SIKU YA KUKUMBUKA KUSHUKA KWA ROHO MTAKATIFU (PENTEKOSTE) WAZO LA WIKI: ROHO MTAKATIFU NGUVU YETU ZABURI 143:1-12; EFESO 1:13-14 SOMO LA MAHUBIRI: YOHANA 20:19-23 WIMBO: TMW 136
Tofauti na injili nyingine, injili ya Yohana
inaeleza habari za kufufuka kwa Yesu na jinsi alivyoendelea kujidhihirisha kuwa yupo hai. Katika Sura hii ya 20:1-10 ni habari za kufufuka kwa Yesu. Yohana 20:11-18 ni habari za Yesu kumtokea Mariamu Magdalena. Ambaye anaonekana kuwa ni shuhuda wa kwanza kumwona Yesu mara tu baada ya kufufuka! Yohana 20:19-23 ambalo ndilo somo letu la mahubiri, ni habari za Yesu kuwatokea wanafunzi wake 10: Yuda Iskariote akiwa alishajinyonga, na Thomaso hatuambiwi alikwenda wapi. Yohana 20: 24- 25 ni habari za Thomaso ambaye hakuwepo wakati Yesu anawatokea wanafunzi wengine anarudi na kusimuliwa kuwa Yesu amewatokea, alikataa na kusema hataamini mpaka aguse maeneo yaliyoumizwa wakati akiwa msalabani. Hayo yote yalitokea siku ya kwanza ya juma, yaani Jumapili.
Yohana 20:26-29, siku nane baadaye Yesu
aliwatokea wanafunzi wake na Thomaso akiwepo. Hapa Yesu alimpa Thomaso fursa ya kwenda kugusa makovu ambayo alisema angeamini ikiwa atagusa. Lakini Thomaso alikataa na kudhihirisha kuwa ameamini. Na Yohana 20:30-31 ni jumlisho juu ya sababu au lengo la kuandikwa kwa injili ya Yohana, na lengo kuu likiwa ni kusisitiza juu ya Uungu wa Yesu.
Katika somo letu la mahubiri tulilopewa
kutafakari siku ya leo, tunapata habari za Yesu kuwatokea wanafunzi 10: Yuda Iskariote alishajinyonga, na Thomaso hatuambiwi alikwenda wapi. Tukio hili lilitokea siku ile ile ya kufufuka kwa Yesu, jioni wanafunzi wakiwa wamejifungia kwa hofu ya Wayahudi kwamba baada ya kusulibiwa kwa Yesu wangeendelea kuwatafuta wanafunzi wake. Yesu aliwatokea chumbani humo ingawa milango ilikuwa imefungwa. Jambo hili liliwashtua sana wakifikiri kwamba walio na pepe aliyeweza kupita ukutani, lakini Yesu aliwatuliza hofu yao baada ya kuwaonesha mikono yake na ubavu wake. Kisha tunaona Yesu akiwakabidhi wanafunzi wake huduma ya kupeleka ujumbe wake kwa mataifa yote. Yaani baada ya kupokea roho Mtakatifu wangekuwa wajumbe wake duniani kote.
Wapendwa, Siku hii ya kwanza ya Juma, siku
ya kufufuka kwa Yesu ni siku ambayo kanisa lilipewa uvuvio wa Roho Mtakatifu. Yesu aliahidi kuwa akija huyo atawafundisha, atawakumbusha sio tu maneno bali hata matendo ya Yesu. Na leo ni sikukuu ya Pentekoste, siku ya kukumbuka kushuka kwa Roho Mtakatifu. Pentekoste ya mwaka jana (28/05/2023) tulitafakari juu ya Roho Mtakatifu msaada wetu. Mwaka huu wazo tulilopewa, linatuongoza kumtazama Roho Mtakatifu kama nguvu yetu. Matendo ya Mitume 1:8 Lakini mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu. Bila shaka huu ni upako wa utumishi unaokuja juu yetu. Maana yake bila Roho Mtakatifu, hatuna nguvu za kufanya huduma ambayo tumepewa. Efeso 3:20 Kwa sababu ya nguvu ya Roho Mtakatifu ndani yetu inamfanya Mungu afanye mambo makubwa kuliko tuombayo, na tuwazayo.
Rumi 8:26 Roho Mtakatifu ndani yetu
anatuwezesha kuomba kama atakavyo Mungu. Roho Mtakatifu ndani yetu anatupa nguvu ya kuishi maisha matakatifu (Rumi 8:8-9, 14). Hutushuhudia kuwa sisi ni Watoto wa Mungu (Rumi 8:16). Roho Mtakatifu ndani yetu ni msaidizi (Yohana 16:7). Anatupa nguvu ya kutambua dhambi (Yohana 16:8). Roho Mtakatifu juu yetu ni kwa ajili ya utumishi, kudhihirisha uweza wa Mungu (Mdo 1:8).
Wapendwa; ni jambo la kushangaza nyakati za
leo, yapo mafundisho potofu ya kutaka Roho Mtakatifu aonekane kama nguvu ya kummiliki, na kumweka katika vitu na vitu hivyo kusimama badala yake, mfano maji ya upako, mafuta ya upako, chumvi ya upako, mchanga wa upako. Hivi ni vitu ambavyo havitakiwi kuchukua nafasi ya Roho Mtakatifu. Na kwa bahati mbaya mahali pengine vitu hivi vinauzwa. Watu wamenunua na vikachukua nafasi ya Yesu au Roho Mtakatifu.
Kwahiyo wapendwa; ni muhimu kuwa
tunapokumbuka kushuka kwa Roho Mtakatifu, tukumbuke kumwomba Mungu atufumbue macho ili tutambue kweli yake na hatimaye tuishi katika kweli hiyo. Mungu atubariki. Amen