Download as pdf or txt
Download as pdf or txt
You are on page 1of 14

PITIO LA AGANO LA KALE

KITABU CHA MWANZO

SEHEMU YA PILI (SURA YA 12 - 50)

Mathayo 22:29 “Yesu akajibu, akawaambia, Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa
Mungu.”

Matendo 17.11 “Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno
kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo”

NA: MWL. ANDREW CAPHACE


Namba ya Simu: 0759660363
Barua pepe: andreakitila92@gmail.com

YALIYOMO

1. UTANGULIZI

2. MGAWANYO WA MWANZO SEHEMU YA PILI (SURA YA 12 - 50)


3. IBRAHIMU
4. ISAKA
5. YAKOBO
6. YUSUFU

1
1. UTANGULIZI

Tumekwishaona na kuyapitia matukio makuu manne yanayozungumziwa katika sehemu ya


kwanza ya kitabu hiki cha Mwanzo ambayo ni UUMBAJI, ANGUKO LA MWANADAMU,
GHARIKA Pamoja na MNARA WA BABELI. Hivyo basi sehemu hii ya pili ya kitabu cha
Mwanzo inayoanzia sura ya 12 hadi ya 50 wapo watu wakuu wanne(4) wanaozungumziwa, Watu
hawa ni mababa wa Israeli IBRAHIMU, ISAKA, YAKOBO Pamoja na YUSUFU.
Katika sehemu ya kwanza ya kitabu tumeona matokeo mabaya ya dhambi yaliyoanza kwanza kwa
mtu binafsi (sura ya 3), kisha katika familia (sura ya 4), na hatimaye ikaenea na kuleta madhara
makubwa katika mataifa (sura ya 6 na 11).
Katika sura ya 12 Mungu anaanza rasmi kutekeleza mpango wake wa ukombozi wa mwanadamu
aliouahidi katika Mwanzo 3:15. Anaanza utekelezaji huu kwa kumchagua mtu mmoja
(IBRAHIMU), kutoka kwa mtu huyu inatokea familia iliyochaguliwa ambayo nayo inazalisha
taifa teule la Israeli na hatimaye kutoka kwenye taifa hili anakuja YESU KRISTO mwokozi wa
wanadamu wote.
Kumbuka mambo makuu ya Kitabu cha Mwanzo katika jedwali lifuatalo :-

MWANZO SEHEMU YA I MWANZO SEHEMU YA 2


(SURA YA 1 – 11) (SURA YA 12 – 50)

MUNGU ANASHUGHULIKA NA WATU MUNGU ANASHUGHULIKA NA ISRAELI


WOTE
Matukio Makuu manne (4) Habari za Watu wakuu wane (4)
UUMBAJI IBRAHIMU
ANGUKO LA MWANADAMU ISAKA
GHARIKA YA MAJI YAKOBO
MNARA WA BABELI YUSUFU

Hivyo basi sehemu hii ya pili ya kitabu cha Mwanzo kuanzia sura yake ya 12 hadi ya 50 habari za
watu wakuu wanne (Ibrahimu, Isaka, Yakobo na Yusufu) zinapatikana.

2. MGAWANYIKO WA MWANZO SEHEMU YA PILI (SURA YA 12 - 50)

Ufuatao ni mgawanyo wa sehemu hii ya pili ya kitabu cha mwanzo (sura ya 12 hadi ya 50) :-
I. IBRAHIMU (SURA YA 12 – 25:18)
II. ISAKA (SURA YA 25:19 - 26)
III. YAKOBO (SURA YA 27 – 37:2a)
IV. YUSUFU (SURA YA 37:2b - 50)
2
3. IBRAHIMU (SURA YA 12 – 25:18)

Tunaweza tukayagawa Maisha ya Ibrahimu katika sehemu kuu tatu kama ifuatavyo:-
I. WITO WA IBRAHIMU (SURA YA 12 - 14)

Mwanzo 12:1-3 “1 Bwana akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako,
na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; 2 nami nitakufanya wewe
kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; 3 nami nitawabariki
wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.”
4 Basi Abramu akaenda, kama Bwana alivyomwamuru; Lutu akaenda pamoja naye. Naye
Abramu alikuwa mtu wa miaka sabini na mitano alipotoka Harani.
Hapa tunaona Mungu anajifunua kwa mara ya kwanza kwa Ibrahimu ambapo anaambiwa atoke
katika nchi yake na jamaa zake aende nchi ambayo yeye Mungu atamuonyesha. Agizo hili la
kutoka linaambatana na ahadi zisizo na masharti kwa Ibrahimu.
Kuna mambo ya msingi kujua hapa juu ya ahadi hizi ambazo Mungu alimuahidi Ibrahimu kama
ifuatavyo:-
 Baadhi ya Ahadi ni za kipekee na zinamhusu Ibrahimu binafsi. Mfano wake ni katika
mstari wa 2 “na kukubariki, na kulikuza jina lako;..”

 Ahadi zingine ni za Kitaifa kama vile “2 nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa”

 Mwisho zipo ahadi zinazohusu ulimwengu mzima kama zile zinazotabiri juu ya masihi
kuwa “na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa”

Ibrahimu aliitikia kwa haraka agizo la Mungu la kutoka katika nchi yake ingawa utii wake
haukuwa kamili maana katika kuondoka kwake bado aliwachukua baadhi ya watu wa jamaa zake
na kuondoka nao. Kuondoka na baba yake Tera kulisababsha kusimama kwa safari yake pale
Harani kwa kipindi Fulani mpaka baba yake alipokufa ndipo Ibrahimu akaendelea na safari yake
ya kuelekea nchi ya ahadi( Mwanzo 11:31-32, 12:4, Matendo 7:2-4). Hapa ipo wazi kabisa uwepo
wa baba yake Tera ulimchelewesha kidogo katika safari yake ambapo hakuwa huru kuingia
Kaanani mpaka baada ya kifo cha baba yake. Hii inatuonyesha kuwa utii usiyokamilika ni kikwazo
kwetu katika kutimiza mapenzi ya Mungu. Mwishowe Ibrahimu akaingia Kaanani kama mwaka
wa 2091 K.K
Kulipotukia njaa Kanaani, Ibrahimu akatoka nchi ya ahadi na kusafiri hadi Misri. Akiwa Misri
akadanganya juu ya mkeo Sara kwa kusema kuwa ni dada yake akiogopa kuuawa na mkeo
kuchukuliwa na Mfalme wa Misri. Kwa kitendo hicho cha Ibrahimu mkeo Sara anachukuliwa na
Farao mfalme wa Misri akitaka kumfanya awe mke wake na hapa ikabidi Maingilio ya moja kwa
moja ya Mungu kwa Farao ili kumnusuru Sara na Ibrahimu mwenyewe. Na hapa tunaona kuwa
Mungu aliingilia kati ili kulinda ahadi ambayo alikwisha muahidi Ibrahimu hapo awali. Sara ndiye

3
mwanamke ambaye uzao wa ahadi utatokea kwake sasa achukuliwe awe mke wa Farao nini
kingetokea? Hapa Mungu akaingilia kati ili uzao wake mtakatifu usiharibiwe.
SURA YA 13 (IBRAHIMU NA LUTHU WANATENGANA)
Ibrahimu anaporudi Kanaani tena akitokea Misri anakutana na changamoto nyingine tena, hakuna
nafasi ya kuwatosha mifugo yake Pamoja na ile ya ndugu yake Luthu(sura ya 13). Hivyo
haiwezekana tena hawa wawili kuendelea kukaa Pamoja na hivyo Ibrahimu akampa ndugu yake
Luthu uhuru wa kuchagua eneo analolitaka Kwenda ambapo akachagua Kwenda SODOMA na
kisha akakaa huko Pamoja na mifugo yake.
Tofauti ya Ibrahimu na Luthu ni kwamba Luthu ni mtu anayeishi kwa mtizamo wa Kimwili lakini
Ibrahimu ni mtu wa Imani. Tunaweza kujua mambo yafuatayo juu ya Uchaguzi wa Luthu na
Ibrahimu: -
i. Kipaumbele cha Luthu katika uchaguzi wake ilikuwa kukuza utajiri wake wa mifugo.
Alichagua Sodoma kwa sababu tu ya mwonekano mzuri wa eneo likiwa na malisho mazuri
ya kijani kwa mifugo yake Pamoja na maji ya kutosha. Kipaumbele chake kilikuwa mali.
ii. Kinyume na Luthu, Ibrahimu ni mtu wa Imani ambaye hayatazami mambo kwa mtizamo
wa kimwili tu bali anayapima mambo Kiroho pia kuona kama yapo katika mpango na
mapenzi ya Mungu.

II. AGANO LA IBRAHIMU (SURA YA 15 - 21)

Katika sehemu hii Mungu sasa anathibitisha Ahadi yake kwa Ibrahimu aliyomuahidi katika sura
ya 12. Katika utamaduni wa maeneo yale Maagano baina ya pande mbili yalikuwa yanawekwa
kwa kugawanya vipande vya sadaka iliyochinjwa katika sehemu mbili halafu pande zote mbili
zingepita katikati yake. Kitendo hiki ilikuwa ishara ya kuweka au kutia muhuri Agano baina ya
pande mbili. Namna hii ilikuwa maagano baina ya pande mbili zilizo na hadhi sawa. Agano la
Mungu kwa Ibrahimu halikuwa Agano baina ya pande mbili zinazolingana ndio maana Mungu
akamletea Ibrahimu Usingizi mzito na kisha akapita katikati ya sadaka ile peke yake ikionyesha
kwamba Agano hili lilitegemea asilimia mia moja uaminifu wa Mungu kulitimiza halikutegemea
Ibrahimu. Lingekuwa Agano la masharti linalotegemea uaminifu wa Ibrahimu ndipo litokee
lisingetokea maana bado Ibrahimu mwenyewe Pamoja na wazao wake walikuwa watu wa kukosea
kosea katika vipindi mbalimbali lakini bado Mungu kwa Uaminifu wake alikuja kulitimiza Agano
hili.
Haya yote yanathibitisha kuwa Mungu lazima atimilize Agano hili, na hakuna kitu binadamu
atakifanya kizuie kutimia kwa Agano hili kwa sababu hili ni aina ya Agano lisilo na
masharti(Unconditional Covenant)
Msingi wa Agano hili limejikita katika Uzao Pamoja na Nchi ya ahadi ya Kanaani. Mungu
anaendelea kumwambia Ibrahimu kuwa kutoka katika Uzao wake litakuwa Taifa kubwa vilevile
kuhusu Nchi ya ahadi anataja mpaka mipaka yake itakavyokuwa(15:18).
Baada ya Agano la sura ya 15, sasa sura zinazofuatia hapo zinajikita juu ya ahadi ya uzao ambayo
Mungu alikuwa anaiendea kuitimiza.

4
SURA YA 16 (IBRAHIMU ANAZAA NA HAJIRI MJAKAZI)
Katika Sura ya 16 Ibrahimu anachepuka Imani na kuzaa mtoto kupitia mjakazi aitwaye Hajiri.
Kupatikana kwa mtoto huyu aitwaye Ishmaeli ambaye siye mtoto wa ahadi ndiyo inakuwa chanzo
cha matatizo katika nyumba ya Ibrahimu ikiwa ni matokeo ya kutokutii kwake kwa Mungu.
Katika Sura ya 17 Mungu alijifunua tena kwa Ibrahimu ikiwa kama matokeo ya udhaifu mkubwa
aliouonyesha Ibrahimu wa Kuzaa na Kijakazi. Na ni katika sura hii ndipo jina lake linabadilishwa
kutoka “Abramu” kuwa “Ibrahimu” yaani “Baba wa mataifa”. Mungu kumbadilishia Ibrahimu
jina ni uthibitisho mwingine kwake kuwa yeye ni mwaminifu na atatimiza ahadi yake ya
kuuzidisha uzao wake. Ni katika sehemu hii pia Mungu anampa Ibrahimu atekeleze Tohara kwa
wanaume wote ikiwa ni Ishara ya Agano hilo. Ishara hii ilikusudiwa kuwa kila itakapotekelezwa
inakuwa alama ya kudumu ndani ya mwili ikimkumbusha mtu kuwa yeye ni mtu wa Agano na
Mungu.
Katika sura ya 18 hadi ya 19 hapa tunapata pia Habari za Sodoma na Gomora miji ambayo
Mungu aliiadhibu kwa sababu ya maasi yao yaliyokithiri na kumhifadhi Luthu na binti zake
wawili.
SURA YA 21 (KUZALIWA KWA ISAKA)
Hatimaye ahadi ya Mungu inatimia kwa Ibrahimu kwa kuzaliwa mtoto wa Ahadi aitwaye ISAKA
katika sura ya 21.

III. KUJARIBIWA KWA IMANI YA IBRAHIMU (SURA YA 22 - 25)

SURA YA 22 (IBRAHIMU KUMTOA ISAKA SADAKA)

Ibrahimu aliingia katika mtihani mkubwa sana pale alipoamriwa na Mungu kumtoa mwanae wa
pekee awe sadaka ya kuteketeza. Ni lazima tukumbuke kuwa mpaka kufikia hapa Mungu
amekuwa akimwandaa Ibrahimu katika majaribu mbalimbali huko nyuma ili kuja kukabiri jaribu
hili kubwa. Imani ya Ibrahimu ilikuwa inakua hatua kwa hatua kuelekea ukomavu wa hali ya juu
kama tutakavyoona mwitikio wake kwa Mungu juu ya jaribu kama hili. Lazima tukumbuke kuwa
jaribu la Ibrahimu kumtoa sadaka ya kuteketezwa mwanae wa pekee lilikuwa zito kwa sababu hata
ahadi za Mungu pia kwake zilimlenga mtoto huyo huyo maana Mungu alikwishasema kuwa uzao
wake mteule ungeendelea kupitia ISAKA na si Ishmaeli. Je ingekuwaje tena huyu mtoto atolewe
sadaka ya kuteketezwa?
Waebrania 11:17-19 “Kwa imani Ibrahimu alipojaribiwa, akamtoa Isaka awe dhabihu; na yeye
aliyezipokea hizo ahadi alikuwa akimtoa mwanawe, mzaliwa pekee;18 naam, yeye aliyeambiwa,
Katika Isaka uzao wako utaitwa,19 akihesabu ya kuwa Mungu aweza kumfufua hata kutoka
kuzimu; akampata tena toka huko kwa mfano.”
Kuthibitisha kuwa Ibrahimu safari hii alikuwa amekomaa Kiimani mwandishi wa waebrania
anatuambia kuwa Ibrahimu alimtii Mungu na kuwa tayari kumtoa Isaka sadaka kwani aliamini
kuwa kama Mungu aliahidi kuwa atatimiza ahadi zake kupitia Isaka basi yeye angekuwa na uwezo

5
wa Kumfufua hata kama angekufa ilimradi tu aweze kutimiza ahadi zake ambazo si za uongo.
Ukomavu huu wa Kiimani kwa Ibrahimu ndiyo ukasababisha Mungu atoa mbadala wa sadaka,
badala ya Isaka akatoa sadaka ya mnyama.

SURA YA 23 (KIFO CHA SARA)


Katika sura ya 23 tunaona kifo cha Sara ambapo kinasababisha Ibrahimu kununua shamba la
kuzikia. Katika hili ikumbukwe kuwa Ibrahimu anapatana na wenyeji na kununua eneo la kuzikia
kwa sababu ardhi bado ni ya ahadi tu haijawa yake.

SURA YA 24 (ISAKA ANAPATIWA MKE, REBEKA)


Katika sura ya 24 Ibrahimu anawapisha mtumishi wake aende kwa Nahori ndugu yake ili amtafutie
Isaka mke. Habari hizi zinaonyesha kuwa Ibrahimu alikuwa makini kulinda uzao wa ahadi ili
usichafuliwe na mataifa mengine ndio maana anamtuma mtumishi akamtwalie Isaka mwanae mke
kutoka kwa watu wa jamaa zake.

SURA YA 25 (KIFO CHA IBRAHIMU)


Katika sura ya 25 tunaona historia ya Ibrahimu inafikia tamati kwa maelezo ya kuoa kwake mke
mwingine aitwaye Ketura na baadae kifo chake na kuzikwa kwake na kisha sura hii inamalizia na
kutaja wazao wa Ishmaeli (25:12-18).

4. ISAKA (SURA YA 25:19 - 26)

Zifuatazo ni sehemu zinazopatikana katika sura hizi zinazoelezea kuhusu maisha ya Isaka:-

I. ISAKA NA KUZALIWA KWA WATOTO WAKE ESAU NA YAKOBO (SURA YA


25)
Kabla hawajazaliwa watoto wawili wa Isaka (Yakobo na Esau), Mungu alitoa ahadi kwa Rebeka
kuwa mataifa mawili yamo tumboni mwake na vilevile mkubwa angekuja kumtumikia
mdogo.(25:23). Utaratibu wa kawaida ulikuwa mzaliwa wa kwanza wa kiume ndiye aliyekuwa
mrithi wa babaye na si vinginevyo ndio maana baada ya Neno hili kutabiriwa na Bwana,
inaonekana Isaka hakulitilia maanani maana kwa desturi alijua kuwa Esau ndiye angekuwa
mrithi.Kadri watoto hawa walivyoendelea kukua tabia zao tofauti ziliendelea kudhihirika. Yakobo
aliyekuwa mtu wa kiroho akawa kipenzi cha mama yake Rebeka na Esau aliyekuwa mtu wa
kimwili zaidi akawa kipenzi cha baba yake Isaka. Upendeleo huu ndani ya familia ya Isaka ukaleta
mgawanyiko mbaya na hili ni fundisho kwetu wa leo kuwa wazazi wanapaswa kuwapenda watoto
wao wote bila upendeleo.

Tabia ya Esau ya kupuuzia mambo ya Kiroho inaonekana wazi katika kitendo chake cha kuuza haki
yake ya mzaliwa wa kwanza kwa kupewa chakula tu na Yakobo (25:27-34). Mungu alijua tabia za
watoto hawa zitakavyokuwa hata kabla ya kuzaliwa kwao ndio maana alimchagua Yakobo kuwa
mrithi wa ahadi za Ibrahimu badala ya Kaka yake Esau. Esau anatoa mfano wa mtu au mkristo
ambaye kipaumbele chake kipo kwenye mambo ya kimwili zaidi ya yale ya kiroho.

6
Tunapaswa tujue hapa kuwa kila mtu ambaye Mungu alimchagua kuwa mrithi na kuendeleza uzao
wa Kimasihi alikabiliana na mtu mwingine wa upande wa pili ambaye alikuwa tofauti naye (akiwa
mtu wa mambo ya kimwili zaidi). Mfano wa watu wa kiroho waliochaguliwa na Mungu pamoja na
watu wasio wa kiroho waliokuwa tofauti nao ni kama inavyoonyeshwa katika jedwali lifuatalo:-

UZAO MTEULE UZAO USIYOCHAGULIWA


(WATU WA IMANI) (WATU WAKIMWILI)
IBRAHIMU LUTHU
ISAKA ISHMAELI
YAKOBO ESAU

Tunaona mwandishi wa kitabu hiki cha Mwanzo katika masimulizi yake yamejikita zaidi katika
uzao mteule na kuacha au kutoa nafasi ndogo sana juu ya uzao usio mteule. Tukianza na Ibrahimu
katika wazao wake (Isaka NA Ishmaeli), Isaka anachukuliwa na Ishmaeli anaachwa. Ukija kwa
wazao wa Isaka (Yakobo na Esau), Yakobo pekee anachaguliwa na Esau anaachwa. Vilevile
tunapoendelea kukichunguza kitabu hiki cha Mwanzo tutaona ni katika Yakobo tu ambapo wazao
wake wote watachaguliwa kuunda taifa teule (Israeli).

II. ISAKA MIONGONI MWA WAFILISTI (SURA YA 26)

Katika sura hii ya 26 tunaona namna matatizo ya baba yanavyojitokeza kwa mtoto. Isaka kwa
sababu ya njaa akiwa miongoni mwa Wafilisti anamdanganya Abimeleki mfalme wa Wafilisti
huko Gerari kuwa Rebeka siyo mke wake bali ni dada yake akihofia kuuawa maana nyakati zile
wafalme wengi walikuwa na tabia wakiona mke mzuri machoni pao wanamuua mme wake na
kisha kumchukua. Katika sura ya 12 ya kitabu hiki cha Mwanzo, Ibrahimu alifanya kosa hili hili.
Isaka anajikuta katika hali ya kukemewa vikali na mfalme huyu asiyemcha Mungu baada ya
Mfalme kutambua kuwa Rebeka ni mke wake na si dada yake kama alivyodai yeye.

Nusu inayofuata ya Sura hii ya 26 ni tukio la ugomvi juu ya visima kati ya wachungaji wa Isaka na
wachungaji wa Gerari (wenyeji wa eneo lile). Matatizo haya mawili (jaribio la mke wa Isaka
kuchukuliwa na mfalme pamoja na kugombania visima katika nchi) yamejikita juu ya kiini cha
ahadi aliyoahidiwa Ibrahimu na Mungu juu ya “Uzao” pamoja na “Nchi ya Ahadi”. Tatizo la
kwanza linalohusu jaribio la Rebeka kuchukuliwa awe mke wa mfalme wa wafilisti linaashiria
uzao wa ahadi ukiwa katika hatari ya kuharibiwa na tatizo la pili la kugombania visima linahusu
Ardhi/Nchi ya ahadi.

7
MFANANO ULIOPO KATI YA MAISHA YA ISAKA NA YESU

Ingawa katika Agano Jipya Isaka hatajwi kama mfano wa Yesu, ila ukichunguza maisha yao kuna
mfanano kama ifuatavyo hapa chini:-

i. Kuzaliwa kwao kimuujiza.

Wote Isaka pamoja na Yesu walizaliwa kimuujiza. Isaka alizaliwa wakati Ibrahimu na Sara
wakiwa wazee sana(Isaka akiwa na miaka 100 na Sara miaka 90). Kwa hali ya kawaida
hakuna binadamu mwenye uwezo wa kuzaa akiwa na umri huu. Yesu naye alizaliwa na
Bikira jambo lisilowezekana katika hali ya kawaida.

ii. Wote wanatajwa kama “watoto wa pekee”

Katika waebrania 11:17 Isaka anatajwa kama “mtoto wa pekee” kwa Ibrahimu, Yesu pia
maeneo mengi katika maandiko anatajwa kama “mwana pekee” kwa Mungu.

iii. Utii wao wa kukubali kifo cha sadaka.

Katika sura ya 22 ya kitabu hiki cha Mwanzo, tunamwona Isaka yupo tayari kabisa
anapotolewa kama sadaka ya kuchinjwa na baba yake na ndivyo ilivyo upande wa Yesu
alikuwa mtii kwa Baba yake hata mauti ya msalaba (Wafilipi 2:8)

5. YAKOBO (SURA YA 27 – 37:2a)

Tunaweza tukayagawa maisha ya Yakobo katika vipindi vikuu vitatu(3) kama ifuatavyo:-

I. Yakobo akiwa nyumbani - Kanaani (sura ya 27)


II. Yakobo akiwa Mbali na Nyumbani/Nje ya Kanaani (sura ya 28 - 32) na
III. Yakobo akiwa Nyumbani tena – Kanaani (sura ya 33 - 36)

I. YAKOBO AKIWA NYUMBANI – KANAANI (SURA YA 27)

Katika sura ya 25 ya kitabu hiki cha Mwanzo tuliona kuwa Yakobo tayari alikwisha nunua haki
ya mzaliwa wa kwanza kutoka kwa kaka yake Esau (25:31-34), kifuatacho ni namna ambayo
Yakobo atazipokea baraka za mzaliwa wa kwanza kutoka kwa baba yake Isaka. Yakobo
alitumia njia ya udanganyifu akishirikiana na mama yake Rebeka katika kupokea baraka hizo za
mzaliwa wa kwanza kutoka kwa Isaka baba yake. Ingawa njia iliyotumika haikuwa sawa,
Yakobo akapata baraka hizo kutoka kwa baba yake Isaka na wakati huo Isaka baba yake
alidhani anambariki Esau. Katika tukio hili tunapata mfano wa mtu anayetaka kufanikisha
jambo jema ila kwa kutumia njia isiyo sahihi. Hapa ifahamike kuwa Mungu tayari alikwisha
sema kuwa atakayekuwa mrithi wa Isaka ni Yakobo na si Esau hata kabla hawajazaliwa, hivyo
kama Yakobo na Rebeka mama yake wangesubiri wakati wa Mungu, Mungu lazima alikuwa na
mpango mzuri usio na makosa wa kutimiliza ahadi hiyo na Yakobo angepokea baraka hizo bila
shida. Kwa sababu ya kutokumwamini Mungu na Kungoja utimilifu wa ahadi zake, Yakobo

8
pamoja na mama yake Rebeka wakaona njia pekee ya kupokea ahadi hiyo ni kufanya
udanganyifu walioufanya. Matokeo yake udanganyifu ule ulimgharimu Yakobo karibu maisha
yake yote. Kwanza ilimlazimu kuondoka nyumbani(Kanaani) kwa hofu ya kumkimbia ndugu
yake Esau aliyeapa kumuua ili kulipa kisasi.

Hivyo sisi wa leo tunapaswa kujiepusha kabisa kutafuta mafanikio kwa njia zisizo sahihi.
Mungu amekwisha tuahidi mafanikio yote ya Kiroho na Kimwili, hivyo tungoje wakati wa
Mungu mafanikio haya yatakuja tu na cha msingi ni kuendelea kutekeleza kile tunachopaswa
kukifanya upande wetu ili tupate haya mafanikio tunayoyatafuta na kisha kumwachia Mungu
afanye upande wake.

II. YAKOBO AKIWA HARANI MBALI NA NYUMBANI/ NJE YA KANAANI. (SURA


YA 28 - 32)

Sura hizi zinazoelezea maisha ya Yakobo akiwa nje ya Kanaani tunaweza kuzigawa kama
ifuatavyo:-

SURA YA 28 SURA YA 29 - 31 SURA YA 32


 Yakobo akimkimbia  Yakobo  Yakobo yupo
Esau kwa hofu ya akiwa mbali njiani kurudi
kuuawa na nyumbani nyumbani ila
 Maono ya Yakobo – akimtumikia bado ana hofu
huko BETHELI Labani huko juu ya Esau
Harani  Anakutana na
Mungu huko
PENUELI

Wakati Yakobo akiwa katika safari ya kumkimbia Esau ndugu yake na wakati akiwa anarudi
Kanaani baada ya miaka mingi alikutana na Mungu katika maeneo na vipindi mbalimbali. Kwanza
anapotoka nyumbani akiwa na hofu kuu ya kuuawa na ndugu yake Esau anapofika Betheli
anakutana na Mungu katika maono ya ngazi ndefu iliyofika mpaka mbinguni. Mara nyingine
ingawa siyo ya mwisho alikutana na Mungu Penueli wakati anarudi nyumbani na safari hii ndipo
aliposhindana na Mungu aking’ang’ania baraka na ndipo alibadilishiwa jina kutoka Yakobo kuwa
Israeli. Kipindi kinachotenganisha matukio haya mawili ya Yakobo kukutana na Mungu ni kipindi
kirefu cha miaka aliyotumika katika familia ya Labani akiwa nje ya Kanaani huko Harani.

Maono ya Yakobo huko Betheli (sura ya 28)

Pale Betheli katika sura ya 28 ya kitabu hiki cha Mwanzo, Yakobo aliona maono ya Ngazi ndefu
iliyofika mpaka mbinguni na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka. Katika maono haya
Mungu alimfunulia Yakobo pamoja na sisi wa leo mambo makuu mawili kama ifuatavyo:-

i. Kuna njia ya kumwendea Mungu.

Ngazi aliyoiona Yakobo iliashiria kuwa ahadi ya baraka aliyoahidiwa Ibrahimu na wazao
wake ingeleta matokeo ya kuwepo kwa mawasiliano kati ya Mungu na wanadamu ambayo
9
yalikatika kwa sababu ya dhambi. Katika Agano Jipya tunaona Yesu kristo ndiye ngazi
hiyo ambaye yeye ndiye njia pekee ya kwenda mbinguni. (Yohana 1:51)

ii. Uwepo wa ulinzi wa Mungu kwa watu wake.

Yakobo alikuwa anamkimbia Esau ndugu yake akiwa na hofu kuwa siku moja atauawa na
huyo ndugu yake aliyekuwa ameapa kumuua. Maono haya ya malaika wa Mungu
yanamthibitishia Yakobo kuwa lipo jeshi kubwa la kiroho lisiloonekana kwa macho ya
nyama linalomlinda siku zote katika safari ya maisha yake hata yote aliyoahidiwa yatimie.
Hili ni fundisho kwetu sisi pia wa leo kuwa katika maisha yetu yote ya kiroho na ya
kimwili lipo jeshi kubwa mno la kiroho ambalo linatulinda dhidi ya maadui usiku na
mchana (Zab 34:7)

Yakobo akiwa Harani akitumika katika familia ya Labani (sura ya 29 -31)

Harani ilikuwa mahali ambapo Rebeka, mama yao na Yakobo na Esau alilelewa na ndipo mahali
Ibrahimu babu yake na Yakobo alikuwa amehamia miaka kadhaa huko nyuma. Labani alikuwa
kaka yake na Rebeka na hivyo mjomba wake Yakobo. Yakobo alikaa kwa mjomba wake Labani
huko Harani akimtumikia kwa kipindi cha miaka ishirini(20). Hii ilikuwa miaka ya shida na
magumu mengi katika maisha ya Yakobo. Yakobo alimtumikia Labani kwa kipindi cha miaka
saba(7) ili ampate mke aliyempenda aitwaye Raheli lakini baada ya utumishi huo Labani
alimfanyia udanganyifu akampa mke mwingine aitwaye Lea ambaye Yakobo hakumpenda. Haya
yaweza kuwa malipo pia kwa Yakobo kwa udanganyifu alioufanya katika kujipatia baraka za
mzaliwa wa kwanza. Hapa tunaona Yakobo anaanza kuvuna kile alichokipanda. Ikabidi Yakobo
atumike tena miaka mingine saba(7) ili ampate mke aliyempenda(Raheli). Jumla ikawa miaka
kumi na nne(14). Baadae akaja akatumika miaka sita(6) ili apate mifugo na hivyo inaleta jumla ya
miaka ishirini(20) ya utumishi wa Yakobo akiwa nje ya Kanaani.

Familia ya Yakobo

Yakobo alikuwa na wake wawili pamoja na vijakazi wa wake zake nao wawili. Kupitia kwa hawa
wake wawili na vijakazi wawili Yakobo akazaa watoto wa kiume kumi na mbili(12) kama
ifuatavyo:-

 Watoto wa LEA - Reubeni, Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari na Zabuloni (watoto 6)

 Watoto wa RAHELI – Yusufu na Benjamini (watoto 2)

 Watoto wa Zilpa (kijakazi wa LEA) - Gadi na Asheri (watoto 2)

 Watoto wa Bilha (kijakazi wa RAHELI) - Dani na Naftali (watoto 2)

Kupitia familia hii Mungu akaanzisha makabila kumi na mbili(12) ambayo yakawa chanzo cha
Taifa teule la Israeli alilolichagua kulitumia kumleta mwokozi wa ulimwengu wote, YESU
KRISTO.

Kurudi kwa Yakobo Kanaani na Kukutana na Mungu huko Penueli (sura ya 32)

10
Yakobo alikuwa ugenini nje ya Kanaani kwa kipindi cha miaka ishirini(20). Wakati huo alienda
ugenini mikono mitupu na sasa anarudi nyumbani Kanaani akiwa tajiri mwenye mifugo mingi
pamoja na familia kubwa. Mungu aliitunza ahadi yake kwa Yakobo (28:15).

Katika kurudi kwake, Malaika wa Mungu wanamkaribisha Yakobo (32:1), kama walivyomtakia
heri wakati wa kuondoka kwake (28:12). Wakati huu Yakobo alikuwa anaingia katika Urithi wake
wa nchi ya Ahadi(Kanaani). Wakati Yakobo akiwa katika safari yake ya kurudi nyumbani
anakumbuka kuwa Esau ndugu yake aliapa kuwa atamuua miaka kadhaa iliyopita (27:41)
kutokana na namna Yakobo alivyofanya udanganyifu katika kupata baraka za mzaliwa wa
kwanza. Yakobo kwa hofu kuu ikabidi atume wajumbe watangulie kwenda kwa Esau wakiwa na
zawadi nyingi ili ikibidi ndugu yake aweze kumsamehe na kutokulipiza kisasi. Yakobo hakuishia
kupeleka zawadi tu kwa Esau bali aliamua kumwomba Mungu ulinzi juu yake dhidi ya ndugu
yake. Wajumbe aliowatuma kwenda kwa Esau walirudi na ujumbe kuwa Esau mwenyewe alikuwa
anakuja kumlaki Yakobo. Yakobo aliposikia habari hizi alizidi kuogopa zaidi na akaona
anamuhitaji Mungu zaidi kuliko wakati mwingine wowote katika maisha yake(32:24-30).

Usiku ule Mungu akamtokea Yakobo katika umbo la binadamu. Yakobo akamng’ang’ania Mungu
mpaka alipobarikiwa na kisha jina lake likawa Israeli badaka ya Yakobo.

Baada ya Yakobo kukutana na Mungu usiku ule, alimwona Esau akija na watu wake na haraka
kwa msaada wa Mungu akatambua kuwa Esau alikuja kwa amani. Kukutana kwao kulikuwa kwa
amani na mapatano. Baada ya hapo wakaachana kwa amani na kisha Yakobo akaingia Kanaani.

III. YAKOBO AKIWA NYUMBANI TENA – KANAANI (SURA YA 33-36)

Kisasi cha Simeoni na Lawi kwa Washekemu juu ya Umbu lao Dina kunajisiwa (sura ya 34)

Katika kurudi kwake Yakobo katika nchi ya Kanaani, shekemu ilikuwa kituo cha kwanza
kusimama. Pale alinunua eneo na kusimamisha madhabahu ya Mungu. Hapa inaonekana kama
Yakobo alikusudia eneo hili liwe makao yake kwa muda. Lakini mauaji ya Simeoni na Lawi
watoto wake kwa wenyeji(wanaume wa shekemu) ambayo yalikuwa malipo ya kisasi baada umbu
lao Dina kunajisiwa na mtoto wa mkuu wa nchi ile ya Shekemu, yalimfanya Yakobo ashindwe
kuendelea kuishi pale na hivyo akaondoka na kwenda Betheli.

Mungu anafanya Upya Agano pale Betheli (sura ya 35)

Betheli ndiyo mahali ambapo miaka ishirini iliyopita Yakobo aliona maono ya Ngazi ifikayo hadi
mbinguni wakati huo akimkimbia Esau. Katika maono yale Mungu alimjulisha kuwa yeye ndiye
mrithi wa ahadi za Ibrahimu na Isaka. Safari hii Mungu anapolifanya upya agano lake
anamthibitishia Yakobo kuwa ahadi hizo zitatimizwa.

Baadae kutokea Betheli, Yakobo akaenda Hebroni, nyumbani kwa Ibrahimu na Isaka. Baada ya
kurudi kwake Yakobo katika nchi ya Kanaani ilipita muda fulani baba yake Isaka akafa akiwa na

11
umri wa miaka 180. Baada ya kifo cha Isaka wote wawili (Yakobo pamoja na Esau) wakamzika
baba yao katika kaburi la familia.

Vizazi vya Esau (sura ya 36)

Sehemu hii inayosimulia habari za Yakobo inamalizikia katika sura ya 36 ambayo inaelezea kwa
ufupi sana vizazi vya Esau na kuonyesha kuwa asili au chimbuko la Waedomu ni Esau. Hivyo
Waedomu walitokana na uzao wa Esau. Waamaleki pia walikuwa tawi la uzao uliotokana na Esau
na hawa ndio walikuja kuwa maadui wakuu wa waisraeli hapo baadae.

6. YUSUFU (SURA YA 37:2b – 50:26)

Mwanzo 37:2-3 “2 Hivi ndivyo vizazi vya Yakobo. Yusufu, aliyekuwa mwenye miaka kumi na
saba, alikuwa akichunga kondoo pamoja na ndugu zake; naye alikuwa kijana pamoja na wana
wa Bilha, na wana wa Zilpa, wake wa baba yake. Yusufu akamletea baba yao habari zao
mbaya. 3 Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake,
akamfanyia kanzu ndefu.”

Kuanzia sura ya 37 hadi ya 50 ya kitabu hiki cha Mwanzo, masimulizi makuu ni juu ya maisha ya
Yusufu mtoto wa Yakobo. Pamoja na kwamba uzao wa Kimasihi hautokani na Yusufu, bado
maisha ya Yusufu yana umuhimu na uzito mkubwa sana kwa sababu yanaonyesha jinsi Mungu
alivyotumia ubaya wa wanadamu huko Misri kulihifadhi taifa lake teule. Hivyo kuwepo kwa
habari za Yusufu zinatusaidia kujua ilikuwaje mpaka taifa la Israeli likaingia Misri. Kadri miaka
ilivyokuwa inaenda, desturi mbovu za kikanaani zilianza kuiathiri familia ya Yakobo ambayo
ilikuwa inaishi Kanaani kwa wakati huo. Hivyo kupitia Yusufu, Mungu anaruhusu kuwahamisha
watu wake waende Misri ili kuutunza uzao wake mteule usiharibiwe na desturi mbovu za
Kikanaani na vile vile akatumie mazingira ya Misri kuiongeza familia ya Yakobo iwe taifa kubwa
ndipo alilete kuja kurithi nchi ya Ahadi (Kanaani).

Maisha ya Yusufu tunaweza tukayagawa katika vipindi vikuu vitatu(3) kama ifuatavyo:-

I. Yusufu kuuzwa utumwani Misri (Sura ya 37 - 38)


II. Yusufu Kutupwa Gerezani Misri (Sura ya 39 - 41)
III. Yusufu Anawaokoa ndugu zake (Sura ya 42 - 50)

SURA YA 37 - 38 SURA YA 39 - SURA YA 42 - 50


41
YUSUFU YUSUFU YUSUFU
KUUZWA KUTESEKA ANAWAOKOA
UTUMWANI GEREZANI NDUGU ZAKE

I. YUSUFU KUUZWA UTUMWANI MISRI (SURA YA 37 - 38)

Hali ya Yakobo ya upendeleo juu ya watoto inaonekana pale ambapo tunasoma kuwa “Basi Israeli
12
akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu
ndefu.””(Mwanzo 37:3). Vazi hili la Yusufu lilionyesha ishara kwa Yusufu kuwa kiongozi dhidi
ya ndugu zake wote. Jambo hili pamoja na ndoto za kinabii alizoota Yusufu na kuwasimulia ndugu
zake zilisababisha achukiwe na ndugu zake na kisha kuuzwa kama mtumwa huko Misri.

Wana wa Yuda (sura ya 38)

Masimulizi ya Yuda katika Sura hii ya 38 ya kitabu cha Mwanzo yanaingizwa kwa sababu kupitia
uzao wa Yuda masihi atatokea.

Masimulizi ya uzao wa Yuda katika sura hii yamekusudiwa kuonyesha chimbuko la ukoo wa
mfalme Daudi na kisha ukoo wa YESU KRISTO. Dhambi ya Yuda na mkwe wake Tamari
inaonyesha kwa nini ilikuwa muhimu kwa familia ya Yakobo kupelekwa Misri kwanza maana
mmomonyoko wa maadili wa wakanaani uliingia ikawa mfumo wa maisha wa kawaida hata kwa
waisraeli pia.

II. YUSUFU KUTUPWA GEREZANI MISRI (SURA YA 39 - 41)

Katika sura hizi tunamwona Yusufu akiwa mtu mwenye tabia njema isiyo na hatia. Yusufu
anaonekana pia kuwa mtu mwenye kipawa cha Uongozi maana kila mahali anapoenda anakuwa
msimamizi wa wenzake. Vile vile mapungufu na udhaifu mkubwa ulioonekana kwa Ibrahimu,
Isaka na Yakobo ukija kwa Yusufu hauonekani kabisa. Yusufu anaonyesha kuwa mtu ambaye
Imani yake imekomaa kama inavyodhihirishwa na kushinda majaribu yote bila kutenda dhambi.
Yusufu anajikuta katika mazingira ya dhambi ya Uasherati anaishinda, Kisha anatupwa gerezani
kwa mashitaka ya uongo na bado anashinda jaribu hilo.

Kitendo cha Yusufu kuonyesha uaminifu wa hali ya juu mbele za Mungu bila kujali yupo kwenye
mazingira gani kunamfanya Mungu amwinue na kumfanya kuwa mtu mkuu ndani ya Misri.(sura
ya 41)

III. YUSUFU ANAWAOKOA NDUGU ZAKE (SURA YA 42 - 50)

Masimulizi katika sura hizi yanaonyesha safari mbili za ndugu zake Yusufu kwenda Misri. Hii
ilisababisha familia nzima ya Yakobo kuhamia Misri na kuishi eneo lililoitwa Gosheni.

Mungu alikuwa amepanga kuwa taifa la Israeli litatunzwa na kukua likiwa Misri. Yakobo
alipoondoka Kanaani kwenda Misri na familia yake, Mungu alimhakikishia kuwa wazao wake
wangerudi kuja kukaa katika nchi ya Ahadi ya Kanaani(46:3-4).

Yakobo anawabariki na kuwatabiria watoto wake (sura ya 49)

Yakobo karibu na kufa kwake aliwaita wanawe ili awabariki pamoja na kuwapasha habari juu ya
mambo yatakayotokea siku za mwisho.

Mwanzo 49:8-10 “8 Yuda, ndugu zako watakusifu, Mkono wako utakuwa shingoni mwa adui
zako. Wana wa baba yako watakuinamia. 9 Yuda ni mwana-simba, Kutoka katika mawindo,

13
mwanangu, umepanda; Aliinama akajilaza kama simba, Na kama simba mke; ni nani atakaye
mwamsha? 10 Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, Wala mfanya sheria kati ya miguu
yake, Hata atakapokuja Yeye, mwenye milki, Ambaye mataifa watamtii.”

Yakobo katika kuwabariki watoto wake tunaona kuwa Yuda anapewa baraka za kipekee
zinazoonyesha kuwa yeye ndiye mrithi na mwendelezaji wa uzao mteule utakaomleta masihi na
mwokozi wa ulimwengu wote(Yesu Kristo). Kabila la Yuda ndilo alikotoka mfalme Daudi na
kisha kutoka ukoo wa Daudi ukamleta Yesu Kristo, na hii ndiyo maana huwa tunasema kuwa
Yesu ni Simba wa kabila la Yuda kwa sababu Yesu ametokea katika kabila la Yuda.

Kifo cha Yakobo na Yusufu (sura ya 50)

Baada ya Yakobo kumaliza hotuba yake ya kuwabariki watoto wake alifariki. Watoto wake
wakauchukua mwili wake na kwenda kuuzika ndani ya Kanaani katika Hebroni.

Yusufu pia akawaapisha wana wa Israeli kuwa siku watakaporudi katika nchi ya ahadi(Kanaani)
waichukue pamoja na mifupa yake. Imani kuwa Kanaani itakuwa makao ya kudumu ya wazao
wao haikusahaulika kabisa miongoni mwa mababa hawa wa Israeli. Miaka 400 baadae walipotoka
katika nchi ya Misri kwenda nchi ya ahadi (Kanaani) waisraeli waliibeba na mifupa ya Yusufu
kama alivyokuwa amewaagiza (Kutoka 13:19)

HITIMISHO LA KITABU CHA MWANZO

Kitabu cha Mwanzo kinaishia na kifo cha Yakobo na Yusufu. Tumesafiri na kitabu hiki toka
bustani ya Edeni mpaka Misri. Kitabu kilichoanza na uhai kinaishia na kifo/mauti. Katika sehemu
ya pili ya kitabu hiki cha Mwanzo (sura ya 12 - 50) tumeona kuwa ahadi za Mungu zisizo na
masharti haziwezi kuzuiwa na mtu yeyote. Kuanzia mwanadamu na hata upinzani wa shetani
hauwezi kubadilisha mpango wa Mungu juu ya maisha yetu. Mungu katika ukuu na uaminifu
wake hutunza na kutimiza ahadi zake zote alizoziahidi kwetu.

MUNGU AKUBARIKI SANA KWA KUPITIA PAMOJA NAMI KITABU HIKI CHOTE CHA MWANZO

Ni mimi ndugu yako:

Andrew Caphace

Mwalimu wa Neno la Mungu.

14

You might also like