Asili Ya Fasihi

You might also like

Download as doc, pdf, or txt
Download as doc, pdf, or txt
You are on page 1of 6

2.2.1.

2 Asili ya Fasihi

Tunaposema asili ya fasihi, tunaongelea fasihi simulizi kwa kuwa kama asemavyo Mulokozi
(2003), uchunguzi katika fasihi simulizi unatuonyesha kuwa karibu tanzu zote za fasihi andishi
tunazozifahamu na kujivunia leo zimechipuka kutokana na fasihi simulizi. Asili ya fasihi ni
jambo ambalo lilishughulikiwa na watafiti tofauti na wenye maoni tofauti. Kutokana na maoni
tofauti kuhusu asili ya fasihi, tunazo nadharia nne tofauti kuhusu asili ya fasihi kama
inavyoelezwa hapo chini.

2.2.1.2.1 Nadharia ya udhanifu

Nadharia hii inaeleza kuwa asili ya fasihi ni Mungu. Waasisi wa nadharia hii ni wasomi wa kale
wa kiyunani, akiwemo Hesiod na Plato. Wanadai kuwa Mungu ndiye aliyempa binadamu
msukumo wa kutunga kazi za kisanii, huyu Mungu ndiye mwenye kumwezesha msanii au
kumpa uwezo wa kutunga kazi yake ya kisanii ikiwemo fasihi simulizi. Kwao, Mungu ndiye
msanii mkuuu; kwani, usanii wake unajidhirisha katika ulimwengu alioumba. Na mwanadamu ni
zao lake. Hivyo, kipaji cha kubuni sanaa kwa mwanadamu kimetoka kwa Mungu.

Dosari za nadharia hii kwa mujibu wa Wanjala (2011) ni kwamba inachanganya vitu viwili,
yaani imani na taaluma na ni nadharia isiyo na uthibitishao wa kisayansi. Na hivyo, ni vigumu
kuijadili kitaalamu. Vilevile inapuuza ukweli kwamba mazingira na jitihada za binadamu huwa
na athari kubwa kwa binadamu katika kujitambua kupitia utamaduni wake.

Dosari hizi ziko wazi kabisa na pasipo uchunguzi wa kina waweza kuziacha kama zilivyo kwa
kudhani kuwa zipo sahihi au si sahihi. Kwa mtu mwenye kupuuza uwepo wa Mungu, hakika ni
sahihi kwake kwa kuziweka dosari hizi katika nadharia hii. Ila ni jambo la kutia dukuduku kama
mtu anaamini uwepo wa Mungu na kukubali kuwa ndiye muumba wa kila kitu, halafu, anapuuza
nadharia hii.

Aidha, ni vigumu kujua moja kwa moja kama imani si sayansi, wakati imani ni njia moja wapo
ya kupata maarifa. Na ni vigumu kukubali kuwa nadharia hii, haijadiliki kitaalamu, kwani wapo
wanataaluma wa fasihi ambao ni waamini wakubwa wa Mungu na wanaamini uumbaji wa
Mungu katika maisha ya binadamu. Wakati huo huo, tunajiuliza kuwa kama kila kitu
kimeumbwa na Mungu, akiwemo binadamu, je huo uwezo na utambuzi alio nao mtu, unaotokana
na mazingira na utamaduni wake uliomzunguka umetoka wapi kama si kwa Mungu
aliyemuumba? Kwa ufupi kila nadharia haiwezi kujitoshereza kwa asilimia mia japo ukweli
mkubwa unakuwemo.

2.2.1.2.2 Nadharia ya Sihiri

Nadharia hii inaeleza kuwa sanaa imetokana na sihiri. Sihiri ni uwezo wa juu au nguvu za
kimiujiza zaidi ya alizo nazo binadamu, ambazo hutumiwa na watu kufanya mambo yasiyo ya
kawaida kwa uwezo wa kibinadamu. Waasisi wake wanaamini kuwa sihiri imechukua nafasi ya
sayansi katika ulimwengu wa sasa, hasa zama za kale, sihiri ilitumiwa na wanadamu katika
kufanya mambo. Kwa hiyo fasihi na sanaa ni mazao yaliyochipuka kutokana na sihiri katika
kujaribu kuyashinda mazingira. Kwa mfano ati, wawindaji wa zamani walichora kwanza picha
ya mnyama amechomwa mishale, waliyetaka kumwinda kabla ya kwenda mwituni kuwinda
wakiamini kuwa kitendo hicho kitatokea kweli, watakapofika msituni huku wakiimba. Na
nyimbo walizoziimba katika kushadadia kitendo hicho ndio ushairi wa mwanzo.

Nadharia hii ina dosari kama ifuatavyo: kwamba yenyewe inachanganya dhima na asili ya fasihi.
Kuwa, kutumika kwa ushairi katika sihiri hakumaanishi au hakudhibitishi kuwa sihiri ni chanzo
cha fasihi. Nyimbo zilizotumika katika sihiri zilikuwa zinakamilisha azma yake kama
inavyojitokeza katika shughuli mbalimbali. Mathalani, wasukuma huwa na nyimbo mbalimbali
ambazo huwa nyenzo muhimu katika kufanya kazi, mfano kulima. Na hii haimaanishi kuwa
nyimbo ndio kulima kwenyewe.

2.2.1.2.3 Nadharia ya Wigo au Uigaji

Nadharia hii husisitiza kwamba binadamu ni mwigaji wa maumbile ya maisha yanayomzunguka.


Plato, naye Aristotle, ni waasisi wa nadharia hii. Plato akisisitiza kwamba wasanii wa sanaa
huiga mambo halisi ya ulimwengu halisi, ambao wengi waliyatafsiri kama mazingira ya
mbinguni. Na hivyo, wasanii hao wanaupotosha ukweli wa mabo halisi yalivyo. Wataalamu
wengine wa fasihi, wameiita nadharia hii kuwa ni nadharia ya umithilishaji. Kwa mtazamo huu,
fasihi hufafanuliwa kuwa chanzo chake ni umithilishaji katika uhusiano wake na maisha; kwa
kuiona kama njia ya kujenga au kuhusisha tukio au hali fulani ya maisha kwa kutumia mchoro na
rangi. Nakungah (2011) anasema kuwa “katika kazi yake ya “Poetics”, Aristotle anaeleza ushairi
kama “umithilishaji” wa vitendo vya mwanadamu. Kwa “umithilishaji” anamaanisha
`uwakilishi', kwa misingi yake. Kwa hivyo, kwa maoni ya Aristotle, shairi humithilisha kwa
kuchukua kitendo fulani cha mwanadamu na kukionyesha upya katika `mtambo' mpya - ule wa
maneno”.  Kwa mantiki hii, ni kwamba fasihi huweza kuiga na kumithilisha maisha.

Moja wapo ya dosari ya nadharia hii, ni kwamba, inasisitiza sana kuiga na kusahau suala la
ubunifu, amabalo ndio uti wa mgongo katika sanaa na fasihi. Dosari hii yaonekana pakubwa
kuwa na mashiko lakini, nadharia ya umithilishaji au wigo ikitafakariwa kwa kina, itagundulika
kuwa ni wazi kabisa kwamba japo tunasema mwanadamu anao uwezo wa kubuni; ni kweli,
lakini yafaa tujiulize kama kubuni huko si zao la wigo, msanii huyo anaiga kutoka wapi wakati
akiishi katika mazingira? Binadamu anaiga mazingira yake aliyoyakuta, kama ahigi basi yeye
ndiye atakuwa muumbaji wa mazingira hayo; jambo ambalo si kweli.

Kuiga si jambo amabalo mwanadamu analifanya kutoka katika ombwe tupu, bali anaiga
kutokana na mazingira anamoishi na mazingira hayo hakuyaumba yeye. Katika kubuni huko,
msanii humithilisha uhalisia wa mambo ambayo kwa uwezo wake hawezi kuyawakilisha kama
yalivyo kwa uhalisia wake. Mfano kitendawili kama “nyumba yangu haina mlango, ‘yai’ ”.
Kitendawili hiki kina umithili ndani yake. Kwamba kilicholengwa hapa ni ‘yai’, lakini
linawakilishwa kwa picha ya nyumba isiyo na mlango. Hakika hakuna nyumba isiyo na mlango,
ila kwa msanii kutaka kutumia sanaa analichukulia yai mithili ya nyumba; yaani kwa maneno
mengine anaiga nyumba kuelezea yai, wala yai si nyumba ki uhalisia.

2.2.1.2.4 Nadharia ya Kiyakinifu

Hii ni natharia ya mtazamo wa ki-marx; ambayo inayaangalia maisha kwa uyakinifu. Karl Marx
na Engel ni waasisi wa nadharia hii (Wanjala 2011). Msisitizo wake ni juu ya chanzo cha
binadamu, kuwa, ni zao la maumbile asili ya ulimwengu na akaanza kubadilika taratibu
kulingana na mazingira. Mabadiliko hayo ni katika nyanja zote za maisha, mfano utamaduni,
falsafa, lugha na fasihi. Katika mabadiliko hayo, mwanadamu alianza kugundua kuwa anaastahili
kuratibu mazingira katika shughuli zake ili aweze kuthibiti mazingira vizuri. Na lugha ilianza
kama njia ya kurahisisha uratibu huo kwa mawasiliano na baadae lugha ikawa chombo cha
sanaa, ambayo ni fasihi. Na hapo fasihi ikaanza kujitenga na shughuli za uzalishaji, ikiwa ni
sanaa ya burudani na shughuli maalumu za kijamii kwa mfano sherehe na ibada. Na huo ukawa
mwanzo wa fasihi.

Dosari moja wapo ya nadharia hii, ni kuipa uwezo mkubwa lugha kuwa ndio sanaa, jambo
ambalo kimantiki si sahihi. Bali, lugha ni njia moja wapo ya kuieleza sanaa ya fasihi na wala
lugha tu haitoshi kuwa sanaa pekee. Sanaa ni picha ya ufundi ya kuwakilisha lengo fulani. Sanaa
ni ufundi wa kuwasilisha hisia na mawazo ya binadamu kwa maandishi, michoro na uchoraji au
uchongaji (Kamusi ya Kiswahili Sanifu). Kwa hiyo, lugha si sanaa kama wanavyosisitiza waasisi
wa nadharia hii; bali, ni njia moja wapo ya kuieleza au kuitoa sanaa, ambapo fasihi kama sanaa
yenyewe huwasilishwa kwa lugha.(dosari hii nimeibainisha mwenyewe).

Baada ya kuangalia mawazo ya wataalamu mbailimbali juu ya asili ya fasihi simulizi au fasihi
kwa ujumla, hasa, kupitia nadharia zao; ni vema sasa, tuone mawazo ambayo yaweza kuwa
mbadala wa nadharia hizi, yakilenga kuleta changamoto kwa nadharia hizi na kueleza asili na
chanzo cha fasihi. Na hii ni baada ya kuzitafakari nadharia zilizoelezwa na kupata mkanganyiko.
Na pengine mtazamo huu waweza kutupa mawazo mengine ambayo yaweza kuelekea katika
ukweli wa asili ya fasihi.

2.2.1.2.5 Asili na Chanzo cha Fasihi ni Binadamu

Fasihi simulizi asili yake ni mwanadamu hasa alipoanza kuongea na kutumia lugha kueleza hisia
na mawazo yake kwa wengine. Tunaposema asili ya fasihi ni binadamu, ina maana ya kuwa
sanaa yoyote ile, fasihi ikiwa ni mojawapo, ni matokeo ya binadamu kudhihirisha uwezo wake
alio nao katika kutumia akili yake kuyamudu maisha. Sanaa kwa ufupi ni ufundi; ufundi ni kipaji
cha asili alichonacho msanii (binadamu), na kwa kuwa akili ndiyo imuongozayo mtu katika
kutimiza jambo, basi hutumia kipaji hicho katika kuhakikisha anayaishi na kuyamudu vema
maisha yake. Fasihi na sanaa nyingine ni matokeo ya mwanadamu kutumia vema akili yake
katika kuishi na kuyamudu mazingira yake. Mwanadamu ndiye kiumbe mwenye akili zaidi hapa
duniani. Na kwa kuwa ana akili, binadamu hutumia akili hiyo kuweza kufanya mambo mengi
ikiwemo kuonesha utaalamu wake (sanaa) wa kipekee kwetu.

Fasihi na sanaa nyinginezo, ni matokeo ya binadamu mwenye uwezo wa kutumia akili yake
katika kuishi. Sanaa kama uchoraji, uchongaji, ufinyanzi, udarizi, muziki na kadhalika ni mazao
au matokeo ya akili ya binadamu, imtumayo kuchora, kufinyanga, kuchonga, kutengeneza ala za
muziki nakadhalika. Hii inatokea pale yeye aonapo kuwa anahitaji kufikisha malengo yake kwa
wanadamu wenzie, basi si budi kwake kutumia mbinu hizi kueleza mawazo yake kwa wengine.
Hivyo hivyo, kwa fashi ijitengayo na sanaa hizi kwa nyenzo ya lugha. Lugha ni chombo
kinachomhusu binadamu, ambapo sauti za zilizo katika mpangilio maalumu na zilizokubaliwa na
jamii hutumika katika maisha ya kila siku kwa ajili ya mawasiliano.

Hivyo baada ya kutumia sanaa nyingine ambazo ni kama ishara pekee kuwasilisha azma ya
msanii, binadamu akaamua kuunda lugha na kuitumia kufikisha ujumbe wake. Na hilo ndilo
chimbuko la fasihi. Kwa kuwa huyu binadamu ana akili, mwanzoni akitumia sanaa nyingine,
akaamua pia kuibua ubinfu mwigine, ambapo akatumia masimulizi, yaani maneno katika
kuumba na kuwasilisha sanaa yake; nayo ni fasihi simulizi. Kwa hiyo sanaa au fasihi,
isichukuliwe kama kitu kilicho katika ombwe tupu au kitu kilichokuwepo kabla hata binadamu
hajawepo, la hasha, fasihi na sanaa vimekuwepo baada ya binadamu na ni zao la binadamu
mwenye kuyatawala maisha. Kwa hiyo, mawe, milima, bahari na mambo mengine ya asili si
sanaa, bali ni asili. Sanaa ni matokeo ya binadamu kutumia asili hiyo.

Mawazo haya yaweza kukutana na upinzani wa hoja mbalimbali ikiwemo ya Mungu kumuumba
mwanadamu na kumpatia uwezo wa kumiliki mazingira. Ni kweli Mungu alimuumba
mwanadamu na kumpa akili na kumuacha atumie akili yake kuishi; na kama binadamu
angepewa kila kitu, basi yeye asingelikuwa anaangaika na kumiliki mazingira yake. Mungu
hakumpa binadamu kila kitu; kama ni hivyo, basi hata dhambi atendazo mtu kapewa kwa uwezo
wa Mungu. Ila si kweli, Mungu alimpa mtu utashi na akili, kupitia vitu hivi viwili binadamu
hupaswa kuvitumia na kuibua mambo mbalimbali. Na kwa hiyo, sanaa na fasihi ni matokeo ya
matumizi ya akili na utashi. Kama binadamu asingeliamua na kuchagua kuwa mbunifu au
kutumia lugha kwa mawasiliano; asingelifanya hivyo na leo hii tusingelikuwa tunasigana kuhusu
fasihi.

Kwa kuhitimisha, ni kwamba, pasipo binadamu, hakuna sanaa, kwani hata nadharia zote
zinazoeleza chanzo cha fasihi hazimtupi mwanadamu japo zinakwepa kumbainisha moja kwa
moja. Chimerah na Njogu (1999), wanadhihirisha wazi kuwa fasihi ni ya binadamu hasa
wasemapo kuwa, “kwa vile fasihi simulizi inapata kubuniwa kutokana na mazingira ya
wanajamii (binadamu) na tabia zao hao wanajamii, basi tunakuta ya kwamba, tangu kuwepo kwa
binadamu ulimwenguni, fasihi nayo imekuwepo na imeeleza mambo aina aina katika nyanja
mbalimbali za taaluma, kama vile taaluma; kama vile lugha, fasihi andishi, historia, jiografia,
falsafa (busara), maadili, elimu na hata sayansi.”

Kwa mantiki hii, hatuwezi kupata fasihi pekee pasi na binadamu. Na kwa maana hiyo, ndio
maana fasihi simulizi ni sanaa inayobuniwa, kuwasilishwa na kusambazwa kwa lugha (ya
mdomo). Vyombo vyake vikubwa ni mdomo na sauti ya binadamu katika hali ya kuimba,
kusimulia, kuiga, kughani, kutamba, kutega na kadhalika – miradi yake yote yanatolewa kwa
mdomo na ishara za mwili (Mazrui na Syambo, 1992). Kwa ufupi ni kuwa hakuna namna yoyote
utaongelea fasihi simulizi au andishi, usimhusishe mwanadamu. Na hivyo, fasihi haipo pasipo
binadamu. Fasihi simulizi ni zao la mwanadamu kuanza kuzungumza, na hasa kuamua kueleza
sanaa au kazi zake kwa lugha; yaani, masimulizi.

Marejeleo

Mazrui, A.M na Syambo, B.K (1992). Uchambuzi wa Fasihi. Nairobi: East African
Educational Publishers.
Nakungah, C. (2011). Kiswahili Taalamifu “Fasihi Simulizi”.http://kiswahilitaalamifunyangeri-
nakungah.blogspot.com/2011/06/fasihi-simulizi.html
Njogu, K na Chimerah, R (1999). Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia na Mbinu. Nairobi:
Jomo Kenyatta Foundation
Wanjala, S.F (2011). Kitovu cha Fasihi Simulizi, kwa shule, vyuo na nadaki. Mwanza:
Serengeti Bookshop.

IDAHEMUKA Magnifique (220018613)

You might also like