Nyumba Ya Majini

You might also like

Download as pdf or txt
Download as pdf or txt
You are on page 1of 48

NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

NILIPAngA NYUMBA
MOJA NA MAJINI
Irene Ndauka
KIMETAYARISHWA NA KUSAMBAZWA NA:
A & S DESIGNING
SIMU: 0713 335560
0788 943433
DAR ES SALAAM

Haki zote zimehifadhiwa. Hairuhusiwi kuiga,


kunakili au kutoa kitabu hiki kwa jinsi yoyote ile
bila idhini ya A&S DESIGNING

ALLY P. KASKASI - MKURUGENZI

1
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

Rais Wasifu Nusura kipenzi cha wananchi ameuawa


kwa kuchomwa sindano ya sumu na baadhi ya viongozi
wa nchi hiyo ya Vikuruti wakishirikiana na baadhi ya
maofisa wa usalama wa taifa ili waurudishe utawala
mbovu madarakani. Watu wa kikosi maalum cha siri
cha kijasusi waliokuwa wakimlinda kwa siri kubwa
walifadhaika sana kwa uzembe hadi rais kuuawa.
Wanaamua kulivalia njuga suala hilo ili kuzuia nchi
isirudi mikononi mwa mafisadi.
kitabu kiTAtoka hivi karibuni... 0713 335560
2
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

DHAHABU Imefika
Ni kitabu kizuri kiutakachofanya ujue chimbuko
la makabila ya watu wa tanzania pamoja na
tamaduni zao. kwa kadili muda unavyokwenda
watu tunazidi kuzarau na kusahau asili, mila
na tamaduni zetu hivyo kitabu hiki na kitunzwe
ili kiwe kumbukumbu kwa vizazi vijavyo kwani
bila ya kitabu hiki hawatakuwa wakijua asili na
tamaduni za mababu zao
kwa maulizo piga 0713 335560

3
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

“KAMA
kuna watu hawayajui haya
nitakayoyaongea basi nawataka kuanzia
sasa wajue kwamba, hapa Dar kuna
mambo makubwa sana ambayo ukisimuliwa unaweza kusema
si kweli, lakini wale wanaoyapata wanajua. Ila wewe omba
yasikukute hata siku moja...”
Ndivyo alivyoanza kusimulia Bw. Humuli Samaki (43), mkazi
wa Buguruni (kwa sasa) ambaye alipata mkasa mzito akidai
alipanga nyumba moja na majini Magomeni, Dar es Salaam.
Anaendelea…

2009, MKASA UNAANZIA HAPA


“Si zamani sana mkasa huu uliponitokea, ilikuwa mwaka 2009
tu. Kwa hiyo naweza kusema ni juzijuzi. Kwa sasa naishi hapa
Buguruni, baada ya kuhama kutoka Magomeni ambako nilipata
mkasa huo mzito na wa kuogopesha. Nilipanga nyumba moja
na majini.
Awali nilikuwa nikiishi Mwananyamala Mwinjuma, jirani
kabisa na Makao Makuu ya Bendi ya TOT, hata Kapteni John
Komba nilizoeana naye kwa kuonanaonana pale CCM-
Mwinjuma, ingawa jina langu najua hakuwa akilifahamu.
Nyumba niliyokuwa nikiishi Mwananyamala iliingia kwenye
mgogoro wa mirathi, familia ilifika mahakamani. Hukumu
ilipotoka ikaamriwa iuzwe kisha ndugu wagawane fedha.
Kwa maana hiyo, mimi na wapangaji wenzangu watano,
tulipewa notisi ya kuhama baada ya mteja kupatikana. Huyu
mteja anaitwa Masawe anafanya kazi Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) lakini sijui ofisi za wapi.
Ilibidi mimi niangalie mwelekeo mwingine, niliamua nibadili
upepo, nikatamani kwenda kuishi Magomeni. Kwa wakati huo
nilikuwa sina familia. Sina mke wala mtoto, hata wa kusingiziwa.
Kwa hiyo nilikuwa naishi peke yangu. Ni mwaka jana ndiyo
nimeoa mke wangu huyu.
Rafiki yangu mmoja anaitwa Mohammed Kombe alinipa
4
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

namba ya dalali kwani yeye anaishi Magomeni hata sasa.


Nilimpigia simu dalali wake, anaitwa Yusuf Mwamba, akaniita
Magomeni pale kwenye nyumba wanayosema aliwahi kuishi
Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Nilikwenda mpaka pale, nilimkuta amesimama nje ya nyumba
hiyo, tukasalimiana, akaniuliza nataka nyumba yenye sifa gani,
nikamweleza.
Akasema nyumba ya aina hiyo ipo moja mitaa ya katikati
kama unatokea pale tulipo kuelekea kwa Sheikh Yahya Hussein
(marehemu).
Tulikwenda kuiona hiyo nyumba. Wakati tukiwa tunaifikia,
nilishangaa kuwaona majirani wakitukodolea macho yasiyo ya
kawaida, lakini sikushangaa sana nikijua ni mambo ya mjini
kitu kidogo tu watu kibao.
Yule dalali alifungua mlango, tukaingia ndani. Tulipita
sebuleni, tukaenda kwenye vyumba viwili, tukaelekea jikoni,
chooni na kumalizia bafuni.
Ni nyumba iliyojitegemea kwa maana kwamba, ilikuwa na ua
wake na mtu akiwa uani hakuna kuona nje. Mlango wa kuingilia
ndani ni mmoja tu.
Kulikuwa na vyumba vingine viwili ambavyo toka mwanzo
dalali aliniambia vyumba hivyo kuna mwanaume anaishi
na mkewe. Chumba kimoja wanalala, kingine wamekifanya
sebuleni, lakini hawana watoto kama mimi.
Nilijiridhisha kwamba ni pazuri. Dalali akaniuliza kuhusu
malipo, nikamwambia tuongozane nikachukue pesa Magomeni
Mapipa kwenye benki moja, akasema wakati mimi nakwenda
kutoa hizo pesa, yeye anakwenda Dawasco Tawi la Magomeni
ana shida muhimu pale.
Tukiwa tunaelekea Magomeni Mapipa, nilimuuliza mwenye
vile vyumba na mkewe wanafanya kazi wapi? Akajibu ni
wafanyabiashara, lakini hata yeye hajui ni wapi. Nilimuuliza
imekuwaje ana funguo, wale wapangaji wengine wakirudi
je, akajibu wana funguo yao na ile yeye alipewa na mwenye
nyumba kwa ajili ya kutafutia mpangaji mwingine.

5
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

***
Baada ya nusu saa nilitoka benki nikiwa na hela, nikampigia
simu dalali, akasema na yeye alishatoka Dawasco na wakati
huo alikuwa anakunywa soda kwenye mgahawa wa Shibam,
upo palepale Mapipa.
Nilimfuata pale, nikampa fedha, akatoa mkataba, nikajaza
kwani kwa madai yake, yeye ndiye aliyepewa jukumu lote na
mwenye nyumba.
“Kwa hiyo upo huru kwenda kuhamia,” dalali aliniambia
huku akinikabidhi funguo.
“Sawa, nitahamia usiku wa leo.”
Nilirudi nyumbani kwa awali na kupangapanga vitu tayari
kwa usiku kuhamia makazi mapya, Magomeni. Niliwaambia
wapangaji wenzangu wote, nao wakanitakia maisha mema
huku wakisema tukumbukane kwani hata wao walikuwa
kwenye mchakato wa kuhama kwenye nyumba ile.

NAPEWA UJUMBE WA AJABU

Saa mbili usiku nilikuwa juu ya lori tukipeleka mizigo makazi


mapya, lakini moyoni nilikuwa na maswali mengi ambayo
mpaka leo hii siyakumbuki na yalikosa majibu. Pia, nilijikuta
nakosa amani ya moyo na sikujua ni kwa nini!
Nje, nilikuta taa inawaka, ndani pia taa inawaka, lakini si
sebuleni bali kwenye korido. Hii iliashiria kwamba, wale
wapangaji wenzangu walisharudi kutoka kwenye shughuli
zao.
Nilishusha vyombo kwa kusaidiwa na wasaidizi wa dereva wa
lile lori, lakini nilishangaa sana kuona kila nikiingia na mizigo,
wale wapangaji wenzangu wanacheka sana chumbani kwao.
Hapa maana yangu ni kwamba, kwa kawaida walitakiwa
hata watoke na kunisalimia ili tufahamiane. Tena kwa wengine,
mume angetoka na kunisaidia kubeba hata stuli tu.

6
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

Ilifika mahali, wale vijana waliokuwa wakinisaidia


waliniuliza:
“Hivi hao majirani zako mbona hawatoki, wanacheka tu
chumbani.”
Niliwajibu mimi mwenyewe sijui, lakini sikumaindi sana. Akaja
mama mmoja aliyesema anaishi nyumba ya pili, akasalimia na
kuniuliza maswali.
“Hamjambo wanangu?”
Tuliitikia wote, akauliza nani anahamia pale kati ya sisi wote.
Tulikuwa watano mbali na dereva.
“Ni mimi,” nilimjibu.
“Ooo, mzima baba?”
“Mimi mzima mama.”
“Unaitwa nani?”
“Humuli Samaki.”
“Unahamia peke yako au uko na mke na watoto?”
“Peke yangu mama.”
“Humuli Samaki ni mwanyeji wa wapi?”
“Usukumani.”
“Haya, naamini uliaga wakati unaondoka nyumbani.”
“Hilo lilikuwa la kwanza mama.”
“Haya, kila la kheri.”
Tuliendelea na kazi ya kuingiza vyombi ndani hadi tukamaliza.
Wale wenye gari wakaondoka, nikabaki mimi peke yangu.
Nilijiwekea malengo kwamba, nihakikishe naweka sawa kila
kitu ili kesho yake nisiwe na kazi hiyo zaidi ya kwenda kazini.
Niliifanya kazi kwa muda wa saa tatu, mpaka kwenye saa saba
na nusu usiku nikamaliza.
Nilibadili nguo, nikavaa taulo na kwenda kuoga. Nilikuta bafu
limetoka kutumika kama dakika kumi nyuma, sikushangaa
kwani si kuna wapangaji wengine ambao tulitakiwa kutumia
bafu moja.
Usiku kabla ya kulala nilizima taa, nikapanda nitandani. Lakini
kabla sijapata usingizi, niliwasikia wenzangu wakicheka sana
7
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

na kuongea huku wameweka muziki. Lakini ule muziki haukuwa


wa kiarabu, kizungu wala kiswahili.
Hata maongezi yao, mimi nilisikia sauti tu lakini kusema
walikuwa wanatumia lugha gani si rahisi. Kuna wakati kama
walikuwa wakiongea kihindi, pia niliwasikia kama wanaongea
kiarabu, nikajua ni watu wa namna hiyo.
Kusema ukweli sikulala mpaka nikampigia simu dalali
kumuuliza kama wale wapangaji wenzangu ni weupe au
waswahili kama mimi, akasema hata yeye hajui kwani hakuwahi
kuwaona hata siku moja.
Basi, nililala.

MARUWERUWE YANAANZA
Asubuhi niliamka nikiwa nimechoka sana. Wakati nakwenda
bafuni kuoga niligundua ni mimi peke yangu ndiye niliyekuwa
nimetangulia kuamka, kwani bafuni hakukuwa na maji
yaliyomwagika kwa muda huo.
Baada ya kuoga nilirudi chumbani kwangu kujiandaa kwenda
kazini. Wakati najiandaa, nilisikia mlango ukifunguliwa, nikajua
ni wenzangu wanakwenda kuoga au chooni kama ilivyo kawaida
kwa wanadamu wakiamka asubuhi.
Niliamua kutumia nafasi hiyo kuwatambua. Nilivizia pale
niliposikia mlio wa maji bafuni na mimi nikatoka kwenda
kupiga mswaki kwa mara ya pili. Sehemu niliyosimama, mtu
akitoka bafuni kwenda ndani ilikuwa lazima nimuone kwa vile
ilikuwa kiasi cha kugeuka tu.
Lakini cha kushangaza, nilikuwa sisikii maji yakimwagika,
nikageuka na kuuona mlango wa bafuni upo wazi. Mbali na
mlango kuwa wazi, pia chini nikaona alama za kandambili nne
zikiwa zimekanyaga, nikajua wametoka.
“Lakini wamepitaje hapa?” nilijiuliza.
Nilirudi ndani, mlangoni kwao nilikuta kandambili pea mbili
zikiwa bado na majimaji kwa mbali, jambo hili lilinifanya
nijiuliuze sana.
Nilijipa ujasiri na kuamua kuchungulia ndani ya chumba hicho
8
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

kwa kutumia nafasi ya katikati ya mlango ambapo niliweza


kuona hadi kitanda lakini sikumwona mtu yeyote.
Niliingia kwangu, nikaweka mswaki, nikava vizuri na
kuondoka zangu. Nilitegemea wenzangu nimewaacha ndani,
kwani nilipofika mlangoni nilikuta umefunguliwa na upo wazi.
Nilirudi ndani hadi kwenye mlango wao.
“Wandugu,” niliita kwa sauti.
“Jamani wandugu.”
Ukimya ndiyo ulinifanya nibaini walishaondoka. Kwani
kulikuwa kimya sana na kandambili zilikuwa pembeni ya
mlango si pale pa kwanza.
Nilifunga mlango mkubwa nikaondoka, mbele nilimwona yule
mama aliyekuja usiku kuniuliza maswali. Alikuwa amesimama
nje ya nyumba yake, aliponiona akashutuka na kuita majina
mawili ya watu.Wakatoka watoto wake wawili, ni mabinti wenye
miaka kama kumi na nane na ishirini na mbili hivi.
“Hujambo kijana?” yule mama alinisalimia kwa furaha.
“Sijambo mama, shikamoo.”
“Marhaba.” Kisha akawaambia kitu wale watoto wake nao
wakanikazia macho.
“Mama umewaona majirani zangu hapa?”
“Majirani zako akina nani?”
“Wapangaji wenzangu.”
“Kijana, kua uyaone ya dunia. We si umeshakua, utayaona ya
dunia.”
Kauli hiyo iliniogopesha sana, nikashtuka na kumuuliza
mama.
“Mama una maana gani?”
“Sisi hatutaki umbeya kijana.”
“We si umeambiwa utayaona kwa hiyo subiri tu,” alidakia
binti yake mkubwa.
Miguu ilitetemeka, mwili uliisha nguvu, nikajikuta nataka
kukaa, lakini sikuweza. Nilichoamua ni kuondoka huku
nikimpigia simu yule dalali.

9
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

“Vipi hujambo bwana?”alinisabahi.


“Mimi sijambo.”
“Za makazi mapya?”
“Si nzuri bwana.”
“Kwanini tena?”
“Sielewielewi.”
“Kivipi?”
“Kuna mambo kama si ya kawaida.”
“Yapi hayo?”
“Wale wapangaji wenzangu siwaelewi kabisa.”
“Kivipi?”
“Ah! Watu gani mimi mgeni nimehamia washindwe kutoka
kunisalimia ili angalau tufahamiane?”
Dalali alicheka sana kisha akasema:
“Wale ndivyo walivyo bwana, si unajua tena malezi,
mwingine kalelewa vile, mwingine hivi. Ila ulichokisema ni
kweli, haiwezekani nyumba mnayoishi mpate mgeni halafu
msitambuane, sasa mkikutana njiani je?”
“Si ndiyo hapo sasa,” nilisema nikijifanya lawama zangu ni
kwa ajili ya hilo tu, lakini kumbe nilikuwa na zaidi ya hapo.
Kazini siku hiyo nilishinda sina amani, sina raha, mwili ulikuwa
kama umetoka kufanya kazi nzito ambayo sijawahi kuifanya
kwa siku nyingi, wenyeji wa Pwani wanaita mavune.
Kwa upande mwingine nilitamani sana jioni ifike ili nikaone
siku hiyo kitatokea kitu gani kipya kwenye nyumba ile.
Kweli bwana, jioni ilifika, nikaondoka kazini, sikutaka
kupitia popote, dukuduku langu lilikuwa kwenda nyumbani
tu. Nilichukua kama saa moja kutoka kazini hadi kufika
nyumbani.

MAAJABU YANAZIDI
Nje nilikuta mfuko wa rambo mweusi, ndani yake ulionekana
kuwa na kitu kwani ulikuwa umetuna sana. Niliinama
kupekenyua ili nijue ndani kulikuwa na nini, nilishangaa kuona
10
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

ni vipande vya nyama za kuchoma tena vilikuwa na moto.


“Kha! Atakuwa nani ameweka?” nilijiuliza mwenyewe,
nikauacha palepale, mimi nikapanda ngazi za kuingia ndani.
Mlango ulikuwa wazi hali iliyoashiria kwamba, wenzangu
walisharudi. Nilisukuma mlango, nikaingia. Nilikutana na
harufu ya pafyumu, nikahisi walikuwa wakijiandaa kutoka.
“Jamani za leo?” nilisalimia kwa sauti ya juu licha ya kwamba,
mlango wao ulikuwa umefungwa, hakuna aliyeniitikia, hilo
sikulijali sana kwani niliamini kwa kuwa walikuwa ndani,
isingekuwa rahisi wasikie salamu yangu.
Niliingia sebuleni kwangu, kisha nikaenda chumbani, kuna
kitu kilinishangaza, nikasimama kwa mshtuko. Nilikuta sehemu
nilipoweka kiberiti asubuhi, nilikiacha juu ya meza, nikakikuta
juu ya kitanda. Niliacha kioo na kitana juu ya kitanda, lakini
nikavikuta kwenye stuli, niliguna!
Nilikishika kioo na kukiangalia kwa umakini kama
kina mabadiliko yoyote, lakini sikuona, nikashika kitana.
Nilipokigaua sana pia sikuona kitu cha tofauti, nikaamua
kuchania, nikahisi kuguswa na kitu kama nywele ndefu kama
za mtu aliyefuga. Nilikiweka kitana juu usawa wa dirishani,
nikaona nywelenywele nene, nyeusi, mwili wote ukasisimka.
Ninavyojua mimi, mwanamke mwenye nywele nyingi
akichania kitana, ndiyo huacha nywele, sasa mimi nilikuwa na
nywele fupi sana zisingeweza kuacha nywele ndefu kwenye
kitana.
“Mh! Hapa kuna kinachoendelea,” nilisema moyoni huku
nikikaa.
Nilishtuka zaidi kuona soksi zikiwa kwenye msumari nyuma
ya mlango wakati niliacha chini.
“Huyu ni nani?” niliuliza kwa sauti ya ukali.
Ghafla nikasikia kicheko kutoka chumbani kwa wale
wenzangu.
Nilikaa kwenye kochi, nikaanza kuangalia sehemu
mbalimbali za mle ndani ambazo niliamini naweza kuona
mabadiliko mengine mbali na yale ambayo nilishayaona,

11
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

lakini sikubahatika.
Nilitoka, nikaenda sebuleni ambako nako nilianza kuangalia
kila kona ya sebule. Nilishangaa kuona glasi ya maji ya kunywa
ambayo niliitumia asubuhi kisha nikaacha maji yamejaa, ikiwa
haina hata tone la maji mbaya zaidi, iliwekwa juu ya kabati
ambapo mimi niliiweka kwenye meza ya katikati ya sebule.
“Mh! Hii kali sasa,” nilijikuta nikisema kwa sauti, mara
nikasikia kicheko tena kutokea upande wa pili kule kwa
wenzangu. Sasa nikaanza kama kuhisi kitu kuhusu watu hao.
Kwanini kila nilipoongea kwa sauti ndipo na wao waliangua
kicheko?
Niliamua kujaribu tena, nikasema kwa sauti:
“Nitakuja kuua mtu, kweli tena.” Nikasikia kicheko tena,
safari hii kilidumu kwa muda.
Moyoni nikasema naanza kufanyia kazi uhusiano wa maneno
yangu na vicheko vya wale majirani.
Nilitoka kurudi chumbani, wakati napita kwenye korido,
nilisimama jirani na mlango wao. Walikuwa wakiongea, lakini
niliposimama mimi, kukawa kimya ghafla kama hakuna watu.
Nilipozama chumbani, nyuma wakaanza kuongea tena.
Sikufunga mlango ili niweze kusikia wanachokiongea, lakini
jamani kwa kusema ule ukweli wa Mungu, sikujua walikuwa
wakitumia lugha gani katika kuwasiliana hata pale nilipojitahidi
kutega masikio kwa umakini wa hali ya juu sana.
Kuna wakati utadhani wanatumia sana neno dotikom, lakini
ukisema usikilize zaidi unasikia wakisema sana kotoko au
kiburate, wakati mwingine sauti ya kike ilisema kaunto, ya
kiume ikarudia hivyohivyo, kaunto.
Nia yangu kubwa ilikuwa kuwaona kwa sura na kufahamu
kama ni ngozi nyeusi au nyeupe. Hilo peke yake lingenipa
mwanga ni watu wa aina gani ninaoishi nao pale ndani ya
nyumba.
Nilisikia mlango wa chumbani kwao ukifunguliwa na mimi
nikatoka haraka sana, cha ajabu sikuona mtu akitoka lakini
mlangoni kulikuwa na kandambili pea moja tu wakati zilikuwa

12
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

pea mbili. Hii ilimaanisha kuwa, pea moja ilivaliwa.


Ilimaanisha kwamba, mmoja wao alitoka kwenda chooni.
Nilichofanya ni kuamua kusimama katikati ya mlango wangu
ili huyo aliyekwenda chooni akirudi nimuone. Ni kweli mmoja
wao alikwenda chooni kwani nilisikia mlio wa maji chooni.
Nilijitahidi kusimama mlangoni kwangu kumsubiria. Kwa
ramani ya nyumba ile ilivyo, asingeweza kutoka chooni bila
mimi kumwona hata kama angekuwa anataka kutoka kwenda
nje au uani.
Mlio wa maji ulikoma kusikika, nikawa natumbulia macho
kule huku moyoni nikisema:
“Leo ndiyo leo, asemaye kesho mwongo, hata afanyaje,
hawezi kunichenga hapa hata kidogo,” nilisema moyoni,
ingawa wakati huo mapigo ya moyo yalikuwa yakinienda kwa
kasi.
Nilipoanza kuhisi muda unakwenda na hakuna mtu aliyetoka,
nikampa dakika tatu kwamba lazima atakuwa anavaa ndiyo
maana anachelewa kutoka:
Baaada ya muda, nikasikia watu wakiongea chumbani kwao,
nikashtuka, nilijikuta nikisema:
“Haa!”
Haraka sana nilitupa macho mlangoni kuangalia kandambili,
nikaziona pea mbili, nikashangaa:
“Ina maana amenipita hapahapa au? Haiwezekani,
asingeweza kunipita hata kama ingekuwaje!” niliwaza.
Nilitoka kuelekea chooni, nikakuta mlango uko wazi,
nikachungulia ndani, hakukuwa na mtu, nikanyoosha mikono,
nikarudi ndani.
Nilifikia kwenye kochi sebuleni kwangu, nikahema kwa
nguvu kwani niliamini nimo ndani ya miujiza mikubwa ya
ndani ya nyumba ile.
“Hivi ni kwa nini dalali alinidanganya hivi?” nilijiuliza
mwenyewe nikiamini kwamba, dalali aliyenipangisha nyumba
ile alijua mchezo mzima ila alitaka kupata fedha tu ndiyo
maana alinipangisha bila kunipa tahadhari.
13
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

Nilitoka sebuleni, nikaenda chumbani, kitandani nikakuta


‘toilet paper’ ikiwa imekatwa sehemu. Mimi niliiacha pembeni
ya dirisha, lakini ikaonesha kuna mtu aliichukua na kunyofoa
kidogo kisha badala ya kuirudishia palepale, yeye aliiacha
kitandani.
Mbali na ‘toilet paper’ pia kuna kikopo chenye vijiti vyenye
pamba za masikio kilikuwa kwenye stuli jirani na kitanda, lakini
kwa muda huo kilikuwa kimeanguka chini halafu vijiti vimebaki
kama vitatu tu kwa maana kwamba, aliyeingia kuchukua ‘toilet
paper’ ndiyo huyo huyo aliyechota vijiti vya pamba.
Nilianza kuhisi kuwa sikuwa kwenye nyumba salama, lakini
kwa uthibitisho upi? Moyoni nikasema nitajua tu, mimi ndiyo
mimi.
Nilikaa ndani kwangu hadi usiku ulipoingia, nikasema nibadili
nguo kwa kuvaa bukta na singilendi halafu nitoke kwenda kula
gengeni kwani siku hiyo sikuwa najisikia kupika chochote. Si
mara nyingi nilipenda kula gengeni.
Nilitoka, nikasimama ili nifunge mlango wa chumbani,
nilipoangalia chini, upande wa wenzangu nilikuta nje ya mlango
wao pana vijiti vya pamba za masikioni vikiwa vimetumika.
Nikiwa katika mshango, mbele nikaona tishu ikiwa imefutiwa
majimaji yenye rangi nyekundu kama damu.

MSICHANA MREMBO, LAKINI WA AJABU

Nilitembea kwa wasiwasi, nikatoka nje, sikufunga mlango kwa


funguo, lakini niliubamiza tu, funguo nilikuwa nazo, nikaenda
gengeni kula.
Pale kwenye genge ambapo si mbali sana na nyumbani, alikuja
yule mama aliyeniuliza mimi ni mtu wa wapi, nilimsalimia, lakini
kabla hajaitikia alishtuka kuniona.
“Upo kijana wangu?”
“Nipo mama, nimetoka kazini nimekuja kupata mlo kidogo.”

14
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

“Pole sana, uoe sasa.”


“Huo ndiyo mpango wangu mama.”
“Ee, uoe halafu mimi nitakupa vyumba viwili pale kwangu,
nakuahidi.”
“Nashukuru sana mama. Naanza kujipanga.”
“Sawa, vipi wenzako lakini?”
Nilisita kumjibu, nikabaki namwangalia tu, naye alibaini
kwamba nimepata mshtuko kwa swali lake.
“Vipi wapangaji wenzako, naamini utakuwa hujaonana
nao?”
“Ni kweli mama, tena hebu nakuomba kidogo,” nilisema
nikienda pembeni kidogo ili na yeye anifuate tukaongee.
“Niambie,” alianza kusema.
Nilimuuliza kama kuna anachokijua chochote kile kuhusu
wale wapangaji wenzangu. Alianza kwa kusema:
“Kusema ule ukweli sina kwa undani, ila napenda kukwambia
kwamba, unaishi na watu ambao unahitajika moyo wa ziada ili
uweze kuendelea kuishi nao.
“Pale mbali na wewe, pameshakaa wapangaji wengine saba,
tena wote kama wewe, hawajaoa. Lakini kinachoshangaza ni
kwamba, wanaondoka baada ya wiki mbili, mmoja aliondoka
baada ya siku tatu tu.”
“Kwa hiyo hakuna hata mmoja aliyewahi kukwambia ameona
nini kule ndani?”
“Hakuna.”
“Lo! Mimi mama mambo ninayoyaona yanatisha.”
“Kama mambo yapi, nisimulie kidogo.”
Nilipotaka kuanza kumsimulia huyu mwanamke, ghafla
alitokea msichana mmoja, mweupe, mrefu kiasi, amejazia
sehemu mbalimbali za mwili, akaguna na kusema:
“Kaka Humuli mambo vipi, za siku?”
Nilipata kigugumizi kikubwa kumjibu mambo poa kwani
sikumjua na sikuwa nakumbuka chochote kuhusu yeye, sura
yake ilikataa kichwani mwangu.
15
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

“Wewe ni nani kwani?” nilimuuliza.


Akaachia tabasamu kwa mbali, uzuri wake ukaongezeka.
“Ha! Humuli, hunikumbuki mimi, kweli?”
“Sikukumbuki hata kidogo.”
“Sasa we binti, kama wewe ndiyo unamkumbuka si
umkumbushe mlionana wapi?” yule mwanamke alisema kwa
sauti ya mshangao.
Lakini yule msichana mrembo alimwangalia yule mwanamke
kwa macho yaliyojaa hasira…
“Mama huhusiki.”
“Najua, lakini unapoteza muda kwa kuzungushazungusha
wakati kumbe wewe unamkumbuka, umeshajua yeye
hakukumbuki na amekwambia tayari.”
Nilishangaa kumwona yule msichana akibetua kichwa kama
aliyekuwa akiweka vizuri nywele zake, ghafla yule mwanamke
niliyekuwa naye akajishika kichwa na kulalamika kinamuuma
sana.
“Jamani kichwa! Kichwa jamani, daa!”
“Vipi mama, imekuwaje kwani?” nilimuuliza.
“Kichwa Humuli, kinavuta ghafla! Uwiii.”
Nilianza kuogopa, nilihisi naangukiwa na msala maana akifa
pale na watu waliona nikienda naye pembeni si nitahojiwa
mimi?
“Kwani mama una kawaida ya kuumwa kichwa?” nilimuuliza
nikimsogelea ambapo yeye sasa alikuwa ameinama.
“Sina, ndiyo nashangaa hapa.”
Niliona hakuna dawa nyingine zaidi ya kumpeleka kwake ili
nikaungane na familia yake kumpeleka hospitali. Lakini kabla
ya kufanya hivyo niliinua macho ili nimwambie yule dada
anisaidie na kama anataka kunikumbusha, hayo yangefanyika
baadaye.
Ile naanza kusema anti huku nikiwa nimeinua macho,
nilishangaa kutomwona yule msichana pale.
“Khaa!” nilijikuta nikisema hivyo.
16
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

“Mama twende nyumbani ili tukupeleke hospitali na watoto


wako.”
“Ha! Mbona kimeachia,” alisema akionekana kushangaa na
kuniangalia, alikuwa amepanua kunywa.
“Kweli?”
“Eee, niko mzima kabisa.”
“Au?” nilitaka kusema neno lakini sikulimaliza, nikahisi ulimi
unakuwa mzito si kwa kushikwa bali kwa matakwa yangu.
“Humuli,” aliita yule mama.
“Naam.”
“Ni kweli yule binti humjui?”
“Simjui mama.”
“Kuna mawili hapo, humjui au humkumbuki.”
“Vyote mama, simkumbuki na pia simjui.”
“Lakini wewe si alikutaja kwa jina?”
“Mwenyewe nilishangaa sana.”
“Basi Humuli nimeshaelewa, kwaheri, nimeelawa ni kwa nini
nimeugua kichwa na yule ni nani, pole sana wewe kijana,”
alisema yule mwanamke huku akiondoka zake kuelekea
kwake.
Nilimtazama, lakini baadaye nilirudi kwenye kibanda cha
chipsi.
“Mzee nakuona na miss jini,” muuza chipsi mmoja alisema.
“Yupi, yule mwanamke?”
“Hapana, yule msichana.”
“Mi simjui, kwani anaishi wapi? Maana kasema ananijua,
ameniita na jina.”
“Khaa! Kumbe wewe kama sisi. Huyu dada anaishi mitaa
hiihii, lakini hakuna hata mmoja anayejua nyumba anayoishi!
“Kuna jamaa mmoja anaitwa Maleke, Maleke aliwahi
kumfuatilia kwa nyuma lakini alishindwa kujua aliingia
nyumba gani!”
“Mh! Au ni jini?” niliuliza kwa mshtuko mkubwa.

17
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

“Ndivyo watu wanavyosema, sasa alipokuja kusimama na


wewe, tukawa tunabishana, wengine wanasema ni miss jini,
wengine siye, lakini alipokuwa anaondoka tukagundua ni miss
jini.”
Basi, tuliishia hapo, nikachukua chipsi zangu na kwenda nazo
nyumbani, niliamua kwenda kulia kule.
Nilifika, nikasukuma mlango mkubwa nikazama ndani
kwangu. Lakini wakati napita kwenye usawa wa chumba cha
wale wenzangu nikasikia vicheko, tena vicheko kwelikweli.
Sikuwajali, nikaingia sebuleni kwangu, nikafunga mlango
kwa ndani, nikaweka chipsi juu ya meza, nikaenda pembeni ya
chumba ambako kuna ndoo ya maji ili nichote ya kunawa.
Wakati naanza kula nilihisi na kugundua kitu. Niligundua
mabakimabaki ya chipsi na kuku juu ya meza yangu wakati
ukweli ni kwamba, tangu nimehamia pale sijawahi kula chipsi
wala kuku.
“Humu ndani kuna mtu anaingia kufanya mambo yake, lini
mimi nimekula chipsi na kuku humu ndani?” nilijiuliza, nikasikia
kicheko kutoka kwa wenzangu.
“Haa! Haaa! Ha! Haaaa…aaaa.”
Niliinua macho kuangalia juu kwenye ‘silingbodi’ kama vile
niliyekuwa nimeona kitu, akili yangu ikawaza kitu cha dakika
chache nyuma, nacho ni hiki:
“Humuli.”
“Naam.”
“Ni kweli yule binti humjui?”
“Simjui mama.”
“Kuna mawili hapo, humjui au humkumbuki.”
“Vyote mama, simkumbuki na pia simjui.”
“Lakini wewe si alikutaja kwa jina?”
“Mwenyewe nilishangaa sana.”
“Basi Humuli nimeshaelewa, kwaheri, nimeelawa ni kwa nini
nimeugua kichwa na yule ni nani, pole sana wewe kijana.”
Nilianza kuamini kwamba, kuna uhusiano mkubwa kati ya

18
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

yule msichana na wale wapangaji wa pale ndani nilipo,


inawezekana alinijua jina kwa sababu naishi nao na wana
uwezo wa kujua jina la mtu kulingana na mazingira yao.
Pia niliwaza kwamba, kuna uwezekano mkubwa yule
msichana alitokea baada ya maono yao kuniona mimi na yule
mama wa jirani tukitaka kuwazungumzia wao kama wapangaji
wenye maajabu hivyo hawakupenda iwe hivyo ndiyo maana
msichana akaibuka na kusababisha mvurugano.
“Itakuwa kweli, ndiyo maana yule mama naye alisema
ameshajua ni kwa nini aliugua kichwa ghafla, alijua yule
msichana ni nani na kwa nini yeye kasikia maumivu ya ghafla
vile.”
“Lakini pia kuna wale wauza chipsi, nao niliwakumbuka
hasa yule mmoja aliyesema yule msichana wanamjua, anaishi
mtaani, lakini hawajawahi kubaini anaishi nyumba gani na
kwa mzee nani wala anajishughulisha na nini,” hayo yote
niliyawaza mimi.
Nilisimama, nikachukua sabuni ya kuogea ambayo
haijafunguliwa, nikaipiga chini kwenye kapeti kwa hasira
huku nikisonya, nikasema kwa sauti ya chini:
“Humu ndani naishi na majini.”
Kule chumbani nikasikia wakicheka.
“Si unaona, nimesema mimi, lazima naishi nao humu ndani,
da! Najuta sana,” nilisema.
Kicheko kikasikika tena, safari hii kilikuwa cha juu zaidi
kuliko kile cha awali.
Moyo ulijaa mawazo, akili ilihisi uchungu wa maisha,
niliwaza fedha nilizozilipa kwa ajili ya kupanga mle ndani,
nikamkumbuka dalali, niligundua alichofanya ni kunitapeli
na hakuna lingine wala hakuwa msaada kwangu.
“Mimi ni mwanaume, kama niliweza kupata fedha za kupanga
hapa, sishindwi kupata nyingine za kupanga sehemu nyingine
tena mbali na hapa,” nilisema kwa moyoni.

19
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

TASWIRA ZA WATU UKUTANI USIKU

Usiku nikiwa nimelala, nilichelewa sana kupata usingizi,


ghafla nikaona taswira za watu ukutani, wawili tena wakiwa
wamesimama, ni mwanamke na mwanaume. Niliogopa sana,
nikainua kichwa polepole kuwaangalia kwa umakini, japo
kulikuwa na giza, lakini niliweza kuona vizuri lakini si kwa
uwazi mkubwa kama ambavyo taa ingekuwa inawaka.
Ni kweli walikuwa watu wawili kama nilivyoona, tena weupe
nikimaanisha si watu weusi. Walikuwa wakionesha vitendo vya
kucheka huku wakijinyonganyonga.
Kuna wakati walitembea mpaka jirani na kitanda changu
kisha wakageuza na kurudi pale ukutani. Nilipeleka mkono
hadi kwenye swichi ya kitanda (bed switch), nikawasha, cha
ajabu sikumwona mtu wala dalili pale ukutani.
Niliamka nikiwa nahema kwa kasi mpaka nikajishika kifuani,
nikafungua mlango na kutoka nje ili nijifanye nakwenda chooni
lengo langu lilikuwa kupata picha kwa wenzangu kukoje maana
niliwashuku wao na wale walioonekana chumbani kwangu.
Kwa wenzangu niliwasikia wakikoroma kwa zamu. Nikajiuliza
ina maana si wao waliokuja chumbani kwangu? Niliona ni utani
wa hali ya juu.
Niliamua kurudi chumbani na kukatisha safari ya kwenda
chooni, nikafunga mlango wangu kwa funguo na kupanda
kitandani, nilizima taa ili nione kama yale mauzauza yatatokea
tena.
Ukimya ulitawala kwa muda bila kujitokeza chochote,
nikaanza kupitiwa na usingizi kwa kusinziasinzia, ghafla ukutani
nikawaona tena walewale watu wawili.
Safari hii walikuja hadi kitandani, wakakaa, wakasimama,
wakaenda kwenye kabati, wakafungua, wakatoa mashuka
na kujifunika, wakayarudisha, wakaenda nyuma ya mlango,
wakatungua mashati yangu mawili, wakagawana na kuyavaa
kisha wakayavua, mmoja mwanaume akaenda sehemu yenye

20
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

redio, akapeleka mkono, nikajua anataka kuiwasha, lakini


hakufanya hivyo.
Nilichoamua kukifanya akilini ni kuwasha taa kwa ghafla
na kuwavamia na nilipanga kumvamia mwanamke nikiamini
ndiye aliyekuja kule kwenye chipsi.
Polepole nilipeleka mkono hadi kwenye swichi, nikawasha
taa kwa ghafla huku macho yangu yakiwa kwao, lakini
sikumwona hata mmoja! Kwangu haikuwa mapambano bali
nilichukulia kama changamoto za maisha.

***
Asubuhi, niliamka nikiwa nimechoka sana, lakini kabla
sijatoka kitandani nilisikia nje ya mlango kukiwa na hali ya
watu kutembeatembea tena kwa kasi, niliinua shingo ili nione
kama nitasikia zaidi, lakini kukawa kimya.
Niliamka, nikatoka, nilikwenda sebuleni kwanza kuangalia
kama kuko salama. Nilishangaa kukuta mezani kuna mfuko
wa rambo uliojaa chipsi kuku kama nilivyonunua mimi, lakini
zangu nilikula, sasa zile sikujua zilitoka wapi.
Niliubeba ule mfuko nikatoka nao,nilifungua mlango mkubwa
wa nje nikautupia pembeni kidogo, niliporudi, nikaenda
chooni. Mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani kwani hata
niliposhika kitasa na kukivuta kilikuwa kigumu.
Hii iliashiria kwamba kuna mtu, kwa hiyo moyoni nilisema
nisimame palepale nje ya mlango hadi atoke. Nilisimama
eneo ambalo akitoka tu, uso kwa uso na mimi.
“Tuone leo, wao si wajanja, leo nimemnasa mmoja wao,”
nilisema moyoni.
Dalili zote zilionesha kwamba mle chooni mlikuwa na mtu
kwani niliweza kusikia hata kuhema kwake, mara mlio wa
maji, mara alikohoa, tena kwenye kukohoa nikabaini mtu
mwenyewe alikuwa ni mwanamke ndiye aliyekuwa mle.
“We kuhoa mpaka utapike, lakini mimi nipo hapa mpaka
utoke,” nilisema moyoni.

21
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

Nilisimama sana, ikafika mahali nikachoka, lakini moyoni


nikasema siondoki hata iweje, lakini nilishtuka kitu, niligundua
muda mrefu sijazisikia zile dalili kama maji au kuhema,
nikafunguka akili.
“Mh! Siyo kwamba ametoka?”
Ile namalizia kusema ‘ametoka?’ nikasikia kicheko kutoka
kwenye chumba chao. Vicheko vikubwa sana cha kike na
kiume.
Nilirudi chumbani mwili ukinisisimka, hapo ndipo niliamini
mia kwa mia kwamba, nilikuwa nadili na watu wasiokuwa wa
kawaida.
Niliingia chumbani, nikampigia simu dalali.
“Haloo,” niliita.
“Haloo. Halooo,” nilirudia lakini sikupokelewa.
Nikiwa nimeachana na simu, mara iliita yenyewe, alikuwa ni
dalali nikapokea.
“Haloo,” niliita.
“Haloo,” niliitikiwa lakini sauti haikuwa ya dalali.
“Mzima bwana?” nilisalimia.
“Tuone leo, wao si wajanja, leo nimemnasa mmoja wao.”
Ha! Nilishtuka sana, nilisikia sauti yangu mwenyewe ikisema
hivyo. Ikaendelea.
“We kohoa mpaka utapike, lakini mimi nipo hapa mpaka
utoke.”
Nilikata simu, nilikuwa nahema sana, mapigo ya moyo
yalikuwa yakienda kwa kasi ya ajabu huku nikishindwa kuona
sawasawa.
“Hii ni hatari sasa,” nilisema.
***
Usiku wa siku hiyo sikulala kusema kweli kwani kila
nilipofikiria maisha yale sikuona sababu ya kuendelea kuishi
pale. Moyoni nilisema kwamba, ni afadhali ningeishi na watu
majambazi kuliko hawa, nafuu ningepanga nyumba moja na
makahaba kuliko kupanga nyumba moja na majini.

22
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

Nilichoamua, asubuhi nikifika kibaruani tu niombe ruksa


kisha nianze kumsaka yule dalali na pia nitafute dalali
mwingine ambaye atanitafutia vyumba kwingine na si maeneo
yale tena kwani niliyaona yana nuksi.

***
Asubuhi kulikucha salama kabisa, tena usiku wa siku hiyo
sikuona mauzauza wala dalili zake.
Nilikwenda kuoga bila kukagua mazingira, moyoni nilisema
liwalo na liwe kwa maana kwamba, wawepo wasiwepo sawa
tu.
Bafuni niligundua wameshaoga kwani kulikuwa na majimaji
ya muda mfupi uliopita. Nilipomaliza kuoga, nilijiandaa na
kutoka. Nje nilikutana na mtu ana mkokoteni, akanisalimia.
“Za asubuhi bwana mkubwa?”
“Salama, karibu sana.”
“Asante, kuna watu fulani wanaishi humu nina shida nao.”
Aliposema hivyo nilishtuka sana, niliamini yeye ni mmoja
wa wale ila amejigeuza kwa kujifanya ana shughuli za
mkokoteni.
“Unawajua kwa sura?” nilimuuliza huku nikiwa na wasiwasi
maana alinikazia macho.
“Siwajui.”
“Sasa una shida nao kivipi watu usiowajua kwa sura?”
“Ni kwamba, kuna binti mmoja huwa wanamtuma niwaletee
maji, nikifika hapa huyo binti anabeba madumu kupeleka
ndani, sasa jana nilikutana na huyo binti nikamuuliza kuhusu
malipo yangu ya mwezi, akasema nije nifuatilie mwenyewe.”
Nilishangaa sana kusikia hivyo. Nijuavyo mimi mle ndani
mna watu wawili, mwanamke na mwanaume, sasa kama kuna
binti hilo lilikuwa jipya kwangu, labda lakini.
“Huyo binti naye anaishi humu au?” nilimuuliza.
“Sidhani, inaonekana kama huwa wanamtuma tu.”
“Kwa nini huamini kama anaishi humuhumu ndani? Hafanani

23
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

na wao wenyewe?” hili swali niliuliza likiwa na mtego mkubwa


sana, nilitaka nijue uhalisia wake.
“Siwezi kusema hafanani wakati wao siwajui kwa sura.”
Hapo ndipo nilipopataka, nilidhani atasema hafanani nao,
ningejua ni walewale.
“Oke, nadhani wameondoka kwenda kazini,” nilimwambia.
“Ah! Sasa mimi fedha zangu nitazipataje jamani?”
“Subiri wakirudi jioni.”
“Wewe utakuwepo?”
Nililishangaa swali hilo, hakuwa akinidai mimi lakini anataka
niwepo?
“Unataka niwepo?”
“Ee.”
“Kwa nini?”
“Naamini utanisaidia kuzipata fedha zangu.”
“Uliwahi kuja wakagoma kukupa?”
“Siyo hivyo, ila kila nikija, nikigonga mlango huwa
hawafungui.”
“Basi nitakuwepo.”
“Asante kaka. Nije saa ngapi?”
“Saa moja nitakuwa nimerudi.”
Aligeuza mkokoteni na kuondoka zake huku akisema:
“Muda huo nitakuwa nimefika kaka.”

DAWA YA MAJINI NI BANGI?


Niliondoka kwenda kazini kuomba ruksa. Lakini wakati
naondoka kazini, mfanyakazi mwenzangu mmoja aliniuliza
nakwenda wapi, nikaamua kumsimulia kwa ufupi kisa
changu.
“Khaa! Sasa hapo tatizo liko wapi, mbona dawa ipo rahisi
sana,” alisema.
“Rahisi! Ni ipi hiyo?”
“Sikia, twende pembeni nikakusimulie,” aliniambia yule
24
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

mfanyakazi mwenzangu huku akiangalia kulia na kushoto


kama mabosi watatokea.
Tulikwenda kusimama pembeni, akaanza kuniambia:
“Sikiliza, kama unaishi nyumba ya namna hiyo, unachotakiwa,
kila siku asubuhi na jioni au usiku unapuliza bangi ndani ya
nyumba, kama ni majini, mapepo sijui nini, utaona mambo poa
kabisa.”
Sikuamini maneno hayo, nikamuuliza mara mbilimbili kama
ni kweli.
“Khaa! Nina mjomba angu aliwahi kuishi kwenye nyumba ya
hivyo, akaenda sehemu akaelekezwa dawa ni hiyo, akaitumia,
mpaka sasa anaishi kwa raha hakuna cha majini wala mapepo,”
alisema.
Nilimsikiliza nikianza kuamini kwa mbali, lakini nilifika
mahali nikamuuliza hiyo bangi mimi nitavuta au nitaiwasha ili
itoe moshi yenyewe?
“Ukishaiwasha, utaiweka mezani au popote ndani kwako,
lakini angalia isizimike ili moshi wake usambae chumba kizima
au sebule nzima.”
“Hilo linawezekana,” nilimwambia nikimtumbulia macho.
Kwa sababu nilikuwa nimeshaaga, ilibidi niondoke tu na
kurudi baadaye. Nilikwenda mtaani, nilitafuta bangi nikapata
maeneo ya Kariakoo, nikaitia mfukoni.
Nilizurura sana siku hiyo, saa tisa kamili nilikuwa njiani narudi
kazini. Nilipiga hesabu za kufika kazini na kuondoka, maana
muda wa kutoka kazini ni saa tisa na nusu.
Wakati napita pale Kituo cha Polisi Msimbazi, fujo zikazuka,
kuna machinga wawili walikuwa wanapigana kwa sababu ya
kugombea sehemu ya kufanyia biashara, katika ugomvi huo
mimi nilibaini mmoja wao ndiyo mwenye kosa.
Nikampa laivu kuwa yeye ndiye mwenye tatizo, alikuja juu,
akachukua boksi lenye viatu na kunirushia, likanipata kwenye
bega la kulia, sikukubali, nikaokota jiwe na kumrushia,
likampata mkononi.
Polisi walifika haraka sana, wakanikamata mimi, yeye na yule

25
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

machinga niliyeona anaonewa, tukapelekwa Msimbazi polisi.


Tulipofika pale, afande aliyetukamata alituamuru kuvua
viatu, mikanda, simu kuweka pembeni. Halafu mmoja alianza
kutusachi mifukoni. Wakati tendo hilo linaanza kwa wenzangu,
ndipo nikakumbuka mimi mfukoni nina vipisi viwili vya
bangi.
Nilitaka kutoka mbio kituoni hapo, lakini sehemu tuliyokaa,
ningesema nitoke, nisingefika nje au hata kama ningefika
ningekamatwa au kupigwa risasi kama mhalifu, nilitetemeka,
mwili uliisha nguvu.
Alipofika kwenye zamu yangu, yeye mwenyewe alishangaa
kuniona nachezesha miguu kama niliyebanwa na haja ndogo,
akaniuliza:
“We vipi, unaumwa?”
Nikamjibu naumwa afande.
“Unaumwa nini?”
“Sijui, nadhani homa.”
Hakunijibu, alianza kwa kutumbukiza mkono kwenye
mfuko usiokuwa na kitu, akahamia wa nyuma ambao una
waleti, akapeleka wa kulia kwangu ambao ndiyo wenye
bangi, aliposhika, akakunja sura, alipotoa akashtuka sana na
kusema:
“Haa! Hii ni bangi siyo?”
Sikumjibu kwani niliamini ameshaijua. Wenzake waliokuwa
kaunta wakaacha mambo yao na kunigeukia mimi, nao
wakashangaa sana.
Mmoja alikuwa amekaa juu ya stuli, akashuka huku
akiniangalia kwa kunikazia macho.
“Unakuja kituo cha polisi na bangi, wewe unatutafuta nini
sisi?” aliuliza yule aliyeshuka kwenye stuli.
Niliambiwa nafunguliwa kesi ya pili, ya kwanza kupigana na
kujeruhi ya pili kukutwa na bangi!
Nilijitetea nikisema bangi ile si kwa ajili ya kuvuta bali
nilikuwa nina shida nayo.

26
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

“Wewe usitufanye sisi watoto wadogo, tunawajua nyie raia,”


alisema yule afande aliyenisachi.
Lakini afande mmoja wa kike ambaye muda wote alikuwa
akiangalia tu, akawaambia wenzake:
“Lakini huyu kaka mbona hafanani na kuvuta bangi, muulizeni
ana shida nayo gani?”
Wale wenzake wakanigeukia na kuniuliza:
“Haya, wewe mwananchi, raia kabisa, unaweza kuwa na shida
gani na bangi mbali na kuvuta?”
Niliwasimulia kila kitu, tena nilifika mahali nikawaambia
kama kuna asiyeamini, tuongozane hadi nyumbani, Magomeni
akaone maajabu ambayo hayahitaji kuelekezwa sana ili
kuamini kama yapo au la!
Palipita ukimya wa sekunde kadhaa, mmoja wao akaniuliza:
“Kama ni kweli au tufanye ni kweli, ni kwa nini umemuumiza
huyu?”
Nilisema kilichotokea, yule chinga niliyemsaidia naye
akanitetea kwa kusema hivyo hivyo, lakini afande mmoja
akasema nilijichukulia sheria mkononi ambapo ni kosa
kisheria.
Niliomba sana wanisamehe kwa yote, nikasingizia kwamba ni
kwa sababu kichwa changu hakipo sawa kwa kuishi nyumba
moja na majini.
Namshukuru mmoja wao aliniambia niondoke lakini
nihakikishe situmii bangi katika kujitibu kwani serikali
haiamini kama bangi ni dawa.
Nilipotoka, nilikwenda kuinunua nyingine, lakini akili iliingia
hisia kwamba, huenda yule dada wa ajabu mle ndani ndiye
anayecheza michezo ili kunikwamisha kwenda na bangi
ndani ya nyumba, nikasema moyoni ngoja ninunue hii nione
kitakachotokea, nikanunua tena misokoto miwili.
Nilitembea kuelekea kituo cha daladala. Njiani nilimpigia
simu yule mfanyakazi mwenzangu aliyenijulisha kuhusu dawa
ya kutibu nyumba yenye majini, nikamwambia sitaweza kurudi
kwani nilipata wakati mgumu kidogo njiani.
27
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

Alinielewa, akaniuliza kama nimepata, nikamjibu kila kitu


kimekwenda sawa, lakini sikumwambia kuhusu timbwili
lililojitokeza.
Nilipanda daladala nikashuka Magomeni, niliingia ATM kutoa
fedha kidogo, kisha nikatoka. Wakati natafuta mwelekeo wa
kwenda nyumbani, nilimkumbuka dalali, nikampigia simu.
“Halo.”
“Halo habari za kazi bwana?”
“Nzuri, pole na kazi na wewe mwenzangu?”
“Nimepoa. Bwana vipi kuhusu nyumba?” Nilimuuliza.
“Nyumba imefanyaje?”
“Si nilikusimulia matatizo yake, umesahau?”
“Kwani ulisema matatizo yake yakoje vile?”
Nilimwelezea kwa kirefu, nikafika mahali nikamwambia hadi
nilivyompigia simu halafu ikapokelewa na sauti ya ajabuajabu,
alicheka sana.
“Wewe bwana acha kunichekesha.”
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Yaani simu yangu mimi halafu apokee mtu mwenye sauti ya
ajabuajabu, kwa nini sasa?”
“Mimi pia sijui.”
“We ulikosea namba.”
“Labda bwana siwezi kukazania sana,” nilimjibu kwa kinyongo
kwani namba yake niliisevu na ninapompigia huwa nasachi
jina tu, sasa nilikosea kivipi?
“Enhe, unasemaje bwana?” aliniuliza.
“Nimeshakwambia bwana.”
“Kwa hiyo unashauri nini?”
“Nataka pesa zangu nikapange kwingine.”
“Da! Hilo halitawezekana kirahisi bwana, maana mpaka
nimpate mpangaji mwingine atoe fedha ndipo nikulipe wewe
na mpangaji atakayekuwa tayari kutoa fedha lazima akute
nyumba tupu, sasa wewe utalikubali hilo?”

28
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

“Naweza kulikubali, ila tuandikishiane.”


“Kwamba?”
“Kwamba unajikomiti nikiondoka, akiingia mpangaji
mwingine tu unanilipa pesa zangu.”
“Ngoja nitakupigia,” alisema dalali na kukata simu.
Nilipokuwa nakaribia nyumbani, nikakutana na yule
msukuma mkokoteni wa maji.
“Kaka za kazi?”
“Nzuri, vipi wewe?”
“Niko sawa, ndiyo unarudi?”
“Ndiyo.”
“Najua jamaa hawajarudi, nitakuja muda uleule tuliopanga.”
“Sawa, karibu sana.”
“Asante sana.”
Niliingiza funguo ili kufungua mlango, lakini nikagundua
kwa ndani kulikuwa na funguo nyingine maana nilichungulia.
Nilipousukuma, ulifunguka. Hii ina maana wale watu wa
ajabu walikuwa wamesharudi, wako ndani. Niliingia ndani,
nikafungua mlango wa sebuleni, nikaingia humo.
Nilifikia kwenye kochi kubwa, nikajilaza. Sikuangalia kama
kweli wenzangu walikuwa wamesharudi, ila nilisikia sauti ya
muziki wa redio, nikajua wapo.
Mara nikasikia mlango wao mmoja ukifunguliwa, nikasikia
mtu akitoka. Kwa mara ya kwanza nilisikia akisema:
“Kama utamkamata anavuta bangi apelekwe polisi, ndiyo
dawa yao watu wa aina hii.”
Nilishtuka, nikakaa. Nikawaza kama ninachosikia ni cha
kweli au?
Huyo aliyekuwa akisema hayo ni mwanamke na ilionekana
alitoka kuelekea uani. Nikatoka ghafla, nikaona kisigino cha
mguu mmoja kikimalizia kuingia chooni.
Nilirudi chumbani huku najiuliza kama hawa watu walisema
vile kwa sababu wamejua mimi nimenunua bangi au? Na ni
kwa nini wazungumze Kiswahili kwa mara ya kwanza siku
29
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

hiyo?
Baada ya dakika mbili, nilimsikia akirejea chumbani kwake
huku akisema:
“Mimi mtu anayevuta bangi siku yoyote na mahali popote pale,
nikimwona nampeleka polisi ajue mimi ni nani. Haiwezekani
watu wawe wanavuta bangi hovyo tu.”
Moyoni nikasema hata iweje, hii bangi leo lazima niichome
humu ndani. Mkienda polisi msipoenda mtajua wenyewe.
“Mimi siwezi kuishi katika mazingira magumu namna
hii wakati pesa ni yangu. Kwa nini ustaarabu usiwepo?”
nilisema moyoni nikipeleka mkono mfukoni ili kutoa ile bangi
niliyonunua mara ya pili.
Niliipata, nikaitoa. Niliiweka kwenye meza kisha nikaendelea
kulala nikiusaka usingizi kwa nguvu zangu zote maana
nilijisikia kuchoka sana. Hapo nilikuwa sijaenda chumbani
kwangu.
Sikumbuki ni muda gani nilipitiwa na usingizi, ila nakumbuka
wakati nalala ilikuwa saa kumi na moja. Nilipokuja kushtuka
ilikuwa saa kumi na mbili na nusu. Ina maana nililala kwa saa
moja na nusu.
Jicho langu moja kwa moja lilitua kwenye bangi pale mezani,
sikuiona.
Nilihamaki kwa kusema ha! Nani amechukua bangi yangu?
Sikujibiwa na mtu, ukimya ulitawala huku akili ikiniambia wale
wapangaji wenzangu watakuwa wanahusika moja kwa moja.
Baada ya muda nilitoka mle sebuleni, nikaenda chumbani.
Nilifungua mlango na kusimama kwanza kabla ya kuzama
ndani. Niliangaza kila kona, nikabaini kitu.
Niligundua kwamba, kuna mtu alikaa kitandani maana
nilipoondoka asubuhi nilikuwa nimekitandika, muda huo kwa
pembeni upande wa mbele kulikuwa na alama za makalio.
Alama hiyo ilinipa picha kuwa, aliyekaa alikuwa na makalio
makubwa! Nilipoangalia chini kwenye kapeti nikabini kitu
kingine kwamba, aliyekaa alikuwa na mafuta kwenye miguu
kwani iliweka alama kuzunguka miguu yake.

30
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

Aidha, nilibaini jambo jingine kwamba, aliyekaa kitandani


pia alikuwa akisimama na kutembeatembea kwani alama
ya miguu yenye mafuta ilionekana sehemu mbalimbali za
chumbani kwangu.
Mara nikasikia hodi ikigongwa mlango mkubwa.
Niliikumbuka ile sauti kwamba ilikuwa ya yule msukuma
mkokoteni wa maji.
“Nakuja,” nilisema kwa sauti kupitia dirishani kwani chumba
changu na sebule yangu vilikuwa upande wa mlango mkubwa
wa kuingilia.
Nilitoka mpaka mlangoni, nikafungua na kumkuta yule
kijana.
“Bro vipi, wapo wale watu ndiyo nimekuja hivi.”
Nilimshika mkono, nikamvuta kumwingiza ndani bila kusema
naye. Nilimwelekeza vyumba vya wale wapangaji wenzangu
kisha mimi nikaingia chumbani kwangu.
Nilikaa kitandani na kutega sikio kitakachotokea huko.
Nilimsikia yule kijana akigonga mlango. Aligonga mara tatu,
kisha nikasikia mlango ukifunguliwa, sikuamini. Nilitaka
kutoka, lakini nikasema nisubiri hadi mwisho nione.
Baada ya mlio wa kufunguliwa kwa mlango, ukafuatia
mlio wa kufungwa halafu ukapita ukimya. Akilini nilijua
wamemkaribisha na wakafunga mlango na sasa wanaongea
naye.
Cha ajabu, kila nilipofuatilia ili kujua kama mlango
utafunguliwa na yule kijana kutoka, sikufanikiwa kugundua
hali hiyo, nikaanza kuingia wasiwasi.
“Ina maana tangu wakati ule hadi sasa bado wapo ndani?
Wanaongea nini sasa? Au wanapigiana mahesabu? Si yule
kijana alisema anadai pesa nyingi?” maswali hayo yote
yalikuwa yangu lakini majibu yake sikuyajua.
Usiku uliingia, muda ukazidi kwenda, sikusikia ishara yoyote
ya yule kijana kutoka. Zaidi sana nilisikia wale wapangaji
wenzangu wakipika kwa kukaangiza kitu kama nyama.
Mimi nilitoka, nikaenda kutafuta chakula, nikarudi nacho
31
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

nyumbani.Nikala,nikaenda kuoga,nikarudi kitandani na kulala,


sikuona dalili ya mawengewenge wala mang’amung’amu.

***
Asubuhi niliamka kwa kushtuka, lakini sijui nini kilinishtua ila
ni kama kuna mtu alinivuta mguu mmoja. Hakukuwa na kitu
chochote chumbani mwangu. Nilitoka na kwenda kusimama
kwenye dirisha, nikachungulia nje. Kulikuwa shwari.
Nilipotoka kuoga nikiwa navaa nguo ili kuondoka, nikasikia
wenzangu wakitoka.
Nilisimama tena dirishani kwani kwa mtu anayetoka kwenye
nyumba ile na kwenda popote ilikuwa lazima apite mbele ya
dirisha langu.
Baada ya muda walifungua mlango mkubwa, nikasikia
wakiufunga, lakini baada ya hapo sikumwona mtu yeyote yule
akipita mbele ya dirisha.
Na mimi nilipomaliza kujiandaa, nilitoka, nikafungua mlango
na kutembea zangu. Mbele kidogo nilikutana na watu kama
kumi wamesimama wakiongea.
Niliwasalimia nikawauliza kama kuna usalama.
“Usalama ni mdogo bwana, kuna kijana mmoja amepotea.
Tangu jana usiku alipotoka kwa mkewe akasema anafuatilia
madeni ya biashara zake hajarudi,” alisema mzee mmoja
ambaye alisimama akiwa amejishika mikono kwa nyuma.
“Ni biashara gani anafanya?” niliuliza.
“Huwa anauza maji kwenye mkokoteni.”
“Ha! Ni yule muuza maji?”
“Huyo huyo,” alisema yule mzee.
Akili za haraka nikasema hapa ndipo pa kujua wale wapangaji
ni akina nani, inabidi niseme ukweli ili waende polisi, najua
polisi watakuja kukagua ndani.
“Lakini mbona jana usiku alikuja kwangu kudai pesa yake?”
nilihoji kwa uso wa wasiwasi.
“Ulipomlipa aliondoka?” mwanamke mmoja aliniuliza.
32
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

“Siyo kwangu, ila mimi ndiye niliyemfungulia mlango.


Alipoingia akawaulizia wapangaji wenzangu, nikamwonesha
chumba, akapiga hodi, akakaribishwa ndani.”
“Hukumuona kutoka?”
“Kwa kweli sikufuatilia maana na mimi nilirudi chumbani
kwangu.”
Wale watu wakaniuliza kama naweza kuwapeleka pale
nyumbani, nikawaambia kwa muda ule hapakuwa na mtu,
wanarudi jioni.
“Basi tunakwenda kuwaambia ndugu zake, jioni watakuja, si
nyumba ile pale?”
“Ndiyo.”
MTU MWEUSI ATOKA NDANI, WAPITA NJIA WAMWONA NI MBWA

Nilipofika kazini na kuanza kazi, akili zangu zikawa


zimefunguka kitu. Nilijiambia wale watu wakijua ni mimi
niliyetoa mchoro wote, je nitakuwa salama kweli?
Nilibaini nimechemsha, lakini nikasema moyoni kwamba
potelea mbali, wajue wasijue sawa tu.
Kuna wakati nilipigiwa simu, namba sikuitambua, yaani
ilikuwa ngeni kwenye kumbukumbu zangu. Nilijiuliza
mwenyewe kwamba anaweza kuwa nani, lakini sikupata jibu.
Awali nilisita kuipokea mpaka ilikata, mpigaji akapiga tena.
Nikaamua kuipokea sasa:

“Halooo,” nilivuta sauti.


“Hujambo bwana?”
“Nani mwenzangu?”
“Hujambo, hata kusalimiana pia unataka kujua nani, ungeitika
kwanza kisha ndipo uniulize nani.”
“Sijambo, nani mwenzangu?”
“Angalia sana bwana,” alisema huyo mtu bila kujitambulisha
kisha akakata simu.
Nilibaki nimeshangaa tu, nikaanza kazi ya kuwaza kwamba
33
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

anaweza kuwa nani na ni kwa nini aniambie angalia sana?


“Atakuwa jamaa wa nyumbani, kwa vyovyote vile,” nilisema
moyoni na kuamini hivyo kwani kwa maisha ninayoishi mimi si
rahisi kuwa na maadui.
Mapigo ya moyo yalianza kwenda mbio kwa wasiwasi. Nilijua
nimeingia kwenye mapambano makubwa na wale wapangaji
wenzangu.
Niliendelea kufanya kazi, lakini sikuwa na amani tena. Mara
alitokea yule mfanyakazi mwenzangu ambaye alinipa ushauri
wa kupulizia bangi ndani ya nyumba ili kuwakimbiza majini
au viumbe wote wabaya.
“Vipi mambo yako, yamekwendaje?”
“Mambo gani?” nilimuuliza huku nikiwa namtazama. Kisa cha
kumtazama kwanza ilikuwa kujiridhisha kama kweli ni yeye au
wale wapangaji wenzangu wameamua kunifuata ‘laivu’.
“Si yale niliyokuelekeza kufanya.”
Nilipomkazia macho sana, akasema ana kazi nyingi, akageuza
na kuondoka.
Mlango ulipojifunga tu, nikajiegemeza kwenye meza na
kuwaza mambo kibao. Ilikuwa kama nataka kusinzia, lakini
nikasikia sauti kichwani zikisemezana hivi:
“Halooo.”
“Hujambo bwana?”
“Nani mwenzangu?”
“Hujambo, hata kusalimiana pia unataka kujua nani, ungeitika
kwanza kisha ndipo uniulize nani.”
“Sijambo, nani mwenzangu?”
“Angalia sana bwana.”
Mara nikasikia tena zikisemazana hivi:
“Vipi mambo yako, yamekwendaje?”
“Mambo gani?”
“Si yale niliyokuelekeza kufanya.”
Nilishtuka na kusimama, nikaondoka kwenda nje. Nilikutana
na yule mfanyakazi tena, akaniuliza kama naondoka.
34
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

“Vipi, unaondoka saa hizi?”


“Bado nipo.”
“Kwanza nilisahau kukuuliza, vipi ulifanikisha ile kitu ya
kuvuta kama nilivyokwambia?”
Moyo ulishtuka, nilijua ni watu wawili kwani huyu angekuwa
yule aliyenifuata muda ule, asingesema alisahau kuniuliza.
“Nilifanikiwa kupata bwana, lakini,” nilisema nikimshika
mkono, nikamvutia pembeni kidogo.
“Kuna mambo makubwa kule. Kwanza unajua kama
nimekuona wewe mara ya pili hii leo?”
“Kivipi?” aliniuliza.
Nilianza kumsimulia kila kitu, kuanzia zile bangi hadi nusu
saa kabla sijaonana naye. Alishangaa sana, akasema yeye
ndiyo kwanza anaingia kazini, alikuwa Kariakoo. Pia akasema
kwa siku hiyo ndiyo kwanza ameniona mimi muda ule.
“Sasa itakuwaje ndugu yangu?” aliniuliza.
“Sielewi.”
“Sasa sikia, mimi ninajua nitapata wapi bangi, we usiku saa
moja niambie tukutane wapi, nitakuja nayo halafu nitaiwasha
na kuivuta mimi.”
“Wewe huogopi?”
“Niogope nini?”
“Kufa.”
“Nani ataniua?”
“Si hao watu wabaya.”
“Hamna, hawawezi.”
Nilimkubalia, nikamwambia nitampigia saa moja ili tukutane
akiwa na hiyo bangi yake.
Akili zangu hazikukaa sawa, niliondoka kwenda kutafuta maji
ya kunywa, kisha nikaenda kupumzika kwenye kibanda cha
kuuza vocha za simu.
Pale, mtu yeyote anayenijua angeniona angebaini nina
matatizo mazito kichwani mwangu, kwani sikuwa sawa hata
usoni. Muda mwingi niliwaza maisha ya kwenye ile nyumba,
35
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

hasa usiku wa siku hiyo ambapo najua wale watu wakija ndiyo
balaa litakuwa kubwa zaidi.
“Halafu usiku wa leo lazima watakuja kunifanyia maajabu
yao, lakini dawa yao nisilale. Oke, kumbe bangi itapulizwa leo,
kidogo itakuwa nafuu,” nilisema moyoni, nikashtuliwa na sauti
ya kike nyuma yangu iliyoita jina langu.
Nilipogeuka nyuma, nikamwona dada mmoja aitwaye
Mwantumu Seleman niliwahi kuishi naye Mwananyamala.
Akaniuliza habari za siku.
Niliamua kumsimulia janga langu, lakini ghafla likaja gari,
akaingia huku akiniambia atanitafuta siku nyingine.
Baadaye nilirudi kazini huku nikiwa na hali ya wasiwasi, hata
kazi zangu zikuzifanya sawasawa kama ilivyo kawaida yangu.
Iliniuma sana!
Muda wa kazi ulipokwisha, niliondoka moja kwa moja
hadi nyumbani. Sikutaka kupitia mahali siku hiyo, lakini
nilishakubaliana na yule mfanyakazi mwenzangu aliyesema
atakuja na bangi yake.
Wakati nafungua mlango mkubwa nilibaini wenzangu
walisharudi maana mlango haukufungwa na funguo, nikaingia
ndani. Nilipofika kwenye mlango wangu wa kuingilia sebuleni,
wakati naufungua nikasikia mlango wa chooni unafunguliwa,
yaani ilimaanisha kwamba kuna mtu anatoka.
Ukisimama mlangoni mwangu, mtu akitoka chooni unamuona
bila kificho, hususan kama anakuja vyumbani. Lakini pia
hata akiwa anatoka kwenda uani, utamuona kwa mgongoni.
Nilisita kuingia nikiamini nitamwona mtu huyo. Nilianza kuona
miguu ikitoka, moyo wangu ukashtuka, mara nikamwona mtu
mwenyewe.
Nilijikuta nikisisimka mwili, niliamini naona kivuli chake na si
yeye. Ni mtu mweusi, wakati nilitarajia angekuwa mweupe.
Alivyozidi kunisogelea, nikabaini kuwa, ni yule kijana muuza
maji kwenye mkokoteni.
“Ha! Wewe vipi, unatafutwa sana unajua?” nilimwambia.
Badala ya kunijibu, alikata kona kuufuata mlango mkubwa.
36
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

Na mimi nikamfuata kwa nyuma, nilimkuta akiwa anamalizikia


kutoka nje.
Niliitupa simu kwenye kochi kisha nikatoka kumfuata, na
mimi nilifungua mlango ambao ulishaanza kurudi baada ya
yule kijana kutoka.
Nilishangaa kutomuona popote kule nje.
Wazee wawili walikuwa wanapita, nikawauliza kama
wamemuona mtu ametokea mlangoni pale, wakasema hapana,
ila kuna mbwa alitokea ndani kazunguka nyumba.
“Mh! Mbwa tena?” niliwauliza wale wazee, nao wakasisitiza
kuwa ni mbwa, tena mweusi.
Mapigo ya moyo yalianza kwenda mbio, wasiwasi uliongezeka
kiasi cha kunifanya niishiwe nguvu. Wakati huo wale wazee
walikuwa wakimalizikia kwa mbali.
Niliogopa kurudi ndani, nikawa nimesimama mlangoni.
Wazo lilinijia kwamba, nimpigie simu yule mfanyakazi
mwenzangu kumuomba aje mapema maana hali ni mbaya
sana.
Lakini simu nayo ilikuwa sebuleni kwenye kochi, nitaipataje,
yaani nitaifuataje kule ndani wakati niliamini tayari
kumeshakuwa ukanda wa kifo?
Niliteremka na kusimama nje kabisa, ghafla kwenye dirisha
la chumbani kwangu nikaona kama mtu anachungulia nje,
nilikaza macho ili kumwangalia vizuri, akapotea.
“Mh! ni kweli?” nilijiuliza mwenyewe. Ukweli ni kwamba
alikuwepo mtu, tena mweusi au niseme Mwafrika kama mimi.
Nilikwenda pale dirishani, nikapanda ili kuchungulia, nikaona
mlango unajifunga kuashiria kuna mtu alitoka maana mlango
ule ulikuwa hauwezi kukaa wazi, ni lazima ujifunge wenyewe
na mbaya zaidi mimi nilikuwa sijaufungua zaidi ya ule wa
sebuleni.
Kuna jamaa mmoja alikuwa anakuja kutokea upande
ninaoondokea kwenda kazini, simfahamu lakini
nilimsimamisha.

37
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

“Bro kuna ishu hapa inatisha kidogo, naomba msaada


wako.”
“Kuna nini?” aliniuliza.
Nilimsimulia kila kitu cha siku ile tu lakini, sikugusia mambo
ya nyuma.
“Du! Kwa hiyo mimi nikusaidieje?”
“Naomba tuingie wote ndani, nataka nikachukue simu yangu
tu nimpigie huyo jamaa.”
“Da! Itakuwa ngumu kidogo, unajua mimi nina haraka sana
leo,” alijitetea yule mtu ambaye kwa umbo ni bonge la mtu.
Nilijua ni uoga tu, hakuwa na kuwahi wala kuchelewa.
Alipopita, akatokea mwingine, mzee mmoja, kichwa chote
kilichafuka kwa mvi. Nilimsalimia huku nikimwonesha tabia
kwamba nataka kuzungumza na yeye.
“Mzee samahani sana.”
“Bila samahani kijana.”
Naye nikamsimulia tukio la siku ile, lakini wakati ananisikiliza,
mara nilimwona anatupia macho dirishani kwangu na mimi
nikageuka kuangalia, lakini sikuona mtu.
“Umeona nini mzee wangu?”
“Nimeona msichana ananizomea.”
“Kweli?”
“Kweli kabisa! Au ndiyo hayo mambo unayonisimulia?”
“Ndiyo hayo mzee.”
“Twende,” alisema, nikaanza kutangulia mbele, mzee
akanifuatia kwa nyuma. Hatukuwa tukiongea chochote, najua
sababu. Kila mmoja alikuwa anaiwaza hatari ye mbele.
Tuliingia ndani, tukafika sebuleni, lakini sikuiona simu
kwenye kochi.
“Ona sasa mzee, simu niliitupia hapa, lakini haipo.”
“Au unayo mfukoni kijana?” aliniuliza.
“Hapana, nina uhakika,” nilisema huku nikijipapasa mifukoni,
hakukuwa na simu.

38
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

“Nitajie namba nijaribu kuibipu,” yule mzee aliniambia huku


akitoa simu yake mfukoni.
Nilimtajia namba zote, akawa anaziandika, kisha akapiga huku
simu akiwa ameiweka kwenye sikio lake la kulia. Nilishtuka
sana kusikia simu yangu inaita kutokea kwenye chumba cha
wale wapangaji wenzangu.
“Si hiyo?” yule mzee aliniambia huku akiniangalia kwa
mshangao mkubwa na macho yaliyojaa wasiwasi.
Mzee alikata kisha akapiga tena, ikaita tena kutokea kulekule,
nilizidi kuogopa, nikamwambia tutoke lakini uzee kweli dawa,
aliniambia hakuna haja ya kutoka dawa ni kupambana tu.
Alinisogelea na kuniambia kwa sauti ya chini:
“Niwagongee mlango?”
“Si watakasirika?”
“Sasa kama unaogopa watakasirika, unadhani simu
yako utaipataje?”
“Haya wagongee. Lakini subiri, kwa nini tusiende
kwanza chumbani tukajua nani alikuwa anachungulia
nje?”
“Kijana unaonekana muogamuoga sana, we mwanaume
bwana, jifunze kukabiliana na hali kama hii, sawa?”
“Sawa mzee.”
“Haya twende huko chumbani kwako unakotaka tukaone
huyo msichana.”
Tulifungua mlango wa chumbani, hakukuwa na mtu, ila shuka
nililioliacha kitandani asubuhi silo, lilitandikwa jingine pia la
kwangu.
“Khaa!” nilishangaa.
“Nini?”
“Hili shuka.”
“Limefanyaje?”
“Silo nililolitandika asubuhi.”
“Lakini la kwako?”

39
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

“Ndiyo langu.”
Niliangalia mazingira mengine ya mle ndani na kubaini
kwamba, kuna vitu vingi sana vilikuwa ndivyo sivyo.
“Si umeona hayupo?” yule mzee aliniuliza, nikamjibu ndiyo,
akasema twende tukachukue simu yetu kwenye kile chumba
ambacho ilikuwa inaita.
Moyo wangu ulikuwa mzito sana, nilihisi kizunguzungu,
nilitamani kukaa chini na kumwona yule mzee asichukue
uamuzi wa kuifuata ile simu, lakini ningeipataje simu yangu
wakati ina namba kibao?
“Kijana, ngoja nikuoneshe dawa moja ya hao viumbe
wasiotaka kuonekana,” alisema yule mzee, nikamuuliza ni ipi
hiyo?
“Tulia wewe,” alisema huku akiingiza mkono mfukoni na
kutoa kimfuko kidogo, akakifungua akatoa kitu. Nilipomuuliza
ni nini akajibu:
“Ni bangi.”
“Sawa kabisa, hiyo ndiyo dawa, ngoja nikupe kiberiti.”
Katika mambo yalinishangaza ni hilo, tulitafuta kiberiti
chumbani hadi sebuleni lakini hakikuonekana, mbaya zaidi
mimi nilikuwa na kawaida ya kununua viberiti bunda zima,
lakini pia sikuona popote.
“Kweli una kiberiti ndani?” yule mzee aliniuliza.
“Kiberiti kipo na uzuri ni kwamba, nina bunda zima, lakini
pia nashangaa silioni.”
Nilimwona yule mzee akisimama wima na kunyoosha mikono
juu kama mtu anayeomba dua kwa Mungu.
“Kijana nimejua sasa, ngoja kidogo,” alisema huku akitoka na
mimi nikimfuata kwa nyuma.
Wakati tunapita kwenye korido jirani na vyumba vile vya
wenzangu, nikaisikia simu yangu ikiita.
“Mzee mzee, hiyo bwana,” nilisema, mzee akasimama na
mimi nikasimama nyuma yake, tukasikia sauti ya mwanaume
ikipokea simu yangu:

40
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

“Haloo…Juma…Juma gani wewe? Nakuuliza Juma gani


maana mimi ndiyo mwenye simu hii, huyo unayemsema simjui
na wala hajawahi kumiliki simu hii,” sauti ya kiume ilisema,
ukapita ukimya kidogo kisha sauti hiyo hiyo ikasema:
“Kama unabisha siyo simu yangu ongea na mke wangu huyu
hapa.”
Mara nikasikia:
“Haloo…ni kwa nini mnapenda sana kumfuatafuata mume
wangu, mara mzungumzie bangi, mara mtusemee kwa watu.”
Nilitamani sana kumwambia yule mzee asiniache katika
safari yake maana kwangu kwa muda ule palishaharibika,
ningeuawa na watu wasioonekana.
“Wewe nisubiri kijana,” mzee aliniambia akiendelea kwenda
nje, sikukubali.
“Mzee humu ndani mimi sikai, nimeshajua sasa.”
“Umejua nini?”
“Huyo Juma anayetajwa hapo nafanya naye kazi na ilikuwa
aje na bangi kwa ajili ya hawahawa viumbe humu ndani.”
Mzee aliniangalia, akaniuliza:
“Wewe kijana unaye Mungu?”
“Ninaye kwa imani yangu.”
“Huwa unakwenda kusali?”
“Sana.”
“Lini umekwenda mara ya mwisho?”
“Ungeniambia tatizo ni kusali au?”
“Si hilo tu, ila una matatizo mengi. Hivi hapa tumesimama,
nyuma yako nimemuona yule msichana amekuinamia
akikung’ong’a kama mara tatu kwa harakaharaka.”

KWA MARA YA KWANZA, JINI ANAJULIKANA


Nilitimua mbio kuelekea kusikojulikana, nikaenda kufunga
breki kwenye mtaa mmoja ambao ukienda kushoto kwangu
unakwenda kutokea kwenye barabara ya kwenda Kigogo
Mbuyuni.
41
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

Baadhi ya watu walioniona nilivyo walitambua nina tatizo,


mzee mmoja aliniuliza kama nakimbizwa nimefumaniwa.
“Sijafumaniwa mzee, lakini kwa tatizo langu afadhali
ningefumaniwa.”
Huyu mzee alikuwa amebeba kibegi kidogo mgongoni, alivaa
suti nyeusi huku akionekana ni mzee mwenye heshima kubwa
katika jamii inayomzunguka.
“Tatizo nini, hebu nisimulie kidogo tu,” alisema huku akinivutia
pembeni. Nilimsimulia kila kitu, alichokuwa akinishangaza
sasa, kila hatua ya maelezo yangu alikuwa akiachia tabasamu
hata pale nilipoamini kwamba ninachokisema kwa wakati huo
asingetabasamu na uso wake ungeonesha kushtuka.
Nilipomaliza nikanyamaza na kumwangalia kwa woga,
nilitaka kuamini ni yule mwanaume aliyepokea simu yangu
kule nyumbani amenibadilikia ili nisiweze kumtambua.
Moyoni nilisema kuwa, kama kweli ni yeye atakapojidhihirisha
tu kwangu nitoke mbio na kwenda kuingia kwenye nyumba ya
mtu yeyote mbele yangu.
“Tatizo ni hilo dogo tu?” aliniuliza.
“Ni hilo tu mzee wangu. Ukiweza kunisaidia nitashukuru
sana.”
“Nyumba yenyewe iko wapi?”
“Kule nyuma nyuma.”
Nilimwona akiingiza mkono mfukoni na kuchomoa simu nyeusi
ndogo, wengi wanaziita za tochi kisha akabonyezabonyeza na
kuiweka sikioni. Moyoni nilisema yaleyale.
“Si ajabu anawasiliana na yule mwanamke wa kule
nyumbani.”
Nikamsikia akiuliza:
“Isdory, bado mpo hapo?”
Nadhani huyo jamaa alijibu yupo maana nilimsikia huyo mzee
akisema:
“Unaweza kuja na akina Tino hapa kwenye kibanda
tulichotuma pesa asubuhi ya leo..? Haya njooni.”

42
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

Niligeuzageuza kichwa na kukiona kibanda cha kutuma


pesa kwa kupitia mitandao mbalimbali ya simu.
Nikajua amewaita watu waje pale.
Baada ya dakika kama tatu, wakafika watu kama saba, wanne
wanawake, watatu wanaume akiwemo Isdory na Tino.
“Huyu bwana anaitwa...” alianza kusema yule mzee
akiniangalia nikajua anataka nijitambulishe jina mimi
mwenyewe, nikafanya hivyo.
Nilipomaliza, ndipo yule mzee akawaambia wenzake kisa
chote cha kwangu,mwanzo hadi mwisho kama nilivyomsimulia
yeye awali.
“Ndugu, sisi wote walokole, kazi hiyo tunaimudu kwa vile
mara nyingi huwa tunatumia jina la Bwana na Mwokozi wetu
kufukuza uchafu kama huo, sasa itabidi utupeleke kwenye
hiyo nyumba,” alisema yule mzee.
Nilianza kutembea mimi na wao wakawa wananifuata
kwa nyuma. Wale wanawake niliwasikia wakizungumzia
mwanamke mmoja aliyeangushwa chini na mapepo akawa
anataka kupigana na wale waliokuwa wakimwombea. Moyoni
nikasema:
“Leo huko sijui.”
Tulifika nje ya nyumba, kitendo cha kwanza ambacho si cha
kawaida, nilimwona yule kijana muuza maji akitoka ndani.
Alivaa kama siku alivyokuja nikamwingiza ndani.
Nilishtuka sana, yeye hakushtuka, ila aliponiona
akaniambia:
“Bro nashukuru sana wamenilipa pesa zangu.”
Sijui ni nini kilinipata nilijikuta nikisema sawa, sikuongeza
neno jingine lolote lile.
“Ni humu waheshimiwa,” niliwakaribisha wale watu nikiwa
nimeshapishana na yule kijana.
Waliingia wote ndani, wakasimama katikati ya korido kisha
wakawa wananiangalia, yule mzee akaniuliza:
“Hivyo vyumba ni vipi?”

43
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

Sikumjibu kwa sauti, nilinyoosha mkono kuelekea kwenye


vyumba vyote viwili. Vilioneshwa kufungwa kwa ndani lakini
hakukuwa na sauti ya muziki wala maongezi ya watu.
“Baba katika jina la Yesu...” yule mzee alianza ghafla.
“Amiiiin...” walijibu wote aliofuatana nao, tena walijibu kwa
sauti ya juu kisha wakatulia kimya.
Akaanza kusali akitaja maneno ya kutisha, nilimsikia akisema
choma moto roho mtakatifu, mara Malaika Michael shuka na
panga likatalo kuwili.
Kifupi yule mzee alisema maneno ya ki-Mungu kwa jinsi
nilivyoelewa mimi. Ikafika mahali akasema:
“Paaza sauti yako.”
Ndipo wengine nao wakapokea kwa kila mmoja kuomba
kivyake. Wengine walisikika wakisema wanaangusha na
kuvunja ngome za ibilisi, wengine wanachoma moto makazi
ya shetani, wengine wanamwagia damu ya Yesu pale ndani.
Nilianza kuhisi amani iliyoje, niliamini ukombozi umefika
tayari kwani sauti tu niliisikia ikipenya hadi kwenye mbavu
zangu.
Waliomba sana, kuna wakati mimi nilihisi kuchoka lakini
wao waliendelea tu hadi moyoni nikasema kweli ni watu wa
Mungu.
Ghafla nilianza kuona moshi mweusi ukitoka chini ya milango
yote ya wale ndugu, mlango wa sebuleni kama sikikosei na
mlango wa chumbani. Moshi ulikuwa mzito kiasi kwamba,
kuna wakati nilihisi kupaliwa na kukohoa kwa nguvu lakini
wao hawakuonesha dalili ya kusumbuliwa na moshi huo.
Mara, milango yote miwili ikaanza kufunguka yenyewe
polepole huku maombi yakiendelea kwa kasi na nguvu ya
ajabu. Milango hiyo ilifunguka hadi ikafika mahali ndani
kukaonekana.
Cha ajabu sasa, vyumba vilikuwa vyeupe, ndani yake
hakukuwa na kitu chochote,hata karatasi.Ilikuwa kama chumba
kilichopigwa deki au kufagiliwa kwa ajili ya maandalizi ya
kuingia mkaaji mpya.

44
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

“Ha! Oneni jamani,” nilijikuta nikisema hivyo. Nilibaini


kwamba, wale watu hawakuona wakati milango inafunguka
kwa vile walipokuwa wakiomba walifumba macho na walikuwa
wakijipigapiga kwenye viganja kwa kutumia ngumi.
Yule mzee alipoona vile akasema:
“Katika jina la Yesu.”
“Amiiin,” walipokea wenzake.
“Sasa tushushe uwepo wa Bwana mahali hapa, kwamba
akapafanye pawe mahali salama, penye amani na utulivu wa
hali ya juu, kila mmoja sasa amwombe Bwana hivyo.”
Wakaanza kuomba tena, safari hii si kwa kukemea kama
mwanzoni, ilikuwa sauti yenye upole na utii, mara nikasikia
mlango mkubwa ukigongwa kwa nguvu.
“Ngo ngo ngo ngoo.”
“Ingia,” nilisema lakini huku nikienda mlangoni, nikaufungua!
Mbele yangu alisimama yule dalali.
“Karibu bwana.”
“Ee bwana nini umefanya sasa?”
ndilo swali lake hata kabla ya salamu.
“Kwa nini?”
“We hujui umefanya nini? Si wako watu humo ndani, wamekuja
kufanya nini hapa? Hujui kama kuna watu umewaumiza? Wewe
ungefanyiwa hivyo ungekubali kweli?”
“Kaka unajua ukija kwangu njoo kwa heshima zako zote na
hoja zenye msingi, usije kama mwendawazimu mpya, wewe
unachokisema mimi sijakisema kwako? Ulichukua hatua gani
wakati naumia mimi?”
“Lini umeniambia?”
“Wewe sijawahi kukupigia simu kukwambia? Tena ukasema
kama vipi nihame lakini sitarudishiwa kodi ya nyumba na mimi
nikakujibu niko tayari kwa hilo…”
“Sasa wewe ulikuwa ukiteswa kwa lipi, weka ushahidi hapa
kwamba ulikuwa ukiteseka sana.”
“Sina haja, mimi ndiyo najua.”
45
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

Wakati tukijibizana hivyo, wale waombaji walikuja juu kwa


kuomba. Walipaza sauti sana wakisema moto uteketeze kila
hila na jambo lolote ambalo linakwenda kinyume na mimi
ndani ya nyumba ile.
Ghafla, nilimwona yule dalali akianza kuyumba kama mlenvi,
alikwenda kulia, kushoto, akasimama, akawa kama ananijia
mimi, nikamkwepa, akaenda kushoto na kuanguka puu!
Kwangu ilikuwa ni furaha kwani nilipata picha kwamba, yule
dalali alikuwa anahusika moja kwa moja na matukio yote ya
ajabu mle ndani. Niliwaita wale watu wanaofanya maombi
na kuwataka washuhudie ambapo walipomwangalia dalali
waliongeza mkazo wa maombi yao.
Mwisho, dalali aliamka akiwa kama hana ufahamu, alikalishwa
chini na kuhojiwa ambapo alisema mambo ya ajabu sana.
Alisema mwanaume aliyekuwa akiishi ndani ya vyumba vile
ni yeye na mkewe, akasema mkewe ni jini kwa asilimia mia
moja ile yeye si jini bali mkewe alimfanya awe na uwezo wa
kutoonekana wala kujulikana na mtu.
Alipoulizwa kama alikuwa anapata faida yoyote kwa kitendo
cha kugeuka kuwa jini alijibu hakuna ila alikuwa anasikia
raha.
“Mfano, huyu bwana tangu ameishi huku hajawahi kutuona
kwa macho lakini sisi tulikuwa tunamuona siku zote, tulikuwa
tunaingia chumbani mwake na kumfanyia mambo yetu yeye
hajui.”
Jambo lingine ambalo lilinishangaza sana ni pale dalali huyo
aliposema yeye alikuwa na uwezo wa kujua anachokusudia
kukifanya mtu hata akiwa Dodoma na akakizuia mapema.
Ila, anashindwa kujua endapo mtu huyo atakuwa anakusudia
kufanya jambo kwa kuliwaza moyoni mwake bila kulisema
kwa mtu.
Nilimuuliza mfano, akajibu mfano ni mimi na mfanyakazi
mwenzangu tulipokuwa tumepanga kutumia bangi
kuwaangamiza yeye na mkewe, walijua kwa sababu tulijadili
kwa sauti ndiyo maana wao walijua.

46
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

Akaongeza hata nilipoingia ndani na yule mzee aliyeshindwa


akaondoka, walijua tumepanga ndiyo maana wakawahi kwa
kuchukua simu na kufanya mahoka mengine.
Yule mzee mkubwa wa wale waombaji akamuuliza:
“Ina maana mkeo jini kwa sasa yuko wapi?”
Yule dalali akajibu atakuwa amerudi ujinini kwa sababu
wakati wanaanza kuomba mkewe ndiye aliyekuwa wa kwanza
kuhisi anaongua moto na kuanza kulia kwa sauti mpaka ndugu
zake wakajitokeza kumtwaa kwenda naye ujinini.
Yule mzee mkubwa wao akauliza swali jingine ambalo na
mimi nilitaka kuuliza. Alimuuliza hivi:
“Sasa watu wanasema majini wana uwezo mkubwa, wanaweza
kupata fedha na mali yoyote ile, sasa kama wewe ulikuwa mume
wa jini kweli ni kwa nini uliamua kuwa dalali?”
Dalali akajibu: “Mimi sikuwa dalali, bali nilijifanya dalali ili
nipate mtu wa kumpangisha ndani kwa sababu mimi na mke
wangu tulipenda kuwachezea watu wanaoishi ndani.
“Mimi nina eneo Ilala la kuuza magari, pia nina duka kubwa
sana Mnazi Mmoja, sina shida ya maisha wala ya fedha.”
Kwa maneno yake hayo nilikubaliana na yeye kwani ni kweli
hali yake haikuwa ya kuchoka. Hata siku ya kwanza nilipokutana
naye nilishangaa dalali gani ana mwonekano wa kibosibosi
ingawa hakuwa na gari. Hapo na mimi nikapata nguvu ya
kumuuliza swali:
“Sasa bwana dalali wa bandia, uliwezaje kusababisha mimi
nipate namba yako ya simu kwa rafiki yangu anaitwa Mohamed
Kombe na akasema wewe ni dalali unaitwa Yusuf Mwamba?”
“Sikia bwana Humuli. Nimeshasema sisi tuna uwezo wa kujua
kile kinachojadiliwa mahali na kukifanyia kazi. Dalali anayeitwa
Yusuf Mwamba yupo, huyo rafiki yako tulimchezesha ulimi
wakati wa kutaja namba, akazitaja zangu badala ya za Yusuf.”
Nilichoka kabisa, yule mzee mkuu akasema tumwingize ndani
maana watu waliokuwa wakipita walianza kukodolea macho
pale nje.

47
NILIPANGA NYUMBA MOJA NA MAJINI

Kule ndani, dalali aliendelea kuzungumza mambo mengi


sana lakini kuna wakati alijipinda na kujishika mgongo akidai
anahisi maumivu makali ya moto. Alisema sehemu hiyo ipo
kama kuna mtu amebandika jiko la mkaa.
“Mungu amekuponya sana labda kama hutajutia matendo
yako ya nyuma,” alisema yule mzee aliyenisaidia.
“Mimi sitaki tena, kwanza najuta kwa nini niligeuka adui na
kufanya vile kwa watu wengine. Naomba mniombee sana kwa
huyo Mungu wetu.”
Yule mzee alimwelekeza kanisa lake ambalo halikuwa mbali
na pale nyumbani, yule dalali akasema atakwenda kesho yake
mapema.
Mimi pia nilialikwa, nikakubali kwenda kesho yake.
Walipoondoka, nilibaki na dalali. Wasiwasi ulinishika lakini
nikawa nasikilizia. Kila baada ya dakika tano dalali aliingia
chumbani kwangu na kuniomba nimsamehe kwa yote
yaliyopita.
Usiku nililala usingizi mzuri hadi kunakucha kiasi kwamba
sikuamini kama ni kweli ile nyumba ilikuwa vile. Kesho yake
nilikwenda kazini, jioni nilikwenda kwenye lile kanisa ambapo
nilimkuta dalali ameshafika.
Tulianza kuwa waumini wa kanisa hilo. Baada ya wiki mbili,
dalali alileta mke wake na mtoto mmoja ndani, kumbe alioa na
familia yake ilikuwa Dodoma. Lakini na mimi baada ya mwezi
mmoja nilihamia hapa Buguruni ambapo nilioa.
Hata hivyo, bado nasali kulekule Magomeni na dalali.
Namshukuru sana Mungu kwa kunipigania. Ile mikono ilikuwa
si salama bila neema ya Mungu. Nadhani shetani alipanga nife
lakini ameshindwa katika jina la Yesu. Amina.

MWISHO.

48

You might also like