vizuri,mwezeshaji amuite


mshiriki mwenye watoto watatu naye agawe vizibo kama mshiriki wa
kwanza. Mshiriki wa tatu na wa nne wafanye zoezi kama walivyofanya
mshiriki wa kwanza na wa pili.

Mwezeshaji:
Waeleze washiriki kuwa baadhi ya familia zimeweza kukidhi mahitaji ya
kulipa ada,chakula na mavazi ingawa bado kuna kipengele muhimu cha
matibabu ambacho kinahitaji kutengewa kipato.

10
Mwezeshaji:
Waeleze washiriki kuwa mtoto mmoja miongoni mwa watoto alionao kila
mshiriki anaumwa malaria na anapaswa kulipiwa gharama za matibabu
ambayo yanagharimu vizibo vitatu.

Mwezeshaji:
Waeleze kila mshiriki kugawa vizibo vitatu vitatu kwa kila mtoto mgonjwa.

Matokeo:
Watajikuta mshiriki namba 1 – ametumia vizibo 13 na amebakiwa na vizibo 7
Mshiriki namba 2 – ametumia vizibo 18 na amebakiwa na vizibo 2
Mshiriki namba 3 – watoto wawili waliweza kupata chakula, mavazi na
ada. Mtoto mmoja amepata chakula mavazi na nusu ya ada. Watoto
wawili wamepata mavazi na chakula na wamekosa ada. Mtoto mgonjwa
amekosa matibabu kabisa.
Mshiriki namba 4 – Watoto wote waliweza kupata mavazi, watoto sita
wamepata chakula, mtoto mmoja amepata chakula kidogo. Watoto
wote saba wamekosa ada za shule na mtoto mmoja mgonjwa amekosa
matibabu.
Mshiriki namba 3 na 4 vizibo vyote vitakuwa vimekwisha na wao watakuwa
hawajakamilisha mahitaji kwenye familia zao (mshiriki namba 3 anahitaji
vizibo 28 na mshiriki namba 4 anahitaji vizibo 38 ili kukamilisha mahitaji
yote ya familia zao)

Mwezeshaji waulize washiriki:


Mmejifunza nini katika mchezo huu wa ugawaji wa vizibo?

11
SEHEMU YA 7:

MAJADILIANO KUHUSU
MCHEZO WA UGAWAJI WA
KIPATO KATIKA FAMILIA (VIZIBO)
Mwezeshaji uliza maswali yafuatayo hapo chini. Ukishauliza swali, acha
washiriki watoe majibu yao na kisha uyalinganishe na majibu ya swali
husika yaliopo.

1. Je mshiriki yupi ameweza kuwa na vizibo vya kutosha kwa mahitaji


yote ya watoto? Na mnafikiri ni kwa nini?
• Jibu: Mshiriki namba moja na mbili tu ndiyo wameweza
• Idadi ndogo ya watoto waliokuwa nao.

2. Je ni mshiriki yupi vizibo havikutosha kukidhi mahitaji ya watoto


aliokuwa nao? na mnafikiri ni kwa sababu gani?
Majibu:
• Mshiriki namba tatu na nne.
• Idadi kubwa ya watoto waliokuwa nao.

3. Washiriki waliobakiwa na vizibo wataweza kufanya nini na vizibo hivyo?


• Watavitunza kwa kukidhi matumizi muhimu ya baadaye.
• Wataweza kukidhi mahitaji ya watoto wao kwa kiwango cha kuridhisha
zaidi.

4. Ni changamoto gani mmeziona wakati washiriki wanajaribu kuhakikisha


kuwa watoto walionao wanapata mahitaji kama walivyoelekezwa?
• Idadi kubwa ya watoto
• Hawakuwa na kipato cha kutosha kukidhi mahitaji muhimu
• Kushindwa kuwapatia watoto mahitaji muhimu kama elimu, chakula,
mavazi na matibabu.
• Kukosa Elimu ya Afya ya Uzazi inayopelekea kutopanga uzazi

12
5. Je Changamoto kama hizi zinajitokeza katika jamii yetu?
• Ndiyo
kwa nini?
• mila na desturi zinaruhusu kuwa na watoto wengi
• Sheria ya ndoa inaruhusu mtoto wa kike (umri 15) kuolewa akiwa na
umri mdogo kwa idhini ya wazazi
• Mengineyo

6. Je watu hufanya nini pindi changamoto hizi zinapojitokeza?


(Washiriki wajadili)

7. Je ni hatua gani wenza(baba na mama) wanaweza kuchukua ili


kupunguza changamoto hizi?
(Washiriki wajadili)

Baada ya hayo mwezeshaji sisitiza ujumbe muhimu tunaoupata kupitia


michezo yote miwili:
• Ni muhimu kupanga uzazi
• Watoto wapishane kwa muda usiopungua miaka mitatu
• Uzazi wa mpango huokoa maisha ya watoto na akina mama.
• Uzazi katika umri mdogo unahatarisha maisha ya mama na vile vile ya
mtoto.
• Uzazi wa mpango husaidia:,
1. Kumpunguzia baba, mama/familia mzigo na msongo wa mawazo
unaotokana na ulezi wa familia isiyopangiliwa.
2. Kukuza uchumi na maendeleo ya familia, jamii na nchi
3. Kupunguza idadi ya mimba zisizotarajiwa na kuharibika kwa mimba
4. Kuboresha maisha ya mama, baba, mwenzi na familia kwa ujumla.

13
SEHEMU YA 8:

NJIA ZA UZAZI WA MPANGO


Mwezeshaji:
Waeleze washiriki kuwa:

Kila mtu ana haki ya kupanga idadi ya watoto ambayo yeye na mwenza
wake wanahitaji kuzaa na kwa wakati gani. Katika sehemu hii tutaona na
kujifunza njia mbalimbali za uzazi wa mpango ambazo wenza wanaweza
kuchagua.

Swali: Ni njia zipi za uzazi wa mpango mnazozifahamu?


Hakikisha kwamba washiriki wote wanachangia kujibu swali

Baada ya kuwa wamezitaja, kwa kutumia kadi 10 (A4) mwezeshaji anza


kuonyesha njia za uzazi wa mpango moja hadi nyingine kama ilivyo kwenye
kadi.

Mwezeshaji:
Baada ya kumaliza kuwaonyesha, waeleze washiriki kuwa pamoja na kuwa
kuna njia nyingi za uzazi wa mpango, njia zote hizi zimegawanyika katika
makundi matatu:
• Kuna njia za muda mfupi.
• Njia za muda mrefu na
• Njia za kudumu.

Pia waeleze kuwa;


• Njia zote za asili (unyonyeshaji na kuhesabu shanga) ni za muda mfupi.
• Vidonge, Sindano, Kondomu za kike au za kiume pia ni njia za muda
mfupi.
• Lupu na Vipandikizi (vijiti) ni njia za muda mrefu.
• Njia za kudumu ni kufunga kizazi kwa mwanamke au kufunga uzazi kwa
mwanaume na ni njia ambayo wenza hawahitaji tena kuzaa.

14
15
SEHEMU YA 9:

UKWELI KUHUSU UZAZI WA


MPANGO
Mwezeshaji:
Waeleze washiriki kuwa watasikia misemo ya kuhusu uzazi wa mpango na
kisha wataijadili kama ni ya kweli au si ya kweli na kwa nini? Mwezeshaji
baada ya kusoma kila usemi waruhusu washiriki wajadili kwa pamoja na
kisha wafafanulie maneno yaliyopo katika kila usemi.

Msemo namba 1.
Uzazi wa mpango si jukumu la wanawake tu.
• Matumizi ya njia za uzazi wa mpango ni jukumu la wote yaani akinababa,
akinamama na vijana. Ni hiari ya mtu au wenza kuamua njia ipi ya uzazi
wa mpango wanaipenda kuitumia baada ya kupata ushauri toka kwa
wataalam. (wajadili kwa pamoja ni lini waanze kuzaa, wazae watoto
wangapi, wapishane kwa muda gani na lini waache kuzaa, waende kwa
pamoja kupata ushauri na elimu ya njia za uzazi wa mpango n.k)

Msemo namba 2.
Si wanawake walioolewa tu ndiyo wanapaswa kutumia njia za uzazi wa
mpango
• Mtu yeyote (mwanaume, mwanamke na kijana) aliyeolewa na asiyeoolewa,
mwenye watoto na asiye na watoto na wenye ulemavu walio kwenye
umri wa kuzaa anaweza kuamua kutumia huduma ya njia za uzazi wa
mpango bila kubaguliwa. Ni haki ya msingi kwa kila binadamu kupata
elimu, taarifa pamoja na huduma za uzazi wa mpango.

16
17
SEHEMU YA 10:

HITIMISHO
Mwezeshaji:
Kabla hujahitimisha waulize / waruhusu washiriki kama wana maswali
kutokana na yale waliyojadiliana na kisha fanya majumuisho kwa kurejea
yafuatayo;
• Uzazi wa mpango ni maamuzi ya hiari ya mtu au wenza juu ya wakati
gani waanze kuzaa watoto, wazae watoto wangapi3, wapishane kwa
umri gani na lini waache kuzaa.
• Uzazi wa mpango si kuwa na watoto wachache tu bali ni jinsi gani mtu na
mwenza wake wanapanga idadi ya watoto wa kuzaa.
• Uzazi wa mpango hukuwezesha kutoa huduma na malezi kwa watoto
kadri ya mahitaji yao na kukupa nafasi nzuri kimaisha.
• Uzazi wa mpango hukuwezesha kusimamia vizuri raslimali ulizonazo.
• Uzazi wa mpango humuwezesha mama na watoto kuwa na afya bora.
• Uzazi wa mpango unasaidia kukuza uchumi na maendeleo ya familia,jamii
na nchi kiujumla.
• Kuna njia nyingi za uzazi wa mpango ambazo zinaweza kuwasaidia wenza
kupanga familia yao.
• Ni juu ya wenza kuamua ni aina gani ya njia ya uzazi wa mpango
wanayoona inafaa kuitumia baada ya kushauriwa na watalaam katika
kituo cha huduma za Afya.
• Kwa maelezo zaidi kuhusu uzazi wa mpango waone watoa huduma wa
afya katika kituo cha kutolea huduma za Afya kilichopo karibu nawe.
• Unaweza ukatuma ujumbe wa simu ulioandikwa m4RH kwenda namba
15014 BILA MALIPO

Mwisho:
Maliza kwa kuwashukuru kwa ushiriki wao katika zoezi zima.

18
19
Fuata nyota ya kijani, Upate mafanikio

20

You might also like