Download as pdf or txt
Download as pdf or txt
You are on page 1of 6

#TANO ZA JUMA KISIMA CHA MAARIFA TELEGRAM; 0717396253

#MAKALA Ya Juma Kutoka Kitabu; It Starts


With Passion (Jinsi Ya Kufanya Kile
Unachopenda Na Kupenda Unachofanya
Ili Kuwa Na Maisha Ya Mafanikio).
Maeneo Manne Ya Kutengeneza Maisha Unayoyapenda Na Yenye Mafanikio
Makubwa.
Rafiki yangu mpendwa,
Hakuna kitu chochote kikubwa ambacho kimewahi kufanya na mtu ambaye
hana mapenzi ya kweli kwenye kile anachofanya. Kama unataka kufanikiwa
kwenye maisha, kama unataka kufanya makubwa na kuacha alama hapa
duniani, lazima kwanza upende kile ambacho unakifanya. Unapaswa kukipenda
kweli kiasi kwamba upo tayari kujitoa kwa ajili ya kitu hicho.
Hivi ndivyo watu wote tunaowaona wana mafanikio makubwa wameweza
kufikia mafanikio hayo. Wengi walipokuwa wanaanza walikatishwa tamaa na
wengine, walikutana na mambo magumu, changamoto na hata kushindwa.
Lakini hawakukata tamaa, kwa sababu ni kitu ambacho walikipenda kweli, kitu
ambacho kilitoka ndani yao.
Mwandishi Keith Abraham kupitia kitabu chake kinachoitwa IT STARTS WITH
PASSION; Do What You Love and Love What You Do, anatufundisha umuhimu
wa kufanya kile tunachopenda au kupenda kile tunachofanya. Njia pekee ya sisi
kufanikiwa ni kujua kile ambacho tunakipenda kweli na kisha kukifanya au
kama hatutajua kipi tunapenda, basi kile ambacho tunakifanya sasa tunapaswa
kukipenda sana.
Kwenye kitabu chake, Keith anatuambia kama unataka kupata zaidi ya
unachopata sasa, kama unataka kuwa zaidi ya ulivyo sasa, basi lazima upende
sana kile unachokifanya. Upendo una nguvu kubwa sana, nguvu ya kuvunja kila
aina ya kikwazo na changamoto, nguvu ya kukuwezesha kuendelea hata pale
unapokuwa umechoka na kukaribia kukata tamaa.
Kwenye kitabu chake, Keith ametushirikisha maeneo manne ambayo
tunapaswa kuyazingatia katika kutengeneza maisha ambayo tunayapenda,
tunapenda kile tunachofanya na tunafikia mafanikio makubwa. Kwenye makala

www.amkamtanzania.com www.kisimachamaarifa.co.tz Kocha Dr. Makirita


#TANO ZA JUMA KISIMA CHA MAARIFA TELEGRAM; 0717396253

hii ya juma tunakwenda kuyaangalia maeneo hayo manne, na hatua


tunazopaswa kuchukua kwenye kila eneo ili tuweze kuwa na maisha bora.
kwenye makala ya TANO ZA JUMA (ambayo inapatikana kwenye telegram tu)
tutachambua kila eneo kwa kina na kujifunza hatua kwa hatua jinsi
unavyoweza kufikia mafanikio makubwa kupitia chochote unachochagua
kufanya.

MAENEO MANNE YA KUTENGENEZA MAISHA


UNAYOYAPENDA NA YENYE MAFANIKIO MAKUBWA.
ENEO LA KWANZA; MAANA – JINSI YA KUTENGENEZA
UHAKIKA KWENYE MAISHA YAKO.
Kila mtu anapenda kuwa na maana kwenye kitu anachofanya kwenye maisha
yake, kazi na hata biashara. Japokuwa wengi wanafanya kazi wanazofanya ili
walipwe, lakini kinachowafanya waridhike na kazi hizo siyo malipo
wanayoyapata, bali maana wanayoipata kupitia kile wanachofanya.
Tunapaswa kujua uhusiano uliopo baina ya kusudi la maisha yetu, kile
tunachopenda kufanya na malengo ambayo tumejiwekea. Vitu hivi vitatu,
yaani kusudi, mapenzi na malengo ndiyo vinatengeneza maana kwenye maisha
yetu.
Tunapokuwa na kusudi kwenye maisha, na tukapenda kile tunachofanya na
kisha kuwa na malengo ambayo tunayafanyia kazi, maisha yetu yanakuwa na
maana kubwa na tutapata msukumo wa kujituma zaidi ili kufanikiwa.
Maana inaanza na KWA NINI unafanya kile unachofanya. Kuna maswali matatu
unayopaswa kuyajibu kupitia kile unachofanya. Maswali hayo ni KWA NINI
(WHY), NINI (WHAT) na VIPI (HOW). Kwa nini inakufanya ujue msukumo
ulionao kwenye kile unachofanya. NINI unafanya hapa ndiyo unachagua kile
unachofanya na VIPI unavyofanya kitu hicho unaelezea hatua unazochukua
katika kufanya kitu hicho.
HATUA YA KUCHUKUA; Tengeneza maana kupitia kila unachofanya kwa kujua
kusudi la maisha yako, kujua kwa nini unafanya chochote unachofanya,
kupenda kile unachofanya na kisha kujiwekea malengo ya kupiga hatua zaidi
kupitia hicho unachofanya.

www.amkamtanzania.com www.kisimachamaarifa.co.tz Kocha Dr. Makirita


#TANO ZA JUMA KISIMA CHA MAARIFA TELEGRAM; 0717396253

ENEO LA PILI; HATUA – JINSI YA KUPATA UWAZI KWENYE


MAISHA YAKO.
Baada ya kujua kusudi la maisha yako na kujiwekea malengo ambayo
unayafanyia kazi, unapaswa kuwa na njia ya kujipima jinsi unavyoyafanyia kazi
malengo hayo. Kwa sababu unapoweka malengo, unaiona ile picha ya mwisho,
lakini zile hatua ambazo unachukua mpaka kufikia picha hiyo ya mwisho
hazionekani.
Hivyo eneo la pili tunalopaswa kulifanyia kazi ni zile hatua ambazo tunapaswa
kupiga ili kufika kule ambapo tunataka kufika, ili kuweza kukamilisha kusudi la
maisha yetu, ili maisha yetu yaweze kuwa na maana.
Kwenye kila ndoto kubwa tuliyonayo, tunapaswa kuivunja kwenye vipande
vidogo vidogo na kisha kuchukua hatua kwenye vipande hivyo. Vipande hivi
vidogo vidogo ndiyo vinatupa uwazi kwenye safari yetu ya mafanikio. Kwa
sababu kama huwezi kupima kitu, huwezi kukielewa wala kukikuza. Vipande
vidogo tunavyogawa tunaweza kuvipima na hivyo kujua kama tunafanya vizuri
au vibaya.
Njia ambayo watu wengi wamekuwa wanatumia kuweka malengo ni kuanza
kuchukua hatua, kufikiri jinsi ambavyo watachukua hatua hizi na kupata hisia
pale ambapo mtu anakamilisha lengo hilo. Njia hii imekuwa inawafanya wengi
kuishia njiani. Mwandishi anatushirikisha njia sahihi ya kujiwekea malengo na
kuyafikia, ambayo inaanza na zile hisia ambazo tunataka kuwa nazo pale
tunapofikia malengo hayo, kufikiria hatua za kuchukua na kisha kuchukua
hatua ili kufikia malengo hayo. Unapoanza na hisia, unapata msukumo
mkubwa wa kufikia malengo yako.
HATUA YA KUCHUKUA; Chukua lengo au ndoto kubwa uliyonayo, kisha gawa
kwenye vipande vidogo, tengeneza hisia ambazo utakuwa nazo baada ya
kufikia lengo hilo, kisha anza nazo. Jua hatua unazopaswa kuchukua kisha anza
kuchukua hatua hizo huku ukiwa tayari una hisia za ushindi. Angalia zile hatua
unazochukua katika kukamilisha vipande vidogo vya lengo lako kubwa. Kadiri
unavyokamilisha, ndivyo unavyopata uwazi na kujiamini zaidi, kitu
kinachokusukuma kuchukua hatua zaidi.

www.amkamtanzania.com www.kisimachamaarifa.co.tz Kocha Dr. Makirita


#TANO ZA JUMA KISIMA CHA MAARIFA TELEGRAM; 0717396253

ENEO LA TATU; MTAZAMO – JINSI YA KUONGEZA KUJIAMINI


KWENYE MAISHA YAKO.
Kila mtu ana uwezo mkubwa sana ndani yake, uwezo wa kufanya makubwa
kwenye maisha. Lakini wengi wamekuwa wanashindwa kutumia uwezo huu
mkubwa ulio ndani yao kwa sababu hawajiamini. Kutokujiamini kimekuwa
kikwazo kwa wengi kufanikiwa kwenye maisha.
Kila mtu anajua nini anataka kwenye maisha na anazijua hatua za kuchukua ili
kupata kile anachotaka. Lakini inapofika kwenye kuchukua hatua, wengi
hukwama, kwa sababu hofu ya kushindwa na ugumu wa safari unawafanya
wengi kusita kuanza. Maneno ya kukatisha tamaa kutoka kwa wengine na hata
hadithi za wale walioshindwa ndiyo zinazidi kuwarudisha nyuma wengi.
Ili kufanikiwa, lazima uanze kwa kujiamini wewe mwenyewe, lazima uwe
mfano wa mtu mwenye uhakika, mwenye kujua wapi anakwenda na kuamini
ana uwezo ndani yake wa kufikia malengo aliyojiwekea.
Hilo linawezekana kupitia mtazamo ambao mtu unakuwa umejijengea,
mtazamo wa kwamba inawezekana, mtazamo wa kwamba unaweza. Kadiri
unavyojijengea mtazamo huu, ndivyo unavyokuwa imara na kuweza kuchukua
hatua kubwa kufikia malengo yako.
Ukishajiwekea malengo, unapaswa kuwa na uhakika kwamba utayafikia,
unapaswa kuondokana na wasiwasi wowote unaoweza kuwa umejijengea na
kuchukua hatua ukiwa unajiamini kwamba utafikia malengo hayo.
HATUA YA KUCHUKUA; Jijengee kujiamini, jua kwamba ndani yako una uwezo
mkubwa ni wewe kuanza kuutumia uwezo huo. Unapoweka malengo, amini
utayafikia na hakuna kinachoweza kukuzuia, kisha chukua hatua kwa kujiamini
na ondokana na wasiwasi wowote unaoweza kuwa nao.

ENEO LA NNE; MWENDO – JINSI YA KUISHI MAISHA YENYE


MSIMAMO.
Hamasa huwa haidumu kwa muda mrefu, na ndiyo maana watu ambao
wanaishi kwa hamasa hawana msimamo. Huwa wanaanza jambo baada ya
kuwa wamepata hamasa, na hamasa hiyo inapoisha wanaacha jambo hilo.
Wakipata hamasa nyingine wanaanza jambo jingine jipya. Hivyo unakuta watu
hawa wanaanza na kuacha mambo mengi na hakuna hata moja ambalo
wamekamilisha.

www.amkamtanzania.com www.kisimachamaarifa.co.tz Kocha Dr. Makirita


#TANO ZA JUMA KISIMA CHA MAARIFA TELEGRAM; 0717396253

Ili kufanikiwa, unapaswa kutengeneza mwendo kwenye maisha yako, kuwa na


msimamo wa kuchukua hatua kwenye jambo moja mpaka upate matokeo
unayoyataka. Kuacha kutegemea hamasa pekee na kuwa na mpango wa
utekelezaji utakaokuwezesha kufanyia kazi malengo yako mpaka kuyafikia.
Njia pekee ya kutengeneza mwendo na kujijengea msimamo kwenye maisha
yako ni kuchagua kuchukua hatua ndogo ndogo kila siku kufikia malengo yako.
Hatua ndogo kabisa ambazo huwezi kuona ugumu kuzichukua. Kwa kufanya
hivyo kila siku, unatengeneza tabia ambayo inakusukuma kuendelea kufanya.
Usisubiri mpaka uweze kuchukua hatua kubwa kwa wakati mmoja. Usiwe mtu
wa kusubiri mpaka kila kitu kiwe tayari ndiyo uanze. Ukishajua nini unataka,
ukishaweka malengo, basi anza kuchukua hatua ndogo ndogo kila siku
kuelekea kwenye malengo hayo. Mpango mzuri ambao unaufanyia kazi leo ni
bora kuliko mpango bora ambao unasubiri mpaka kesho.
Unapotengeneza mwendo kwenye maisha yako, inakuwa rahisi kuendelea
kuliko kuanza. Hivyo hakikisha kila siku kuna hatua unachukua kuelekea
kwenye lengo lako.
HATUA YA KUCHUKUA; Usitegemee hamasa ya mara moja kufanya mambo
makuba, badala yake chukua hatua ndogo ndogo kila siku, hizi zitakujengea
mwendo ambao utakusukuma kuendelea kuchukua hatua zaidi. Kila siku piga
hatua kuelekea kwenye malengo yako, na utajikuta unayafikia bila ya kujua.
Rafiki, hayo ndiyo maeneo manne ya kuzingatia katika kujenga maisha
unayoyapenda na yenye mafanikio makubwa. Kwenye makala ya TANO ZA
JUMA tutajifunza kwa kina kile eneo na hatua muhimu zaidi za kuchukua ili
kuwa na maisha yenye mafanikio makubwa, maisha ambayo unayapenda na
yenye maana kwako na kwa wengine pia.
Uchambuzi huu wa kitabu umeandaliwa na Dr. Makirita Amani.
Dr Makirita ni daktari wa binadamu, kocha wa mafanikio, mwandishi na
mjasiriamali. Kuendelea kupata chambuzi hizi za vitabu kwenye TANO ZA
JUMA, hakikisha unajiunga na channel ya TANO ZA JUMA ambayo ipo kwenye
mtandao wa telegram.
Kujiunga ni bure kwa juma la kwanza, kisha baada ya hapo unachagua kulipa
tsh elfu moja kwa juma, au elfu tatu kwa mwezi au elfu 30 kwa mwaka. Kwa
maelezo zaidi tuma ujumbe kwenda namba 0717396253, ujumbe utumwe kwa
njia ya telegram pekee.

www.amkamtanzania.com www.kisimachamaarifa.co.tz Kocha Dr. Makirita


#TANO ZA JUMA KISIMA CHA MAARIFA TELEGRAM; 0717396253

Karibu sana.

www.amkamtanzania.com www.kisimachamaarifa.co.tz Kocha Dr. Makirita

You might also like