Download as pdf or txt
Download as pdf or txt
You are on page 1of 11

24 MACHI 2024

DOMINIKA YA MATAWI
KATIKA MATESO YA BWANA
MWAKA B

Kukumbuka Kuingia kwa Bwana Yerusalemu

INJILI Marko 11:1-10

Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Marko.


Walipokaribia Yerusalemu, mbele ya Bethfage na Bethania karibu na Mlima
wa Mizeituni, [Yesu] aliwatuma wawili wa wafuasi wake, akiwaambia,
“Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu. Mara mnapoingia mtamwona
mwanapunda amefungwa, naye hajakaliwa bado na mtu. Mfungueni,
mkamlete. Na endapo mtu atawauliza, ‘Mbona mnafanya hivi?’ jibuni
‘Bwana anamhitaji, atamrudisha mara.’” Wakaenda, wakamwona
mwanapunda amefungwa mlangoni nje barazani, wakamfungua. Baadhi ya
watu waliosimama huko wakawaambia, “Je, kwa nini mnamfungua huyo
mwanapunda?” Wakawaambia kama Yesu alivyowaagiza, nao
wakawaruhusu. Wakampeleka mwanapunda kwa Yesu, wakamtandika
mavazi yao mgongoni. Akaketi juu yake. Wengi walitandaza mavazi yao
njiani, na wengine matawi waliyokuwa wameyakata mashambani. Watu
waliotangulia na waliofuata walishangilia wakiimba: “Hosana! Mbarikiwa
anayekuja kwa jina la Bwana! Umebarikiwa ufalme ujao wa baba yetu
Daudi! Hosana juu mbinguni!”
Injili ya Bwana... Sifa kwako Ee Kristu.

Au:
Yohane 12:12-16
Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Yohane.
Wakati ule: Umati mkubwa wa watu waliokuja kuhudhuria sikukuu
walipata habari ya kwamba Yesu anakuja Yerusalemu, wakatwaa matawi ya
mitende, wakatoka mjini kumlaki, Wakapaza sauti wakisema, “Hosana!
Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana, Mfalme wa Israeli.” Yesu akakuta
mwanapunda, akapanda juu yake, kama ilivyoandikwa: “Usiogope, binti
Sioni; Tazama, Mfalme wako anakuja amepanda mwanapunda.” Kwanza
wafuasi wake hawakufahamu matukio hayo, lakini baada ya kutukuzwa
Yesu, walikumbuka ya kuwa yameandikwa juu yake, na wenyewe
walimtendea hayo.
Injili ya Bwana... Sifa kwako Ee Kristu.

Misa

SOMO LA KWANZA Isaya 50:4-7

Somo katika kitabu cha Nabii Isaya.


Bwana Mungu amenipa ulimi wa hao wafundishwao, nipate kumjibu
yule achokaye kwa neno la kumwamsha. Kila asubuhi, yeye
huliamsha sikio langu ili nisikie kama mwanafunzi; Bwana Mungu
amenizibua sikio langu; nami sikukataa, sikurudi nyuma. Niliwatolea
mgongo wangu wale walionipiga, na mashavu yangu kwa wale
walioning'oa ndevu; wala sikuuficha uso wangu ili usifedheheshwe
na kutemewa mate. Bwana Mungu ndiye anayenisaidia, ndiyo
maana sihangaiki na hayo; ndiyo maana nimefanya uso wangu
mgumu kama jiwe, najua ya kwamba sitaaibishwa.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.

2
ZABURI YA KUITIKIZANA Zaburi 22
(K) Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?
Wote wanaoniona hunicheka; hunyonga midomo
kwa kunidhihaki; na kutikisa vichwa vyao:
“Alimwamini Bwana, acha amwokoe;
acha amuopoe, kwa kuwa anapendezwa naye.” (K)

Kwa maana mbwa wengi wamenizunguka;


kundi la waovu wananisonga.
Wamenitoboa mikono na miguu
naweza kuhesabu mifupa yangu yote. (K)

Wanagawanya nguo zangu kati yao;


wanaipigia kura kanzu yangu.
Nawe, ee Bwana, usiwe mbali;
ewe msaada wangu, fanya haraka kunisaidia. (K)

Nitawasimulia ndugu zangu jina lako;


katikati ya mkutano nitakusifu:
“Enyi watumishi wa Bwana, msifuni!
Enyi wote, wazao wa Yakobo, mtukuzeni;
enyi wote, wana wa Israeli, mtumikieni!” (K)

SOMO LA PILI Wafilipi 2:6-11

Somo katika barua ya Mtakatifu Paulo kwa Wafilipi.


Kristo Yesu, ijapokuwa alikuwa namna ya Mungu, hakuchukulia kwamba
kuwa sawa na Mungu lilikuwa jambo la kushikamana nalo. Bali alijishusha
mwenyewe, akatwaa umbo la mtumishi, akawa ana mfano wa wanadamu,
na alipoonekana ana umbo la mwanadamu, alijinyenyekeza mwenyewe,
akawa mtii mpaka mauti, yaani mauti ya msalabani. Kwa sababu hiyo

3
Mungu alimtukuza, akampa jina lipitalo kila jina, ili kwa jina la Yesu wote
wapige magoti, wote walioko mbinguni, duniani na kuzimu. Na kila ulimi
ukiri kwamba Yesu Kristo ndiye Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.

SHANGILIO LA INJILI
K. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.
K. Kristo alijinyenyekeza mwenyewe, akawa mtii mpaka mauti,
yaani mauti ya msalabani.
Kwa sababu hiyo Mungu alimtukuza,
akampa jina lipitalo kila jina.
W. Sifa na utukufu kwako, ee Kristo.

INJILI Marko 14:1—15:47

M — Msomaji
W — maneno ya Watu mbali mbali
 — maneno ya Yesu
M. Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo yalivyoandikwa na Mathayo.
M. Ilikuwa siku mbili kabla ya Sikukuu ya Pasaka na Mikate Isiyotiwa
Chachu. Makuhani wakuu na Waandishi walitafuta nafasi ya
kumkamata Yesu kwa hila na kumwua. Walisema,
W. “Lakini isiwe wakati wa sikukuu, isije ikatokea ghasia kwa watu.”
M. Yesu alipokuwako Bethania katika nyumba ya Simoni mkoma na kukaa
mezani, aliingia mwanamke na chupa ya alabasta, imejaa manukato
azizi ya nardi safi yenye thamani. Akafungua chupa, akammiminia

4
manukato kichwani. Baadhi ya wenye kuhudhuria wakaona chuki
wakasemezana,
W. “Ya nini uharibifu wa manukato azizi hayo? Ingaliwezekana kuuza
manukato kama hayo kwa zaidi ya dinari mia tatu na kuwapa maskini.”
M. Wakamkemea mwanamke. Yesu akasema,
 “Mwacheni. Mbona mnamsumbua? Amenitendea mema. Maskini
mnao kwenu siku zote, mnaweza kuwatendea mema mnapopenda.
Lakini mimi sitakuwapo pamoja nanyi siku zote. Aliyoweza
ameyatenda. Huyu ni wa kwanza kupaka mwili wangu manukato
kuutayarisha kwa mazishi. Amin, nawaambieni, kila mahali duniani
pote patakapohubiriwa Injili, tendo lake litatajwa kwa ukumbusho
wake.”
M. Hapo Yuda Iskariote, mmojawapo wa wale Kumi na Wawili, akatoka,
akaenda kwa makuhani wakuu kusudi amtie mikononi mwao. Nao
walifurahi kusikia hayo, wakaahidi kumpa fedha. Basi akawa anatafuta
nafasi nzuri ya kumsaliti. Siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate
Isiyotiwa Chachu, ndiyo siku ya kumchinja mwanakondoo wa Pasaka,
wafuasi wake walimwambia Yesu,
W. “Unataka tuende wapi kukuandalia karamu ya Pasaka?”
M. Akatuma wawili wa wafuasi wake, akawaambia,
 “Nendeni mjini. Huko mtakutana na mtu amechukua mtungi wa maji.
Mfuateni. Anapoingia, mwambieni mwenye nyumba, ‘Mwalimu
anasema, Kipo wapi chumba nipate kula humo karamu ya Pasaka
pamoja na wafuasi wangu?’ Naye atawaonyesha chumba kikubwa
ghorofani kilichotayarishwa. Humo, tuandalieni karamu.”
M. Wafuasi wakatoka, wakaenda mjini, wakakuta yote kama
alivyowaambia; na wakaiandaa karamu ya Pasaka. Ilipokuwa jioni,
alikuja pamoja na wale Kumi na Wawili. Walipokaa mezani na kula,
Yesu alisema,
 “Amin, nawaambieni, mmoja wenu anayekula pamoja nami
atanisaliti.”
M. Hapo walianza kuhuzunika na kumwuliza, mmoja mmoja,
W. “Ati, ni mimi?”

5
M. Akawaambia,
 “Ni mmoja wa hao Kumi na Wawili anayemega chakula katika sahani
moja nami. Basi, Mwana wa Mtu anakwenda zake kama Maandiko
yasemavyo, lakini ole wake mtu huyu anayemsaliti Mwana wa Mtu!
Ingemfaa kama mtu huyu asingelizaliwa.”
M. Pale karamuni Yesu alitwaa mkate, akashukuru, akaumega, akasema,
 “Twaeni; huu ndio mwili wangu.”
M. Akatwaa kikombe, akashukuru, akawapa, nao wakakinywea wote.
Aliwaambia,
 “Hii ndiyo damu yangu ya agano, itakayomwagika kwa ajili ya wengi.
Amin, nawaambieni, sitakunywa tena mzao wa mzabibu mpaka siku
nitakapokunywa upya katika ufalme wa Mungu.”
M. Walipokwishaimba zaburi, wakatoka wakaenda kwenye Mlima wa
Mizeituni. Kisha Yesu akawaambia,
 “Ninyi nyote mtakwazwa kwa sababu yangu mimi, kwa maana
imeandikwa: ‘Nitampiga mchungaji, na kondoo watatawanyika.’ Lakini
baada ya ufufuko wangu, nitawatangulia kwenda Galilaya.”
M. Petro akamwambia,
W. “Hata kama wote watakwazwa, lakini mimi sivyo.”
M. Yesu akamwambia,
 “Amin, nakuambia, leo, usiku huu, kabla ya kuwika jogoo mara mbili,
utanikana mara tatu.”
M. Naye akazidi kusema,
W. “Hata ikinipasa kufa pamoja nawe, sitakukana.”
M. Vivyo hivyo wakasema wote. Kisha wakaenda katika shamba liitwalo
Gethsemane, akawaambia wafuasi wake,
 “Kaeni hapa muda ninapoenda kusali.”
M. Akawachukua Petro, Yakobo na Yohane wakaenda pamoja naye.
Akaanza kufadhaika sana na kusononeka. Akawaambia,
 “Roho yangu ina huzuni nyingi hata kiasi cha kufa. Kaeni hapa na
kukesha.”

6
M. Akaenda mbele kidogo, akaanguka chini, akaomba kwamba, kama
ingewezekana, saa ile imwepuke; alisema,
 “Abba, Baba, yote yawezekana kwako. Uniondolee kikombe hiki, lakini
si nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe.”
M. Aliporudi, aliwakuta wamelala usingizi. Akamwambia Petro,
 “Je, Simoni umelala? Hukuweza kukesha walau saa moja? Kesheni na
kusali msije mkaingia katika kishawishi. Kwa maana roho ni tayari, ila
mwili ni dhaifu.”
M. Akaenda tena, akasali kwa maneno yale yale. Akarudi, akawakuta
wamelala tena usingizi, maana macho yao yalikuwa mazito.
Hawakujua la kumjibu. Akarudi mara ya tatu, akawaambia,
 “Mnalala bado na kupumzika? Imetosha, saa imefika. Tazameni,
Mwana wa Mtu anatiwa mikononi mwa wakosefu. Simameni, twende
zetu. Tazameni, anayenisaliti amekaribia.”
M. Alipokuwa akisema bado, Yuda, mmoja wa wale Kumi Wawili, alifika,
na pamoja naye watu wengi waliochukua panga na rungu mikononi.
Walikuja kwa amri ya makuhani wakuu na Waandishi na wazee. Yule
msaliti alikuwa amepatana nao ishara akisema,
W. “Nitakayembusu ni yeye; mkamateni, mkampeleke salama.”
M. Alipofika, alimjongea, akasema,
W. “Mwalimu.”
M. Akambusu. Hapo wakanyosha mikono, wakamkamata. Mmoja wao
waliosimama pale alichomoa upanga, akampiga mtumishi wa kuhani
mkuu, na kumkata sikio. Yesu akawajibu,
 “Je, mmekuja na panga na rungu kunikamata kana kwamba ni
mnyang'anyi? Kila siku nalikuwa hekaluni nikifundisha, wala
hamkunikamata; lakini sharti Maandiko yatimie.”
M. Hapo wote wakamwacha, wakakimbia. Basi kijana mmoja alimfuata
akiwa amejifunika shuka ya kitani. Wakamkamata, lakini aliwaachia
Shuka, akakimbia uchi. Walimpeleka Yesu kwa kuhani mkuu, huko
walikusanyika makuhani wote na wazee na Waandishi. Petro
akamfuata kwa mbali mpaka uani kwa kuhani mkuu, huko akakaa kati
ya watumishi, akiota moto. Makuhani na baraza lote walitafuta

7
ushuhuda wapate kumshtaki Yesu na kumwua, wasiupate.
Walimshuhudia uongo, walakini ushuhuda wao haukupatana, Wengi
wakasimama, wakamshtaki kwa ushuhuda wa uongo, wakisema,
W. “Sisi tulimsikia akisema, ‘Mimi nitalibomoa hekalu hili lililofanyika kwa
mikono na kwa siku tatu nitalijenga jingine lisilofanyika kwa mikono.’”
M. Lakini hata hivyo ushuhuda wao haukupatana. Kisha kuhani mkuu
akasimama katikati yao, akamwuliza Yesu,
W. “Je, hujibu neno kwa mashtaka wanayokushuhudia watu hawa?”
M. Lakini yeye alinyamaza wala hakujibu neno. Kuhani mkuu akamwuliza
tena,
W. “Wewe u Kristo, Mwana wa Aliyebarikiwa?”
M. Kisha Yesu akajibu,
 “Mimi ndiye; nanyi ‘mtamwona Mwana wa Mtu ameketi kuume kwa
Mwenyezi akija juu ya mawingu ya mbinguni.’”
M. Hapo kuhani mkuu akararua kanzu yake akisema,
W. “Je, tuna haja gani tena ya mashahidi? Mmesikia kufuru yake.
Mwaonaje?”
M. Wote wakaamua kwamba anastahili kufa. Wengine wakaanza
kumtemea mate. Wakamfunika uso, wakampiga makofi na
kumwambia,
W. “Agua!”
M. Hata watumishi walimpiga. Petro alipokuwa chini uani, akaja mmoja
wa vijakazi wa kuhani mkuu. Akamwona Petro akiota moto, akamkazia
macho, akasema,
W. “Nawe ulikuwa pamoja na Mnazareti huyu, Yesu.”
M. Lakini Petro alikana, akisema,
W. “Sijui wala sielewi usemalo.”
M. Akaondoka akaenda nje ukumbini. Jogoo akawika. Na yule kijakazi
akamwona huko, akaanza tena kuwaambia watu waliosimama pale,
W. “Huyu ni mmoja wao.”
M. Naye akakana tena. Kitambo kidogo wale watu waliosimama pale
wakamwambia Petro,

8
W. “Hakika, wewe u mmoja wao, kwa maana u Mgalilaya.”
M. Akaanza kulaani na kuapa,
W. “Simjui mtu huyu mnayemtaja.”
M. Mara hapo jogoo akawika mara ya pili. Petro akalikumbuka neno
aliloambiwa na Yesu, “Kabla ya kuwika jogoo mara mbili, utanikana
mara tatu.” Akahuzunika akalia machozi. Mara kulipopambazuka,
makuhani wakuu pamoja na wazee na Waandishi, ndiyo baraza lote,
walifanya shauri pamoja. Wakamfunga Yesu, wakampeleka na kumtoa
kwa Pilato. Pilato akamwuliza,
W. “Wewe u mfalme wa Wayahudi?”
M. Naye akajibu,
 “Wewe wasema.”
M. Makuhani wakuu walimshtaki mambo mengi. Pilato akamwuliza tena
akisema,
W. “Je, hujibu neno? Sikia mashtaka mazito wanayokushtaki.”
M. Lakini Yesu hakujibu neno lolote, hata Pilato akashangaa. Wakati wa
sikukuu Pilato alizoea kuwafungulia mfungwa mmoja waliyemwomba.
Basi, palikuwa na mtu, jina lake Baraba, aliyekuwamo gerezani pamoja
na waasi wengine waliofanya uuaji katika uasi. Watu wengi walijongea
huko juu, wakaanza kuomba awafanyie kama alivyozoea kila mwaka.
Pilato akawajibu,
W. “Mnataka niwafungulie mfalme wa Wayahudi?”
M. Kwa maana alikuwa ametambua ya kuwa makuhani wakuu walimtoa
kwa husuda. Lakini makuhani wakuu waliwachochea watu wadai
awafungulie Baraba. Pilato akawauliza tena,
W. “Basi, nifanye nini na huyu mnayemwita mfalme wa Wayahudi?”
M. Wakapaza sauti,
W. “Msulibishe!”
M. Pilato akawauliza,
W. “Kwa nini? Amefanya ubaya gani?”
M. Wakazidi kupaza sauti,
W. “Msulibishe!”

9
M. Pilato alitaka kuwaridhisha umati wa watu, basi, akawafungulia
Baraba. Akamtoa Yesu apigwe mijeledi, kisha asulibiwe. Kisha askari
walimpeleka katika behewa ya ndani, ndio ukumbi wa boma,
wakakusanya kikosi kizima. Wakamvika joho lenye rangi ya zambarau,
wakasuka taji la miiba, wakamtia kichwani. Wakaanza kumwamkia,
W. Salamu, mfalme wa Wayahudi!
M. Wakampiga mwanzi kichwani na kumtemea mate. Walimpigia magoti
kwa kumsujudia. Baada ya kumdhihaki, walimvua joho la zambarau,
wakamvika tena mavazi yake. Wakampeleka nje kusudi wamsulibishe.
Wakati ule Simoni wa Kirene, baba wa Aleksanda na Rufusi, alikuwa
akirudi kutoka shambani, akapita huko. Nao wakamshurutisha
achukue msalaba wake. Wakampeleka mahali paitwapo Golgotha,
(yaani, Fuvu la Kichwa). Wakampa divai iliyochanganyika na
manemane. Lakini alikataa kunywa. Wakamsulibisha na wakagawana
mavazi yake kwa kuyapigia kura, yaani ijulikane nani apate nini. Ilikuwa
saa tatu walipomsulibisha. Palikuwa na hati ya maandishi iliyotaja
alichoshtakiwa. Ilisema, “Mfalme wa Wayahudi.” Pamoja naye
waliwasulibisha wanyang'anyi wawili, mmoja kulia kwake na mmoja
kushoto kwake. Watu waliopita njiani walimtukana, wakatikisa vichwa
vyao na kusema,
W. “Aha! Wewe uwezaye kulibomoa hekalu na kulijenga kwa siku tatu,
ujiokoe mwenyewe. Shuka msalabani.”
M. Kadhalika makuhani wakuu pamoja na Waandishi walimdhihaki
wakisemezana,
W. “Aliwaokoa wengine; hawezi kujiokoa mwenyewe. Kristo, Mfalme wa
Israeli, shuka sasa msalabani, tupate kuona na kusadiki.”
M. Hata wale waliosulibiwa pamoja naye walimtukana. Saa sita giza
liliifunika nchi yote mpaka saa tisa. Na saa tisa Yesu alilia kwa sauti
kubwa,
 “Eloi, Eloi, lema sabakthani?”
M. Maana yake,
 “Mungu wangu, Mungu wangu, kwa nini umeniacha?”
M. Baadhi ya wale waliosimama pale na kusikia walisema,

10
W. “Tazama, anamwita Eliya.”
M. Mtu mmoja akaenda haraka, akajaza sifongo siki, akaitia juu ya
mwanzi, akampa anywe akisema,
W. “Acheni, na tuone kama Eliya atakuja kumteremsha.”
M. Lakini kwa mlio mkubwa Yesu alikata roho.

Wote wanakaa kimya kwa muda mfupi.

M. Hapo pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu mpaka chini.
Akida aliyesimama mbele yake, alipoona jinsi alivyokata roho alisema,
W. “Hakika, mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu.”
M. Pale palikuwa na wanawake waliotazama toka mbali. Miongoni mwao
walikuwapo Maria Magdalena, na Maria, mama wa Yakobo mdogo na
Yosefu, na Salome. Hao walikuwa wamezoea kumfuata na kumtumikia
alipokaa Galilaya. Palikuwapo na wanawake wengine wengi
waliopanda pamoja naye kwenda Yerusalemu. Kulipokuchwa siku ile
ya maandalio, ndiyo siku inayotangulia sikukuu, alikuja Yosefu wa
Arimathea, mtu mheshimiwa wa baraza kuu, aliyetazamia mwenyewe
ufalme wa Mungu, akathubutu kumwendea Pilato na kumwomba
mwili wa Yesu. Lakini Pilato aliona shaka kama kweli amekufa.
Akamwita akida, akamwuliza kama amekwisha kufa. Alipopata hakika
kwa akida, alimpa Yosefu maiti. Naye akanunua sanda, akamteremsha,
akamzungushia sanda, akamweka katika kaburi lililochongwa
mwambani. Akavingirisha jiwe mbele ya mlango wa kaburi. Maria
Magdalena na Maria, mama wa Yose, walishuhudia alipowekwa.
M. Injili ya Bwana... Sifa kwako Ee Kristu.

11

You might also like