Siku za hivi karibuni mpaka sasa tumeendelea kusikia taarifa
mbalimbali za matendo yanayokiuka maadili yetu kama taifa. Si utamaduni wetu wala taifa halijawahi kufundisha mahala kwasababu tukisoma miongozo mbalimbali ya elimu hakuna sehemu tunaweza kuyapata mafundisho yenye kuvunja maadili yetu, ni mambo ya kushangaza na ya aibu katika jamii zetu.
Nilizungumza na mzee John Mollel kupata maoni yake kuhusu
masuala haya kujitokeza zaidi nyakati hizi. Yeye kwa upande wake akahusisha mambo haya na imani za kishirikina anasema “haiwezekani baba mzazi kumlawiti mwanaye bila imani za kishirikina, kwasababu siyo mambo ambayo tumekua tukiyaona tangu utoto wetu” Wengine wanadai uasi juu ya Mungu ni mkubwa pamoja na kwamba, tunazo nyumba nyingi za ibada. Wengine wanadai ni mmomonyoko wa maadili kutokana na utandawazi, mitazamo juu ya masuala haya ni mingi.
Lakini wakati haya yakiendelea mnamo tarehe 13 February 2023
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda akajitokeza mbele ya waandishi wa habari akiwa na orodha ya vitabu 16 alivyovipiga marufuku kwa mamlaka aliyopewa chini ya kifungu cha 59 cha Sheria ya Elimu sura 353 ili visitumike katika shule za umma wala binafsi. Akaeleza kuwa vitabu hivyo vina maudhui yanayokinzana na mila, desturi na utamaduni wa Mtanzania na vinahatarisha malezi bora ya watoto na vijana wetu.
Baadhi ya vitabu hivyo ni Diary of a Wimpy kid-cabin, Diary of a
Wimpy kid, Diary of a wimpy kid-Rodrick Rules, Diary of wimpy kid-Last Straw, Diary of wimpy kid-Dog days, Diary of wimpy kid-The ugly Truth. Vingine ni Is for TRANSGENDER, Is for LGBTQIA na Sex Education a Guide to life. Prof.Mkenda hakuishia hapo tu lakini pia akatoa namba za simu ikiwa vitabu kama hivyo vitaonekana mahala popote basi watu waweze kutoa taarifa katika kupitia zifuatazo 02622160270 au 0737962965. Mwisho akamaliza kwa kuwaomba wazazi na walezi kufuatilia kwa karibu kubaini kama aina ya vitabu hivyo vitatumika au vingine vyenye maudhui kama hayo. Taarifa hii ikanifanya nipate maoni ya baadhi ya watu, mmojawapo ni Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi ndugu Joseph Selasini ambaye kwa maoni yake kwanza, alieleza umuhimu wa nchi kulinda ustaarabu wake kwa maana ya maadili kama, pili akawa na maswali kadhaa ambayo anasema waziri alipaswa kuyajibu katika maelezo yake.
Swali la kwanza vitabu hivyo viliingiaje nchini? Je, vilipitia uwanja
wa ndege au bandarini?, licha ya kuingia nchini viliingiaje mashuleni? Je, ni shule gani za Serkali au binafsi? je, idara ya ukaguzi Tanzania imekufa? Au wanakagua nini? Kama wanakwenda kukagua huwa hawakaguwi vitabu vya kufundishia? Je idara ya usalama wa taifa kazi yake ni kulinda viongozi tu? Je wakati wa uingije wake TRA walipokea kodi bila kukagua na kama walikagua waliruhusuje ikiwa vinakwenda kuharibu maadili ya watoto wetu?
Selesini aliendelea kuhoji kwanini shule hazikutajwa, je watoto
walipewa vitabu na nani? Kama vilikutwa mashuleni kwanini hizo shule hazikutajwa ili kuondoa sintofahamu? Je wakati watoto wanavitumia uongozi wa shule na walimu kwa ujumla hawakujua kama havistahili? Mwisho ndugu Selesini akatoa ushauri kwa Serikali kwamba kuna umuhimu wa kubaini wale wote waliohusika kuhakikisha vitabu hivyo vinatumika mashuleni wanajulikana na hatua kali zichukuliwe dhidi yao na akaongeza kuwa wao kama chama cha NCCR-Mageuzi wanapinga vikali masuala hayo kwasababu yanakwenda kuharibu maadili na utamaduni wa kitanzania.
Kwa maoni yangu nadhani bado kuna jambo kubwa la kufanyika
taarifa juu ya kufungia vitabu tu haitoshi kama alivyohoji ndugu Selasini hapo ni jambo zito hilo. Lazima tathimini na uchunguzi wa kina ufanyike kubaini athari za vitabu hivyo, vimeshaathiri watoto kwa kiasi gani? Tangu vimeanza kutumika vina muda gani? Je madhara yake ni makubwa kiasi gani ili tusije kuwa tunahangaika na matawi, wakati mizizi ilisha mea zamani pengine inawezekana tuhuma za baadhi ya shule kuhusika na uchafu huo ni matokeo ya vitabu hivyo.
Kutaja majina ya shule ilikuwa na tija zaidi kwasababu ingesaidia
wazazi kuhamisha watoto wao katika shule hizo, kwasababu maadili na malezi ni muhimu zaidi kuliko biashara ya mtu. Hatuwezi kukubali watoto wetu waharibike kwa kufanikisha biashara za mtu, kutotaja majina ya shule maana yake wazazi wataendelea kupeleka watoto wao katika shule hizo bila kujua. Kama shule inafikia hatua ya kufundisha au kukubali vitabu vya aina hiyo vitumike, maana yake watoto wameshafundishwa mengi zaidi. Kwahiyo pamoja na uchunguzi wa vitabu, ufanyike uchunguzi wa kidaktari juu ya watoto wote wanaosoma kwenye shule zilizokutwa na vitabu hivyo.
Kama tutaona haya kuyakemea mambo haya waziwazi maana
yake tunaandaa taiba la ajabu sana, tutapoteza nguvu kazi ya taifa hili, hatutakuwa na vijana wenye uwezo wa kuijenga nchi kwa hapo baadaye, na hapa walegwa zaidi ni watoto wa kiume, tukatae ujinga huu kwa vitendo ni bora tule nyasi kuliko kukubali taifa liangamie.
Mwisho nimshukuru waziri mwenye dhamana kwa hatua
alizochukua, lakini hatua zaidi zinahitajika. Kwa upande wa wazazi nao ni muhimu kulinda watoto wetu, tusiamini sana shule wanakosoma kwasababu matendo haya sasa yanafanywa popote, tuliyokuwa tunawaamini nao siku hizi wanatuhumiwa, hata nyumbani tusiaminiane sana maana unyanyansaji wa kijinsia umekuwa ukifanywa na watu wa karibu kabisa, ambao huwezi kuamini unakuja kushtuka mtoto alishaharibiwa.
Lakini kama jamii lazima tutafakari kwa kina tumepatwa na nini?
Kwanini matukio haya yanaongezeka kwa kasi zaidi? Tunataka kuifanya nchi hii kuwa Sodoma na Gomora? Hatuoni kama tunamkosea Mwenyezi Mungu? Tunalalamika mvua hakuna kwa maasi kama haya neema itatoka wapi? Mashirika yachunguzwe ikiwa ni pamoja na fedha wanazopewa tukiacha holela tu tutaangamia.
0689157789 magabilomjalifu@gmail.com DAR ES SALAAM-TANZANIA