Juma La Maombi La Kabla Ya Mavuno: Idara Ya Huduma Za Familia Za Kiadventista

You might also like

Download as pdf or txt
Download as pdf or txt
You are on page 1of 22

Idara ya Huduma za Familia

za Kiadventista

JUMA LA MAOMBI LA KABLA YA


MAVUNO

“Na katika wewe Familia zote Duniani


Zitabarikiwa”

Machi 24 – 30, 2024

Pr. Dr. John Kamiza

1
Yaliyomo
Siku ya Kwanza
Kuwiwa Kusema …………………………………………...............03

Siku ya Pili
Mungu Humwezesha Amwitaye……………………………….....05

Siku ya Tatu
IBADA YA FAMILIA ILETAYO MABADILIKO………............08
Fungu Kuu: Ufunuo 14:6-7

Siku ya Nne
Kukuza Vikundi Vidogo…………………………………...............11

Siku ya Tano
Kuzingatia Uhusiano Uliopo na Watu Wasikivu…………….....14

Siku ya Sita
AHADI ZA UONGOAJI WA ROHO: Kuleta Mapinduzi
katika Uinjilisti……....................................................................17

Siku ya Saba
Kuitwa na Mungu ili Kuwaimarisha Wengine……………….....20

2
Siku ya Kwanza
Unawiwa Kusema
“Yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha
ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia
ndani yetu neno la upatinisho” (2 Wakorintho 5:19).
Andiko hili linaufanya uinjilisti kuwa jambo la lazima kwa
yeyote aliyekubali huduma ya upatanisho. Ni mwitikio wa mara
moja wa neema ya Mungu. Linathibitisha umuhimu wa uinjilisti
na kuuweka kama jambo la lazima kama Paulo asemavyo—
“Maana, ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; tena ole wangu
nisipoihubiri Injili” (1 Wakorintho 9:16).
Aya hii inasisitiza mabadiliko ambayo upatanisho huu
unafanya kwa ajili yetu sisi tunaoamini. Kama Paulo, mwandishi
aliyevuviwa wa fungu hili, yeye mwenyewe alikuwa katika
uhasama wa wazi na Kristo katika wakati wa kutokujua, mtesaji
wa Kanisa la Yesu Kristo. Alipopokea upatanisho, alibadilika na
kuwa mfuasi hodari wa Kristo na Neno Lake. Katika Maandiko
yaliyovuviwa, anaonesha furaha ya kupatanishwa kama mtu
ambaye tayari ameshaanza kufurahia manufaa ya upatanisho
huo na ambaye hapa anazungumzia amani ya kweli na halisi kwa
watu wote.
Bila shaka, Maandiko hayazungumzi juu ya Mungu
kupatanishwa na wanadamu. Kimsingi inaeleza kwamba ni
wanadamu ambao walikuwa na uadui dhidi ya Mungu na
walihitaji kupatanishwa Naye (Warumi 5:10). Ilikuwa ni kupitia
kifo cha upatanisho cha Kristo ambapo Mungu alibadilisha uadui
kati ya wanadamu na Yeye Mwenyewe kuwa uhusiano wa amani
na kirafiki.
Badiliko hilihalitokei ndani ya mtu ambaye bado ana chuki na
Mungu, mpaka pale atakaposikia na kuamini mwaliko wa injili
wa kupatanishwa na Mungu.
Kwa hiyo, inakuwa ni shauku yetu kwa makusudi kabisa
kuwalenga wale ambao hawajafikiwa na kupanua wigo wa
imani ipasavyo ili kujumuisha watu wapya na wengi ambao
wanaongoka kwa kumwamini Yesu kuwa Mwokozi. Shauku
3
hii— ya uinjilisti—basi haipaswi kuwekewa mipaka katika nyanja
maalum na ya kitambo1 bali inapaswa kuwa:
a) Endelevu—Petro na washirika wake walikuwa “Kila siku,
ndani ya hekalu na nyumbani mwao, hawakuacha kufundisha
na kuhubiri habari njema za Yesu kwamba ni Kristo” (Matendo
5:42).
b) Kuenea—“Basi nyumba yote ya Israeli na wajue yumkini ya
kwamba Mungu amemfanya Yesu huyo mliyemsulubisha
kuwa Bwana na Kristo. Walipoyasikia haya wakachomwa
mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine,
Tutendeje, ndugu zetu?” (Matendo 2:36 – 37), na
c) Wakuvutia—“Bwana akamwambia mtumwa, “Toka nje
uende barabarani na mipakani, ukawashurutishe kuingia
ndani, nyumba yangu ipate kujaa” (Luka 14:23); “Nawiwa
na Wayunani na wasio Wayunani, nawiwa na wenye hekima
na wasio na hekima. Kwa hiyo, kwa upande wangu, mimi
ni tayari kuihubiri Injili hata kwenu ninyi mnaokaa Rumi”
(Warumi 1:14 – 15).
Kwa hiyo, uinjilisti ni sifa bainifu ya watu waliopatanishwa,
ambao wamekuwa wanafunzi wa Yesu Kristo, kuanzia kwa mtu
mmoja mmoja, kuelekea katika familia na kupanuka kuelekea
maisha endelevu ya ushuhudiaji wa kikanisa. Ni shauku kuu ya
Bwana wetu kubariki familia zote duniani kupitia mwili Wake
yaani Kanisa. Ni mtazamo wa makusudi, wenye mkazo wa kiroho
wa hali ya juu ambao huamsha maisha ya kiroho yanayotakiwa
ya mtu binafsi, familia na Mwili wa Kristo, na kuleta manufaa
makubwa zaidi kwa wote tunaokutana nao.
Maombi:
· Omba kwamba tutambue moyo wa Mungu unaowaonea
shauku waliopotea na kwamba wapate kupatanishwa.
· Omba kwamba tutambue wajibu ulio juu ya waliopatanishwa
ili kutangaza habari njema.
· Omba kwamba kutangaza huku kuwafikie wote tunaokutana
nao kila siku.

1. Robert Emerson Coleman, The Master Plan of Evangelism, Second Edition, (Michigan:
Fleming H. Revell. 1993), uk. 17.
4
Siku ya Pili
Mungu Humwezesha Amwitaye
“Basi sasa, enenda, nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na
kukufundisha utakalolinena” (Kutoka 4:12). “… Nami nitakuwa
pamoja na kinywa chake, na kuwafundisheni mtakayoyafanya”
(Kutoka 4:15).
Sura ya nne ya Kutoka inaelezea visingizio kadha wa kadha
ambavyo Musa alitoa mbele za Mungu kwa ajili ya upingaji wake
wa kuitikia wito wa kwenda Misri kupeleka ujumbe wa Mungu
wa ukombozi kwa wana wa Israeli waliokuwa watumwa.
“Musa akajibu akasema, Lakini, tazama, hawataniamini, wala
hawatasikia sauti yangu; maana watasema BWANA hakukutokea”
(Kutoka 4:1).
“Musa akamwambia BWANA, Ee Bwana, mimi si msemaji,
tokea zamani, wala tokea hapo uliposema na mtumishi wako;
maana mimi si mwepesi wa kusema, na ulimi wangu ni mzito”
(Kutoka 4:10).
“Akasema, ‘Ee Bwana, nakuomba, tuma kwa mkono wake
huyo utakayemtuma” (Kutoka 4:13).
Musa alikuwa akisema, hakuwa anafaa kwa kazi aliyopewa.
Musa anaonekana kujitathmini kulingana na uwezo na historia
ya nyuma iliyomfanya kukimbia kutoka Misri na inaonekana
alijishusha hadi kuhitimisha kwamba angekabiliwa na maafa.
Hakika, alitambua kwamba mwito huo ulikuwa ukimwalika ili
kutumika katika hali ambazo zilikuwa nje ya uwezo wake wa asili.
Je! Musa anasimama peke yake katika kuukataa wito wa Mungu
kwa ajili ya utume? Si kweli! Ushahidi wa kuwa na washiriki
wachache katika Divisheni nzima unaonesha kwamba sisi pia ni
wakataa wito katika zama zetu. Sura ya nne ya kitabu cha Kutoka
inaangazia mashaka yetu na kutafuta kutupilia mbali hofu zetu.
Jibu la Mungu kwa Musa lilikuwa kwamba haikuwa ikihusiana
na jinsi Musa alivyokuwa, bali jinsi BWANA Alivyo. Ijapokuwa
Musa alisimama kando ya kijiti kilichokuwa kikiwaka moto,
ambacho hakikuteketea na akiwa amevua viatu vyake kwa sababu
uwepo wa BWANA ulilifanya eneo ambapo alikuwa amesimama
5
juu yake kuwa takatifu, hakupata uelewa wa haraka wa kuweza
kumwamini BWANA.
Mazungumzo yaliyofuata, yanamwonesha BWANA kuwa
mvumilivu sana, na Aliye tayari kuondoa shaka moja baada ya
lingine. BWANA alimhakikishia Musa kwa kudhihirisha sifa Zake
kwamba MIMI NIKO AMBAYE NIKO (Kutoka 3:14). “Ninachagua
kuwa vile Nitakavyo kuwa au Ninaumba kile Ninachokiumba”:
hii ni kumaanisha kwamba, maajabu ya asili na matukio yaliyopita
yametokea kutokana na mapenzi ya Mungu ambaye ni Muumba
na Bwana.2 Mungu amechagua kujitambulisha Yeye Mwenyewe
kwa namna hii. Inajumuisha kile Alicho, na jinsi tunavyopaswa
kuhusiana Naye.
Mungu alimhakikishia Musa kwamba Angeenda pamoja
naye na angekuwa akimfundisha yale ambayo angesema na
yale ambayo angeyafanya. (Kutoka 4:12, 15). BWANA alikuwa
amechunguza eneo lote na maandalizi yote kwa ajili ya utume
yalikuwa tayari. Alitaka Musa awe wakala wa kibinadamu kama
ilivyoelezwa katika Amosi “Hakika Bwana MUNGU hatafanya
neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri Yake”
(Amosi 3:7).
BWANA ametoa mwito Wake kwa kila mmoja wa wanaoamini
ili kushuhudia katika jamii mbali mbali (Matendo 1:8). Cha
kusikitisha, Yeye husikia kutoka katika midomo yetu mara nyingi,
tukitoa visingizio vya kutokufaa kwa kazi hiyo na majibu kwamba
tuma mtu mwingine.
Inatia moyo, basi kupima heshima ambayo Bwana ameweka juu
yetu katika wito wa kuwa mashahidi Wake katika Utume Mkuu.
Ni jambo la kutia moyo kwamba MIMI NIKO ambaye alifuatana
na Musa katika kufikia mafanikio makubwa yanayoelezwa katika
Kutoka, ndiye MIMI NIKO aliyesema “Amin, amin, nawaambia,
yeye Ibrahimu asijakuwako, MIMI NIKO” (Yohana 8:58). Yeye
ndiye aliyefanikisha mambo makubwa zaidi kwa ajili yetu
msalabani kwa kifo na ufufuo Wake, na “wala si kwa damu ya
mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara
moja tu katika Patakatifu, akiisha kupata ukombozi wa milele”
2 Anderson, Bernhard W, The Living World of the Old Testament, Third Edition, (England:
Longman Group Limited, 1975), uk. 54.
6
(Waebrania 9:12). Pia, Alitimiza ahadi ya kumtuma Roho Mtakatifu
kwa jamii inayoshuhudia.
Utimilifu wa mpango wa Mungu ulioelezwa kwa ufasaha katika
Maandiko unasubiri kutangazwa kwa injili kama ilivyoainishwa
katika Isaya “Bwana ameweka wazi mkono Wake mtakatifu
Machoni pa mataifa yote; na ncha zote za dunia zitauona wokovu
wa Mungu wetu” (Isaya 52:10). Wazo hili linawekewa mkazo
katika Luka “Na wote wenye mwili watauona wokovu wa
Mungu” (Luka 3:6). Sio dhahiri kwamba mtu anaweza kufahamu
ulinganifu huu kati ya ahadi ya uzima wa milele na utume
aliopewa. Ni kwa Roho Mtakatifu pekee tunaweza kuongozwa ili
kuelewa.
MIMI NIKO bado yuko katika kazi ya kutoa wito. Bado
anavumiliana na vipingamizi vyako. Anasema katika Waebrania
“Kwa hiyo, kama anenavyo Roho Mtakatifu, Leo, kama mtaisikia
sauti yake, Msifanye migumu mioyo yenu…” (Waebrania 3:7–8).
Haikutegemei wewe peke yako, ni uthibitisho kutoka kwa
MIMI NIKO, hata hivyo, unaweza kuwa sehemu muhimu ya
jumuia ya washuhudiaji kama ukichagua, tafadhali chagua.
Kwa wale ambao wameupokea vyema, wanapaswa kuwa na
uhakika kwamba “Yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu
ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu” (Wafilipi 1:6). Juhudi zako za
kushuhudia zitazaa matunda ya milele.
Maombi:
· Omba ili Mungu aondoe wasiwasi wowote unaokunyemelea
akilini mwako, ili uchague kutoka na kuwashuhudia washiriki
wenzako.
· Omba Mungu aiangazie akili yako ili kufahamu kwamba
katika kutekeleza Utume Mkuu unapaswa kuwa na uwepo wa
Roho Mtakatifu ndani yako ili kukufundisha nini cha kusema
na kufanya.

7
Siku ya Tatu
Ibada ya Familia Iletayo Mabadiliko
“Kisha nikaona malaika mwingine, akiruka katikati ya mbingu,
mwenye inlili ya milele, awahubiri hao wakaao juu ya nchi, na
kila taifa na kabila na lugha na jamaa, akasema kwa sauti kuu,
Mcheni Mungu na kumtukuza kwa maana saa ya hukumu Yake
imekuja. Msujudieni yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari
na chemchemi za maji.” (Ufunuo 14:6-7)
Kama familia za Waadventista wa Sabato, tunafurahia
kuelekeza utambulisho wetu kwa Ujumbe wa Malaika Watatu
katika Ufunuo 14. Katika aya ya 6-7, Ibada kimsingi ni kitendo
kinachofanywa na wanadamu kwa lengo la kumtukuza Mungu.
Katika kitabu cha Warumi 12, Paulo anatoa uchanganuzi wa kina
sana kuhusu maana ya ibada. Aya ya 1–2 Biblia inasema:
“Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu,
itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza
Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana. Wala msiifuatishe namna
ya dunia hii, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate
kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza,
na ukamilifu.”
Na tafsiri ya J B Phillips inaisuka Warumi 12:1-2 kwa kushangaza
kama:
“Nawasihi ndugu zangu, huku mkiwa mnaziona rehema
za Mungu waziwazi, kama tendo la ibada ambayo mnaifanya
mkiwa na akili timamu, mpeni miili yenu, ili iwe dhabihu iliyo
hai, iliyowekwa wakfu Kwake na inayokubalika mbele Zake.
Usiruhusu ulimwengu unaokuzunguka ukufinyange kama
utakavyo wenyewe, bali mruhusuni Mungu azifanye upya akili
zenu kutoka ndani, ili mpate kudhihirisha kwa vitendo kwamba
mpango wa Mungu kwa ajili yenu ni mwema, ukikidhi matakwa
Yake yote na kufikia kwenye lengo la ukuaji wa kweli.”
Fasili anayoitoa Paulo kwa ajili ya ibada, inajumuisha na kudai
namna kamili ya maisha yetu ya kila siku. Kwa hiyo, ni vyema
kwa familia kuwa na maisha ya ibada yasiyo na kikomo. Inazitaka
familia na watu binafsi kuishi katika uwepo wa Mwenyezi
Mungu Aliye katika uhusiano unao-okoa pamoja nasi. Kwa hiyo,
8
familia zinapaswa kukubali kwa makusudi kile ambacho Mungu
anatufanyia kama jambo bora zaidi tunaloweza kufanya.
Bwana anazitaka familia kuwa mawakala wa kuleta mabadiliko
ya kitamaduni, “Tofauti na tamaduni zinazokuzunguka,
zinazokuburuta hadi katika kiwango chake cha kutokukomaa,
Mungu atakufanya kuwa bora zaidi na kukuza ukomavu
ulioundwa vizuri ndani yako.”
Ibada ambayo inaagizwa na Ufunuo 14 na Warumi 12, ni
kuachana na kufuata tamaduni zinazotuzunguka ambazo
zinatuvuta bila kukoma hadi katika kiwango chake cha kukosa
ukomavu. Bwana anatuita kuishi maisha ya uthubutu—Ibada—
kwa manufaa ya kuleta mabadiliko kwa wengine. Shauku ya
Mungu ni kwamba atubadilishe kutokea ndani kwenda nje. Ibada
ambayo Paulo anataka tuizingatie ni ya kutufanya kuwa bora
zaidi kadiri tunavyokaza macho yetu kwa Bwana daima.
Ibada kama tendo la kuabudu lina visawe kadha wa kadha:
upendo, kicho, heshima, uchaji Mungu, kusifu mno, kuonesha
heshima ya hali ya juu na kadhalika. Tendo la kuabudu ni kiini
katika ibada, ni ushirika binafsi wa heshima kati ya mwabudu na
Mungu unaotumika kwa kila uwanda maishani. Mwenendo huu
wa kuabudu haukomei katika eneo takatifu—jengo la kanisa—
lakini ni tabia inayoendelea kwa kuagizwa na Roho Mtakatifu
aliyeko siku zote ambaye anakaa ndani yetu sisi tunaoamini.
“Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe
tamaa za mwili. Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho”
(Wagalatia 5:16, 25).
Familia za Waadventista zinahitaji kudhamiria kufuata njia safi
na sahili ya kutembea daima katika uwepo wa Mungu. Katika
ibada, mawazo yetu yanawekwa kwenye mambo ya juu.
“Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo
juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini
yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi” (Kol. 3:1–2).
Wakati ambapo, Mkristo, huishi maisha yote katika ibada, hata
hivyo, kuna mambo tunayoyafanya ambayo yameoneshwa kuwa
muhimu katika Ibada: Ushirika: Matendo 2:42; Tafakari ya Neno:
Zaburi 19:14; 2 Tim. 2:15; Uwakili Katika Familia: Zaburi 24:1; na
Uinjilisti.
9
Sharti Ibada iwe na lengo la uinjilisti. Paulo anaeleza kwamba
ubora na mtindo wa kuabudu lazima uwe wenye kuleta heshima
kwa Mungu na pia ujikite katika uinjilisti (1 Kor. 14:23 – 25).
Akiwa na shauku hiyo hiyo, Yakobo alitoa taarifa sahihi juu ya
ubaguzi kwenye mikutano ya kanisa. Ukaribisho wa ukarimu ulio
sawa kwa wale wanaoamini na wasioamini wakati wa Ibada una
maana kubwa sana kwa ajili ya uinjilisti na utunzaji/malezi kwa
waongofu (Yakobo 2:2–4).
Hubiri wakati wa ibada linapaswa kuundwa kwa mtazamo wa
malezi pamoja na uinjilisti, likitolewa katika wingi wa visa vya
Biblia, na wakati huo huo likizingatia namna yake ya kushughulikia
mahitaji ya kanisa na ya mtu binafsi, na hivyo kuhitimishwa na
wito wa kuwaita watu ili kufanya mabadiliko.
Yakobo alisema, “Ibada ya kweli ni, kuwatunza yatima na
wajane na kujilinda na dunia pasipo mawaa” (Yakobo 1:27).
Ibada ni hali ya kudumu kuwepo na ni tendo la maisha yote (1
Thes. 5:17). Kumwabudu Mungu ni kama jukumu la maisha yote
kujitoa kikamilifu katika kumtumikia Yeye. Msamaria mwema
katika matendo yake ya ukarimu kwa aliyejeruhiwa, alijihusisha
katika kumwabudu Mungu.
Utume Mkuu unatangazwa katika mazingira ya Ibada kwamba;
Nao walipomwona, walimsujudia (Mt. 28:17), kisha Bwana wetu
Yesu Kristo aliendelea kutangaza Mamlaka Yake (aya ya 18) na
hatimaye aliwaagiza kwenda (aya ya 19) wakiwa na uthibitisho
wa uwepo Wake daima.
Kukuza vielelezo vizuri vya ibada ya familia ambayo inahusisha
na kuwakubali jirani zetu wasioamini kupitia matendo ya ibada
na huduma hujenga msingi mzuri kwa ajili ya kupanda mbegu za
injili.
Maombi:
· Omba kwamba Mungu atuwezeshe kukaza usikivu wetu
Kwake.
· Omba kwamba Mungu atubadilishe kutokea ndani.
· Tuombe kwamba, bila kusita tutambue kile ambacho Mungu
anakitaka toka kwetu na kwa haraka tufanye kama atakavyo.
· Omba kwamba Mungu atufanye kuwa bora na kukuza ukuaji
ulio bora ndani yetu ili tuweze kuwa nyenzo katika uinjilisti.
10
Siku ya Nne
Kukuza Vikundi Vidogo
“Tukaangaliane sisi kwa sisi na kuhimizana katika upendo
na kazi nzuri; wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo
desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa
kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia” (Waebrania 10:24,
25).
Dhana ya kulikuza kanisa kwa njia ya kuongeza mtandao wa
vikundi vidogo ilisemwa kwa sauti kubwa na Ellen G. White.
Aliandika:
Uundaji wa makundi madogo kama msingi wa juhudi za
Kikristo ni mpango ambao umewasilishwa mbele yangu na Yeye
asiyeweza kukosea. Kama kuna idadi kubwa ya washiriki kanisani,
hebu na wagawanywe katika makundi, ili kufanya kazi sio tu kwa
washiriki wa kanisa bali pia na kwa ajili ya wale wasioamini.3
Katika ulimwengu wa kibiashara, Tom Peters alikuwa na maono
ya kuwa na kampuni yenye mafanikio katika miaka ya 1990, kwa
namna ambayo ingeleta mabadiliko kutoka kwenye mustakabali
wa kuhodhi madaraka kufikia malengo yake ya mustakabali wa
ugawanyaji wa madaraka.4
Utawala jangwani ulikuwa chini ya Musa peke yake mpaka
pale Yethro alipotokea katika kambi ya wana wa Israeli wakati wa
Kutoka. Yethro aligundua hali ya kuchosha iliyokuwa ikimuathiri
Musa na wana wa Israeli (Kutoka 18:17–18), na kufanya iwe vigumu
kuendelea kuwapatia watu maarifa ya kujua amri za Mungu na
sheria Zake (Kutoka 18:13–16). Yethro akapendekeza mabadiliko,
yanayopatikana kutoka kwenye kanuni iliyovuviwa na kuamriwa
na Mungu (Kutoka 18:23), alimshauri Musa kuchagua viongozi
wenye sifa zifuatazo: Uwezo, Wacha Mungu, Waaminifu na
Waadilifu, na kisha awagawe watu katika makundi ya watu 1,000,
100, 50 na 10, na kila kundi kulipatia kiongozi (aya ya 21). Kila
mtu alijihusisha katika kila kitengo kuanzia na 10 kwa mpangilio

3 White, Ellen G., Evangelism (Washington D. C: Review and Herald Publishing Associa-
tion, 1946), uk. 115.
4 Peters, Tom, Thriving on Chaos (New York: Alfred A. Knopf, 1987), uk. 50.
11
wa kupanda. Baba mkwe wa Musa—mshauri na msimamizi wa
kweli—alitamani kuwa na washiriki wengi zaidi katika kushiriki
madhumuni ya jumla ya safari na kuhakikisha haki inapatikana
kambini (aya ya 20). Ufahamu huu uliruhusu uasisi wa uongozi
wa usimamizi ambao uliwezesha kutolewa kwa maarifa, ujuzi na
uhamasishaji ambao ulipatikana kwa watu ili kuleta mafanikio
mema kwa wahamiaji wote (aya ya 22).
Kanisa la karne ya kwanza, kama ilivyonakiliwa katika Kitabu
cha Matendo ya Mitume, lilikuwa na vikundi vidogo vidogo,
na kwa ajili hiyo, kanisa likapata ukuaji mkubwa (basi wale
waliolipokea neno wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu
wapata elfu tatu; Matendo 2:41), na siku baada ya siku walidumu
ndani ya hekalu kwa moyo mmoja, wakimega mkate nyumba
kwa nyumba, na kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa moyo
mweupe (Matendo 2:46). Walijikumbusha wao wenyewe kuhusu
amri ya maonyo ya Maandiko haya: “Kwa hiyo imetupasa
kuyaangalia zaidi hayo yaliyosikiwa tusije tukayakosa. Kwa
maana, ikiwa lile neno lililonenwa na malaika lilikuwa imara, na
kila kosa na uasi ulipata ujira wa haki, sisi je! Tutapataje kupona,
tusipojali wokovu mkuu namna hii? Ambao kwanza ulinenwa na
Bwana, kisha ukathibitika kwetu na wale waliosikia” (Waebrania
2:1–3).
Mathayo ananakili maneno mazuri ya Bwana, kwa kuwa
walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami
nipo papo hapo katikati yao (Mathayo 18:20). Hili linaangazia
umuhimu wa kukusanyika katika familia, na katika jamii. Kwa
hiyo, pale wawili au watatu wanapopanga kukutana katika
Bwana, hapo kwa hakika Maandiko yatafunguliwa, na ajenda
ya uinjilisti haitaachwa. Mishna (inayosomwa kwa kurudia-
rudia) inafundisha kwamba pale watu wawili wanapokaa pamoja
na maneno ya Torati kutolewa katikati yao, Uwepo wa Mungu
unakaa miongoni mwao (Mishna 3:3) kunakuwa na Shekina—kiti
cha rehema.
Katika mkutano wa kikundi kidogo mbele za Bwana, na
kunapokuwa na malengo ya uinjilisti katika majadiliano, hakika
rehema itawabubujikia wale ambao hawajafikiwa. Wakati
12
vikundi vidogo vidogo vilipojitolea kwa mafundisho ya mitume,
na katika ushirika, na kwa kushiriki chakula pamoja, na katika
maombi, kicho cha hali ya juu kilikuja juu yao wote, na mitume
wote walionesha ishara za miujiza na maajabu mengi sana…
Waliabudu pamoja hekaluni kila siku, walikutana majumbani…
wakati huo huo wakimsifu Mungu, na kufurahia wema wa watu
wote. Na Bwana akalizidisha kanisa kila siku kwa wale waliokuwa
wakiokolewa (Matendo 2:42–47).
Maombi:
· Omba kwamba tuweze kuona kile Ellen G. White
alichoking’amua kuhusiana na huduma za vikundi vidogo-
vidogo.
· Omba Mungu atusaidie ili tutumie vikundi vidogo-vidogo
katika makanisa yetu ili kuzingatia utume.

13
Siku ya Tano
Kuzingatia Uhusiano Uliopo na Watu
Wasikivu
“Ili kwamba ushirika wa Imani yako ufanye kazi yake,
katika ujuzi wa kila kitu chema kilicho kwetu, katika Kristo”—
(Filemoni 1:6).
Tumezungukwa na fursa nyingi mno za kueneza upendo
wa Yesu ijapokuwa sisi tunaopaswa kuwafanya watu kuwa
wanafunzi tunaweza kwa namna fulani kuingia katika matatizo
makubwa ya kujitafutia fursa zetu wenyewe kwa ajili ya uinjilisti.
Kazi hii ni rahisi, tambua tu fursa ambazo tayari ziko karibu yako.
Maombi ni muhimu sana katika kutuwezesha kuona fursa kwa
ajili ya kufanya wanafunzi ambazo zimewekwa wazi mbele yetu
na Roho Mtakatifu. Wakati Bwana Yesu alipokuwa amejawa na
shauku ya kupumzika katika kisima cha Yakobo huko Samaria
baada ya kazi ya kuchosha, hata hivyo aliitumia fursa hiyo ili
kumvuta mwanamke Msamaria—aliyekuja kuteka maji—kwa
mambo ya kiroho. Hili lilipotokea, kama tujuavyo, lilitengeneza
msururu wa mafuriko ya jamii nzima ya Samaria (Yohana 4:4–42).
Mungu anatengeneza kila nafasi kama sehemu ya majibu ya
maombi yetu. Alituumba ili tuishi katika familia, ili kuwa msingi
wa muunganiko katika jamii kwa kuwa kila mtu anamhitaji
mwenzake. Anaitaka kila familia ya wanaoamini kuleta
mabadiliko katika jumuia kwa kushiriki pamoja nao imani na
upendo Wake. Ili tuweze kuwa thabiti katika kushiriki imani yetu
na wengine, tunahitaji mtazamo wa kifursa ambao unazingatia
masuala mawili: uhusiano uliopo na watu wasikivu.
Wanaotengeneza mtandao wao wa uhusiano, na kisha kuangalia
na kuomba kuhusu ni yupi kati ya watu hao wasio waumini katika
mtandao wao Mungu angependa kuwafikia na kwa njia gani.
Kufanya uinjilisti kimtandao ni njia mbadala inayokuwa aina
bora zaidi ya uinjilisti. Hii inakuwa wazi pale unapoangalia
takwimu zinazohusiana na sababu za watu kuja kanisani kwetu.
Takribani watu tisa kati ya kumi wanakuja kama matokeo ya

14
kuwa na uhusiano nasi. Hivi ndivyo Maandiko yanavyodokeza
juu ya kaya zetu kuwa kitovu kikuu cha uinjilisti:
a) Mjumbe wa mbinguni, malaika, anaiangalia kaya—
“Akatueleza jinsi alivyomwona malaika aliyesimama
nyumbani mwake na kumwambia, ‘Tuma watu kwenda Yafa
ukamwite Simoni aitwaye Petro, atakayekuambia maneno
ambayo yatakuokoa, wewe na nyumba yako yote’” (Matendo
11:13–14).
b) Wakala wa kibinadamu anayeshiriki habari njema
anaiangalia kaya—“Akataka taa ziletwe, akarukia ndani,
akitetemeka kwa hofu, akawaangukia Paulo na Sila; kisha
akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini
nipate kuokoka? Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu,
nawe utaokoka pamoja na nyumba yako” (Matendo 16:29–31).
c) Mtandao wa uhusiano hupanua upokeaji kwa kaya
nyingi—“Na Krispo, mkuu wa sinagogi, akamwamini Bwana
pamoja na nyumba yake yote. Wakorintho wengi waliposikia,
waliamini, wakabatizwa” (Matendo 18:8).
d) Mwongofu anaihimiza kaya katika msimamo wa kuamini—
“Basi babaye akafahamu ya kuwa ni saa ile ile aliyoambiwa na
Yesu, Mwanao yu hai. Akaamini yeye na wote wa nyumbani
mwake,” (Yohana 4:53).
e) Mchakato wa ufundishaji au uleaji wa kiroho unaweza kuwa
rahisi katika ngazi ya kaya—“Hata alipokwisha kubatizwa,
yeye na nyumba yake, akatusihi, akisema, kama mmeniona
kuwa mwaminifu kwa Bwana, ingieni nyumbani mwangu
mkakae. Akatushurutisha” (Matendo 16:15).
Aya zinazoendelea zinafafanua kipengele, ambacho kimepuuzwa
sana na mbinu zetu za kisasa za uinjilisti, kwamba kuja kwa
Yesu kulikusudiwa kuwa tukio la kifamilia au la kimtandao.
Utafiti unathibitisha ukweli kwamba watu wengi huja kwa
Yesu katika mpangilio wa ushirikiano wao katika kikundi.
Uinjilisti wa uhusiano unatoa muunganiko wa asili kwa ajili
ya kushiriki na wengine injili ya upendo wa Mungu uokoao.5

5 S. Joseph Kidder, “The Power of Relationships in Evangelism,”


Ministry, Julai 2008, 6-7.
15
Inafanywa kuwa rahisi zaidi na mifano ya kibiblia kwamba
mbinu ya mtu kwa mtu pia ina kipengele cha uhusiano:
i. Andrea alimleta kaka yake Petro kwa Yesu
ii. Philipo alimleta rafiki yake na mwanakijiji mwenzake
Nathanieli kwa Yesu. Andrea, Petro na Filipo walikuwa
wenyeji wa Bethsaida.
Je, umeshawaleta jamaa na rafiki zako wote—na wale wa
mahali ambapo unapewa upinzani—kwa kuwafanya wote kuwa
waumini na washiriki wa Kanisa?
Kama sivyo, kwa nini basi msiandae na kuweka mkazo
wenu kama familia kwa familia nyingine katika uga wenu wa
uhusiano, na uwasilishe maombi yenu kwa Mungu kwa niaba
yao ili kumruhusu Roho Mtakatifu kufanya kazi akilini mwao ili
kukubali upatanisho unaotimizwa katika Yesu Kristo?
Maombi
· Hebu na tuombe kwamba Mungu atusaidie kujenga madaraja
kupitia ukuzaji wa uhusiano ambao utatusaidia kuleta kaya
na rafiki zetu kwa Yesu.
· Omba kwamba Mungu atusaidie tuweze kuweka mkazo wetu
kwa watu wasikivu. Dunia imejawa na watu wasikivu ambao
mioyo yao Mungu ameiandaa ili kumpokea. “Hamsemi
ninyi, ‘Bado miezi minne, ndipo yaja mavuno’? Tazama, mimi
nawaambieni, Inueni macho yenu myatazame mashamba,
ya kuwa yamekwisha kuwa meupe, tayari kwa mavuno”
(Yohana 4:35).

16
Siku ya Sita
AHADI ZA UONGOAJI WA ROHO:
Kufanya Mapinduzi Katika Uinjilisti
“Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu
mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya
nguvu itendayo kazi ndani yetu; naam, atukuzwe katika Kanisa
na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na milele.
Amina”—(Waefeso 3:20–21).
Je! Hatuwezi kufanya mabadiliko ya kimapinduzi katika
maisha yetu, ili kuondoa mashaka na kuelekeza juhudi zetu katika
maombi ya kumwomba Mungu atusaidie ili tuweze kuongoa
angalau kaya moja kwa ajili ya Yesu katika mwaka mmoja? Laiti
kama tungeamini kwamba Mungu aliweza kufanya hasa yale
ambayo Waefeso 3:20–21 inaelezea kuhusu uongoaji wa roho,
tusingekuwa tunaongelea kufikia idadi ya washiriki 10,000,000
mnamo mwaka 2025 kama suala la kuzidisha idadi yetu ya sasa
ya washiriki wetu mara mbili zaidi katika fursa ya mafuriko ya
watu 450,000,000 ambao hawajafikiwa bado katika eneo letu la
Divisheni. Kwa kurudia-rudia, tumetakiwa kumwomba Mungu
sana katika Maandiko. Yakobo analiweka hili wazi kwetu kwamba
“hamna kitu kwa kuwa hammwombi Mungu” (Yakobo 4:2).
Kuamini ukweli huu sahili kwamba uweza wa Mungu wa
kufanya ni mwingi mno kungetosha kuongeza washiriki kwa kiasi
kikubwa. Paulo anaangazia zaidi shauku na uwezo wa Mungu
kutubariki akiupanua zaidi ya kile tunachoweza kuomba na
kile tunachoweza kukifikiria. Hili linaweka wazi mafanikio yetu
yasiyo na kikomo katika kuongoa roho ikiwa tunaweza kuamini
na kutupilia mbali pingu zinazotufunga.
Ahadi nyingine ya muhimu ilitamkwa wakati Yesu na
wanafunzi Wake walipokuwa wakijadiliana katika eneo la
Kaisaria-Filipi; Yesu alimwambia Petro akiwa na wanafunzi
wenzake walipokuwa wamekusanyika pamoja Naye kwamba:
“Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote
utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote
17
utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni” (Mt.
16:19). Tayari mbingu imeshafungua mlango wa uwezekano wa
kupata uzima wa milele kupitia kifo cha upatanisho cha Bwana
wetu Yesu Kristo. “Funguo” ni vipaji mbalimbali vilivyotolewa ili
kuelewa na kueleza kinagaubaga kweli za Injili na agizo kutoka
kwa Yesu ili kuupeleka mbele utume Wake. Utoaji unamaanisha
kuagiza kufunguliwa kwa mlango wa imani kwa njia ya kuihubiri
injili kwa Wayahudi (Matendo 2:1–47) na kisha kwa Wamataifa
(Matendo 10:1–48; 15:7, 14).
Injili inamaanisha ufalme wa mbinguni, ambayo inatoka
mbinguni, inamtangaza Masihi mfalme kuwa Mwenye Enzi
juu na katika maisha yetu. Inahusisha kuisimamisha na
kuipanua, ikionesha utajiri wa neema Yake. Inamaanisha Yesu
ni Bwana, ikimaanisha kuwa anatuamuru kuupatia utume Wake
kipaumbele. Ni kweli kusema kwamba Yesu hawezi kumwamuru
mtu ambaye hamwiti Yeye Bwana (Mt. 26:21–25). Aya hizo hapo
juu yanaangazia tofauti kati ya wale wanaomtambua Yesu kuwa
Bwana na kuchukua juu yao wajibu wa kufungua milango ambayo
imekwishafunguliwa kwa ajili ya wengine kuingia pia, na wale
wasiojali lakini tu wanafurahia mafundisho ya Rabi.
Asili ya mwanadamu haiwezi kwa yenyewe kuuchuchumilia
wokovu, lazima awepo mchukuzi ambaye analeta habari njema
kutoka nje yetu. Mahali pa kuanzia ni kwamba mbingu imetuletea
wokovu, na Roho Mtakatifu kupitia wakala wa kibinadamu
analeta ujumbe ubadilishao kwa watu ili kwamba waweze
kupokea wokovu. Hivyo basi, uinjilisti, unahusisha kutoa
mafunzo ya Biblia ambako kunahusisha mambo mengi zaidi
kuliko kusambaza tu habari kuhusu Biblia. Ni kuwahudumia
watu, kuwakomboa kutoka katika mtazamo hafifu wa kumtambua
Mungu, kuwawezesha kujua maana ya kuishi maisha ya uaminifu,
kuwawezesha kuachana na njia za zamani za kujitumainia nafsi
na badala yake, waasili tabia za uchaji Mungu.6
Inatia moyo kufahamu kwamba Bwana Yesu, kwa njia ya Roho
Mtakatifu anayekaa ndani yetu, ametupatia mamlaka ya kufungua
macho ya watu ili wapate kutambua uhalisi kamili wa ukweli
6 James C. Wilhoit and Leland Ryken, Effective Bible Teaching, Second Edition, (Michigan:
Baker Academic, 2012), uk.36.
18
wa mbinguni. Kwa hiyo, Paulo, akiwa anatambua kipaumbele
cha mbinguni ili kufungua na kufunga, anawaagiza Wakolosai
“Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na
shukrani; mkituombea na sisi pia, kwamba Mungu atufungulie
mlango kwa lile neno Lake, tuinene siri ya Kristo, ambayo kwa
ajili yake nimefungwa, ili niidhihirishe, kama inipasavyo kunena”
(Wakolosai 4:2–4).
Maombi
· Omba kwamba macho yako yaweze kufunguliwa ili kuona
uhalisi wa mbinguni kwa njia ya maono ambayo Mungu
anataka kukupatia. Taja kile ukitakacho na kwa uwazi.
· Omba kwamba Mungu aachie uwezo kwa familia yako wa
kuleta mema zaidi katika mahubiri yajayo ya uinjilisti wa
familia.

19
Siku ya Saba
Kuitwa na Mungu ili Kuwaimarisha
Wengine
“Enendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa
wakati” (Wakolosai 4:5).
Katika sura ya kwanza ya waraka kwa Wakolosai Paulo anafanya
ugunduzi unaogusa wa maisha yake katika huduma kwa ajili ya
Kristo. Ameshikiliwa gerezani, lakini hili halimzuii kuendelea
na utume, na wala hakatishwi tamaa na mateso aliyokuwa
akiyapitia. Badala yake, kwa makusudi yeye huvivuka vikwazo
vyote vya mateso yaliyokuwa yanamzunguka. Anafurahia (aya
ya 24), anaichukulia kuwa fursa ya pekee kuwa mhudumu wa
injili (aya ya 25), siri ambayo watu wacha Mungu katika zama na
vizazi vilivyopita walitamani kuiona kwa sasa imefunuliwa kwa
watakatifu Wake—ambayo ni Yesu kukaa ndani yenu, tumaini
lenye utukufu (aya ya 27). Msisitizo ni kwamba Wamataifa pia,
wanaikumbatia injili na wanaidhihirisha siri hii “Kukaa kwa Yesu
ndani yenu.”
Katika aya ya 28, inafafanua wajibu wa Mkristo: kutumia
hekima yote katika kuhubiri na kufundisha, ukiunganishwa na
kutoa maonyo kwa kila mtu katika kujitahidi kumfanya kila mtu
mkamilifu katika Kristo Yesu (aya ya 29).
Aya ya 29 ina maana kubwa mno. Ili kufikia malengo endelevu,
“nilijitahidi kwa kadiri ya kutenda kazi Kwake atendaye kazi
ndani yangu kwa nguvu.” Maana inayoelezwa katika tafsiri ya
Kigiriki hapo kama kufanya kazi ni kufanya kazi hadi kuchoka
kabisa. Neno kujitahidi kama lilivyotumiwa katika aya hii inabeba
kidokezo cha mashindano ya riadha. Unapata medali ya dhahabu;
huwezi kuikwapua tu. Na ni kwa jinsi gani wanaweza kuipata?
Ukweli wa kuburudisha moyo katika yote haya ni kwamba
inapatikana kutokana utendaji kazi wa Kristo atendaye kazi ndani
yake kwa nguvu. Ukweli unaovutia ni kwamba sisi ni onesho
lililo hai la Habari Njema katika jamuiya zetu kwa wema wa Roho
Mtakatifu akaaye ndani yetu.
20
Agizo—Enendeni kwa hekima (Wakolosai 4:5) linapokelewa
na kufanyiwa kazi kwa busara za Kikristo kila siku maishani.
Kwa kutumia kila fursa katika mtazamo wa muda uliosalia kabla
ya kurudi kwa Yesu. Mtazamo uliowasilishwa katika fungu hili
unaangazia kipindi hiki kama kilichojawa na moyo wa ibada
makini, tunapaswa kuzingatia kwamba utendaji wetu wote
unaakisi tabia na dai lake maalum.7
Kwa hiyo, ni dhahiri kwamba, kila kukutana bila kutarajia,
nafasi ya kukutana, kukutana na, au kuonana na mtu mwingine
kunapaswa kutumiwa kwa makusudi ili kufanikisha kitu kwa ajili
ya uinjilisti au kufundisha ili kumruhusu Roho Mtakatifu aunde
sura ya Yesu Kristo kwetu.
“Kuna wimbi katika matukio ya wanadamu ambalo,
likizingatiwa, huongoza katika mafanikio; yasipozingatiwa, safari
yote ya maisha yao inafungwa katika kupungukiwa na kuwa tabu
tupu. Katika bahari hiyo kamili tunaelea sasa; na lazima tutumie
kila fursa inapojitokeza, vinginevyo tutakosa shabaha.”8
Kuwafikia watu kwa injili halikuwa wazo letu. Sio jambo
tuliloanzisha na sasa tunamwomba Mungu atusaidie kulifanikisha.
Hapana. Ni kinyume chake kabisa. Alikuwa ni Baba wa mbinguni
ambaye “aliupenda sana ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe
pekee; ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa
milele” (Yohana 3:16). Alikuwa ni huyo Mwana, Yesu, ambaye
alihiari “kuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea” (Luka 19:10),
na kisha akatuagiza kwenda ulimwenguni kote kufanya vivyo
hivyo (Mathayo 28:18 – 20). Yesu pia alituahidi kutupatia Roho
Mtakatifu, ambaye kutoka Kwake tutapokea nguvu ili kwamba
tuweze kuwa mashahidi Wake Yerusalemu, na katika Uyahudi
wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi (Matendo 1:8). Kwa
hivyo, utume wa Mungu wa kuwaokoa wana na binti waliopotoka
sasa umekuwa utume wetu—na jambo zuri ni kuwa aliahidi kuwa
pamoja nasi daima, hata ukamilifu wa dahari” (Mathayo 28:20).9

7 L. Houlden, Paul’s Letters from Prison, (London: SCM Press Ltd, 1977), uk. 217
8 William Shakespeare, Julius Caesar
9 Mark Mittelberg, Contagious Faith: Discover Your Natural Style for Sharing Jesus with
Others (2021), uk. 5-6.
21
Maombi
· Omba kwamba Mungu atusaidie ili tuendelee kuwa vyombo
vya kutumiwa na Roho Mtakatifu katika Utume Mkuu.
· Omba kwamba Mungu atubidishe kufuatisha mfano wa Paulo
katika kuwa na bidii kwenye utume tuliokabidhiwa.

22

You might also like