Safari Ya Bulicheka Na Mke Wake - USER

You might also like

Download as pdf or txt
Download as pdf or txt
You are on page 1of 38

SAFARI YA BULICHEKA NA

MKE WAKE

(someni kwa furaha kitabu cha 2b)

ALFONSO LOOGMAN
YALIYOMO
Safari ya Bulicheka na mke wake
Sehemu ya pili
Sehemu ya tatu
Safari ya Bulicheka na mke wake

Bulicheka alikuwa mwalimu wa shule ya Kilakala. Alikuwa anatamani


kujua mambo mengi, kusudi ya kuwafundisha watoto wa shule yake.
Siku moja akamwambia mke wake, “Lizabeta twende kufanya safari
tupate kuiona dunia.”
Lizabeta akasema, “Ukitaka kufanya safari ya kuiona dunia nzima, nenda
mwenyewe peke yako. Mimi siendi.

Bulicheka akajibu, “Haifai hata kidogo mtu kwenda safari ya mbali na


kumwacha mke wake peke yake nyumbani. Utafanyaje nyumba ikiteketea,
je? Au wevi wakija, je, utafanyaje? Au akija bwana simba mwenyewe, je,
utamfukuza na nini?”
Lizabeta akakubali, akasema, “Hii ni kweli. Sijui la kufanya nyumba
ikiteketea. Na wevi wakija nitaogopa. Na bwana simba akifika atanirukia
bila shaka. Umesema kweli. Safari unataka kwenda wapi?”
“Nataka kwenda Mombasa.”
Basi, Bulicheka na Lizabeta wakaenda Dar es Salaam kwanza,
wakanunua nguo safi, wakanunua vyakula, wakalipa gharama ya meli,
wakasafiri.
Meli ilikuwa kubwa sana. Kulikuwa na milingoti miwili, na bomba mbili
zikatoka moshi. Ndani ya meli kulikuwa na vyumba vingi. Wakapata
chumba kimoja mahali pao pa kukaa. Kulikuwa na watu wengine wengi
sana, mabaharia na abiria. Wote wakafurahi kwa ajili ya safari.
Wakatoka katika bandari ya Dar es salaam, wakaiona nchi toka mbali,
ikawa nzuri sana. Wakaona kumbe ni kutamu kusafiri baharini. Kwanza
Lizabeta alikuwa ameogopa kidogo, lakini sasa haogopi tena.
Bulicheka akasema, “Kumbe, kutamu sana kusafiri namna hii.
Tukishafika Mombasa tutaendelea mbele mpaka Arabuni.”

Lizabeta akajibu, “Vizuri sana, hata mimi napenda.”


Basi wakaendelea hivi muda wa siku kumi. Mambo yote yakawa mazuri.
Lakini siku ya kumi kukawa upepo mkali kwa ghafula; meli yao ilianza
kukokotwa na mawimbi. Hawakuweza tena kusimama sawa. Watu wote
wakashika nguzo na milingoti na mabomba, ili wasipate kuanguka. Loo!
Hatari ikawa kubwa sana.
Lizabeta akaanza kulia machozi kwa hofu, lakini Bulicheka akamwambia,
“Usilie machozi. Hivyo ndivyo yalivyo mambo ya bahari, mara huwa
tulivu, mara huchafuka. Upepo ukisha, bahari nayo itatulia tena.”
Lakini wakati huo huo alipokuwa akiyasema maneno hayo, wimbi kubwa
kabisa likawaangukia juu yao, likawachukua wote wawili, na
kuwavurumushia majini. Kwa bahati njema, meza moja ilichukuliwa pia,
wakaogelea kwa nguvu hata wakaipata. Wakapanda juu yake na kuikalia.
Lizabeta akasema, “Sasa tumekuwa salama.” Kweli ilikuwa bahati yao
kwa sababu meli yao ilikuwa imevunjika, na kuzama. Wakabaki baharini
peke yao, wala haikuwako nchi kavu karibu nao. Mambo yote yakawa
mazuri.
Wakafunga kitambaa katika mguu mmoja wa meza yao, kiwe kama
bendera. Meli yoyote ikija watu wapate kuwaona na kuja kuwaokoa.
Lakini siku ya kwanza walishinda mchana kutwa, bila kuiona nchi wala
meli yoyote. Bulicheka alikuwa anazo bado karanga chache mfukoni,
wakazila. Na Lizabeta akawa bado na mkate wa mofa katika mkoba wake,
wakaula pia. Aidha, siku ya pili hawakuona kitu, na siku ya tatu wakaanza
kuona njaa. Vilevile, wakaona kiu kwa sababu huwezi kuyanywa maji ya
bahari maana yana chumvi.
Siku ya nne, wakaiona nchi kavu, wakafurahi sana. mawimbi ya bahari
yakaipeleka ile meza polepole ili ikaribie nchi kavu, nao hao wawili
wakapelekwa juu yake, kama vile wangekuwa juu ya chombo kizuri cha
kusafiria.
Mara wakafika pwani. Bulicheka akamwambia Lizabeta, “Sasa tutoke ili
tukaiona nchi hiyo, na kuzungumza na wenyeji. Wakatoka katika meza yao,
wakayavuka maji ya pwani, mpaka wakafika salama. Nchi ilikuwa
tambarare kidogo, vilikuwako vichaka kadhalika miti na minazi; bali
hawakuona nyumba yoyote wala dalili ya watu.

Lizabeta akasema, “Hakuna wenyeji wowote katika nchi hii. Tutakipata


wapi chakula? Mimi naona njaa. Sijala kitu chochote leo.”
Bulicheka akajibu, “Juu ya chakula, hakuna shida. Ipo hii minazi; ngoja
nikwee, nikakuchumie dafu unywe na nazi ule.”
Akakwea haraka, haraka, kwani yeye alikuwa hodari sana kupanda miti.
Akazichuma nazi nne, tano hivi na madafu machache, wakaja wakala, na
wakanywa wakashiba.

Halafu, wakaenda kuipeleleza nchi. Wakaendelea mbele kwa muda wa


nusu saa, hatimaye, wakafika tena pwani, wakaona ya kwamba nchi ile
ilikuwa imezungukwa na bahari pande zote; ilikuwa peke yake katikati ya
bahari. Bulicheka akaeleza, “Kumbe! Leo tumefika katika kisiwa.”
Lizabeta akajibu, “Loo! Tuondoke haraka.”
Bulicheka akasema, “La! Hatuwezi kuondoka pasipo mashua, au labda meli
ifike kutuchukua.”
Lizabeta akasema, “Lakini tutapa wapi nyumba ya kukaa hapa katika nchi
hii?”
Na kweli hata Bulicheka akaona hilo ni tatizo kubwa sana, wataipata wapi
nyumba ya kukaa?
Akafikiri, akafikiri, hata akaumwa kichwa. Akakizungukia kile kisiwa ili
aone ya kwamba kuna uwezekano wa kulipata hata likiwa pango. Lakini
pango lina hatari ya kukaliwa na wanyama nyakati za usiku. Mara akaiona
minazi minne iliyoota karibu karibu, ikiwa imekaribiana vizuri, hata
akapatwa na wazo la kuitumia minazi hiyo katika kujijengea nyumba yake
ya ajabu.
Kwanza alikwenda pwani kuichukua ile meza yake, akaipeleka mpaka
kule kwenye minazi ile minne.

Akasokota kamba ndefu sana, akaivuta juu ile meza, akailaza vizuri sana
katikati ya magogo, halafu akaifunga kwa kamba yake. Kazi hii ilikuwa
ngumu sana kiasi cha kumchosha kabisa, hata hivyo, hakukubali
kushindwa, mwishowe akafaulu.
Lizabeta akasema, “Je, Bulicheka, nitawezaje kuupanda mti hadi nifike
nyumba yetu?”
Bulicheka akajibu, “Wewe usiwe na hofu, nitatengeneza ngazi ya kamba
itakayokuwezesha kupanda kwa urahisi. Nyumba yetu ikiisha kuwa tayari
utaona ajabu kweli kweli. Siyo watu wengi duniani walio na nyumba kama
hii yetu sisi. Tena ni nyumba yenye usalama kamili. Wanyama hawawezi
kutuingilia usiku. Leo ukiwa na njaa huna budi kula nazi tena, kesho
nitakwenda kuwinda paa.
Bulicheka akatengeneza kuta za nyumba kwa kutumia makuti ya mnazi,
akayasukasuka vizuri. Akawahi hata kufanya dirisha ukutani ili wapate
kuyatazama mambo ya nje; mwishowe, ikawa nyumba ndogo, lakini nzuri,
mahali pa kuwatosha watu wawili. Akatengeneza pia ngazi ya kuteremkia
chini. Alichukua vijiti, akaviunganisha kwa kamba toka juu mpaka chini;
bali wakati wa usiku alikuwa akiipandisha juu ili isiwepo hatari ya mtu
kuingia upande ule.
Bulicheka akafikiri: Sasa nitakwenda kuwinda paa. Lakini sina silaha
yoyote. Haidhuru, nitajitengenezea silaha vilevile. Akalitafuta tawi
litakalofaa kuwa upinde, akalichonga vizuri, likawa na ncha mbili. Halafu
akalifungia kamba likawa uta.

Lakini uta peke yake hautoshi. Akakata na mishale pia, akaichonga, ili
zile ncha zake ziwe kali sana kama sindano, hapo akawa mata tayari.
Bulicheka alitaka kuwinda paa. Akatafuta kila mahali asimpate paa, awe
mkubwa awe mdogo. Wanyama aliowahi kuwaona ni mbuni, wale ndege
wakubwa wenye miguu yenye nguvu, kazi yao kutembe chini chini ardhini
bali hawawezi kuruka angani. Akajisemea, “Ikiwa siwezi kumpata paa,
basi, haidhuru, nitajaribu kumpata mbuni. “
Lakini, kumbe, ilikuwa ni kazi. Kwa maana yeye Bulicheka akakaribia,
mbuni humwona na kutoroka.
Akafanya jambo moja. Kwanza alijificha nyuma ya mti. Akajifungia
majani nyuma mithili ya manyoya ya mbuni, akachukua fimbo mkononi juu
yake ikiwa ina tunda linalofanana na kichwa, halafu akajitokeza hivi akiwa
kama mbuni. Ndege wale wakimwangalia kwa mshangao! Mbuni wa
namna gani huyu? Wala hawakutoroka. Hata Bulicheka alipomkaribia zaidi,
akampiga mmoja wao, akamwua.

Kwa furaha kubwa, alimshika shingoni kwa mkono wake, kwa sababu
hakuweza kumbeba kwani alikuwa mzito mno. Akashika njia kurudi
nyumbani akiwa amejaa furaha moyoni, na wimbo mdomoni. Kumbe, mzee
mamba naye alimwona akipita. Yeye pia alikuwa na njaa, akatamani kumla
yule mbuni. Akamnyemelea polepole, akienda taratibu nyuma ya
Bulicheka, kama ilivyo desturi yake, alimkamata yule mbuzi kwa ghafla,
hata akawahi kummeza karibu wote mara moja tu.

Kwanza maskini Bulicheka alikuwa hana habari, akaendelea na safari


yake huku akiimba wimbo wake, mpaka hapo alipohisi ya kwamba kuna
mshindo nyuma yake. Akageuka nyuma, akaangalia, akamwona mzee
mamba. Lo! Akaruka kwa hofu na kwa kushtuka mno. Kofia yake
ikaanguka chini, upinde ukamponyoka, akatetemeka sana. mara akaanza
kukimbia, akakimbia mpaka akachoka.
Alipofikiri kwamba sasa yu salama, akaliona namna jabali kando kando
ya njia yake, akaona afadhali apumzike kidogo. Basi akalikalia hilo jabali.
Lakini, lo! Mara jabali lenyewe likainuka na kuanza kutembea, na yeye
mwenyewe Bulicheka akiwa juu yake! Hilo lilikuwa siyo jabali hata
kidogo, bali alikuwa ni faru, mwenye pembe juu ya pua yake. Akaanza
kwenda mwendo wa kasi. Bulicheka alipojiona yupo karibu na mti akaruka,
na kuukwea ili apate kujiokoa; lakini alipoangalia juu ya mti huo aliona
joka kubwa likimwangalia usoni.

Hapo akashtuka zaidi kiasi cha kukata tamaa ya kutoka salama kutokana na
hatari hizo nyingi. Kwa ajili ya hofu kubwa, aliuachilia ule mti, akaanguka
chini. Yule faru alikuwa ameendelea mbele na safari yake, wala
hakumwona. Basi Bulicheka hakuwa na hamu ya kuendelea kuwinda
wanyama tena, badala yake, kwa siku hiyo, alitamani tu kurudi nyumbani.
Wakati huo huo, Lizabeta alikuwa akimngojea Bulicheka arudi, kwani
aliona ya kwamba alikuwa anakawia: Bulicheka huyu alikuwa ameondoka
asubuhi na mapema, na sasa ni saa kumi ya jioni bado hajarudi. Yuko wapi,
maskini? Labda ametumbukia shimoni, au labda amekumbwa na simba.
Kila mara Lizabeta alikwenda kuketi dirishani ili apate kuangalia kama
Bulicheka anarudi au hapana. Lakini ni kazi bure tu. Hata akiangalia mara
kumi au zaidi, hamwoni Bulicheka. Anaiona minazi na miti mingine,
anayaona mawingu, anaiona bahari, kwa sababu yupo katika kilele cha
mnazi wake, lakini mtu yeyote alikuwa hamwoni kabisa.
Mpaka ikatimia saa kumi na moja! Lizabeta akachungulia dirishani ndipo
akamwona Bulicheka akija mbio. Upinde na mishale yake yote imepotea,
anakuja kwa haraka sana, wala haangalii nyuma. Lizabeta akamnyoshea
mkono kumlaki kwa furaha, lakini Bulicheka alikuwa haoni kitu,
amekazana tu kuja mbio. Mwishowe, akafika ngazini, akapanda kwenda juu
haraka haraka akaingia nyumbani mwao, akasimama, akiduwaa, asiweze
kusema neno lolote kwanza, ameshtuka mno! Miguu yake inatetemeka
bado. Lakini Lizabeta anamtuliza moyo, anasema, “Usiwe na hofu hivyo,
Bulicheka. Hapa hakuna hatari. Kama huwezi kuwinda paa wala kanga au
kobe, tutaendelea kula nazi tu, au mbata. Hatuwezi kufa kwa njaa.”
Sehemu ya pili

Siku moja, walipochungulia dirishani saa za asubuhi, wakakiona kitu cha


ajabu. Wakaiona mashua moja inakuja. Kwanza wakaliona tanga peke yake,
lakini halafu, ilipokaribia, wakaona ya kwamba walikuwamo watu ndani,
watu wa namna namna. Watu wasiokuwa na desturi nzuri.
Lizabeta akasema, “Lo! Watu hawa ni watu wa ajabu. Wamevaa singa za
wanyama kichwani, na wameshika mikuki mkononi. Lo! Naogopa, huenda
wakawa wala watu.”
Bulicheka akajibu, “Haifai kuogopa kabla. Ngoja wafike kwanza. Labda
hawatuoni hapa tulipo!”
Wakaipweleza mashua yao, wakashuka pwani. Mmoja wao alikuwa
mnene kabisa, mwenye uso mkali sana, akiwa amevaa upanga. Bulicheka
na Lizabeta wakamtambua kwamba ndiye mfalme wao.
Basi, watu wale walisimama kwa muda kidogo, halafu wakaanza
kukizungukia kile kisiwa kila upande, hatimaye, wakafika pale mahali
ilipokuwapo ile minazi minne ya Bulicheka, na nyumba yake ikiwa
mwenye makuti.

Mfalme yule akawaonyesha wenzi wake na kuwauliza, “Je, ni ndege wa


aina gani awezaye kujenga kiota kule mnazini? Mmepata kumwona ndege
wa namna hiyo?”
Wakajibu, “Hatujapata kumwona bado ndege mwenye kiota kama hicho.
Akasema, “Hebu , tupige makelele mengi ili atoke.”

Wakapiga makelele mengi kwa sauti kubwa, hata Bulicheka akalifungua


dirisha lake, akachungulia nje. Akawauliza, “Je, nyinyi mnataka nini hapa?”

Mfalme mwenyewe akamjibu, “Wewe unafanya nini hapa petu msituni,


tena unakaa mtini kama vile ndege? Shuka chini.”
Bulicheka akasema, “Mimi ninakaa mnazini kwa hiari yangu! Hili si shauri
lako. Ondoka hapa, kuna faru mkali sana. atakuchoma kwa pembe lake.”

Mfalme akajibu, “Wewe unanidanganya tu. Ni mtu wa aina gani wewe?


Umekujaje hapa?

Bulicheka akasema, “Mimi nimekuja kwa mashua kama mlivyokuja nyinyi.


Nikajenga nyumba yangu hapa juu! Je, wataka nini?”
Bulicheka akaona ya kwamba hawataki kuondoka. Walikuwa watu wenye
kutisha na kutia hofu kweli kweli. Walikuwa hawakuvaa nguo yoyote ile
isipokuwa singa za mbega vichwani mwao, na ukindu viunoni, wakishika
mikuki mikononi. Yule mfalme mwenyewe alikuwa amevaa upanga
mkubwa sana, na shingoni kwake alikuwa amevaa ushanga.
Wale watu walipoona ya kwamba Bulicheka amekataa kuteremka chini,
wakapiga makelele mengi zaidi. Mfalme akamwamuru ashuke, lakini hata
hivyo, hakutaka, kwa maana aliogopa kwamba hao huenda wakawa wala
wala-watu, wenye hatari. Mwishowe, alianza kuwatupia nazi, kwa sababu
alikuwa hana silaha ya aina nyingine; upinde wake ulikuwa umebaki
mwituni.
Mmoja wao akasema, “Hakika hatuondoki hapa mpaka umepigana na
sisi.”
Bulicheka akajibu, “Mimi sina ugomvi na nyinyi. Aliyeanza kunichokoza
ni huyu mfalme wenu. Mkitaka, nitapigana naye, lakini nawaambieni kweli
kwamba nitamshinda tu.”
Wote wakayakubali maneno yake, wakaona ya kwamba inafaa iwe hivyo.
Kwa sababu walikuwa hawampendi mfalme wao kwa dhati.
Basi, Bulicheka akashuka. Kila mmoja wao akapewa rungu ili wapigane
kila mtu akiwa upande wake, walikuwa hawana ruhusa kuwa na silaha
nyingine yoyote.
Yule mfalme, ambaye jina lake ni Huhihuihui, akadhani atamshinda
Bulicheka kwa dhoruba moja tu, kumbe sivyo!

Bulicheka alikuwa mwerevu kabisa, alikuwa akiangalia sana Huhihuihui


anazungukia upande gani na hivyo akawa analiepa kila pigo; papo hapo
yeye mwenyewe akilitumia rungu lake vizuri. Alikuwa mwerevu kiasi cha
kumshinda mfalme Huhihuihui, bila kuzichafua nguo zake.
Labda mnafikiri watu wale walikasirika kwa sababu Huhihuihui alikuwa
ameshindwa, lakini sivyo hata kidogo. Kama niivyosema, mfalme huyo
alikuwa mbaya sana, watu wake walikuwa hawampendi kwa sababu
aliwasumbua wenyeji.
Basi, walifurahi sana kwa sababu mfalme wao alikuwa ameshindwa,
wakamfukuzia mwituni aende kujitafutia chakula chake peke yake;
wakamweka Bulicheka awe mfalme wao. Akapewa upanga ule mkubwa
wa Huhihuihui, ambao ala yake ni ngozi ya chatu, na mpini wake wa
pembe. Akapewa vilevile ule ushanga wa kifalme auvae.

Bulicheka akamwita mwenzi wake, “Lizabeta, shuka sasa. Usiogope tena.


Sasa umekuwa malkia. Angalia bahati yetu kubwa! Tulifikiri tumepotea,
kumbe tumekuwa wafalme. Sasa tufunge safari yetu kwenda nyumbani
hasa.
Lizabeta akashuka, watu wote wakamwinamia kwa heshima kubwa. Sasa
siku zao za kukaa kisiwani zimekwisha, watakwenda kutawala.
Lizabeta akamwambia Bulicheka, “Waulize ni watu wa kabila gani hao?
Utawezaje kuwa mfalme wa watu usiowajua kabila lao?”
Bulicheka akasema, “Kweli. Ngoja niwaulize.”
Akawauliza, “Ati, nyinyi ni watu wa kabila gani? Sisi hatujapata kuwaona
watu kama nyinyi.”
Wakasema, “Sisi tu Wagagagigikoko. Nchi yetu ni nzuri sana. ukiisha
kuiona utashangaa.”
Basi walitaka kurudi sasa katika nchi ya Wagagagigikoko. Wakafanya
maandamano, wakienda mmoja mmoja, kila mtu akishika mkuki wake na
Bulicheka pamoja na Lizabeta wakifuata nyuma, mpaka kufika pwani.

Mashua yenyewe ilikuwa imepwelezwa juu ya mchanga. Mkubwa


mmoja akawaamuru wengine kuishusha majini. Ilikuwa ni kazi kubwa kwa
sababu mashua ile ilikuwa nzito.
Ilikuwa ajabu jinsi mashua ile ilivyoundwa. Karibu yote ilikuwa
imetengenezwa kwa magamba ya mti fulani, yaliyoshonwa pamoja na uzi,
kama vile wenyeji wa Lamu wanavyoishona mitepe yao.
Bulicheka na Lizabeta wakasimama pwani kuwangoja watu wote wawe
tayari, Bulicheka akiwa ameushika upanga wake na kuuinua juu kama
ishara ya enzi yake.
Hatimaye, watu wote wakawa tayari, wakaingia wote ndani ya mashua,
kila mtu akakaa mahali pake. Wagagagigikoko wakatweka tanga, wakaanza
safari ya kwenda katika nchi yao.
Lizabeta alikuwa akiogopa kidogo kusafiri tena kati ya mawimbi, lakini
kwa bahati nzuri, hawakupata upepo mkali, wakaendelea vizuri kabisa.

Baada ya saa chache wakafika katika nchi ya Wagagagigikoko. Hakika,


ilikuwa ni nchi nzuri sana. Toka baharini, wakaziona nyumba nyingi
zilizotengenezwa na kujengwa kwa mtindo wa pekee na namna yao
wenyewe, siyo kama zilivyojengwa nyumba za Dar es Salaam au zile za
Mombasa, Morogoro au Nairobi. Nyumba za mji huo zilikuwa nzuri sana,
lakini zote zilikuwa zimejengwa juu ya nguzo nyingi, na mtu akitaka
kuingia humo alikuwa hana budi kutumia ngazi.
Mambo hayo yote waliyaona toka mashuani. Mabaharia wakashusha
tanga, , wakaipeleka mashua karibu ya nchi, palipokuwa na ulalo wa
kuwapokelea wageni.
Wenyeji wengi walikuwa wamekusanyika pale ili kumlaki mfalme wao.
Lakini, mtu mmoja alijitokeza kwanza, akawapasha wenyeji wote habari ya
kwamba yule mfalme wa zamani, Huhihuihui alikuwa amefukuzwa, na
badala yake, walikuwa wamemleta mfalme mpya, jina lake Bulicheka.

Hapo Bulicheka akasimama wima, na Lizabeta vile vile. Wenyeji wote


wakarukaruka kwa furaha, wakapiga vigelegele walipomwona mfalme wao
mpya akitoka mashuani na kuikanyaga nchi yao.
Mara Bulicheka na Lizabeta wakapelekwa kwenye nyumba yao ya
kifalme. Nyumba iliyokuwa kubwa na nzuri kuliko nyingine zote.
Askari wawili wakasimama mlangoni, na mbele ya mlango zilikuwako
nguzo nguzo mbili kubwa sana zilizochongwa kwa ubao na fundi hodari.
Wakaongozwa ndani hadi kwenye chumba kimoja kizuri, kilichopambwa;
wakaambiwa waketi juu ya viti viwili ambavyo navyo vimetengenezwa
kwa ufundi mkubwa. Lakini, Bulicheka akakumbuka ya kwamba walikuwa
hawajapata kula chakula cha maana kwa muda wa siku nyingi,
akamwambia wale Wagagagigikoko waliokuwapo kwamba yeye anaona
njaa, na Lizabeta vile vile.
Mara wapishi wa mfalme wakatoka kwa haraka wakaenda kupika vyakula
vingi vya kila namna; na baada ya nusu saa wakarudi, msafara mzima wa
watu, kila mmoja amechukua mkononi sahani, au bakuli au kikapu
kilichojaa chakula.

Mtu wa kwanza, akaleta sahani kubwa ya wali, yaani ndicho chakula cha
kwanza. Watu husema, “Wali ni sultani ya chakula, watawazwa katika kiti.”
Wa pili akaleta kikapu kilichojaa vitumbua vya sukari. Wa tatu, akaubeba
mkungu mzima wa ndizi zilizo kubwa sana. Wa nne akaja na kuku, kila
mkono umemshika kuku mmoja. Wa tano, akaleta sahani ya mayai. Basi,
wakala, wakashiba.
Saa za jioni, kukawa na ngoma. Ngoma yao ya ajabu. Watu wote
wakapiga, wakapiga hata kukawa na muungurumo wa kuziba masikio. Mtu
mmoja alikuwa na mbiu moja ndefu sana kiasi cha kushindwa kuuinua kwa
mikono yake, ikalazwa chini, naye akapuliza ndani yake, akiyavimbisha
mashavu yake mithili ya balungi. Tena mtu mwingine alikuwa na namna ya
zeze ambalo lina umbo kama pembe la nyati, mwenyewe akilipiga, linatoa
sauti kama mlio wa ndege.

Ngoma hizo ziliendelea kwa muda wa saa nyingi sana. Giza lilitanda juu
ya nyumba za watu, lakini mwezi ukaonekana katika minazi.

Hatimaye, wakaenda kulala, kwa maana Bulicheka na Lizabeta walikuwa


wamechoka sana kwa sababu ya safari na kukaa siku nyingi katika nyumba
yao mnazini. Na watu wote walipokuwa wamelala usingizi, mtu mmoja
alikuwa akisimama juu ya mnara, kama mlinzi, ili apate kuulinda mji
pasitokee hatari yoyote ya kushambuliwa kwa ghafula
Sehemu ya Tatu
Siku moja Bulicheka alikuwa chumbani mwake saa za usiku. Mara
akasikia mlio wa ajabu. Akasikiliza zaidi, akafikiri labda mnyama wa
msituni au wa porini ndiye aliyepaliza sauti yake. Kumbe, sivyo!
Mlinzi yule mwenye kazi ya kuulinda mji wakati watu wamelala, alikuwa
akiipiga mbiu yake kwa nguvu zake zote.

Watu wote wakashtuka, wakazindukana katika usingizi wao, wakaruka


kutoka vitandani, wakatoka nje kuangalia kuna nini? Karibu wote
walichukua mikuki yao, kadhalika mishale na ngao, wakifikiri kuna vita.
Kumbe haikuwako vita yoyote, bali mji wao ulikuwa ukiteketea kwa moto.

Nyumba mbili zilikuwa zimekwisha shika moto. Moshi mzito ulitoka


katika mapaa, na cheche za moto zikarushwa angani, zikapeperushwa na
upepo na kuangushwa katika nyumba nyingine.
Watu wote wakahangaika sana kuyaezua manyasi juu ya mapaa, na
kuvitoa vyombo vyao nje, ili wasipate hasara kubwa mno.
Hata Bulicheka alikwenda, kwa haraka sana, kuwasaidia watu wake.
Aliona ni jambo muhimu kwa mfalme kuwasaidia watu wa nchi yake.
Akaingia katika nyumba zilizoshika moto, ili apate kuangalia kama watu
wote walikuwa wamekisha kutoka, na kama vyombo vyote vimeondolewa
au hapana.
Bulicheka akawa shujaa sana. akapitapita katikati ya ndimi za moto bila
kuogopa hata kidogo. Moshi ukamwingia machoni, lakini hakujali. Mikono
yake ikapata malengelenge, bali yeye akavumilia tu. Watu wote
wakahakikisha kwamba huyu ni shujaa kweli kweli.
Mwishowe, akakutana na mtu mmoja aliyekuwa akilia machozi, anapiga
yowe na kulalamika.
Akamuuliza, “Kuna nini, mama? Una uchungu gani?”
Akajibu, “Mtoto wangu amebaki ndani ya nyumba yangu, nami siwezi
kuingia nimtoe sababu ya moto.”
Bulicheka akasema, “Niambie upesi yumo katika nyumba gani?”
Akajibu, “Yumo ndani ya nyumba ile inayowaka kabisa.”

Basi, Bulicheka hakusitasita. Mara ile akaingia ndani ya nyumba hiyo.


Watu wote wakastaajabu. Mtu huyu haogopi kitu chochote!

Hawakuweza kumuona kwa sababu ya moshi mwingi, na ndimi za moto


zikauzuia mlango. Watu wakasimama nje kumngoja Bulicheka atoke tena,
lakini alikawia kuonekana.
Hatimaye, akajitokeza, uso wake umetapakaa masizi na nguo zake
zimechafuka, lakini mkononi alikuwa amemshika mtoto mchanga, naye
anapiga makelele kwa hofu ya moto.

Watu wote waliosimama nje walipomuona, wakapiga vigelegele kwa


shangwe, wakimshangilia sana. na mama mwenyewe, akampokea mtoto
wake kwa shukrani kubwa. Mwana alikuwa mzima kabisa, wala hakupata
hasara yoyote ile.
Kwaajili ya ujasiri wake huo, Wagagagigikoko wakampenda sana
Bulicheka.
Siku moja akawauliza, “Je, nyinyi mwaweza kuunda merikebu kubwa?”
Wakasema, “Hatujui sisi.”
Bulicheka akawaambia, “Basi, nitawafundisheni.”
Wakaiunda merikebu nzuri sana. ilipokuwa tayari wakaenda baharini ili
wapate kuijaribu.
Kwanza safari yao ilikuwa nzuri sana. wakaipeleka kwanza upande wa
kaskazini, halafu upande wa mashariki, halafu upande wa magharibi tena,
kadiri ya upepo ulivyowafaa, na mwisho wakaipeleka upande wa kusini,
wakaiona merikebu yao kuwa ni nzuri kabisa, wakafurahi.
Lakini siku ya tatu walipokuwa wanataka kurudi kwao, upepo ulianza
kuvuma kwa nguvu sana. kweli, nguvu ya upepo ule, ilikuwa nguvu ya
ajabu.
Siku hiyo, upepo ulivuma mchana kutwa, na hata wakati wa usiku
haukutulia. Minazi ilitikiswa kama mianzi, madafu yote yakaangushwa
chini, na makuti yakapeperushwa.
Hata nyumba za watu zikasukwasukwa ovyo juu ya nguzo zao, kama vile
zinaelekea kuanguka na kubomoka. Usiku huo hakuna mtu aliyelala
usingizi.

Bulicheka hakurudi na watu wake alivyokwenda nao katika merikebu.


Asubuhi yake Lizabeta akapanda juu ya mnara ili apate kuangalia
baharini kama meli inakuja, lakini hakukiona hata kitu kimoja. Akalia
machozi.

Lakini machozi yake yote yalikuwa ya bure tu. Kwa maana upepo ule
ulipoanza kuvuma na kuikokota ile merikebu, Bulicheka na watu wake
walifanya kazi kubwa sana ya kukiongoza chombo chao vizuri. Wakajaribu
kwa bidii yao yao yote kuirudisha bandarini, bali hawakufaulu.
Kwanza, usukani wenyewe ulivunjika vipande vipande. Halafu, hata
mlingoti ukapasuka kama kijiti kwa ajili ya upepo uliokuwa ukivuma mno.
Mwishowe, wakakagongana na jabali, merikebu ikatoboka, na kuanza
kuzama. Hapo, wakawa hatarini kweli kweli. Merikebu yao ikasukwasukwa
huku na huku mara kwenye jabali, mara baharini. Hapakuwa tena na mtu
aliyeweza kusimama wima.

Siku ya tatu, upepo ukatulia. Bulicheka na wenzake wakaondoka katika


chombo chao, wakajaribu kulipanda lile jabali. Hali yao ilikuwa mbaya
sana. jabali tupu, hakuna mti wala mnyama, wala mtu.
Bulicheka akasema, “Ni afadhali tujenge hema hapa. Tunavyo bado
vipande vya mlingoti, na tanga ambavyo vitatufaa. Basi wakapiga hema ili
kujilinda na ukungu wa bahari, wakapumzika, wakalala.
Asubuhi yake, wakatazamana, wafanye nini sasa? Kisha kuwa hawana
jahazi, dau wala ngalawa au mtepe, na kuogelea ni mbali mno hadi huko
kwenye nchi kavu.
Walipokuwa katika kulifikiria hili, wakakiona kisiwa kimoja ng’ambo ya
bahari, na kuna namna ya ngalawa ndogo inayokuja toka kisiwani. Na
ngalawa ile ilipokaribia wakaona inaongozwa kwa makasia, na mtu mmoja
aliyekuwa mzee.
Mtu yule akafika, akapanda jahazi, akaja kusimama mbele ya hema,
akapiga hodi. Mara Bulicheka akatoka nje, akampokea vizuri sana,
akamuuliza, “Wewe ni nani?”

Mzee akamjibu, “Mimi jina langu Miraji. Nimekaa katika kisiwa changu
kwa miaka kumi na mitatu, na sijawahi kumuona mtu yeyote. Leo
nimekuona katika jabali hili, basi, nimekuja kukuchukua.”
Lo! Bulicheka na wenziwe wakafurahi sana kuokolewa katika taabu yao.
Wakamfuata mzee Miraji katika ngalawa, naye akawapeleka mpaka
nyumbani kwake.
Mzee Miraji alikuwa na nyumba nzuri. Ilikuwa kama pango katika mlima,
lakini mbele yake kulikuwako kiambaza chenye mlango na dirisha moja.

Akawapokea vizuri sana, hata akawapikia chakula, akatandika meza. Kwa


maana, mle ndani ya pango mlikuwa kama nyumba hasa mkiwa na meza,
viti na vikombe.
Bulicheka akastaajabu, akamuuliza, “Kwa nini umetuambia ya kwamba
umekaa hapa katika kisiwa peke yako kwa muda wa miaka kumi na mitatu,
na kumbe kila kitu unacho?”
Mzee Miraji akamjibu, “Kweli, hasa! Bali nguo sina. Katika mavazi
yangu yote, sasa nimebakiwa na gunia tu. Sikiliza bwana, sikuja kwa hiari
yangu katika kisiwa hiki. Nilitupwa kwa nguvu za upepo kama
ulivyofanywa wewe. Wenzangu wote walizama pamoja na merikebu yao,
ila mimi nikasalimika. Basi, nilipopanda mlima huu, nikayakuta haya yote.
Mtu mwingine alikuwa akiishi hapa, lakini mimi sikumkuta tena. Na juu ya
meza hii, nilikuta barua moja, inayoeleza habari ya kuwako hazina, lakini
sijui ni mahali gani ilipo. Nimeitafuta kila mahali, lakini mpaka sasa
sijafaulu kuipata.

Alipokuwa alisimulia mambo hayo, mara wakasikia namna ya ngurumo


chini ya ardhi.
Bulicheka akauliza, “Kitu gani hicho?”
Mzee Miraji akamjibu, “Ngurumo hiyo inatoka kwenye mlima ule ulioko
karibu. Mlima huo ni volkeno, hutoa moshi na mara moja moja, hutoa hata
moto.”
Bulicheka akashtuka kuisikia habari kama hiyo. Akasema, “Hivi kuna
hatari hapa?”
Mzee Miraji akajibu, “Hatari yenyewe siyo kubwa sana, lakini sijui hapo
siku za mbele.”
Wakatoka nje kwenda kuuangalia mlima huo. Kweli ulikuwa ukitoa
moshi mzito sana, na hata moto ukaonekana kidogo.
Mara walipokuwa katika kuuangalia, nchi yote ikaanza kutetemeka sana,
ngurumo ikawa kali mno, na moshi ukaenea juu ya kisiwa chote. Mawe
yakaporomoka toka mbinguni, hata mzee Miraji na Bulicheka wakarudi
mbio nyumbani mwao, ili kujilinda na mvua ya mawe iliyoanza kunyesha.

Bulicheka akaichukua nguzo moja iliyokuwa mbele ya mlango,


akaiegemeza ili ipate kuuzuia mlango usifunguke. Kwa maana kulikuwa na
makelele, mshindo na ngurumo ya ajabu. Nchi yote na hata mlima
ukatetemeka, ukatikiswa hasa, ikawa wasiwasi tena kusimama wima.

Mara wakausikia mshindo mkubwa sana kama vile ukuta wa nyumba yao
umepasuka.
Wakaangalia, kumbe wakaona ni kweli, upande wa kushoto, jabali
lilipasuka kabisa, na kutokana na kupasuka huko, hazina yenyewe
iliyofichika kwa miaka mingi, ikaonekana, sarafu za fedha na dhahabu
zikatawanyika ovyo chini, zikajifiringisha huku na huku na kuijaza nyumba
nzima.
Lo! Kwanza Bulicheka na mzee Miraji walipigwa na mshangao. Halafu
wakakumbuka, kumbe hiyo ndiyo hazina iliyokuwako, sasa tumeipata.
Wakachukua magunia, kila mtu gunia lake, wakayajaza sarafu tele, kadiri
walivyoweza.

Mzee Miraji akasema, “Kwanza, nitanunua nguo, halafu nitanunua


nyumba nzuri na kitanda cha samadari.”
Bulicheka akauliza, “Kweli, nilikuwa nimesahau, kumbe, yote ni bure tu!”
Wakati huo, wakaona mlima wa volkeno umetulia sasa. Bulicheka
akafungua mlango ili apate kupunga hewa, akaangalia kama nje kungali
kumetanda bado au kumepambazuka vizuri.
Alipokuwa akiangalia nje hivi moyo wake ulianza kudundadunda
gogogogo, kwa sababu alikuwa ameiona meli moja ikikaribia, ndiyo nafasi
ya kuondoka katika kisiwa chao.
Wakawasha moto upesi, wakakipepea kitambaa kwa nguvu, hata mwisho
nahodha wa meli akaona. Akawatuma watu wake katika mashua kusudi ya
kuwachukua Bulicheka, mzee Miraji na Wagagagigikoko wale waliosafiri
pamoja na mfalme wao.
Wakapokelewa vizuri na nahodha wa meli. Bulicheka akamuuliza,
“Unasafiri kwenda mji gani?”
Nahodha akajibu, “Tunakwenda Mombasa sasa.”
Bulicheka akasema, “Vizuri sana, mimi vile vile nataka kwenda
Mombasa, lakini kwanza sina budi kumchukua mwenzangu ambaye yuko
katika nchi ya Wagagagigikoko. Naomba twende kwanza upande ule, mimi
nitakupa nauli yoyote utakayoitaka.”
Nahodha akakubali, “Wakarudi kwanza katika bandari ya nchi ile ya
Wagagagigikoko, nao wakafurahi ajabu. Hasa Lizabeta alifurahi mno,
akacheka mpaka mashavu yakamwuma.
Bulicheka, akamwita waziri mkuu akamwambia, “Ama, napenda sana
kuiangalia nchi yetu. Meli hiyo iliyotuleta hapa itakwenda Mombasa, nami
nitakwenda pamoja nayo. Wewe chukua ushanga huu wa ufalme, utatawala
hadi hapo nitakaporudi tena.”
Waziri huyu akaona ameheshimiwa sana, akashukuru akasema kwamba
atafanya bidii ya kutawala vizuri kabisa, wenyeji wote wakafurahi.
Mwishowe, Bulicheka na Lizabeta wakapanda meli, wakaenda zao.

You might also like