Download as pdf or txt
Download as pdf or txt
You are on page 1of 20

SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.

ME/SOMAVITABUTANZANIA

UCHAMBUZI WA KITABU; Mindset


(Saikolojia Mpya Ya Mafanikio – Sehemu
Ya Kwanza)
UTANGULIZI.
Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu Mindset: the new psychology of success
kilichoandikwa na mwanasaikolojia Carol S. Dweck.
Hiki ni kitabu kinachoelezea mitazamo ambayo watu tunayo na jinsi
inavyoathiri maisha na mafanikio yetu.
Kupitia kazi zake, tafiti mbalimbali na maisha ya wengine Carol anawagawa
watu kwenye makundi makuu mawili;
Kundi la kwanza ni wale wenye MTAZAMO MGANDO ambao anauita FIXED
MINDSET.
Huku kundi la pili wakiwa wale wenye MTAZAMO WA UKUAJI ambao anauita
GROWTH MINDSET.
Tofauti hii moja na ndogo tu kwenye mtazamo, ndiyo inaleta tofauti kubwa
kwenye maisha kati ya wale wanaofanikiwa sana na wale wanaokuwa na
maisha ya kawaida.
Mtazamo ambao mtu unakuwa nao, uwe ni mgando au wa ukuaji, unatokana
na imani ambazo umekuwa nazo kwa maisha yako yote. Imani hizo hujengeka
mapema tangu ukiwa mdogo, kulingana na mazingira yanayokuzunguka.
Kile ambacho wengi tunaita haiba, ni mtazamo wa kuendesha maisha ambao
mtu unakuwa umeuchukua na kwenda nao maisha yake yote. Na kitu ambacho
kimekuwa kikwazo kwa wengi kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yao,
ni aina ya mtazamo wanaokuwa nao.
Kwenye kitabu hiki, Carol anakwenda kutuonesha jinsi mitazamo tuliyonayo
inavyojengwa, jinsi inavyokuwa kikwazo kwa mafanikio na pia jinsi ya kubadili
mtazamo ambao mtu unao na kuwa na mtazamo bora zaidi.
Kitabu kimesheheni tafiti mbalimbali pamoja na mifano ya wale waliofanikiwa
na kushindwa kwenye michezo, biashara na hata elimu, kutokana na aina ya
mtazamo ambao mtu anakuwa nao.
JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Kitabu pia kinatusaidia jinsi ya kuwajenga watoto kwenye mtazamo sahihi


ambao utawawezesha kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yao.

Kuhusu mwandishi.
Carol S. Dweck (kuzaliwa Oktoba 17, 1946) ni mwanasaikolojia wa nchini
Marekani. Ni profesa wa saikolojia kwenye chuo kikuu cha Stanford lakini pia
amefundisha kwenye vyuo vikuu vikubwa kama Columbia, Harvard na Illinois.
Carol anafahamika zaidi kupitia tafiti zake kwenye eneo la uwezo wa binadamu
pamoja na motisha. Ni kupitia kazi hizo ndiyo ameweza kuja na kitabu hiki
kinachoelezea aina mbili za mtazamo ambao watu wanakuwa nayo na jinsi
zinavyoathiri mafanikio yao.

Karibu kwenye uchambuzi.


Uchambuzi wa kitabu hiki utakuwa na sehemu tatu;
Sehemu ya kwanza tutajifunza kwa kina kuhusu aina mbili za mtazamo ambao
watu tunakuwa nao, kisha tutaingia ndani zaidi kwenye kila mtazamo na kisha
kuona jinsi mitazamo hiyo inavyoathiri uwezo ambao mtu anakuwa nao.
Sehemu ya pili tutaona jinsi mitazamo ambayo watu wanayo inavyokuwa na
madhara kwenye michezo, biashara na mahusiano. Kwenye michezo tutaona
jinsi mitazamo inavyowatofautisha wanaoshinda na wanaoshindwa, kwenye
biashara na kazi tutaona mitazamo inavyowajenga au kuwabomoa viongozi na
kwenye mahusiano tutaona jinsi mitazamo inavyochangia kuimarika au
kuvunjika kwa mahusiano.
Sehemu ya tatu tutajifunza jinsi mitazamo inavyojengeka kuanzia utotoni,
tukiona michango ya wazazi, walimu na makocha katika kujenga mtazamo wa
mtoto. Na mwisho tutajifunza jinsi mtu unavyoweza kubadili mtazamo wako
kutoka mtazamo mgando kwenda mtazamo wa ukuaji ili uweze kufikia
mafanikio makubwa.
Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu cha MINDSET, uweze kujua aina mbili za
mitazamo, kujua mtazamo ulionao na jinsi unavyoathiri mafanikio yako na
hatimaye kubadili au kuboresha mtazamo wako ili uweze kufikia mafanikio
makubwa.

AINA MBILI ZA MTAZAMO.


Tangu enzi na enzi, watu wamekuwa wanafikiri, kutenda na kupata matokeo
tofauti kwenye maisha. Hata kama watu wanaanzia eneo moja na kufanya vitu
JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

vinavyofanana, mwisho wa siku matokeo wanayopata na hata maisha yao


yanakuwa tofauti kabisa.
Matokeo haya ya tofauti yaliwafanya wenye udadisi kuanza kuuliza nini
kinachowatofautisha watu, nini kinawafanya baadhi kufanikiwa huku wengine
wakishindwa. Lengo la swali hilo ni kuona kama kuna namna watu wanaweza
kujifunza na wakafanikiwa kama wengine.
Wataalamu mbalimbali walikuja na nadharia ya kile kinachowatofautisha watu.
Wapo walioeleza kwamba kinachowatofautisha watu ni sifa fulani walizozaliwa
nazo, ambazo wengine wamezikosa. Hawa walieleza jinsi muundo wa mwili,
akili na vipaji vinavyowatofautisha watu na haviwezi kuigwa.
Kwa upande wa pili, wataalamu wengine walieleza kwamba
kinachowatofautisha watu ni mazingira waliyokulia ambayo yamewapa
mafunzo na uzoefu tofauti yanayopelekea wafikiri na kufanya tofauti. Walio
kwenye kundi hili waliona kile ambacho waliofanikiwa wanacho, kinaweza
kuigwa na wasiofanikiwa na wakaweza kufanikiwa pia.
Mmoja wa wale waliotetea kwamba tofauti za watu zinatokana na mazingira
na zinaweza kufundishwa alikuwa Alfred Binet mwasisi wa kipimo cha akili
kinachojulikana kama IQ test. Alfred alibuni kipimo hiki ili kuweza kuwatambua
watoto ambao hawajapata nafasi ya kujengewa uwezo mzuri, ili wapewe
vipaumbele tofauti. Lakini cha kushangaza, kipimo chake kikaja kutumika
vibaya, kuwaweka watu kwenye kundi la wenye akili na wasio na akili.
Alfred mwenyewe aliwahi kunukuliwa akisema; “Kuna baadhi ya wanafalsafa
wanaamini uwezo wa kiakili wa mtu una ukomo na hauwezi kukuzwa zaidi,
tunapaswa kukataa hilo. Kupitia mafunzo na mazoezi mbalimbali, mtu anaweza
kuwa na akili zaidi ya aliyokuwa nayo.”
Mpaka sasa bado wataalamu mbalimbali wamegawanyika kwenye makundi
mawili, wale wanaoamini akili ina ukomo, yaani mtu anazaliwa akiwa na
kiwango fulani cha akili na hawezi kukibadili. Huku wengine wakiamini akili
haina ukomo, kwamba kupitia mazingira na kujifunza, mtu anaweza kukuza
zaidi uwezo wa akili yake.
Lakini maendeleo ya sayansi na teknolojia yanaweka mambo wazi zaidi.
wanasayansi wanazidi kujifunza jinsi watu walivyo na uwezo wa kuifunza na
kukuza zaidi ubongo wao, kitu kinachokuza uwezo wao wa kiakili. Licha ya
kwamba watu wanaweza kuzaliwa na sifa fulani, lakini jinsi wanavyokuzwa,

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

kwa mazingira wanayokuwa nayo na yale wanayojifunza, kunachangia kwenye


uwezo wanaokuwa nao.
Hivyo kwa sasa wataalamu wengi wanakubaliana kwamba akili siyo kitu
ambacho mtu anazaliwa nacho, bali ni kitu kinachotengenezwa. Japokuwa
utotoni watu wanaweza kuonesha tofauti za uwezo, mbeleni
kinachowatofautisha siyo walichozaliwa nacho, bali kile walichofanyia kazi.

Hii ina maana gani kwako?


Wataalamu na hawa wanataaluma mbalimbali wanaweza kubishana kuhusu
dhana mbalimbali, kwa sababu hiyo ndiyo kazi yao.
Lakini kwenye hili la uwezo, iwapo mtu anazaliwa nao au unajengeka, swali la
kujiuliza ni je ina maana gani kwako?
Kulingana na jinsi ulivyokuzwa tangu ukiwa mtoto, unaweza kuwa kwenye
mtazamo wa aina moja kati ya hizi mbili;
Unaweza kuwa unaamini kwamba uwezo uliozaliwa nao hauwezi kubadilika, ni
kitu cha kudumu na hakibadiliki. Huu ndiyo mtazamo mgando ambao
unakufanya uamini akili na uwezo wako vina ukomo na hivyo utaona hakuna
namna ya kuvibadili.
Au unaweza kuamini kwamba uwezo ulionao ni kitu kinachoweza kubadilika, ni
kitu ulichokitengeneza mpaka hapo ulipofika sasa na unaweza kukitengeneza
zaidi kulingana na hatua mbalimbali unazoweza kuchukua. Huu ndiyo mtazamo
wa ukuaji ambao unakupa nafasi ya kukua zaidi ya pale ulipo sasa.
Wale wenye mtazamo wa ukuaji huwa hawajidanganyi kwamba wanaweza
kuwa chochote wanachotaka kuwa au kuwa kama wengine, ila wanachoamini
ni kwamba uwezo wao wa ndani ni mkubwa kuliko wanavyoutumia sasa na
hakuna anayeweza kupima ukubwa wa uwezo huo.

Waliofanikiwa walionekana hawawezi.


Ukiangalia historia za watu wengi walioweza kufikia mafanikio makubwa kwa
kufanya mambo makubwa, walionekana hawana uwezo mkubwa walipokuwa
wadogo. Hawakuwa watoto ambao walionekana wana uwezo au vipaji vya
kipekee. Walionekana ni watoto wa kawaida na ambao watakuwa na maisha
ya kawaida.
Wengine walikatishwa tamaa kabisa kwa kuambiwa na wazazi, walimu au
makocha wao kwamba hawawezi kufanikiwa kwenye eneo walilochagua.
JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Waliambiwa hawana uwezo au kipaji kinachohitajika hivyo bora wafanye vitu


vingine.
Lakini watu hao waliishangaza dunia kwa kuweza kufikia mafanikio makubwa
kwenye maeneo hayo, huku wakiwaacha nyuma wale walioanza wakiwa na
uwezo mkubwa na vipaji vya kipekee kwenye maeneo hayo.

Hatari na juhudi.
Ni kitu kinachojulikana wazi kwamba huwezi kufanikiwa bila ya vitu hivi viwili;
juhudi na hatari. Ni lazima uweke juhudi kwenye kile unachofanya na lazima
uchukue hatua za hatari, kwa kujaribu vitu vipya ambavyo havijazoeleka
vyenye hatari ya kushindwa.
Lakini jinsi watu wanavyochukulia juhudi na hatari inatokana na mtazamo
walionao.
Wale wenye mtazamo wa ukuaji huwa wanakuwa tayari kuchukua hatua za
hatari na kuweka juhudi, kwa sababu wanajua wana uwezo mkubwa,
hawakwami katika kufanya yaliyo makubwa.
Lakini wale wenye mtazamo mgando huwa hawapo tayari kuweka juhudi na
kuchukua hatua za hatari. Wao wanaamini kiwango cha uwezo walichonacho
ndiyo ukomo, hakuna namna wanaweza kukibadili, hivyo wanapaswa kufanya
kile walichozoea kufanya badala ya kujaribu vitu vipya na kushindwa.
Kwa wenye mtazamo wa ukuaji, kujaribu vitu vipya ni kujifunza na kukua
wakati kwa wenye mtazamo mgando kujaribu vitu vipya ni kushindwa na
kujidhalilisha.
Hii inaelezea kwa nini wale watoto wanaoonekana kuwa na uwezo mkubwa
utotoni huwa hawafanikiwi sana, wakati wale ambao wanaonekana hawana
uwezo mkubwa wakija kufanikiwa zaidi. Hiyo ni kwa sababu wanaoanza na
uwezo mkubwa wanakuwa na imani kwamba uwezo wao ndiyo huo na
haubadiliki, huku wanaoanza na uwezo mdogo wakiamini wanaweza kubadili
uwezo wao zaidi.

Kwa nini siri za mafanikio hazifanyi kazi.


Vitabu vingi vimeandikwa kuhusu siri za wale waliofanikiwa sana. Kila
aliyefanikiwa ameandika kitabu chake au kuna watu wameandika kitabu
kuelezea mafanikio yake. Vitabu hivyo huwa vinawapa watu hamasa kubwa
wanapovisoma, lakini siku chache baadaye watu wanarudi kwenye mazoea.

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Changamoto ya siri nyingi za mafanikio ni hazigusi mzizi wenyewe, zinagusa


vitu vya juu juu tu kama weka juhudi, chukua hatua za hatari, jiamini na
mengine. Lakini mzizi mkuu wa mafanikio ni ule mtazamo mkuu ambao mtu
anakuwa nao kwenye uwezo wake. Kama huo hautabadilika, haijalishi ni
mambo gani ya nje anafanya, hataweza kufikia mafanikio makubwa.
Unapoelewa kuhusu mtazamo mgando na mtazamo wa ukuaji, unaona ni jinsi
gani mitazamo na imani ambazo mtu anakuwa nazo zinaathiri mafanikio yake.
Unapoamini kwamba unaweza kufanya zaidi ya unavyofanya sasa, unapoondoa
ukomo kwenye uwezo wako na kujua unaweza kufanya zaidi, hapo unakuwa
umefungua mlango wa mafanikio ya kweli.
Mtazamo ulionao unaathiri imani ulizonazo, jinsi unavyokabiliana na
changamoto, juhudi unazoweka, utayari wa kuchukua hatua za hatari na hata
ubunifu ambao mtu unakuwa nao.
Tutakwenda kuona hayo kwa kina kwenye kitabu hiki.

Hatua za kuchukua.
Hatua za kuchukua hapa ni kujua aina ya mtazamo ulionao. Kujua aina yako ya
mtazamo, jibu maswali haya kwa kujitafakari na kuona kama ni NDIYO au
HAPANA.
1. Unaamini uwezo wako wa kiakili ni kitu ambacho hakiwezi kubadilika.
2. Unaamini unaweza kujifunza vitu vipya, lakini huwezi kubadili uwezo wako
wa kiakili.
3. Unaamini haijalishi una akili kiasi gani, unaweza kuongeza uwezo wako wa
kiakili.
4. Unaamini mara zote unaweza kujiongeza na kuwa na akili zaidi.
Swali la 1 na 2 yanaonesha mtazamo mgando, huku swali la 3 na 4 yakionesha
mtazamo wa ukuaji. Je wewe unakubaliana na maswali yapi?
Unaweza kuwa na mchanganyiko wa mtazamo wa ukuaji na mgando, lakini
wengi huegemea upande mmoja, mtazamo wa ukuaji tu au mtazamo mgando
tu.
Pia unaweza kupima mtazamo wako kwa maswali hayo kwenye maeneo
mengine, badala ya akili, weka kitu kingine kama sanaa, uandishi, biashara na
kadhalika.

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Tambua mtazamo ulionao sasa ili uweze kujua hatua sahihi za kuchukua na
kufanikiwa zaidi kwenye maisha yako.

KILICHO NDANI YA MITAZAMO MWILI.


Mitazamo miwili ambayo tumeiona inazalisha imani tofauti juu ya uwezo
ambao mtu anao.
Wale wenye mtazamo mgando wanaamini uwezo wao una ukomo na hivyo
wanachopaswa kufanya ni kuthibitisha uwezo huo kwa wengine na kuhakikisha
hawatoki nje ya uwezo wao.
Huku wale wenye mtazamo wa ukuaji wanaamini uwezo wao hauna ukomo na
hivyo wanachopaswa kufanya ni kuuendeleza kupitia kujifunza.
Hivyo mitazamo hiyo miwili inazalisha uwezo wa aina mbili; uwezo mgando
ambao unapaswa kuthibitishwa kwa wengine na uwezo wa ukuaji ambao
unaweza kuendelezwa kupitia kujifunza.

Tofauti ya mafanikio kwenye mitazamo.


Mafanikio yanatofautiana kwa namna mtu anavyochukulia uwezo.
Kwa wenye mtazamo mgando, mafanikio ni kuthibitisha kwa wengine kwamba
una uwezo, akili na vipaji, wakati kwenye mtazamo wa ukuaji mafanikio ni
kupiga hatua zaidi, kutoka chini na kwenda juu.
Unaweza kuona ni kwa nini wale wanaoanza wakiwa hawana uwezo mkubwa
wanafanikiwa kuliko wanaoanza wakiwa na uwezo mkubwa. Ni kwa sababu
wasio na uwezo mkubwa wanakazana kujifunza na kujiendeleza, huku
wanaoanza na uwezo mkubwa wakiwa hawajisumbui kujiendeleza.
Ni sawa na shuleni, kunakuwa na wanafunzi wanaoonekana kuwa na akili,
huku wengine wakionekana hawana akili sana.
Wale wenye akili wanakuwa na mtazamo wa kutaka kuonekana kwamba wana
akili na uwezo mkubwa, hivyo hawajisukumi kusoma zaidi, maana
wakionekana wanasoma sana wataonekana hawana akili. Huku wale
wasiokuwa na akili sana wakijua kwamba ili wafaulu basi wanapaswa kusoma
sana, hapo wanaweka juhudi na matokeo yanapotoka wengi wanashangaa,
ambao walionekana hawana akili sana wanakuwa wamefaulu kuliko
walioonekana kuwa na akili sana.

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Tofauti ya kushindwa kwenye mitazamo.


Kushindwa pia kunatafsiriwa kwa namna tofauti kulingana na mtazamo ambao
mtu anao.
Kwa wenye mtazamo mgando, kushindwa ndiyo mwisho wa dunia yao. Pale
anapokutana na kikwazo kama kufeli mtihani, kushindwa pambano, kufukuzwa
kazi au kupata hasara, mtu huyo anatafsiri kwamba hicho ni kiashiria kwamba
uwezo wake au kipaji chake kimefika mwisho, hakuna namna anayoweza
kwenda zaidi ya hapo. Kwa watu hawa, kushindwa ni hukumu kamba
hawawezi kufanya tena, ni mwisho wa safari yao. Unaposhindwa maana yake
huna akili, huna uwezo na huna kipaji na hayo yote yanahitimisha kwamba
huna nafasi ya kufanikiwa.
Kwa upande wa wenye mtazamo wa ukuaji, kushindwa ni hatua ya kufanikiwa.
Pale wanapokutana na vikwazo vinavyowazuia wasipate wanachotaka,
hawachukulii kama mwisho kwao, bali wanachukulia kama sehemu ya
kujifunza na kufanya vizuri zaidi ili wapate wanachotaka. Kwa kuwa wanaamini
uwezo ulio ndani yao ni mkubwa, wanapokutana na kikwazo au changamoto
wanajua ni sehemu ya wao kukua zaidi, hivyo wanakuwa tayari kujifunza na
kujaribu vitu vipya, kitu kinachowapelekea kufanikiwa zaidi.
Tumeona hapa jinsi mitazamo inavyoleta matokeo tofauti kwenye kushindwa
na kufanikiwa, matokeo yale yale, yanatafsiriwa kwa namna tofauti kulingana
na mtazamo ambao mtu anao. Ndiyo maana mtazamo una nguvu ya kumjenga
au kumbomoa mtu kwenye mafanikio.

Mtazamo na kujifunza.
Mtazamo ambao mtu anao, una athari kubwa kwenye utayari wake wa
kujifunza.
Wale wenye mtazamo mgando, huwa wanakuwa tayari kujifunza pale vitu
vinapokuwa rahisi kwao. Lakini vitu vinapokuwa vigumu, wanaacha kujifunza
kwa sababu wanaamini uwezo wao una ukomo.
Kwa wenye mtazamo wa ukuaji, huwa tayari kujifunza vitu viliwa rahisi, lakini
huendelea kujifunza hata vitu vinapokuwa vigumu, huwa wanaendelea
kujifunza kwa sababu wanajua ugumu huo unawafanya wafikie uwezo mkubwa
ulio ndani yao.

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Mtazamo kwenye mahusiano.


Kwenye mahusiano watu wenye mtazamo mgando huwa wanataka kuwa na
watu wasiowapinga, wanaowasifia na kuwafanya wajione wamekamilika.
Hawataki watu wanaowakosoa na kuwafanya waonekane hawajakamilika. Kwa
kifupi wanataka watu ambao watawatukuza muda wote.
Wenye mtazamo wa ukuaji huwa wanataka kuwa na mahusiano na watu
ambao wanaona makosa na madhaifu yao na kuwaambia ili waweze
kuyafanyia kazi. Huwa wanapenda kupewa changamoto na kusukumwa
kujifunza vitu vipya. Hawataki watu wa kuwasifia tu muda wote na kuficha
madhaifu yao.
Kwa tofauti hii unaweza kuona ni mahusiano yapi yanayodumu na yanayokuwa
na manufaa, iwe ni kwenye ndoa, kazi, biashara na mengine. Wenye mtazamo
mgando huwa hawadumu kwenye mahusiano kwa muda mrefu na hata
wakidumu huwa hayawi bora kwa sababu wanataka watu wa kuwasifia tu.

Ugonjwa wa mafanikio (CEO disease)


Mwandishi anatushirikisha kwa mifano jinsi mtazamo unavyoharibu mafanikio
ya wengi kupitia aina ya mahusiano wanayoyajenga.
Anatumia mifano ya wale wanaokuwa wameanzisha biashara zao, wanaanzia
chini kabisa na kupambana kufanikiwa. Watu hao wanakuwa na mtazamo
mgando na unawasaidia kufikia mafanikio makubwa. Lakini mtazamo huo,
unakuwa kikwazo kwao kukua zaidi na unakuwa chanzo cha kuanguka vibaya.
Anaeleza pale mtu mwenye mtazamo mgando anapofanikiwa au kufika ngazi
ya juu, anachagua kuzungukwa na watu wanaomtukuza na kumsifia, badala ya
wale wanaomkosoa na kumshauri vizuri.
Watu hao pia wanarudia kufanya kile ambacho kimewafikisha kwenye
mafanikio hayo, wakiwa hawapo tayari kujaribu vitu vipya. Kwa kurudia yale
yale, wanakuwa wanajiweka kwenye hatari ya kuanguka vibaya.
Viongozi wenye mtazamo mgando pia huwa wanapatwa na ugonjwa huu,
kadiri wanavyofikia ngazi za juu za mafanikio, ndivyo wanavyoshindwa kuuona
uhalisia kwa sababu wanakuwa wamechagua kuzungukwa na watu ambao
hawawakosoi na kuwasukuma kukua zaidi. Kwa namna hiyo, wanadanganywa
na wale wanaowazunguka na kuishia kufanya maamuzi yanayowagharimu,
yasiyoendana na uhalisia.

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Kujilinganisha na wengine.
Changamoto kubwa ya mtazamo mgando ni kujilinganisha na wengine, na hili
huwa na madhara ya aina mbili.
Moja ni pale mtu anapokuwa anajiona ana uwezo mkubwa kuliko wengine,
hapo husukumwa kuthibitisha uwezo wao mkubwa na hivyo kuacha kujifunza.
Upande wa pili ni pale mtu anapojiliganisha na kuona wengine wana uwezo
mkubwa kuliko yeye na hivyo kujidharau na kuona hawezi.
Kwa wenye mtazamo wa ukuaji, hawajilinganishi na wengine, bali
wanajilinganisha na wao wenyewe, kwa kujipima jinsi wanavyoendelea kukua
na kuwa bora zaidi kila siku.
Tafiti pia zinaonesha pale wenye mtazamo mgando wanaposhindwa, huwa
wanatafuta walioshindwa zaidi yao ili kujilinganisha nao, kitu kinachowafanya
wajisikie vizuri.
Badala ya kuangalia wale waliofanikiwa kuliko wao na wajifunze kwao, wao
wanatafuta walioshindwa zaidi, lengo siyo kujifunza, bali kujisikia vizuri, kwa
sababu wanaamini uwezo wao una ukomo.

Mtazamo na Lawama.
Wenye mtazamo mgando na wa ukuaji huwa wanatofautiana pia kwenye
lawama wanazotoa pale wanaposhindwa.
Kwa wenye mtazamo mgando, mara zote huwa wanawalaumu watu wa nje.
Kwa sababu wanaamini ndani yao wana uwezo fulani, kama wanashindwa basi
kuna mtu wa nje anayehusika. Mfano mzuri ni mwanafunzi anayefeli mtihani
na kusingizia mwalimu kumsahihishia vibaya.
Wenye mtazamo wa ukuaji huwa wanamiliki makosa na kushindwa kwao. Kwa
kuwa wanajua wana nafasi ya kukua zaidi, huwa wanaangalia wapi
walipokosea na kuona hatua zipi za tofauti wanaweza kuchukua ili
wasishindwe tena.
Mwandishi anamnukuu mmoja wa makocha bora kabisa John Wooden,
aliyewahi kusema hujashindwa mpaka pale unapoanza kulaumu wengine.
Akimaanisha kwamba kama unashindwa lakini hulaumu wengine, maana yake
unajifunza na kupiga hatua, hivyo hujashindwa ila uko kwenye mchakato wa
mafanikio. Ila unaposhindwa na kutupa lawama kwa wengine, basi hapo wewe
ni mshindwa na hakuna hatua unazoweza kupiga.
JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Mtazamo na Sonona.
Kushindwa huwa kunawaumiza sana wale wenye mtazamo mgando kiasi cha
kuwapelekea kupata sonona. Hiyo ni kwa sababu wanaposhindwa wanajiona
hawafai na hilo linawafanya waingie kwenye sonona na kukata tamaa.
Wale wenye mtazamo wa ukuaji huwa hawapati sonona wanaposhindwa, kwa
sababu wanajua kushindwa siyo hukumu ya maisha yao, bali ni mchakato wa
kufanikiwa zaidi. Hawatumii muda mwingi kufikiria jinsi walivyoshindwa, bali
wanaangalia jinsi gani wanaweza kupiga hatua zaidi.
Ubaya wa sonona ni kwamba ikishamuingia mtu, inamkatisha tamaa na hawezi
kujaribu tena. Ndiyo maana wenye mtazamo mgando huwa wanakata tamaa
mapema na hawafanikiwi, kwa sababu sonona wanayoipata inawafanya
wajione hawawezi tena.

Mtazamo na juhudi.
Wenye mtazamo mgando wanaamini hawahitaji kuweka juhudi sana kwa
sababu haziwezi kubadili uwezo wao. Na kwa kuwa wanataka kuthibitisha kwa
wengine uwezo wao, hawapo tayari kujisukuma zaidi, maana wakionekana
wanaweka juhudi, watu watajua hawana uwezo.
Lakini wenye mtazamo wa ukuaji, wako tayari kuweka juhudi zaidi kwa sababu
wanajua wanaweza kuwa zaidi ya walivyo sasa. Hawahangaiki kujionesha na
kupata uthibitisho wa wengine, bali wanakazana kupiga hatua zaidi wao
wenyewe.
Hili la kutokutaka kuweka juhudi limejengwa sana kwenye jamii zetu, ambapo
mashujaa huwa wanaonekana ni watu waliozaliwa na uwezo wa kipekee na
hawahitaji kusumbuka kama wengine. Huku wale wanaoweka juhudi sana
wakionekana kama wanalazimisha kitu ambacho hawana uwezo nacho.
Lakini ukiangalia kwenye uhalisia, wale wote ambao wamefikia mafanikio
makubwa ni matokeo ya kuweka juhudi kubwa, walianzia chini kabisa,
wakapambana na kuanguka mara kadhaa kabla hawajafika kwenye kilele cha
mafanikio.
Kuna sababu kuu mbili kwa nini wenye mtazamo mgando wanahofia sana
kuweka juhudi;
Sababu ya kwanza ni kuamini kwenye ujiniazi. Wenye mtazamo mgando
wanaamini uwezo wa mtu ni wa ukomo na wale wenye uwezo wa juu ni

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

majiniazi ambao hawahitaji kuweka juhudi kupata matokeo makubwa. Hivyo


wakionekana wanaweka juhudi, watu watawadharau kwamba siyo majiniazi.
Hili ndiyo linapelekea baadhi ya wanafunzi wanaoambiwa wana akili kufeli
mitihani, kwa kuwa wanasifiwa wana akili, hawajisumbui kusoma, maana
wakionekana wanasoma sana itaonekana ufaulu wao siyo kwa sababu ya akili
kubwa walizonazo, bali kwa kusoma sana.
Sababu ya pili ni kuogopa kukosa sababu. Wale wenye mtazamo mgando huwa
hawapendi kukosa sababu ya kushindwa. Kwa kuwa wakishindwa huwa
wanatafuta kitu cha nje cha kulaumu, basi huhakikisha hawaweki juhudi, ili
wanaposhindwa basi waone ni kwa sababu hawakuweka juhudi. Mfano
mwanafunzi mwenye akili anapofeli mtihani huku wasio na akili wakifaulu,
atajiambia kama angesoma kama wao, basi angefaulu. Hivyo hapo amejipa
sababu rahisi ya kufeli kwake, kwa kuwa hakusoma kama wengine.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye maisha, mtu haweki juhudi, ikitokea
amefanikiwa anajisifia ni akili yake kubwa na ikitokea amefeli basi ana sababu
kwamba hata hivyo hakuweka juhudi kubwa.
Iwapo mwenye mtazamo mgando ataweka juhudi kubwa halafu akashindwa,
hilo litamuumiza na kumpoteza kabisa.
Kwenye mtazamo wa ukuaji, mtu akishataka kitu basi anahakikisha anafanya
kila anachoweza ili kupata kile anachotaka, hatafuti sababu wala pa kujificha,
kwa sababu anajua anaweza kufanya zaidi ya anavyofanya sasa.

Maarifa tofauti na uelewa tofauti.


Vitabu vingi kuhusu mafanikio vinaeleza wazi kabisa kwamba ili ufanikiwe mtu
unapaswa kuwa wewe, unapaswa kushindwa na kujifunza kupitia kushindwa
kwako ili ufanikiwe, unapaswa kuweka juhudi kubwa na kuchukua hatua za
hatari.
Lakini wale wenye mtazamo mgando wanaposoma vitabu vya aina hiyo,
wanaelewa tofauti. Kwa kuwa mtazamo walionao ndiyo unaojenga imani kuu
wanayokuwa nayo, wanaposoma vitabu hivyo wanachoelewa ni mafanikio ni
kuwa zaidi ya wengine, kushindwa ni kiashiria kwamba uwezo wako ni mdogo
na juhudi ni kwa wale ambao hawana uwezo au vipaji.
Japokuwa mtazamo ulionao una nguvu kubwa kwenye imani zako na hata
uelewa wako, uzuri ni kwamba unaweza kubadili mtazamo ulionao na maisha

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

yako yakabadilika kabisa. Kwa kujifunza sifa hizi mbalimbali za mitazamo hiyo
miwili, unajua wapi ulipo na hatua zipi za kuchukua ili kubadili mtazamo wako.
Pamoja na kwamba juhudi ni muhimu kwenye mafanikio, lakini pia mazingira
na ‘koneshneni’ ambazo mtu anakuwa nazo zina mchango mkubwa kwenye
mafanikio yake. Mtu anapoanza na mtazamo sahihi, ni rahisi kwake kuyatumia
mazingira yake vizuri kufanikiwa.

Mtazamo na kupenda unachofanya.


Wale wenye mtazamo wa ukuaji, huwa wanapenda sana kile wanachokifanya
na wapo tayari kukifanya hata wanapokutana na magumu. Wale ambao
wamefanikiwa na kudumu kwenye mafanikio yao, wamekuwa wanapenda
sana kile wanachofanya.
Na cha kushangaza ni kwamba wengi wenye mtazamo wa ukuaji ambao
wamefanikiwa, hawakupanga kufika kwenye mafanikio makubwa. Wao
walipanga kufanya wanachopenda na kujisukuma kufikia uwezo wao mkubwa.
Kwa kufanya hivyo bila kukata tamaa wanajikuta wakiwa wamefika kwenye
mafanikio makubwa.
Kwa upande wa pili, wenye mtazamo mgando huwa hawapendi kile
wanachofanya, wanakifanya kwa sababu tu wanataka kuonesha uwezo wao
kwa wengine. Hawa huwa wanasukumwa na hitaji la kufika kwenye mafanikio
makubwa, lakini wengi huwa hawayafiki kwa kuwa wanakata tamaa haraka.
Na hata wale wachache ambao wanafika kwenye mafanikio hayo makubwa
huwa hawadumu na mafanikio hayo, huanguka kwa sababu hawana msukumo
wa kuendelea kufanya kile kilichowafikisha kwenye mafanikio hayo.
Wenye mtazamo wa ukuaji hawafurahii pale wanapopata matokeo, bali
wanafurahia kwenye hatua wanazochukua, ndiyo maana wanafanya kwa muda
mrefu na kufanikiwa.
Wenye mtazamo mgando huwa wanasubiri mpaka wapate matokeo ndiyo
wafurahie, kwa kuwa matokeo huwa yanachelewa, hukata tamaa mapema.
Wenye mtazamo mgando huwa wanasubiri mpaka wawe wakamilifu au
wajiamini ndiyo waanze kufanya kitu. Huku wenye mtazamo wa ukuaji
wakianza kufanya hata kabla hawajawa na ukamilifu, kabla hawajajiamini, kwa
sababu wanajua watajifunza kadiri wanavyokwenda.

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Haya ndiyo yaliyo ndani ya mtazamo miwili wanayokuwa nayo watu na ndiyo
yanayoathiri matokeo ambayo mtu anayapata kwenye maisha.

Hatua za kuchukua.
Kila mtu huwa anazaliwa akipenda kujifunza, lakini mtazamo mgando
unapoingia, mapenzi ya kujifunza yanaondoka. Kumbuka kipindi ambacho
kulikuwa na kitu unapenda sana kujifunza, inaweza kuwa mchezo fulani au
hata mafumbo, lakini kujifunza kulipoanza kuwa kugumu ukawa unaacha.
Kuanzia sasa unapoamua kujifunza kitu na kukutana na ugumu usikubali
kuacha, bali endelea kujifunza na hapo utakuza zaidi uwezo wako.
Epuka kuchagua kuzungukwa na watu wanaokusifia na kukusujudu, badala
yake chagua watu walio tayari kukuonesha makosa na madhaifu yako, hilo
litakusaidia kukua zaidi. Kama unataka kuzungukwa na wanaosifu, nenda
kanisani, lakini kwenye maisha yako, zungukwa na walio tayari kukuonesha
ukweli usioupenda.
Je kuna matokeo yoyote umewahi kuyapata kipindi cha nyuma kwenye maisha
yako na kuyatumia kujipa hali fulani? Labda ulifeli mtihani na kujiona wewe
huwezi, au ulipata hasara kwenye biashara na kujiona wewe huwezi biashara?
Sasa badili hilo, badala ya kujiona mshindwa, jione ulikuwa mafunzoni, angalia
kila ulichofanya kisha jiulize ni yapi umejifunza na unawezaje kufanya kwa
ubora zaidi ili upate matokeo mazuri zaidi. Kisha anza kuchukua hatua hizo
mpya.
Unapopanga kufanya kitu kisha ukashindwa, huwa unajisikiaje? Unakata tamaa
na kupata sonona au unaona ni sehemu ya kujifunza? Kuanzia sasa kila kikwazo
unachokutana nacho usione kama ni mwisho, bali ona kama darasa ambalo
linakufundisha kile unachopaswa kujua ili upate matokeo makubwa.
Je kuna kitu chochote umekuwa unapanga kufanya kwenye maisha yako lakini
huanzi kwa sababu unajiona hujawa tayari? Usiendelee kusubiri, weka
mipango na anza kukifanya, ukiwa tayari kuweka juhudi na kuchukua hatua za
hatari, ukijifunza na kukazana kwa ubora zaidi. Kwa njia hii utaweza kupiga
hatua kuliko kuendelea kusubiri mpaka uwe tayari, kitu ambacho huwa
hakitokei.

UKWELI KUHUSU UWEZO NA UFANIKISHAJI.


Hadithi za mafanikio zimekuwa zinatudanganya sana, zimekuwa zinawaonesha
wale waliofanikiwa kama mashujaa ambao walipambana wenyewe mpaka
JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

kufikia mafanikio. Tunaoneshwa mtu mmoja ambaye alianzia chini kwa sababu
ya uwezo mkubwa alionao au juhudi kubwa alizoweka akaweza kufanya
makubwa.
Lakini huo siyo ukweli, kila aliyefanya makubwa kwenye maisha yake, kulikuwa
na watu wengi waliohusika, kumsaidia kukamilisha kile alichofanya. Kulikuwa
na walimu, washauri, wenza na hata wengine wa kusaidia kwa namna fulani
mpaka kufikia pale.
Hapa mwandishi anatupa nafasi ya kuona mchango mwingine wa mafanikio
ambao huwa hauzungumziwi sana, mchango unaowatofautisha wale
wanaofanya makubwa na wale wanaoshindwa kufanya makubwa.

Mtazamo na mabadiliko ya kimaisha.


Mwandishi anatushirikisha utafiti uliofanywa kwa wanafunzi ambao walikuwa
wanapitia mabadiliko makubwa ya kimaisha, ya ndani na nje ya mwili. Kwa
ndani ya mwili walikuwa wanapitia kipindi cha balehe huku nje ya mwili
wakipitia mabadiliko ya kutoka shule ya msingi kwenda shule ya sekondari.
Utafiti ulionesha katika kipindi hiki, ndipo mtazamo wa mwanafunzi unapata
nguvu kubwa na kuamua maisha yake yote ya baadaye.
Wale wanaokuwa na mtazamo mgando wanazidi kuimarisha mtazamo huo,
kwa kuepuka ujaribu vitu vipya na kulinda uwezo wao ambao wanaamini una
ukomo. Hawa matokeo yao yalikuwa yakishuka kadiri muda ulivyokuwa
unakwenda.
Wale wenye mtazamo wa ukuaji walizidi kuimarisha mtazamo huo, kwa kuwa
tayari kujaribu vitu vipya na kushirikiana na wengine. hawa matokeo yao
yalikuwa yanakua kadiri mtu ulivyokuwa unakwenda.
Wanafunzi waliokuwa na mtazamo mgando walikuwa wanayachukulia
mabadiliko wanayopitia kama hatari kwao, yalikuwa yanawaweka kwenye
hatari ya kuonesha madhaifu yao na kuwageuza kutoka kuwa washindi mpaka
kuwa washindwa. Mara zote walikuwa wakijilinganisha na wengine na ili
kuhakikisha hawajioni wako chini kuliko wengine, waliacha kujaribu vitu vipya
au hata kujituma zaidi kwenye masomo.
Kwa wenye mtazamo wa ukuaji, kipindi cha mabadiliko walikichukulia kuwa
kipindi kizuri kwao kukua zaidi. Walikuwa tayari kujaribu vitu vipya na kujituma

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

zaidi kwenye masomo. Walitumia muda huo kujaribu vitu tofauti tofauti ili
wajue nini wanapendelea zaidi kufanya.
Wanafunzi hao waliendelea kufuatiliwa kwa miaka miwili na matokeo yalizidi
kutofautiana. Wenye mtazamo wa ukuaji waliendelea kufanya vizuri na hata
walipofeli mtihani mmoja, baadaye walifanya vizuri. Lakini wanafunzi wenye
mtazamo mgando walikuwa wakifanya vibaya na pale alipofeli somo moja,
hakuweza kufanya tena vizuri.
Walipofuatiliwa zaidi kwenye mtindo wa usomaji, kulikuwa na tofauti kubwa.
Kwa wanafunzi wenye mtazamo mgando walisoma kwa mtindo huu,
walichukua kitabu cha somo husika na kupanga kukisoma na kukariri kila kitu
kwenye kitabu hicho. Hivyo walipofanya vibaya, walijiambia pamoja na
maandalizi makubwa waliyofanya wamefeli, hivyo hawana uwezo kwenye
somo husika.
Wanafunzi wenye mtazamo wa ukuaji walijifunza kwa mtindo tofauti, badala
ya kusoma kwa kukariri, wao walisoma kwa kuelewa, walitafuta kuelewa
misingi mikuu ya dhana husika na kujifunza kwa namna wanavyoweza
kuielezea vizuri. Kwa njia hii walijifunza na kuelewa na kwenye mtihani
walifanya vizuri. Walifanya vizuri siyo kwa sababu walikuwa na uwezo kwenye
somo hilo, ila kwa kuwa walikuwa na mtazamo mzuri.
Kingine kilichoonekana ni wanafunzi wenye mtazamo wa ukuaji walikuwa
tayari kushirikiana na wengine, huku wenye mtazamo mgando wakiwa hawapo
tayari kushirikiana na wengine wakati wa kujifunza.
Hitimisho la utafiti huu ilikuwa kwamba kile ambacho mtu kuna mtu
amejifunza hapa duniani, basi na wengine pia wanaweza kujifunza iwapo
watakuwa na mtazamo sahihi na mazingira sahihi ya kujifunza kitu hicho.

Mtazamo mgando ni kikwazo kwa mafanikio.


Mtazamo mgando huwa unawajaza watu fikra zisizo sahihi, unawafanya waone
kuweka juhudi ni kujidhalilisha na hivyo watu hawajifunzi kwa njia sahihi.
Mbaya zaidi mtazamo huu unawazuia wasiweze kushirikiana na wengine,
maana hawawaoni kama washirika, bali kama washindani kwenye mtazamo
wao wa kujilinganisha na kutaka kuthibitisha uwezo wao mkubwa. Wanaona
wakiomba msaada kwa wengine wataonekana hawana akili, kitu
kinachowanyima fursa ya kujifunza zaidi.

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Mafanikio yoyote yale kwenye maisha yanahitaji mtu kuweka umakini kwenye
kile anachofanya, kuweka juhudi kubwa, kuwa na mikakati sahihi pamoja na
kuwa na watu ambao mtu anashirikiana nao. Kwa kuwa wenye mtazamo wa
ukuaji wapo tayari kwa yote hayo, wanapata nafasi ya kufanikiwa zaidi kuliko
wenye mtazamo mgando, ambao wanayapinga hayo.

Sifa zinawaharibu watoto.


Mwandishi anatushirikisha utafiti mwingine ambapo watoto waligawanywa
kwenye makundi mawili, kundi moja wakasifiwa kwa juhudi wanazoweka, huku
kundi jingine wakasifiwa kwa uwezo wao.
Wote walianza kwa kupewa zoezi ambalo ni rahisi, kisha kundi la kwanza
wakasifiwa kwamba wameweka juhudi kubwa na zimewasaidia kukamilisha
zoezi hilo. Kundi la pili walisifiwa kwamba wana uwezo mkubwa na ndiyo
maana wameweza kukamilisha zoezi hilo.
Baada ya hapo, walipewa zoezi jingine ambalo ni gumu zaidi ya lile la kwanza.
Na hapo matokeo yalikuwa tofauti, wale waliosifiwa kwa juhudi walifanya kwa
muda mrefu na kukamilisha zaidi kuliko waliosifiwa kwa uwezo.
Wale waliosifiwa kwa juhudi waliona juhudi zao ndizo zinawapa matokeo na
hivyo walikuwa tayari kuendelea kuweka juhudi, huu ndiyo mtazamo wa
ukuaji.
Wale waliosifiwa kwa uwezo, waliona uwezo wao ndiyo umewapa matokeo,
hivyo kwenye zoezi gumu, hawakujisumbua kwa sababu waliona hawana
uwezo, huu ndiyo mtazamo mgando.
Hili linatupa funzo kubwa kwamba ufanikishaji unaathiriwa sana na mtazamo
ambao mtu anao kwenye uwezo au juhudi. Wale wanaojipima kwa uwezo
hawafanikishi makubwa kama wanaojipima kwa juhudi.
Pia inatufundisha kuwa makini na sifa tunazowapa watoto, zinachangia
kuwajengea mtazamo wa aina fulani. Kama umekuwa unamsifia mtoto wako
anafanya vizuri kwa sababu ya uwezo mkubwa alionao, unamjengea mtazamo
mgando. Lakini kama unamsifia kwa juhudi kubwa anazoweka, unamjengea
mtazamo wa ukuaji.

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Mtazamo na ubaguzi.
Kwenye jamii kuna makundi mbalimbali ambayo huwa yanatofautiana na
makundi hayo yamekua yanatumika kujenga ubaguzi. Mfano ni kwenye jinsia
(wanawake na wanaume) na rangi (weusi na weupe).
Mwandishi anatushirikisha utafiti uliofanyika ambapo pale mtu
alipokumbushwa kuhusu kundi alilopo, iliathiri sana uanisi wake. Lakini athari
zilitegemea mtazamo ambao mtu anao.
Kwa utafiti ambao mwandishi ameshirikisha, pale mshiriki alipowekwa kwenye
nafasi ya kufikiria kuhusu kundi lake, wale walio kwenye kundi la kubaguliwa
(wanawake na watu weusi) walifanya vibaya kuliko wakiwa kwenye mazingira
ambayo hayawafanyi kukumbuka kundi walilopo. Hiyo inaonesha kitendo cha
kujiweka tu kwenye kundi linalobaguliwa, kinamfanya mtu ajione ana uwezo
wa chini.
Lakini hilo halikutokea kwa watu wa aina zote, walioathiriwa zaidi na hali hiyo
ni wale wenye mtazamo mgando. Wenye mtazamo mgando wanapofikiria
kuhusu kundi walilopo, wanajiona hawana uwezo kama ambavyo kundi hilo
limekuwa linachukuliwa na hali hiyo inawapelekea kutokuwa na ufanisi mzuri.
Lakini wenye mtazamo wa ukuaji, kukumbushwa kuhusu kundi walilopo
haikuwa na athari kwenye ufanisi wao. Hii ni kwa sababu wanaamini uwezo
wao hauna ukomo, hivyo kuwekwa kwenye kundi fulani hakuhusiani na uwezo
ulio ndani yao. Hata pale wanapojikuta wako nyuma ya wengine, hawakati
tamaa, badala yake wanaweka juhudi zaidi na hilo linawapelekea kufanya
vizuri.
Hili linatupa funzo kubwa kwamba mtazamo unaathiriwa sana na hali za
kijamii. Mtu anapokuwa na mtazamo mgando, akipewa sifa nzuri au mbaya
zote zinamuathiri. Akipewa sifa nzuri anaogopa hataifikia na hivyo kuacha
kuweka juhudi, akipewa sifa mbaya anaona ndiyo anayostahili na kukubaliana
nayo.
Njia pekee ya kuweza kufanikisha makubwa kwenye maisha ya mtu, ni
kuondokana na mtazamo mgando ambao unamfanya mtu kuwa mwathirika wa
yale wanayofanya wengine. Mtazamo mgando unathamini zaidi vile wengine
wanavyomchukulia mtu kuliko anavyojichukulia mwenyewe. Kama unataka
kuweza kuishi uwezo wako na kufanya makubwa, unapaswa kuwa na mtazamo
wa ukuaji.

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Hatua za kuchukua.
Fikiria kuhusu mashujaa ambao unao kwenye maisha yako, wale
unaowaangalia na wanakuhamasisha, je unawaona kama watu waliozaliwa na
uwezo mkubwa au watu walioweka juhudi kufika walikofika? Kama hujaingia
kwa kina kujifunza kuhusu watu hao, utakuwa unawaona kwa uwezo, sasa
nenda kayaangalie kwa kina maisha yao na utaona jinsi juhudi zimewafikisha
pale walipofika.
Kumbuka kipindi ambacho watu wengine walikushinda kwenye kitu
mlichokuwa mnafanya pamoja. Jiulize ulichukuliaje, je uliona wana uwezo
kuliko wewe au wameweka juhudi zaidi? Kama uliona ni uwezo ulijidanganya,
angalia tena na utaona ni juhudi, na jua kwamba hata wewe unaweza kuweka
juhudi zaidi na ukafanya makubwa.
Huwa unawasifiaje watoto wako, je unawasifia kwa uwezo au juhudi? Kuanzia
sasa anza kuwasifia watoto na hata watu wengine kwa juhudi walizoweka na
siyo kwa uwezo walionao. Angalia juhudi fulani waliyoweka na isifie hiyo,
utamsukuma kuweka juhudi zaidi.
Sehemu kubwa ya watu kwenye jamii wapo kwenye kundi ambalo limekuwa
linabaguliwa, inaweza kuwa kwa sababu ya jinsia (wanawake) au rangi (watu
weusi). Unapokuwa kwenye kundi linalobaguliwa, usijipime uwezo wako kwa
kujilinganisha na kundi, badala yake kazana kuweka juhudi kwenye chochote
unachofanya. Na kama uko kwenye kundi lisilobaguliwa, basi wasaidie walio
kwenye kundi linalobaguliwa ili hali hiyo isiwe kikwazo kwao.
Huu ni mwisho wa sehemu ya kwanza ya uchambuzi wa kitabu cha MINDSET
ambapo tumejifunza kuhusu mitazamo ya aina mbili, kilicho ndani ya mitazamo
hiyo na kuhusu uwezo na ufanikishaji.
Kwenye sehemu ya pili itakayofuatia tutajifunza athari za mitazamo hii kwenye
maeneo matatu; michezo, biashara na mahusiano. Usikose uchambuzi huo ili
uone jinsi mitazamo tunayokuwa nayo inavyoweza kupelekea kufanikiwa au
kushindwa kwenye maeneo hayo.
Umejifunza mambo muhimu sana kupitia uchambuzi huu wa kitabu. Sasa kazi
ni kwako kwenda kuyaweka kwenye matendo ili uweze kupiga hatua na
kufanikiwa kwenye maisha yako.

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007
SOMA VITABU TANZANIA WWW.T.ME/SOMAVITABUTANZANIA

Kuendelea kupata chambuzi za kina za vitabu na vitabu vilivyochambuliwa,


jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA, kwa kufungua
www.t.me/somavitabutanzania
Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na
mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na
upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua;
https://amkamtanzania.com/somavitabuapp

JIUNGE KUPATA UCHAMBUZI WA VITABU TUMA UJUMBE KWA TELEGRAM NAMBA 0678 977 007

You might also like