Download as pdf or txt
Download as pdf or txt
You are on page 1of 3

5 MEI 2024

DOMINIKA YA SITA
YA PA SA KA
MWAKA B

SOMO LA KWANZA Matendo ya Mitume 10:25-26, 34-35, 44-48

Somo katika kitabu cha Matendo ya Mitume.


Petro alipokaribia nyumba, Korneli alitoka amlaki, akamwangukia miguuni
akamwabudu. Petro akamwinua, akasema, “Simama. Mimi ni mwanadamu
tu.” Petro akafumbua kinywa, akasema, “Hakika, sasa nimeng'amua ya
kuwa Mungu hana ubaguzi. Bali, katika kila taifa, mtu yeyote mwenye
kumcha yeye na kutenda yaliyo haki hukubaliwa naye.” Petro alipokuwa
bado katika kusema hayo, Roho Mtakatifu aliwashukia wote waliolisikia lile
neno. Wale Wayahudi waamini waliokuja pamoja na Petro walishangaa
kwa sababu Watu wa Mataifa pia wamemiminiwa kipaji cha Roho
Mtakatifu, kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha na kumtukuza
Mungu. Hapo Petro akasema, “Awezaje mtu kuwanyima ubatizo wa maji
hawa waliompokea Roho Mtakatifu sawa na sisi?” Akaamuru wabatizwe
kwa jina la Yesu Kristo. Kisha wakamwomba akae kwao siku chache.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.
ZABURI YA KUITIKIZANA Zaburi 98
K. Bwana ameufunua wokovu wake
mbele ya macho ya mataifa.
au: Aleluya.
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
kwa maana amefanya mambo ya ajabu.
Mkono wake wa kuume, na mkono wake mtakatifu,
umemletea ushindi. K.

Bwana ameujulisha ushindi wake;


mbele ya macho ya mataifa ameifunua haki yake.
Amekumbuka wema na uaminifu wake
kwa nyumba ya Israeli. K.

Miisho yote ya dunia imeuona


wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote;
pigeni kelele za furaha; imbeni zaburi. K.

SOMO LA PILI 1 Yohane 4:7-10

Somo katika barua ya kwanza ya Mtakatifu Yohane.


Wapendwa, tupendane, kwa kuwa upendo watoka kwa Mungu. Na kila
apendaye amezaliwa na Mungu na anamjua Mungu. Asiyependa, hamjui
Mungu, kwa maana Mungu ni upendo. Upendo wa Mungu umeonekana
kwetu namna hii: Mungu amemtuma Mwana wake mzaliwa wa pekee
afike ulimwenguni tuupate uzima kwa yeye. Huu ndio upendo: si kwamba
sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma
Mwana wake awe malipizi ya dhambi zetu.
Neno la Bwana... Tumshukuru Mungu.

2
SHANGILIO LA INJILI
K. Aleluya.
W. Aleluya.
K. Mtu akinipenda, atalishika neno langu,
asema Bwana;
na Baba yangu atampenda,
nasi tutakuja kwake na kufanya makao kwake.
W. Aleluya.

INJILI Yohane 15:9-17

Somo la Injili takatifu ilivyoandikwa na Yohane.


Wakati ule: Yesu aliwaambia wafuasi wake, “Kama Baba alivyonipenda
mimi, vile nami nimewapenda ninyi. Dumuni katika pendo langu. Mkishika
amri zangu, mtadumu katika pendo langu, kama nami nilivyozishika amri
za Baba yangu na kudumu katika pendo lake. Hayo nimewaambia, ili furaha
yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu iwe kamili. Hii ndiyo amri yangu:
mpendane, kama mimi nilivyowapenda. Hakuna upendo kupita upendo wa
mtu atoaye nafsi yake kwa ajili ya rafiki zake. Ninyi mu rafiki zangu,
mkitenda ninayowaamuru. Siwaiti tena watumishi, kwa sababu mtumishi
hajui atendalo bwana wake. Nawaita rafiki, kwa kuwa nimewajulisha yote
niliyoyasikia kwa Baba yangu. Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi
niliyewachagua ninyi, kusudi mwende mkazae matunda, na matunda yenu
yadumu, ili Baba awapeni lolote mwombalo kwa jina langu. Haya
nawaamuru ninyi: mpendane ninyi kwa ninyi.”
Injili ya Bwana... Sifa kwako Ee Kristu.

You might also like