Download as docx, pdf, or txt
Download as docx, pdf, or txt
You are on page 1of 22

MWOLHOBERYA BOAZ

SWALI: Eleza kikamilifu maana ya neno mofolojia. Toa maelezo kuhusu dhana muhimu
kama vile mofimu, mofu, alomofu, mzizi na uundaji wa maneno ya Kiswahili kwa ujumla

Mofolojia

Dhana ya mofolojia imeshughulikiwa na wanaisimu wengi kama vile Matthews (1974), Hartman
(1972), Richard et.al. (1985) miongoni mwa wengine. Neno hili limetoholewa kutoka kwa neno
la Kiingereza morphology. Neno hili limetumika katika taaluma zingine kama vile: Utabibu
(human morphology and anatomy) Sayansi ya mimea (plant morphology) Jiografia
(geomorphology)

Katika taaluma ya isimu neno hili limekuwa likitumika kwa zaidi ya karne moja na linatumiwa
kwa maana ya somo au tawi la isimu ambalo huchunguza maumbo ya maneno na aina zake.
Tawi hili la isimu hushughulikia hasa kipashio cha neno. Wanaisimu mbali mbali wameeleza
maana ya dhana ya mofolojia.

Mathews (1974) anaeleza mofolojia kama tawi la taaluma ya isimu ambalo linachunguza
maumbo ya neno hususan maumbo ya mofimu.

Katika kufafanua dhana ya mofolojia Posner (1975) anaeleza kuwa mofolojia ni tawi la taaluma
ya isimu ambalo huchunguza maumbo ya maneno hususan maumbo ya mofimu.
Habwe, J na karanja, P (2004) wanasema kuwa mofolojia ni tafsiri ya neno la kiingereza
‘morphology’. Neno hili linatokana na neno la kiyunani lenye maana ya muundo au umbo.
Hivyo basi mofolojia ni neno linalotumiwa kumaanisha utanzu wa isimu unaoshughilikia
muundo wa maneno.

Mathew (1974) anasema kwamba mofolojia ni tawi la taaluma ya isimu ambalo huchunguza
maumbo ya maneno hususani maumbo ya mofimu.
Kamusi Sanifu ya Isimu na Lugha (1990) inaeleza mofolojia kama tawi la isimu ambalo
huchunguza maneno na aina za maneno.

Naye Hartmann na Stork (1972) anadai kuwa` mofolojia ni tawi la sarufi ambalo hushughulika
na uchunguzi na uchambuzi wa maumbo, fani na aina za maneno yalivyosasa pamoja na historia
zao. Tukizingatia maelezo haya ni wazi kuwa mofolojia kama tawi la isimu hujishughulisha na
maumbo ya maneno.

Kwa hivyo, mofolojia ni taaluma ya isimu inayojihusisha na uchunguzi wa miundo ya maneno.


Taaluma hii inachunguza miundo ya maneno ili kutambua vipashio vinavyojenga maneno na
kueleza kazi zavyo katika tungo za lugha.

Wanaisimu wanakubaliana kwamba mofolojia inaweza kugawanywa katika makundi mawili


makuu (matawai ya mofolojia)

Mofolojia ambishaji/ mofolojia ya mnyamniliko

Mofolojia nominishaji/ mfolojia ya uundaji wa maneno

(i) Mofolojia Ambishaji Hii ni mofolojia ya mnyambuliko wa maneno. Hapa vipashio hupachikwa
na kuongezewa kwenye mizizi ya maneno na kuzalisha maneno ya ziada yenye maana tofauti.
Mzizi wa neno haubadiliki kamwe. Matokeo ya minyambuliko si kupata neno jipya bali ni
kuongezea maana fulani ya kisarufi katika neno hilo. Kila lugha ina taratibu zake zinazoongoza
minyambuliko. Mzizi maneno yaliyonyambuliwa mtu jitu, watu cheza chezwa, chezea,
chezacheza, chezeana nk. ruka rukia, rukiana, rukiwa, rukaruka, rukwa nk.

(ii) Mofolojia Nominishaji Aina hii ya mofolojia pia hujulikana kama mofolojia ya uundaji.
Katika aina hii ya mofolojia, viambishi mbali mbali huongezwa kwenye mzizi wa neno tukapata
neno jipya kabisa. Neno linalozalishwa huenda likawa si la aina moja na neno asilia. Kwa mfano,
katika Kiswahili nomino huundwa kutokana na vitenzi. vitenzi nomino imba wimbo, mwimbaji,
kuimba, mwimbishaji, kivumishi kitenzi refu refusha.

Mofu
Matinde (2012) akiwanukuu TUKI (1990) wanaeleza kuwa mofu ni kipashio cha isimu maumbo
kiwakilishacho mofimu.

Matinde (2012) Mofu ni umbo kamili ambalo huwakilisha mofimu. Umbo hilo hudhihirika
kifonolojia na kiothografia (uwezo wa kutamkwa na kuandikwa).

Katika lugha ya kitaalamu umbo linalowakilisha mofimu hujulikana kama mofu (Massamba na
Wenzake, 2013:14).

Kwa ujumla mofu ni umbo au maumbo yanayowakilisha mofimu na ambayo yanaweza


kudhihirika kwa kutamkwa au kimaandishi.

Kama wanavyoeleza Nida (1949), Massamba na wenzake (2004:14) mofu ni umbo la neno
ambalo huwakilisha mofimu na ambalo hudhihirika kifonolojia linapotamkwa na kiothografia
linapoandikwa. Hii ina maana kuwa mofu ni umbo linaloonekana na mofimu ni dhana dhahania
inayowakilishwa na umbo hilo. Aidha mofu moja inaweza kudhihirisha maumbo tofauti ambayo
Matinde (2012:100) anayarejelea kama alomofu.

Aina za Mofu

Matinde (2012) ameainisha mofu kwa kuzingatia vigezo viwili ambavyo ni:

(i) kigezo cha isimu maana

(ii) kigezo cha isimu maumbo

Katika kigezo cha isimu maana tunapata aina kuu tatu za mofu ambazo ni;

(i) Mofu huru

(ii) Mofu funge

(iii) Mofu tata

(i) Mofu huru


Ni mofu ambazo zinaweza kukaa peke yake kama maneno kamili yenye maana inayoeleweka
bila kusaidiwa na mofu nyingine. Mofu huru zinaweza kuwa nomino, kivumishi, kiwakilishi,
kielezi, kitenzi au kiunganishi.

(ii) Mofu funge au tegemezi

Ni mofu ambayo haiwezi kukaa peke yake kama neno lenye maana kamili. Mofu hizi huhitaji
kuambatanishwa na mofu nyingine ili kupata maana sawa au neno kamili.

Mfano: M-toto – w-atoto

Ki-su – vi-su

M-ti – mi-ti

Ji-tu – ki-ji-tu

Wakati mwingine mofu funge inaweza ikatokea katika mizizi ya vitenzi:

Mfano: {-l-} katika neno kula

{-f-} katika neno kufa

{lim-} katika neno lima

{-j-} katika neno kuja

{-nyw-} katika neno kunywa

(iii) Mofu tata

Ni mofu ambayo huwa na maana zaidi ya moja yaani kuanzia mbili na kuendelea. Mofimu tata
hutokea katika vitenzi vilivyopo katika kauli ya kutendea.

Mfano: Alimpigia = a-li-m-pig-i-a.

Alimchezea = a-li-m-chez-e-a.
Alimchomekea = a-li-m-chom-ek-e-a.

Hivyo mofu {-i-} na {-e-} ni mofu ambazo zinaonyesha kauli ya kutendea na ndizo zinaleta utata
katika vitenzi hivyo.

Kigezo cha isimu maumbo

Matinde (2012) anaeleza kuwa katika kigezo hiki cha isimu maumbo kuna aina kuu mbili za
mofu. Aina hizo za mofu ni;

(i) Mofu changamani

(ii) Mofu kapa

(i) Mofu changamani

Ni mofu inayoundwa kutokana na mwambatano wa mizizi miwili ambayo inaweza ikawa ni


mizizi sahihi miwili kama vile;

{Askari} + {Kanzu} = Askarikanzu

{Gari} + {Moshi} = Garimoshi

{Fundi} + {Chuma} = Fundichuma

Pia inaweza ikawa mofu funge + mofu huru

Mfano: {Mw-} + {-ana} + {nchi} = Mwananchi

{Mw-} + {-ana} + {hewa} = Mwanahewa


(ii) Mofu kapa

Ni mofu za pekee ambazo hazina umbo. Mofu kapa hazitamkwi wala kuandikwa. Mofu kapa
hazionekani katika neno lakini athari zinazotokana na mofu kapa hueleweka.

Mfano; Umoja wingi

U-kucha – ⱷkucha
U-kuta – ⱷkuta

U-funguo - ⱷfunguo

Nomino zilizo na kiambishi cha wingi tu cha umoja hakipo

Mfano; umoja wingi

ⱷkasha Ma – kasha

ⱷdebe Ma – debe

ⱷjembe Ma – jembe
Sifa za mofu

Mofu ni sehemu halisi ya neno.

Pia ni umbo amalo huweza kudhihirika kifonolojia yaani, kimatamshi linaweza kusikika na
kiothografia yaani, kimaandishi linaweza kuandikwa.

Mofu huakilishwa kwa ishara ya mabano.

Mifano

Watoto (wa)+ (toto)

Anasoma (a) (na) (so) (ma)

Baba (baba) mofu maja amabayo ni mofu huru n.k

Mofimu

Mofimu ni kipashio kidogo cha kisarufi kilicho na maana (Hockett, 1988). Ni tamko ndogo lenye
maana.

Booij (2012:8) anataja mofimu kama viungo vya kuundia maneno.

Kwa mujibu wa Matinde (2012:101) mofimu ni maana inayowakilishwa na mofu. Pia mofimu ni
dhana ambayo ni sehemu ya umilisi kwa watumiaji wa lugha husika.
Massamba na wenzake (2013), wanaeleza kuwa mofimu ni kipashio kidogo kabisa katika umbo
la neno kilicho amilifu yaani kilicho na kazi ya kisarufi au kileksia na ambacho hakiwezi
kuvunjwa au kugawanywa katika vipande vingine vidogo bila kupoteza maana au uamilifu wake.

Mofimu ni vipashio vidogo vya msingi vinavyotumika kuunda maneno ya lugha. Mofimu ni
vipashio vinavyoonyesha uhusiano uliopo kati ya sauti za msingi za lugha yaani fonimu na
maana maalumu katika sarufi ya lugha (Besha 1994).

Naye Kamusi ya TUKI (1990) anaeleza mofimu kama kipashio kidogo kabisa amilifu katika
maumbo ya maneno. Hii ina maana kuwa maneno huundwa kwa mofimu na kwamba kila
mofimu huwa na maana.

Crystal (1971), anasema kuwa mofimu ni kipashio kidogo kabisa katika lugha chenye maana
zaidi ya hayo, maana hiyo hutofautiana na zile za mofimu zingine katika lugha hiyo. Mambo
mawili yanabainika hapa. Kwanza ni kuwa ukiongeza au kupunguza mofimu kutoka tamko
fulani, bila shaka maana ya tamko itabadilika.

Crystal (1971) anaendelea kusema: Kuwa mofimu hiyo inazo sifa kadhaa zinazoibainika.
Kwanza, mofimu ni kipashio chenye umbo halisi. Mofimu ina umbo lake la kifonetiki. Pili,
mofimu huwa na maana. tatu, kila mofimu huwa na nafasi yake ya kisintaksia katika
(kushirikiana na vipashio vingine) Kuunda vipashio vikubwa zaidi.

Hivyo tunaweza kusema kuwa kabla ya kuasisiwa kwa sarufi zalishi dhana ya mofimu ilichukua
maana ya mofu kama ilivyojadiliwa katika sehemu iliyotangulia hapo juu. Lakini baada ya
kuasisiwa sarufi zalishi mofimu ina maana inayowakilishwa na mofu hivi kwamba mofimu ni
dhahania ambayo ni sehemu ya umilisi wa mtumiaji wa lugha husika kutokana na fasili hii
mofimu ni lie maana iliyowakilishwa na mofu. Kwa misingi ya mantiki mofu ni sehemu halisi,
hutamkika, huandikika na kuonekana ilhali maana mofimu ni dhahania na huwa imo akilini mwa
mtumiaji wa lugha husika.

Mofimu ina sifa zifuatazo.

(i) Mofimu ina umbo halisi


(ii) Ina umbo la kifonetiki

(iii) Huwa na maana

(iv) Ina nafasi ya kisintaksia katika kuunda vipashio vikubwa vya kisarufi.

kmf. neno mtoto lina mofimu {m} + {toto} {m}- mofimu ya ngeli ya /1/ {toto} - mzizi

Ilhali neno anasoma lina mofimu zifuatazo: {a} - {na} - {som} - {a}

nafsi - wakati - mzizi – kiishio.

Kuna aina kadha za mofimu.

(i) Mofimu Huru Ni mofimu zinazojisimamia kimaana na ambazo haziambatanishwi na


viambishi vingine. Zinakaa peke yake na zina maana kamili. Zinajitosheleza kimaana bila
kuunganishwa na viziada vyovyote kmf. kalamu, paka, taa. Aina hii ya mofimu hujitokeza kama
mofimu za kileksia na mofimu za kiwamilifu (Yule, 1985).

Mofimu za Kileksia Kundi hili huwa na maneno ya kawaida pamoja na vivumishi. Mofimu hizi
ndizo hubeba ujumbe au maana ya ujumbe katika sentensi kmf. Sungura, Nairobi, Kenya, kaka,
kalamu, simba nk.

Mofimu za Kiwamilifu Haya ni maneno yanayotenda kazi fulani katika lugha nayo huwa ni
viunganishi, vihusishi au vielezi. Tazama:

Viunganishi: lakini, aidha, bila, ilhali, lakini nk. Vihusishi: nje, ndani, juu, pekee, kwa nk.
Vielezi: sana, leo, saa tatu nk.

Kwa hivyo, Mofimu huru ni maneno halisi.

(ii) Mofimu Funge Mofimu funge haijitoshelezi kimaana bila viziada. Huambatanishwa na
viambishi vingine kuleta maana kamili. Hazikai peke yake na lazima ziunganishwe na mofimu
zingine ili zikamilike. kmf. kiambishi cha ngeli ya kwanza /m/ katika neno m-kora ni mofimu
funge. Hali ya mofimu hizi kukosa kujisimamia imepelekea wanaisimu kuziita mofimu
tegemezi. Zimegawanyika katika makundi mawili.
Mofimu Ambishi. Mofimu hizi ni viambishi ambavyo haviwezi kujisimamia na mara nyingi
havibadilishi mzizi wa neno. Kuna viambishi vifuatavyo:

mwanzo m-kulima kati a-li-tumbukiz-a mwisho som-ek-a (ek ni mofimu mwisho kabla ya
kiishio cha kibantu -a)

Mofimu Nominishaji: Hizi ni mofimu ambazo hutumiwa kuunda maneno mapya. Maneno
yaliyoundwa mara nyingi huwa katika kikundi tofauti na maneno asilia.kmf.

kitenzi nomino pika mpishi, mapishi, upishi ongoza kiongozi, mwongozo, uongozaji

(iii) Mofimu Tata Mofimu tata huwa na maana zaidi ya moja. kmf. panda, paa, tunda, mbuzi nk.

(iv) Mofimu Changamano Huelezwa katika mkabala wa muundo. Mofimu changamano ni


mofimu ambazo huundwa kwa kuweka pamoja angalau mashina au mizizi miwili ya maneno
ambayo kwa kawaida huwa huru kmf. mwanahabari, mwanasiasa, kiinuamgongo.

(v) Mofimu Kapa Hizi ni aina za mofimu ambazo hazidhihiriki kwani ni za kidhahania. Mofimu
kapa hazionekani katika neno. Mofimu hizi hatuzioni, hatuziandiki wala kuzitamka ijapokuwa
athari zake zinahisika na kueleweka kmf. Nomino za ngeli ya 9/10 katika lugha ya Kiswahili
huwa na mofimu kapa. Tazama: nguo – nguo (neno hili lina mofimu kapa kwani halibadiliki
katika wingi. Pia maneno kama vile samaki au maji ambayo yanapatikana katika ngeli ya 9/10.
Maneno mengine katika ngeli ya tano na sita (Ji/Ma) pia huwa na mofimu kapa katika umoja na
wingi; kmf. debe, kasha nk.

(vi) Mofimu Mzizi Mofimu mzizi ni ile sehemu ya mofimu ambayo haibadiliki na ambayo
hubeba maana ya kimsingi ya neno. Hii ni mofimu ambayo inatufafanulia maana ya neno na
mara nyingi mofimu za ziada huambatanishwa nayo katika unyambuaji. Tazama mfano ufuatao;
kutokana na mofimu mzizi pik (pik-a) tunapata pikapika , pikwa, kupika, pikiwa, pikiana nk.

Juu ya hizi aina za mofimu, Aidha Holt (1975) anatambua aina mbili za mofimu ambazo ni:
Mofimu huru na mofimu funge. Kulingana naye mofimu huru huweza kujisimamia peke yake na
kuwa na maana kamili kama neno. Lakini mofimu funge ni sharti ziambatanishwe na mofimu
zingine ili kuleta maana. Mfano neno mama lina mofimu moja kwa sababu haliwezi kugawa
katika vijisehemu vidogo vyenye maana na liiwa peke yake tunaelewa maana yake kikamilifu.
Neno mtoto lina mofimu mbili m-toto ambazo kila mojawapo ina maana-m- inawakilisha umoja
na –toto- ni mofimu ambayo ni mzizi. Hivyo kila mojawapo ya hizi mofimu imeundwa kwa
fonimu. Iwapo fonimu hizo zitabadilika basi maumbo ya mofimu yatabadilika.

Aidha Holt (1975) anaeleza kuwa baadhi ya mofimu funge huja kabla ya mzizi wa neno na
zingine hupatikana baada ya mzizi wa neno. Aidha kwa mujibu wake ni kuwa mofimu funge
zinatokana na mifanyiko ya kimofolojia ya unyambuaji na uambishaji. Anaeleza mofimu za
unyambuaji kama mofimu ambazo huwekwa kabla au baada ya mzizi na hulenga kuunda neno
jipya. Aidha mofimu hizo huweza kubadili kategoria ya kisarufi ya neno. Mfano neno imba lina
mofimu mbili imb-a na kategoria yake ya kisarufi ni kitenzi. Neno hili likiongezwa mofimu -wa-
kabla ya mzizi na mofimu -ji- baada ya mzizi –imba- tutaunda neno jipya mwimbaji ambalo
kategoria yake ya kisarufi ni nomino. Kwa upande mwingine mofimu za uambishaji ni zile
mofimu ambazo uongezewa kwenye mzizi wa neno hili kuongeza maana katika neno hilo bila
kubadilisha kategoria ya kisarufi ya neno. Mfano, katika neno mtoto m-ni mofimu ya umoja na -
toto ni mzizi wa neno. Mofimu wa- ikiwekwa kabla ya mzizi neno hili litakuwa watoto. Katika
hali hii neno mtoto litabakia kuwa nomino ila mofimu wa imeongezea maana ya wingi.
Ufafanuzi wa mofolojia na dhana za kimofolojia kama mofu na mofimu ni muhimu kwa utafiti
huu kwa kuwa mofolojia ni sehemu ya mofofonolojia.

Alomofu

Matinde (2012:100) Alomofu ni maumbo mawili au zaidi yanayowakilisha mofimu moja na


hutokea katika mazingira maalum ya utokeaji.

Besha (1994:55) anaeleza kuwa Alomofu za mofimu ambazo zinatokea katika mazingira
maalumu ya kifonolojia ya utokeaji wake unaweza kutabirika.

Hivyo basi, Alomofu ni maumbo mawili au zaidi yanayowakilisha mofimu ileile moja na
ambayo huweza kutokea katika mazingira maalum. Yaani ni maumbo au sura tofauti ya mofimu
moja.

Alomofu ina sifa mbalimbali.

(a) Umbo halisi ambalo ni sehemu ya neno.


(b) Ni mofu mojawapo ya mofu za mofimu moja.

Kanuni za alomofu katika kauli ya kutendeka.

Matinde (2012:192) anasema kuwa alomofu {-ik-} hutokea katika shina likiwa na irabu
mojawapo kati ya a, i au u na mzizi huo huishia na konsonanti ambayo huonyesha ubora wa
jambo fulani au uwezekano wa kitu kufanyika.

Mfano; {imb-} + //-ik-// + {-a} = imbika

{umb-} + //-ik-// + {-a} = umbika

{fany¬-} + //-ik-// + {-a} = fanyika

{pit-} + //-ik-// + {-a} = pitika

{tup-} + //-ik-// + {-a} = tupika

Habwe na Karanja (2007:110) anasema alomofu /-ek-/ hutokea iwapo mzizi wa kitenzi ndani
yake una irabu e au o na mzizi huo huishia na konsananti na huonyesha ubora wa kitu/jambo
kufanyika au uwezekano wa jambo fulani kufanyika.

Mfano; {jeng-} + //-ek-// + {-a} =jengeka

{pony-} + //-ek-// + {-a} = ponyeka

{chom-} + //-ek-// + {-a} = chomeka

{tosh-} + //-ek-// + {-a} = tosheka

{som-} + //-ek-// + {-a} = someka

{tek-} + //-ek-// + {-a} =tekeka

Mzizi
Mzizi kwa mujibu wa Massamba na wenzake (2001) ni kipashio ambacho ndicho kiini cha
maneno. Ni maumbo ambayo hayawezi kugawika tena katika sehemu nyingine bila kupoteza
uamilifu wake wa kuwa kiini cha maana.

"Mzizi wa neno" ni sehemu ya msingi ya neno ambayo inabaki baada ya kuondoa vifungu vya
kuanza au kuisha, kama vile awali au kikokotoo cha neno. Katika lugha nyingi, neno linaweza
kuundwa na mzizi wa neno pamoja na vifungu vingine kama vile viambishi, ambavyo hutumika
kuonyesha muda, nafsi, umoja/ wingi, na kadhalika.

Kwa mfano, katika neno "kutembea," mzizi wa neno ni "tembea." Ikiwa tunapata maneno kama
"ninaenda kutembea" au "alitembea," bado mzizi wa neno ni "tembea." Mfano mwingine ni
katika umbo pig. Neno hili ni mzizi katika maneno kama pigana, pigwa, pigia, kupigiwa nk

Mzizi wa neno lolote huwa na sifa zifuatazo

Kwanza, mzizi wa neno lolote ni mofu muhimu zaidi kuliko mofu nyingine tena katika neno kwa
kuwa mzizi wa neno huwa kama mhimili wa neno yaani ndiyo sehemu inayolifanya neno
lisimame au liwe neno.

Sifa nyingine ni kwamba, mzizi hauwezi kuondolewa katika neno. Mfano katika neno cheza,
mzizi ni chez na ukiondoa mzizi neno halitabaki.

Mzizi pia unauwezo wakati mwingine wa kukaa peke yake kama neno kamili. Kwa hivyo, neno
linaweza kuwa halina kiambishi chochote lakini kila neno lazia liwe na mzizi

Mizizi fulani inaweza kuwekwa Pamoja kuunda mizizi changamano

Kwa mfano mzizi paza+sauti neno = pazasauti, amri+jeshi=amrijeshi.

Mzizi wa neno ni msingi wa lugha ambao unaweza kubadilishwa au kuongezewa viambishi na


maneno mengine ili kuunda aina tofauti za neno, kama vile nomino (kutembea), vitenzi
(tembea), majina ya sifa (tembelezi), na kadhalika.

Sifa nyingine ya mzizi ni kwamba, miziziz huwa haibadilikibadiliki yaani umbo la mzizi ni moja
tu na haiongezeki wala kupungua. Viambishi ndivyo vinavyoongezwa kwa mzizi na
vinapoongezwa havibadilishi umbo la mzizi. Mfano mzizi kama imb, tunapata imba, imbisha,
imbishaji, imbika nk. Mzizi kama -j- tunapata kuja, siji, hakuja nk

Aina za mizizi

Kuna mizizi ya aina mbili yaani mizizi huru nz mizizi tegemezi.

Mizizi huru ni mizizi ambayo inaweza kusimama peke yake bila viambishi vyovyote na ikawa na
maana kamili. Mifano hapa ni halafu, mama, nywa nk

Mizizi tegemezi ni aina ya mizizi ambayo haijitegemei yaani ni lazima kuwekwe kiambishi
kimoja ndipo neno lilete maana inayoeleweka yaani ikiwa peke yake haileti maana. Mfano ya
mizizi kama hii ni la, ja, fa, kita nk
Uundaji wa maneno

Kwa mjibu wa Matinde (2012), uundaji wa maneno ni mabadiliko ya istilahi na muundo


unaosababishwa na mabadiliko ya sayansi na tekinolojia katika nyanja mbalimbali za jamii ili
kukidhi dhima ya lugha kama chombo kinachojitosheleza katika mawasiliano. Ili kukidhi haja hii
kuna mbinu mbalimbali zinazotumika katika uundaji na ukuzaji wa istilahi ya maneno katika
lugha.

Hivyo basi uundaji wa maneno ni ujenzi au uzalishaji au utengenezaji wa maneno mapya.


Uundaji wa maneno mapya husaidia kuongeza msamiati katika lugha ili kukidhi mahitaji ya
mawasiliano. Uundaji wa maneno mapya husababishwa na mabadiliko ya kiuchumi, kisiasa,
kiutamaduni na maendeleo ya kisayansi yanayotokea katika jamii. Kwa mfano tunayo maneno
mapya kama vile ufisadi, uwekezaji, ujasiriamali, ukeketaji na mengine mengi kutokana na
mabadiliko ya kijamii.

Katika uundaji wa maneno tutajifunza kuhusu mbinu ya kuunda msamiati na istilahi mpya za
Kiswahili. Mbinu hizi ni kama zifuatazo;

Mwambatano, unyambuaji, ukopaji, ufupishaji, kubuni, kuradidi, ugeuzaji, uhamishaji, muigo au


utumiaji wa tanakali za lugha.

Mwambatano
Mbinu hii inahusu kuunganishwa kwa maneno mawili ili kuzua neno moja lenye maana mpya

Tofautu na maneno yaliyoundwa. Maneno haya yanaweza kuwa nomino na nomino nyingine,
nomino na kivumishi, nomino na kitenzi au kitenzi na nomino na kadhalika

Hapa chini ni jinsi tutakavyoona kwenye mifano.

Nomino na nomino

Mwana + Jeshi = Mwanajeshi

Duara + Dufu = Duaradufu

Mwana + Kondoo = Mwanakondoo

Bata + mzinga = Batamzinga

Nomino na kivumishi,

Mja +mzito = Mjamzito

Pembe + nne = Pembenne

Chungu + nzaima = Chungunzima

Nomino na kitenzi au kitenzi na nomino

Nukta + tuli = Nktatuli

Pima + mvua = Kipimamvua

Change + moto = Changamoto

Chemsha + bongo= Chemshabongo

Fungua + mimba = Kifungua mimba

Unyambuaji

Ni maneno yanayoweza kunyambuliwa kwa kuongeza au kupachika viambishi awali na tamati ili
kupata maneno tofauti kwa kutumia mzizi
Mfano

Pik-pika, pikia, pikiwa, pikika, mpishi. Katika maneno haya, mzizi wa kitenzi ni “pik” sauti
/a/, /iwa/, /ika/, /shi/ mfululizo ni viambishi tamati ambavyo vimeongezwa kwa mzizi /pik/ na
kuunda maneno mapya na sauti /m/ katika neno mpishi ni kiambishi tamati.

Kitenzi na nomino

Tafiti Utafiti/mtafiti

Chuma Uchumi

Soma Msomi/masomo

Ufupishaji

Rubanza (1996) anaeleza kuwa baadhi ya majina ya maneno katika lugha nyingine za dunia
hutokana na ufupishaji wa maneno yanavyotumiwa kwa pamoja kwa kutumia herufi au silabi za
mwanzo tu za maneno hayo. Njia hii ameita Akronimu.

Matinde (2012) anaeleza kuwa ufupishaji ni mbinu ambayo hutokana na kitenzi ‘fupisha’ chenye
maana ya kufanya kitu kiwe kifupi au kupunguza urefu wa kitu.

Kuna mbinu kadhaa zinazotomika katika kufupisha maneno ukapata mapya

Ufupishaji mkato

Akronimu

Uhulutishaji

Ufupishaji wa mkato

Matinde, (2012) anatofautiana na Rubanza (1996) kwa kuongeza mbinu nyingine ya ufupishaji
ambayo ni ufupisho mkato. Katika mbinu hii baadhi ya vipashio au silabi hudondoshwa na
kuacha sehemu tu ya neno asilia.

Mifano
Daktari- Dkt

Bwana- Bw

Bibi- Bi

Akronimu

Kwa mfano katika Kiswahili tuna maneno ambayo yametokana na herufi au silabi za mwanzo za
maneno kama vile;

UKIMWI -Ukosefu wa kinga mwilini

UVIKO-19-Ugonjwa wa virusi vya korona

TUKI -Taasisi ya kinga mwilini

Uhulutishaji

Huu ni ufupishaji wa virai, mfano katika lugha ya Kiswahili tunaweza kupata maneno kama vile

Chakula cha jioni Chajio

Mtu asiye na baba Msibaba

Maziwa lala Mala

Rununu maninga Runinga

Taja vijisehemu vilivyowekwa pamoja si lazima viwe mwanzoni mwa maneno kama vile
kwenye rununu maninga

Ukopaji

Kukopa ni mbinu inayotumiwa na lugha zote za ulimwengu kurutubisha msamiati wake.


Kiswahili kimeazima maneno kutoka kwa lugha za Kiarabu, Kiingereza, Kifaransa, Kihindi,
Kijerumani na hata lugha za Kiafrika

Mfano
Lugha asili maneno ya mkopo

Kihindi - pesa, bima, laki, godoro

Kituruki - baruti, bahasha, korokoroni

Kijerumani - hela, barawani, shule

Kiarabu - rehema, faraja, alhamisi

Kikuyu - matatu, githeri

Kiingereza - daktari, mei, kampuni

Kwa hivyo hakuna lugha ambayo hujikamilisha, lugha huwa zinaombana na kukopa- pia maneno
ya kibantu pia huwezwa kukopwa- ukopaji ua aina nyingi kwa mfano

Aina za ukopaji

Kukopa kwa tafsiri

Tafsiri ni uhawilishaji (uhamishaji) wa mawazo, ujumbe, au taarifa iliyopo katika maandishi ya


lugha moja (chanzo kuenda kwa lugha lengwa bila kupoteza maana ya msingi na mtindo
uliotumika katika matini chanzi.

Mifano

Kiingereza Kiswahili

Free Market Soko huria

Rulling Party Chama tawala

Opposition Party Chama cha upizani

Commissioner General Kamishena mkuu n.k

Ubora wa mbinu hii.


Mbinu hii huzingatia kigezo cha maana zaidi kuliko muundo wa maneno yaliyochukuliwa toka
lugha chanzi na kutafsiriwa huafiki utamaduni wa lugha lengwa. Hali hii husaidia katika kuunda
maneno yenye maana iliyo wazi na inayokubalika katika lugha lengwa.

Udhaifu wa mbinu hii.

Mara nyingi huwa vigumu kutafsiri baadhi ya maneno kutoka lugha chanzi kwa kufuata kigezo
maana.

Kuna uwezekano wa kupata tafsiri ambazo hazina maana wala mantiki katika lugha lengwa

Kukopa sisisi

Huu ni ukopaji wa moja kwa moja. Hapa maneno yanachukuliwa yalivyo katika lugha asili na
kutumiwa katika lugha kopaji

Lugha asili Neno

Kipare Kitovu

Kinyamwezi Ikulu

Kikuyu Githeri

Luyha Nyuni

Utohozi

Ni mbinu ambayo maneno kutoka lugha chanzi hutoholewa toka lugha chanzi na hatimaye
hufanyiwa marekebisho kwa kufuata kaida au sheria za kifonolojia na kimofolojia za lugha
pokezi kabla ya kutumiwa. Neno linapotoholewa hutamkwa na kuandikwa kwa utaratibu wa
lugha pokezi, hata hivyo maana ya neno lililotoholewa hubakia ileile ya awali. (Matinde, 2012)

Kiingereza Kiswahili

Doctor Daktari

Agenda Ajenda
Budget Bajeti

Dollar Dola

Office Ofisi

Maneno kutoka lugha nyingine yanapotoholewa hubadilishwa kimatamshi ili yafuate kanuni za
lugha husika.

Katika lugha ya Kiswahili maneno yanayotoholewa hayana budi kusanifishwa na baraza la


Kiswahili la Taifa ndipo yaruhusiwe kutumiwa rasmi.

Ubora wa mbinu hii:

Mbinu hii ya utohozi ni mbinu rahisi ya kutumiwa katika uundaji wa msamiati. Mzungumzaji
yeyote anaweza kutumia mbinu hii hata bila kuhudhuria kozi yoyote ya isimu au kufundishwa.

Maneno mengi huweza kuundwa kwa kutumia mbinu hii ili kukidhi mahitaji ya matumizi katika
lugha mbalimbali.

Udhaifu wa mbinu hii:

Mbinu hii hulemaza ubunifu wa wanajamii katika kuunda msamiati mpya wenye kuakisi
utamaduni wa jamii husika.

Lugha tohoaji huonekana kukosa uasilia yaani lugha huonekana kuwa chotara.

Baadhi ya maneno katika Kiswahili ambayo yametoholewa kutoka lugha ya Kiingereza katika
lugha ya Kiswahili hutamkwa kwa namna tofauti kabisa.

Kubuni

Matinde (2012) anasema ubunifu ni mbinu ya kubuni msamiati katika lugha husika na kurejelea
dhana au vitu vipya ambavyo hapo awali havikuwepo katika jamii husika. Ni mbinu ambayo
hutumiwa badala ya kuchukua maneno kutoka lugha nyingine. Mfano kubuni kwa kuongozwa na
vigezo maalum kama ifuatavyo:-

Uakisi wa umbo la kurejelewa


Pembetatu hurejelea umbo kwenye pembe tatu

Uakisi wa sauti au mlio

Pikipiki-pik-pik—pik—pik

Uakisi wa tabia

Kifaurongo Uakisi wa tabia ya mdudu huyu-mdudu ambaye hujifanya amekufa ilhali hajafa

Tuktuk- Tuk—tuk-tuk-tuk

Kuradidi

Hii ni mbinu ya kurudia neno au sehemu ya neno ili kuleta maana mpya

Mfano

Mbali Mbalimbali

Pole Polepole

Sawa sawasawa

Kizungu Kizunguzungu

Pilka Pilkapilka

Kwa ujumla uundaji wa maneno hupanua mipaka yake ya matumizi kwa kuongeza msamiati.
Lugha nyingi ikiwemo lugha ya Kiswahili hutohoa baadhi ya msamiati kutoka lugha nyingine za
dunia kutokana na mwingiliano wa watu. Lakini hata bila kutohoa maneno kutoka lugha
nyinginezo kila lugha ikiwa pamoja na lugha ya Kiswahili kuna njia mbalimbali zitumikazo
katika kukuza msamiati wake.
MAREJELEO.

Besha, R.M. (2007). Utangulizi wa Lugha na Isimu. Dar es Salaam: Macmillan Aidan Ltd
Cambridge: Cambridge University Press.

Habwe, J. & Karanja, P. (2007). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers.

Hartman, R. 1972: Dictionary of Language and Linguistics. London: Applied Science Publisher.

Hockett, C. F. 1958: A Course in Modern Linguistics. Newyork: Macmillan.

Katamba, F. (1993). Morphology. London: Macmillan Press Ltd.


Kenya: Longhorn Publishers.

Masebo, J. A. (2010). Nadhari ya Lugha Kiswahili 1. Dar-Es Salaam: Nyambari Nyangwine

Massamba, D.P.B na Wenzake. (2013). Fonolojia ya Kiswahili Sanifu. Dar es Salaam: TUKI

Matinde, R.S. (2012). Dafina ya Lugha Isimu na Nadharia: Kwa Sekondari, Vyuo vya Kati na
Vyuo Vikuu. Mwanza: Serengeti Educational Publishers (T) Ltd.

Matthews, P. 1974: Morphology: An Introduction to the Theory of Word Structure.

Mdee, D. (2007). Nadharia za Leksikografia. Dar es Salaam: TUKI.


Mgullu, R.S. (1999). Mtalaa wa Isimu, Fonetiko, Fonolojia na Mofolojia ya Kiswahili. Nairobi

Nida, E. A. 1949: Morphology: The Descriptive Analysis of Words. Michigan: Michigan


University Press.
Publisher.

Rubanza,Y. I.(1996). Mofolojia ya Kiswahili. Dar-Es Salaam: Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania.
TUKI. (1990). Kamusi ya Isimu na Lugha. Dar es Salaam: TUKI
Vyuo Vikuu. Mwanza: Serengeti Educational Publishers.

Yule, G. 1985: The Study of Language. Cambridge: Cambridge University Press.

You might also like