Download as pdf or txt
Download as pdf or txt
You are on page 1of 68

NIDHAMU YA PESA

Mbinu za Kuhakikisha Pesa Unazopata


Hazipotei Kwenye Matumizi Usiyoyapanga

Joel Nanauka
©2023 Joel Nanauka

Haki zote zimehifadhiwa. Huruhusiwi kunakili,


kudurufu au kutumia sehemu ya kitabu hiki bila idhini
ya mwandishi. Kufanya hivyo itakuwa ni ukiukwaji wa
haki za mwandishi, na ukiukwaji wa taratibu hii
unaweza kupelekea mashitaka toka kwa waandaaji
wa kazi hii.

Joel Arthur Nanauka


P.O.Box 34743, Dar es salaam
Simu: +255 756 094875 / 0745 252 670
Barua pepe: jnanauka@gmail.com
www.joelnanauka.com

Kimesanifiwa na Andrew Rwela


Simu: 0743 200 738
Barua pepe: rwelaandrew@gmail.com
Yaliyomo

Dalili 6 Zitakazokuonesha Kuwa Hali Yako Ya 01


Kifedha Iko Kwenye Hatari

Mbinu 5 Za Kutumia Ili Pesa Zako Zisipotee. 09

Epuka Tabia Hizi 7 Zinazopoteza Pesa Za Watu


Wengi. 21

Maswali 5 Ya Kujiuliza Kabla Haujatumia Pesa 37


Yoyote
Utangulizi

Utafiti uliowahi kufanywa na Benki ya Standard


Chartered iliyoko nchini Uingereza, ulionesha kuwa ni
5% tu! ya wastaafu waliowahi kufanya kazi maisha
yao yote huwa wanakuwa na hali nzuri ya kiuchumi
baada ya kustaafu.

Bila kujali kiwango cha pesa walichokuwa wanalipwa,


ilionekana kuwa 95% ya wastaafu baada ya miaka 3-5
ya kustaafu kwao, huwa wanajikuta wakiwa na hali
ngumu sana ya kifedha.

Wengi wao walifanya kazi mfululizo kwa muda wa


miaka 30-40 na walikuwa wakiingiza pesa kila mwezi,
ila pesa hizo zilipotea na hazikuwasaidia kuishi vizuri
baada ya kustaafu.

Angalia na wewe usije ukawa mmoja wao!

Pesa huwa inamkimbia mtu asiyekuwa na nidhamu


na huwa inamkimbilia mtu mwenye nidhamu. Wale
wenye pesa kidogo ila wana nidhamu, wana uwezo

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | i


mkubwa wa kufanikiwa kuliko wale wenye pesa
nyingi ila hawana nidhamu.

Kwenye mafanikio ya kifedha yanahitajika mambo


matatu makubwa: Maarifa ya kifedha (Financial
Intelligence), Mpango wa Kifedha (Financial Plan) na
Nidhamu ya Kifedha (Financial Discipline).

Viwili vya kwanza vinakupa mwanga na njia ya


kufanya, ila nidhamu ya kifedha ndio inakuwa uwezo
wa kufanya uliyoyajua.

Kumbuka kuwa, wakati mwingine unachohitaji sio


kuwa na kipato cha ziada, bali unahitaji nidhamu ya
ziada. Usipokuwa na nidhamu ya ziada kuhusu pesa,
basi wanaofadika na pesa zako ni watu wengine.

Hata ukiongezewa mshahara mara dufu au


ukaongeza faida ya biashara zako mara dufu, kama
haujajenga nidhamu ya kutumia pesa zako, basi
itakuwa ni changamoto kubwa sana kwako
kufanikiwa kifedha.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | ii


Karibu tujifunze namna ya kujenga nidhamu ya pesa.

See You At The Top

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | iii


Sura Ya Kwanza

Dalili 6 Zitakazokuonesha
Kuwa Hali Yako Ya Kifedha
Iko Kwenye Hatari

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 1


Mara nyingi matatizo ya kifedha yanasababishwa na
kutumia zaidi ya unavyoingiza, kupungua kwa kipato
chako wakati majukumu hayajapungua au
kuongezeka majukumu wakati kipato chako
hakijaongezeka.

Kwenye changamoto ya kifedha unayopitia leo, je


unadhani ni kipi kati ya haya matatu ambacho
kitakuwa kimechangia zaidi?

Unapokuwa kwenye matatizo ya kifedha au


unaelekea kwenye matatizo ya kifedha, huwa kuna
dalili unaweza kuziona.

Ukipuuzia dalili hizi, unaweza kujikuta unaingia


kwenye matatizo makubwa ambayo itakuwa ngumu
sana kwako kujitoa:

Dalili Ya Kwanza: Unakopa Mara Kwa Mara Kwa


Mahitaji Ya Msingi.

Ni kawaida kabisa kwa mwanadamu kupata


changamoto za kifedha, ila ukiona changamoto zako
zinajirudia rudia kila wakati, ujue kuna tatizo.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 2


Ukiona kila wakati unakopa kwa ajili ya mahitaji ya
msingi kama vile:

Una madeni mengi ya chakula dukani, unadaiwa sana


mavazi (nguo, viatu n.k), kila ikifika wakati wa kulipa
kodi lazima ukope, kila wakati wa kupeleka shule
lazima ukope ada ya watoto n.k

Hapa sizungumzii jambo ambalo huwa linatokea


mara moja moja tu, bali lile ambalo huwa linatokea
mara kwa mara.

Dalili Ya Pili: Haujui Pesa Zako Zinaenda Wapi.

Umekuwa muajiriwa kwa miaka mingi sana,


umekuwa ukilipwa mshahara. Na mshahara wako wa
leo sio ule wa zamani.

Lakini ukiangalia maisha yako, ni kama hayabadiliki.


Ukijaribu kujumlisha pesa zote ambazo zimepita
mkononi mwako tangu ulipoanza kulipwa mshahara,
hauwezi kujua zimeenda wapi.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 3


Tangu umeanza kufanya biashara ni muda sasa, ila
ukiangalia faida unayopata kwenye biashara yako
hauwezi kujua imeenda wapi.

Yaani ukiangalia pesa ulizowahi kushika, ukiulizwa


zimefanya nini, haujui, ukiona hii dalili basi ni ya hatari
sana.

Dalili Ya Tatu: Unakopa Ili Kulipa Madeni.

Zamani ulikuwa unakopa pesa kwa ajili ya kutatua


matatizo fulani yaliyokuwa yanakukabili, ila kwa sasa
umeanza kukopa pesa ili ulipe madeni. Yaani
unatatua deni ila kwa kutengeneza deni lingine.

Ukiona umeanza tabia ya kukopa kwa mtu mmoja ili


ukamnyamazishe mtu mwingine, tayari ni dalili
inayotakiwa kukuamsha, kuwa kuna tatizo kwenye
eneo lako la pesa.

Dalili Ya Nne: Unaishiwa Kabla Ya Mwisho wa Mwezi.

Hii haswa ni kwa wafanyakazi, yaani wewe kila mwezi


pesa zako huwa zinaishia njiani. Ingawa mshahara

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 4


unaolipwa huwa unaambiwa ni kwa ajili ya mwezi
mzima, ila wewe huwa unaishia njiani kabla mwezi
haujafika.

Kuna watu kwenye ofisi zao huwa wanajulikana kwa


kuomba “Salary Advance”, yaani haiwezi kuvuka
miezi miwili kabla hawajaomba kutanguliziwa
mshahara.

Wengine huwa wanakopa kila mtu ofisini wakiwaahidi


kuwa watawalipa mwisho wa mwezi.

Yaani, kuna watu ambao kabla mshahara haujaingia


kwenye akaunti yao, tayari umeshaisha. Ukiona
unaishi kwa namna hii, basi endelea kusoma kitabu
hiki kwa sababu kuna nidhamu unahitaji kuzijenga.

Dalili Ya Tano: “Stress” Zako Nyingi Zinatokana na


Pesa.

Ni kweli kila mtu huwa anapitia “Stress”, ila wewe


ukijichunguza, kila wakati stress zako huwa
zinatokana na mambo yanayohusiana na pesa.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 5


Kuna watu wengi wazuri ambao umewapoteza
kwenye maisha yako kwa sababu ya mambo
yanayohusiana na pesa.

Kila wakati, matatizo yanayokukosesha usingizi,


yanayokunyima furaha, siku zote huwa yanahusiana
na pesa tuna sio vitu vingine.

Ukiona stress zako nyingi zinatokana na mambo ya


pesa, basi ujue kuwa kuna tatizo kubwa kwenye eneo
lako la pesa.

Dalili Ya Sita: Umeanza Kuwakimbia Wanaokudai.

Ukianza kufanya vitu kwa ajili ya kuwakimbia


wanaokudai, basi ni dalili mbaya inayoonesha kuwa
kuna tatizo kubwa ambalo linakukabili.

Ukianza kuona umeanza kubadilisha namba za simu


ili wasikupate, umeanza kuzima simu ili usipatikane
au umeanza kuwablock kwenye simu yako, hii
inaonesha tatizo la kifedha ulilonalo ni kubwa.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 6


Kuna wakati utaona umeanza kukosa uhuru wa
kuweka “status” mambo yako au hata kuogopa
kuchangia kwenye makundi ya “WhatsApp” kwa
kuogopa kujulikana kuwa upo.

Ukiwa kwenye dalili hii, utagundua kuwa umeanza


kukwepa kwenda maeneo fulani kwa sababu ya hofu
ya kukutana na wadeni wako.

Wakati mwingine hata kwenye nyumba za ibada


aidha unaacha kwenda, au unahama au unaamua
kuwa wa mwisho kuingia na wa kwanza kutoka.

Ukiona umeanza kuwakimbia wadeni wako, basi hii ni


dalili inayoonesha kuwa kuna kitu hakiko sawa
kwenye eneo lako la kifedha.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 7


Tafakari Ya Sura Ya Kwanza

1. Ukiangalia maisha yako ya sasa kwenye eneo la


kifedha, je unaona dalili zipi katika hizi zilizotajwa?

2. Ukiona una dalili zaidi ya tatu basi ujue uko kwenye


hali mbaya zaidi na unahitaji kuyafanyia kazi kwa
haraka yale utakayojifunza kwenye sura ya pili.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 8


Sura Ya Pili

Mbinu 5 Za Kutumia
Ili Pesa Zako Zisipotee

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 9


Eneo mojawapo ambalo watu wengi huwa
wanapoteza sana pesa zao ni pale wanapokuwa
wanazitoa kwa ajili ya kuwapa wengine.

Ukitulia na ukapiga mahesabu yako vizuri, utagundua


kuwa, kuna pesa nyingi sana ambazo zinapotea kwa
sababu umewapa watu wenye uhitaji.

Kwa taarifa yako ni kuwa, hadi unakwenda kaburini


utakutana na watu kila siku ambao watakuwa
wanakuomba pesa, usipojiwekea mikakati ya kuwa
na nidhamu yako binafsi, utajikuta kila pesa
unayopata inapitiliza na kwenda kwenye mikono ya
wengine na kukuacha wewe ukiwa hauna kitu.

Ingawa ni jambo jema sana kusaidia watu wenye


uhitaji, ila usisahau kuwa wewe una kikomo cha
kusaidia wengine kwani hauna uwezo wa kumsaidia
kila mtu (You are not omnipotent).

Ili kujenga nidhamu zitakazokusaidia usipoteze pesa


zako hovyo, unatakiwa kutumia mbinu zifuatazo:

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 10


Mbinu ya 1: Usitoe taarifa hovyo za fedha
zako/Matumizi yako.

Watu wengi huwa wanakuomba pesa, pale ambapo


wanajua unazo. Moja ya kosa ambalo unatakiwa
kuliepuka kwenye maisha yako ni kutoa taarifa zako
za pesa hovyohovyo.

Jizoeze kutozungumzia na kutaja kipato chako kwa


watu ambao sio lazima wajue. Jizuie kutoa taarifa za
faida kubwa ya pesa uliyopata n.k

Kadiri watu wanavyokuwa hawajui kiwango cha pesa


unachoingiza, ndivyo ambavyo haitakuwa rahisi kwao
kukuomba pesa, kwa sababu hawatajua kama unazo.

Kuna watu wakiongezewa mshahara tu ofisini, ukoo


mzima watajua kuwa wameongezewa. Matokeo yake,
watu wanaamini kuwa una pesa nyingi na wataanza
kukuomba kila wakati.

Usisahau kuwa, watu wengi wanaweza kujua kipato


chako ila wasijue majukumu yako, hivyo wakijua pesa
unazoingiza huwa wanaona nyingi zinazotosha na

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 11


kuwagaia na wao wote. Epuka kuzungumzia na
kutaja kipato chako kwa watu wasiohusika ambao
hawatakiwi kujua. Inapofika kwenye suala la nidhamu
ya pesa, ukimya wako juu ya kipato chako, ndio huwa
usalama wako zaidi.

Njia nyingine ya kuzuia watu kujua kipato chako ni


kuepuka kuonyesha maisha ya kifahari. Unakuta mtu
akinunua gari anaonyesha, akienda hoteli ya kifahari
anaonyesha, akinunua saa ya gharama anaonyesha
n.k

Ukifanya hivi, ni sawa na kuwatangazia watu kuwa


unazo pesa za kutosha zinazokuzidi na
unawakaribisha kukuomba pia. Hakuna ubaya wa
kuonyesha kwa nia ya kumshukuru Mungu au kutaka
kuwatia hamasa wengine, ila ujiandae kuombwa na
wale watakaoona.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 12


Mbinu ya 2: Usitoe matumaini kwa mtu kama hauna
uwezo kwa wakati huo/hauko tayari kumpa pesa yako
(Respond Promptly, Be clear).

Kuna watu wengi wameingia kwenye mtego wa kutoa


pesa hata pale ambapo wanakuwa wamebakiwa
nazo kidogo kwa sababu ya huruma.

Kumbuka kuwa, unaweza kuwa na huruma, ila kama


hauna uwezo wa kuihudumia huruma kipesa,
usijilazimishe.

Mtu anapokuomba pesa, huwa anatarajia unaweza


kusema NDIO au HAPANA. Ukijijua kuwa uko kwenye
changamoto za kipesa, usimpe mtu matumaini ya
kuwa unaweza kupata na kumpatia baadaye.

Achana na majibu kama “Ngoja niangalie kwanza”,


“Tuombe Mungu nitakuchek baadaye”, “Kuna hela
naisubiria, nikipata nitakupatia”.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 13


Kwa tafiti zangu ndogo ni kuwa, mtu ukishampa jibu
lolote la matumaini, kwanza anaacha kutafuta
kwingine kote na pili anatarajia kuwa lazima utampa,
hii ndio maana lazima atakusumbua tu.

Kwa sababu hii, mtu akikufuata na ukagundua kuwa


unaweza usiwe na uwezo wa kumsaidia, mwambie
moja kwa moja kuwa “Kwa sasa sitaweza kukupatia
siko kwenye nafasi nzuri”.

Ingawa jibu hili linaweza kuonekana kuwa la kikatili


na la moja kwa moja, ila litakuweka huru sana.

Nimeshakutana na watu ambao, walitoa aina ya jibu


la kumpa mtu matumaini, na matokeo yake
wakalazimika wanakopa ili kumpa huyo mtu kwa
sababu alikuwa anawasumbua sana.

Mbinu Ya 3: Weka Pesa Yako Kwenye mfumo usio wa


Pesa Taslimu (Avoid cash )

Kwa kawaida kila mtu ana huruma na huwa anajisikia


wajibu wa kumsaidia mtu anapokuwa anamuomba
pesa. Na ukiwa na dhamiri hai, ni ngumu sana

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 14


kumuona mtu anateseka na ukashindwa kumpa pesa
kama unayo pesa hiyo mfukoni au hata benki.

Ili kuepuka urahisi wa kutumia pesa yako au


kushtakiwa na dhamira yako, epuka kuweka pesa
zako kwenye mfumo wa “cash”.

Unachoweza kufanya ni kuzigeuza pesa zako ziwe


katika mfumo ambao itakuwa ngumu kwako kumpa
mtu na hautajisikia kama umemnyima.

Baadhi ya njia unazoweza kutumia ni :

Kununua bidhaa za biashara unazoweza kuuza.

Kununua mifugo utakayouza baadaye.

Kununua bidhaa za ndani kwa uwingi na kuziweka


(chakula n.k).

Kulipia bili kwa jumla (Bili ya Umeme, Bili ya Maji,


Ada kwa miezi ya mbele, Kodi Ya Nyumba n.k).

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 15


Kuwekeza kwenye masoko ya kifedha kama vile
hisa za kampuni (Shares), hati fungani (Bills and
Bonds) au mifuko ya pamoja (Mutual Funds).

Kama ungependa kujifunza zaidi kuhusu hisa, hati


fungani na mifuko ya pamoja, tafadhali tafuta kitabu
changu kinachoitwa ONGEZA KIPATO CHAKO,
kitakusaidia sana.

Kumbuka utakapoweka pesa zako huku, utakuwa una


pesa ila katika mfumo ambao sio rahisi kuuchukua
na kumpa mtu anayekuomba, hivyo hata ukiombwa
na ukasema sina, hautajisikia vibaya na dhamira yako
itakuwa salama kabisa.

Hii ndio maana, ni muhimu sana kuwa na mfumo


unaohakikisha pesa ambayo umeamua kuitenga kwa
ajili ya akiba na uwekezaji, unaitengenezea mazingira
ya kuipeleka huko kwa haraka sana.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 16


Mbinu Ya 4: Tumia mfumo wa pesa yako kukatwa juu
kwa juu au kuiweka kwenye akaunti maalumu.

Kuna watu wengi sana ambao wana mipango mingi,


ila tatizo huwa ni pale pesa inapofika tu mkononi
mwao. Yaani, ikishaingia tu mkononi mwao hawawezi
tena “kuicontrol”.

Kama wewe ni mmoja wao, njia bora ya kutumia ni


kuhakikisha kuwa pesa kabla haijafika mkononi
mwako imeshaenda mahali salama.

Kama umeajiriwa na unalipwa pesa yako kwa njia ya


Benki, basi unaweza kufungua akaunti maalumu
ambayo unaweka “Standing Order” na kuwaambia
Benki kuwa kwa kila tarehe fulani ambayo unajua
mshahara utakuwa umeshatoka, basi kuna kiwango
maalumu unachowekwa, kinakatwa na kinawekwa
moja kwa moja kwenye akaunti uliyoichagua.

Kama kipato chako huwa akipitii Benki kutokana na


aina ya shughuli unayofanya, unachoweza kufanya ni
kufungua akaunti ambayo unaweza kuwa unaweka tu
na hairusu kutoa hadi baada ya muda fulani ambao

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 17


utauchagua (Kwa mfano unaweza kuweka kwa miezi
12 bila kutoa). Ukifungua akaunti hii, inamaanisha
kuwa, hata ukiwa na shida ya namna gani hauwezi
kuitoa hiyo pesa hadi muda uliokubaliana na Benki
utakapotimia.

Ili kurahisisha, unaweza kuunganisha akaunti hiyo na


simu ili uwe unatumia simu yako kuweka hela, ila
hautaweza kuitoa benki kwa simu hadi muda
ulioweka utakapotimia. Hii itakusaidia sana kuwa na
nidhamu kwa pesa unayoipata.

Benki nyingi sana huwa zinatumia huduma hii,


unaweza kutembelea kwenye tawi la benki yako na
ukauliza.

Mbinu ya 5: Tumia vikundi/mchezo wa kupeana


(Vicoba, Saccoss etc)

Njia ya tano unayoweza kuitumia kujijengea nidhamu


ya kutotoa pesa yako hovyohovyo ni kujiunga katika
vikundi ambavyo vitalazimisha upeleke pesa zako
huko kuweka akiba au kuwekeza.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 18


Hapa nazungumzia vikundi kama VICOBA, SACCOS
au michezo ya kupeana kila mwezi au kila wiki.

Faida ya njia hizi ni kukutengenezea nidhamu ya


kuweka akiba pesa zako bila kughairisha, hata pale
unapokuwa unakabiliwa na changamoto kubwa ya
kipesa.

Mara nyingi katika vikundi hivi, kunakuwa na sheria


na taratibu ambazo zinakulazimisha kupeleka
kiwango fulani cha pesa kila baada ya muda fulani.
Hii itakusaidia kwa kuwa itakuwa ni kama njia ya
lazima ya kukufanya uwe unapeleka pesa huko.

Kutokana na taratibu ambazo ziko kwenye vikundi


hivi, sio rahisi kabisa mtu akakuomba pesa na
ukaenda kuchukua kwenye kikundi. Hivyo ukiombwa
pesa, ni rahisi kabisa kusema sina na ukabakia na
amani yako.

Jaribu kuangalia njia hii na uone kama inaweza


kukufaa ili uanze kuitumia.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 19


Tafakari Ya Sura Ya Pili

1. Katika njia ambazo zimejadiliwa kwenye sura hii za


kukusaidia kujenga nidhamu ya pesa, je kuna yoyote
ambayo tayari umeshaanza kuitumia?

2. Ipi katika hizi ambayo unaona unaweza kuanza


kuitumia kuanzia sasa hivi ili kuongeza nidhamu yako
ya kutumia pesa?

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 20


Sura Ya Tatu

Epuka Tabia Hizi 7 Zinazopoteza


Pesa Za Watu Wengi

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 21


Kuna watu wengi sana ambao wamepitisha pesa
nyingi sana mkononi mwao, ila wakijaribu kuangalia
na kutafakari hawazioni zimeenda wapi.

Katika maisha ya watu wengi, baada ya kuwaambia


wapige mahesabu, waligundua kuwa ukiacha kutumia
kwenye mahitaji ya msingi (Chakula, Malazi, Ada za
watoto, usafiri, matibabu ) pesa nyingi zimeenda:

Kusaidia ndugu.

Michango ya sherehe na misiba.

Misaada kwa wenye shida mbalimbali


wanaowaomba.

Gharama za matumizi ya simu (airtime and


bundle).

Mavazi na urembo na...

Starehe/Burudani: Vinywaji, Muziki n.k.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 22


Je, wewe ukiangalia namna unavyotumia pesa zako
kwa sasa, unaona kuwa pesa zako nyingi zimeenda
wapi zaidi?

Kuna aina fulani za tabia ambazo ukiwa nazo


zinaweza kuwa ni chanzo kikubwa cha wewe
kupoteza pesa nyingi ambazo zinapita mikononi
mwako.

Tabia 1: Kutembea na pesa taslimu bila bajeti

Pesa ambayo unatembea nayo bila kuiwekea


mipango, mara nyingi utaitumia bila kutarajia. Kuna
watu wengi sana wakiwa na pesa, utakuta ameenda
kuzitoa kiwango fulani bila hata kupanga anaenda
kuzifanyia nini na anaanza kutembea nazo
mfukoni/kwenye pochi.

Pesa huwa ina kawaida ya kupiga kelele kutaka


kutumiwa ili ijisikie vizuri, ukiwa nayo mfukoni wakati
haujapanga unataka kuitumia wapi, itakushawishi
uitumie kwenye vitu ambavyo haukutarajia au
utashangaa wanajitokeza watu wenye uhitaji ambao
utalazimika kuwasaidia.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 23


Hii ndio maana ni muhimu kuacha tabia ya kutembea
na pesa ambayo haujapanga kuitumia kwa sababu
itapata matumizi ambayo haukuyatarajia. Msimamo
ni kwamba, “Kama haujapanga matumizi yake,
usitembee nayo mfukoni”.

Tabia 2: Kuahidi michango kwa kujilinganisha na


wengine

Ni jambo zuri sana na la muhimu kuchangia kwenye


masuala ya kijamii, ila ni jambo la hatari sana
kuchangia zaidi ya uwezo wako. Kwa kawaida jamii
inaweza kukuwekea presha kubwa sana kufanya kitu
zaidi ya uwezo wako, usiingie kwenye mtego huo.

Siku zote jifunze kutoa ahadi zako kulingana na


uwezo ulionao kwa wakati huo. Usikubali
wanachofanya wengine, kikuendeshe wewe.

Usikubali ahadi za wengine zikulazimishe ufanye


zaidi ya unavyoweza. Kumbuka ukishaahidi mchango
wa harusi, kanisani, msikitini au msiba, wewe ndio
utakayeteseka kutafuta hiyo hela.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 24


Usisahau kuwa, hata kama wakati unaahidi
watakupigia makofi na kukusifia kwa kuahidi kiwango
kikubwa, wakati wa kuitafuta utakuwa uko peke yako,
hivyo basi ahidi kulingana na uwezo wako.

Moja ya dalili mbaya kabisa ya kifedha, ni pale


unapoanza kukopa ili utoe michango ambayo wakati
unaahidi ulijua kabisa kuwa iko juu ya uwezo wako.

Tabia 3: Kukubali Kulazimishwa kukopa vitu

Unakuta kuna kitu kinauza ofisi kwao au mtu


amepitisha, pengine ni nguo, viatu, pochi n.k Baada ya
kuambiwa ununue, unasema “Kwa sasa sina hela”,
halafu anakuambia “Usijali, utalipa mwisho wa
mwezi”, baada ya kuambiwa hivyo na wewe
unakubali.

Kuna watu wengi sana ambao wamejikuta wameingia


kwenye madeni ya kununua vitu ambavyo
hawavihitaji kwa sababu walifikiria kuwa kuchukua na
kulipa baadaye ni unafuu.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 25


Ukweli ni kuwa, aidha ulipe sasa hivi au ulipe mwisho
wa mwezi, inayotumika pale ni pesa yako.

Jifunze, kutokubali kununua vitu kwa sababu ya


kuambiwa utalipa baadaye, kama haukihitaji
usikichukue. Jenga ujasiri wa kusema kuwa hauhitaji
kwa wakati huo.

Haujawahi kuona mtu anachukua kitu kwa mkopo na


anakitumia mara moja au hakitumii kabisa, kinabakia
ndani tu?. Kuna watu wengi sana ambao wamejaza
viatu, nguo, saa n.k ambazo baada ya kununua ndio
wakagundua walikuwa hawazihitaji kabisa.

Clive Hamilton aliwahi kusema kuwa “People Buy


Things They Don’t Need, With the Money They Don’t
Have, To Impress People They Don’t Like” (Watu
hununua vitu ambavyo hawavihitaji, kwa pesa ambayo
hawana ili kuwaridhisha watu ambao hawawapendi).

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 26


Tabia 4: Kufuatilia sana matatizo/changamoto za
watu.

Ni jambo zuri kuwa na moyo mwema wa kusaidia


watu pale wanapokuwa na uhitaji. Hata hivyo ni
muhimu sana kujua kuwa, hautakuwa na uwezo wa
kuwasaidia watu wote unaokutana nao ambao wana
uhitaji, lazima ujiwekee nidhamu.

Usipofanya hivyo, pesa zako zote zitaishia kusaidia


wenye uhitaji na bado utakuwa haujamaliza matatizo
yao na wewe utajiacha kwenye matatizo.

Watu wengi wakikushirikisha changamoto zao za


kifedha hasa wanapokuomba, kama hauna ni vizuri
uwaambie mapema.

Hata hivyo ukiendelea kila wakati kuwaulizia ulizia


wanavyoendelea, kuna wengi huwa wanaanza
kuweka tumaini kuwa kuna msaada utawapatia.

Kwa sababu hiyo, utajikuta wanaanza kukupigia simu


na kukueleza kila hatua ambayo wanakwama kifedha
kwa lugha itakayokuwa inaashiria kuwa wana

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 27


matumaini kuwa utawasaidi. Kama mtu amekupata
taarifa ya changamoto yake ya shida ya kifedha na
ukaona hauna uwezo wa kumsaidia kwa wakati huo,
basi epuka kuuliza maswali mengi na “details” nyingi
ambazo zinaweza kumuonyesha kuwa unataka
kupanga namna nyingine ya kumsaidia.

Yaani ni sawa na mtu akisema ana njaa na wewe


hauna pesa ya kumsaidia, mwambie moja kwa moja
kuwa hauna badala ya kuanza kuuliza maswali kama:

Kwa mfano hapa ukipata chakula utapenda chakula


kipi, Au unamuuliza, kikipatikana chakula baada ya
masaa mawili itakuwa sawa?

Maswali haya yataamsha matumaini ya kuwa kuna


kitu unataka kumfanyia, achana kabisa na kuuliza
maswali ya kutoa matumaini kama unajua hauna
uwezo wa kusaidia.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 28


Tabia 5: Kutotenga pesa zako katika makundi
maalumu.

Njia nzuri ya kuhakikisha pesa yako inaenda mahali


ambapo umepakusudia ni kuigawa pesa yako kwenye
makundi mbalimbali. Ili kufanikisha hili, inatakiwa kila
pesa inayofika mkononi mwako uigawe kwa kutumia
mfumo wa bajeti.

Kama ungependa kujifunza vizuri kuhusu mifumo ya


bajeti nashauri tafuta vitabu vyangu (Money Formula
na Ongeza Kipato, nimeeleza kwa kirefu sana).

Pesa yako inatakiwa igawiwe kwenye makundi


makubwa matatu: Kundi la kwanza ni sehemu ya
akiba/uwekezaji, sehemu ya pili ni kwa ajili ya
mahitaji muhimu (chakula, afya, malazi, ada za shule
n.k) hizi huitwa “needs” na sehemu ya tatu ni kwenye
matumizi ambayo sio ya lazima yanayoitwa “wants”.

Hii itakusaidia kutumia pesa kulingana na kiwango


ambacho umekiweka kwenye kundi husika na
kutovuka juu ya bajeti yako.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 29


Ukijifunza zaidi kupitia vitabu nilivyopendekeza,
utaona jinsi kanuni ya 50/30/20 ilivyobadilisha
maisha ya watu wengi kifedha, nawe ukijifunza
itakupa matokeo makubwa sana.

Tabia 6: Kuwa na kiwango maalumu cha kusaidia


watu.

Hata uwe na pesa kiasi gani, hautakuwa na uwezo wa


kumsaidia kila mwenye tatizo. Pia ni muhimu sana
kujua kuwa, hakuna hata siku moja matatizo ya watu
yataisha, yataendelea sana kuwepo.

Hatari ambayo unatakiwa kujiepusha nayo ni kuwa


mtu ambaye unasaidia watu bila mpangilio, halafu
wewe mwenyewe unabakia kwenye changamoto ya
pesa na hakuna mtu wa kukusaidia.

Ili kuepuka mtego huu, unatakiwa kuwa na bajeti


maalumu ya kusaidia jamii, unaweza kuiita “Social
Fund”.

Hii ina maana, utatenga kiwango fulani maalumu cha


pesa kila mwezi/kila unapopata ambacho utakuwa

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 30


unakitoa kusaidia wenye uhitaji. Unaweza kuamua
kiwe ni asilimia fulani ya kipato chako au kiwango
fulani maalumu. Cha muhimu hapa ni kuhakikisha
kuwa, unajitahidi kadiri unavyoweza kukaa ndani ya
bajeti yako siku zote bila kuyumba.

Usipojiwekea utaratibu huu, unaweza kujikuta


unatumia pesa nyingi sana kusaidia watu zaidi ya
kipato chako.

Jaribu kufanya mahesabu kwa miezi sita iliyopita,


umetoa jumla ya misaada/michango kiasi gani?

Tabia ya 7: Kununua kitu kimoja kimoja

Njia mojawapo nzuri ya kuhakikisha kuwa unapata


thamani kubwa kwa kila pesa unayotumia, ni kununua
vitu kwa ujumla au kwa uwingi badala ya kununua
kitu kimoja kimoja.

Kumbuka unaponunua kitu kidogokidogo kila siku,


gharama sio tu bei unayonunulia bali pia nauli
ambayo unatumia mara kwa mara na hata nguvu na
muda ambao unatumia.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 31


Hivyo basi, katika eneo hili, jaribu kuangalia namna
ambavyo unaweza kununua vitu kwa ujumla (Mfano
chakula, mafuta. LUKU n.k) ili kupunguza gharama ya
manunuzi yako.

Unaponunua kwa ujumla inakusaidia kwenye maeneo


makubwa MATATU: Moja, inakupunguzia gharama
kwa sababu unaweza kupunguziwa bei.

Lakini pia gharama inapungua kwa sababu kama ni


nauli/mafuta utatumia mara moja tu kwenda
kununua.

Eneo la pili linakusaidia kuokoa muda na nguvu zako


ambazo ungetumia kwenda mara kwa mara kufanya
manunuzi hayohayo.

Tatu, unaponunua kwa uwingi au kwa ujumla


inakusaidia kutokukosa mahitaji kwa kupeleka pesa
kwenye mambo mengine. Ukiwa na pesa taslimu
(cash) ambayo ilitakiwa inunue bidhaa fulani,
unaweza kujikuta mtu amekuja na tatizo umempatia
na unalazimika kuanza kukopa kwa ajili ya mahitaji
muhimu.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 32


Kuepuka hilo, hakikisha unapopata pesa yako
unaitumia kwa kununua vitu vinavyohitajika kwa
uwingi ili hata ukiishiwa pesa, bado utakuwa na vitu
vya kutumia.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 33


Tafakari Ya Sura Ya Tatu

1. Katika tabia hizi saba ambazo zimesababisha watu


wengi sana wapoteze pesa, je kuna tabia zipi ambazo
wewe ukijikagua unaona zinachangia pia kukupotezea
pesa zako.

Zitambue na weka mikakati ya kuzibadilisha.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 34


MUHIMU: Njia yangu pekee ambayo naitumia
kutimiza malengo yangu ya kuwasaidia watanzania
kutumiza malengo yao ni kutumia mitandao ya
kijamii.

Ila ukweli ni kwamba wengi wanakijaji kitabu kwa


kuangalia kava lake (Na reviews/shuhuda za
waliokisoma)

Kama umeona kitabu/eBook hii ni nzuri na mafunzo


yake ni mazuri.

Tafadhali unaweza chukua muda kidogo sasa hivi na


kuandika au kurecord video na kunipatia Mrejesho
wako wa haki (honest review) kuhusu eBook/kitabu
hiki?

Itakugharimu Tsh 0 na sekunde chini ya 150 tu!

Review/Mrejesho wako utasaidia...

... mtanzania mmoja kusupport familia yake.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 35


...mtu mmoja kutimiza malengo yake ambayo yamkini
asingeweza kuyatimiza hapo kabla.

....badiliko moja la maisha ya mtu kuwa bora.

Kufanya hilo litokee...

Unachotakiwa kufanya ni...na hii itachukua chini ya


sekunde 150 kuandika au kurecord video ya shuhuda
yako.

Bofya hapa sasa hivi


👇

https://testimonial.to/joel-nanauka

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 36


Sura Ya Nne

Maswali 5 Ya Kujiuliza Kabla


Haujatumia Pesa Yoyote

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 37


Kabla pesa yako haijatoka mkononi mwako kufanya
matumizi ya aina yoyote yale, ni muhimu sana
kujiuliza baadhi ya maswali ambayo yatakusaidia
kujidhibiti ili usitumie kwa namna ambayo utajilaumu.

Ukijizoeza kujiuliza maswali haya, yatakusaida sana


kuhakikisha kuwa unaweza nidhamu katika matumizi
yako ya kila siku.

Swali La Kwanza: Kitu hiki kilikuwa kwenye bajeti


yangu?

Utafiti ambao ulifanywa na Thomas Stanley na


William Danko nchini Marekani ulipelekea kuchapisha
kitabu cha “The Millionaire Next Door” ambacho
kilielezea tabia za watu wanaofanikiwa kifedha.

Moja ya kitu walichokigundua ni kuwa 93% ya matajiri


wote huwa hawatoki nje ya bajeti yao
walioyoitengeneza, wakati wengi walio maskini huwa
hawana bajeti au hawazingatii kabisa bajeti yao.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 38


Moja ya tabia muhimu ambayo unatakiwa kuijenga
kwenye maisha yako ni kutengeneza bajeti na
kuifuata.

Kabla haujanunua kitu chochote kile jiulize “Je, hiki


ninachonunua kipo kwenye bajeti yangu?”. Isipokuwa
tu kwa vitu vya dharura au vitu ambavyo ni fursa
kubwa iliyojitokeza ghafla, jizoeze kununua vitu
kulingana na bajeti yako. Imegundulika kuwa,
matumizi mengi ambayo watu huyafanya nje ya bajeti
yao huwa wanakuja kujilaumu sana hapo baadaye.

Usisahau kuwa kadiri unavyotumia pesa nje ya bajeti


yako, ndivyo ambavyo utazidi kupoteza pesa zako.

Swali La Pili: Kwa nini nataka kununua/kuwa nacho


(Motive)?

Kulingana na utafiti uliowahi kufanywa na Profesa


Gerald Zaltaman wa Harvard Business School,
ilionekana kuwa 95% ya maamuzi ya kununua kitu
huwa inaongozwa na hisia (Emotions) zaidi ya akili
(Logic).

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 39


Kwa sababu hiyo, ni muhimu sana kila wakati
kujiuliza sababu inayokusukuma kufanya baadhi ya
manunuzi kwenye maisha yako.

Hii ni muhimu kwa sababu kuna mara nyingi unaweza


kuongozwa na hisia ambazo baadaye hazitakuwa na
maana tena.

Watu wengi sana wameingia kwenye kununua vitu


kwa sababu wameongozwa na hisia za kutaka
kuonyesha kuwa hawajapitwa na wakati, wengine
wametaka kuonyesha kuwa wana pesa na wengine
wanataka kushindana na wengine kuonyesha na wao
wanaweza pia.

Hisia hizi na zingine zinazofanana na hizi, huwa


zinawaingiza watu kwenye madeni, kupoteza pesa,
kuishi juu ya uwezo wao na kununua vitu ambavyo
hawavihitaji kabisa.

Je, wewe unapotaka kununua nguo fulani, simu


fulani, saa, gari n.k nini hasa ambacho kinakusukuma
kufanya hivyo?

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 40


Kumbuka kuwa, kitu chochote kile unachotaka
kukinunua kwa sababu ya kutaka kuwaonyesha watu
huwa kinapoteza thamani ndani ya muda mfupi sana,
kwa sababu wakishakiona hakitakuwa tena na
thamani.

Lakini pia, inaweza kutokea kuwa wakakiona na


wasikipe thamani kama ulivyofikiria watakuthamini,
watakusifia n.k ikitokea hivi itakupa “stress” sana na
utajilaumu kila wakati.

Swali La Tatu: Ni lazima nitumie sasa hivi?(72 Hrs


Rule)/Nikikikosa kwa sasa ninapata hasara gani?

Watu wanaouuza vitu huwa wanatumia mbinu ya


“FOMO” (Fear of Missing Out), yaani hapa
wanakufanya uone kuwa, ukichelewa kununua leo
basi hautaweza kukipata tena.

Hii inatumika pale uanpoambiwa “Vimebakia 10 tu”


au “Leo ni siku ya mwisho” au “Ofa ni kwa watu 10 wa
kwanza tu” n.k.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 41


Ukiingia kwenye mtego huu, ni rahisi sana kujikuta
kila wakati ukifanya manunuzi ya vitu ambavyo
hauvihitaji kabisa na utaishia kujilaumu kila wakati.

Hii ndio maana ni muhimu sana kujipa muda kabla


haujafanya manunuzi ya vitu ambavyo sio muhimu.
Kanuni mojawapo ya kukusaidia ni kutumia “72Hrs
Rule”.

Yaani unajipa saa 72 kuanzia unapopata hisia za


kununua na kuchukua hatua ya kununua.

Hii itakusaidia kujipa muda wa akili yako kufanya


tathmini na kujua kama kweli hasa unahitaji kitu
hicho lakini pia itasaidia kufanya hisia ambazo sio
halisi kuhusiana na maamuzi yako kupotea.

Ukikutana na hisia za kukuhimiza kununua kitu fulani


kwa ghafla/kutumia pesa zako kwa ghafla. Tafakari,
kama hicho kitu sio cha dharura, jipe saa 72 kabla
haujafanya maamuzi.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 42


Swali La Nne: Nimetafuta kulinganisha bei? (Price
Comparison)

Kwa kila bidhaa ambayo unataka kununua/huduma


unayotaka kuipata kuna watu zaidi ya mmoja au
kampuni zaidi ya moja ambayo inauza/kutoa huduma
hiyo.

Ili kuhakikisha kwamba unanunua kwa bei nzuri sana


(best deal), hakikisha umeulizia angalau maeneo
matatu wanaouza.

Hii ndio maana hata kwenye tender za kampuni, huwa


wanaita watu mbalimbali na kulinganisha bei zao.
Uzoefu umeonyesha kuwa unaweza kuokoa takribani
20% ya matumizi ya pesa yako kwa kuulizia bei
maeneo tofauti tofauti.

Kumbuka kuwa, hauwezi kuulizia kwa kila kitu


unachotaka kununua, ila kwa matumizi yoyote
ambayo unayachukulia kuwa ni makubwa na ya
muhimu kwenye maisha yako ni vizuri ukafanya
ulinganifu wa bei kabla haujanunua.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 43


Usipofanya hivyo, unaweza kushangaa unanunua kitu
halafu unakuja kugundua kuna mahali pengine
ungepata kwa bei rahisi sana na ungeokoa pesa
zako.

Swali La Tano: Matumizi ninayofanya yako kwenye


kundi gani? (Uwekezaji, yaliyo ya lazima, yasiyo ya
lazima)?

Pesa yoyote unayoitoa ni vizuri kujua inaenda kwenye


kundi gani la matumizi yako.

Kama bado unahangaika na kujua hili tafadhali


usisahau kutafuta kitabu cha MONEY FORMULA
(Elimu Ya Fedha Isiyofundiswa Shuleni) na ONGEZA
KIPATO CHAKO (Maarifa Juu Ya Fedha, Biashara na
Uwekezaji), vitakusaidia sana.

Ni lazima ujifunze kutumia pesa yako kimkakati,


yaani uamue kuwa inaenda wapi na inaenda kufanya
nini. Hii itakusaidia kutotumia pesa ambayo
inatakiwa kwenda kwenye uwekezaji ikaishia kwenye
kujiburudisha.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 44


Kumbuka kwenye makundi ya matumizi yako,
utagundua kuwa yako yale ambayo ukitumia pesa
ndio inapoteza kabisa, nyingine inaenda kukaa na
utaikuta ilivyo na nyingine inaenda kuzaa na itakupa
zaidi ya uliyoweka.

Kila wakati kabla haujatumia jiulize, hii ninayotoa


inatoka kama kundi gani?

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 45


Hitimisho

Bila kujali unafanya kazi gani na unalipwa kiasi gani,


kujenga nidhamu ya matumizi ya pesa yako ni kitu
muhimu sana kwenye maisha yako.

Kadiri unavyochelewa kujenga nidhamu muhimu za


kukusaidia, ndivyo utakavyozidi kupoteza pesa zaidi.

Tumia maarifa uliyoyapata kwenye kitabu hiki,


kujikagua, kugundua na kuamua maeneo muhimu
ambayo unatakiwa kuanza kuyafanyia kazi kwa
haraka sana.

Kumbuka kuwa ukipata maarifa bila kuyafanyia kazi


hayatakusaidia.

Unaweza kuungana na wengine ambao wanapata


matokeo makubwa kwa kutumia kanuni
zilizofundishwa kwenye kitabu hiki.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 46


Nasubiria kwa hamu kusikia ushuhuda wa mabadiliko
makubwa ya kifedha ambayo utayapata kwenye
maisha yako.

Muda wowote utakapokuwa tayari kunijulisha namna


ambayo eBook/kitabu hiki kimekusaidia
Bofya hapa
👇

https://testimonial.to/joel-nanauka

See You At The Top

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 47


Kuhusu Mwandishi

Joel Arthur Nanauka ni mwandishi wa vitabu na


mwalimu katika maeneo ya uongozi, biashara na
kujitambua.

Ni mhitimu wa masomo ya biashara na uongozi


kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam na Stashahada
ya juu ya Diplomasia ya Uchumi kutoka kituo cha
mahusiano ya nje (Centre For Foreign Relations).

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 48


Mwaka 2022 alikabidhiwa Tuzo Ya Kitaifa na Mh.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa kutambua
mchango anaoutoa katika Taifa kutengeneza
Rasilimali watu (Human Capital Development) kwenye
Kongamano la 6 la Baraza la Taifa la Uwekezaji
lililofanyika Dodoma, Tanzania.

Tuzo hizo zilikuwa zimeandaliwa na Baraza la Taifa la


Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi NEEC.

Mwaka 2020 alitajwa katika orodha ya vijana 100


wenye ushawishi zaidi katika bara la Afrika na pia
kijana mwenye ushawishi zaidi Tanzania katika eneo
la ufundishaji watu kujitambua (Personal
Development).

Pia aliwahi kutajwa kama kiongozi bora kijana wa


Dunia mwaka 2012, nchini Taiwani, China. Amekuwa
mkufunzi wa wakurugenzi wa kampuni binafsi na
mashirika ya umma kupitia taasisi ya wakurugenzi
Tanzania (IoDT) katika eneo la kuendesha mabadiliko
katika taasisi (Change Management)

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 49


Joel ni mwalimu (Certified Trainer) katika eneo la
biashara na ujasirimali anayetambuliwa na kutumika
kufundisha mitaala ya vyuo vikuu vya Regent na
Joseph Business School vyenye makao yako makuu
nchini Marekani.

Pia amekuwa mlezi wa wajasiriamali wa Afrika


kupitia shindano maalumu la Africa Entrepreneurship
Award linalofanyika kila mwaka chini ya Benki ya
BMCE iliyoko nchini Moroco.

Joel alikuwa ni mmoja wa timu maalumu ya


wataalamu walioteuliwa na serikali chini ya Baraza la
Uwezeshaji la Taifa (NEEC) katika kuandaa muhtasari
wa mtaala maalumu wa ujasiriamali wa Taifa.

Joel Arthur Nanauka amekuwa mkufunzi wa vyombo


vya habari tangu mwaka 2018 kupitia taasisi ya
Tanzania Media Foundation (TMF) katika eneo la
biashara na uongozi.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 50


Amewahi kufanya kazi na Umoja wa Mataifa (UN)
kupitia shirika la UNESCO na baada ya hapo
alianzisha taasisi ya Africa Success Academy
ambayo kwa sasa ndiye mkurugenzi wake.

Joel amemuoa Rachel na wamebarikiwa Watoto


watatu wa kike: Joyous, Joyceline na Jonel.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 51


Vitabu Vyangu Vingine

HARDCOPY (Nakala ngumu)

1. Timiza Malengo Yako (Mbinu 60 walizotumia watu


maarufu kufanikiwa)

2. Ishi Ndoto Yako (Siku 30 za kuishi maisha


unayotamani)

3. Tabia 12 Zinazoleta Mafanikio.

4. Ishinde Tabia Ya Kughairisha Mambo.

5. Ongeza Kipato Chako (Maarifa juu ya fedha,


Biashara na uwekezaji)

6. Nguvu Ya Mwanamke.

7. Mbinu Za Kufanikisha Ndoto Katikati Ya


Changamoto.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 52


8. How To Pass Your Exams With Ease.

9. Uzalendo Na Ujenzi Wa Taifa.

10. Ufanisi Kazini.

11. Boresha Mahusiano Yako.

12. Money Formula.

13. Core Genius.

14. Vita Ya Mkombozi Wa Familia

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 53


eBooks / SOFTCOPY (Nakala laini).

1. Money Formula (Elimu ya fedha isiyofundishwa


shuleni)

2. Hatua Sita Za Kujiajri

3. Muongozo Wa Mafanikio

4. Core Genius (Jinsi ya kugundua uwezo wako wa


kipekee)

5. Jinsi Ya Kufanikiwa Katikati Ya Nyakati Ngumu.

6. Saikolojia Ya Mteja

7. Mbinu Za Kujenga Ujasiri Na Kujiamini.

8. Surviving The Crisis.

9. Namna Ya Kuondokana Na Madeni

10. Uzalendo Na Ujenzi Wa Nchi.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 54


11. Mbinu Za Kuongeza Kipato.

12. Strategy 2021, Siri Za Kupata Matokeo Makubwa


Ndani Ya Mwaka Mmoja.

13. Nifanye Biashara Gani?

14. Marafiki.

15. Ufanisi Kazini.

16. Kiongozi Wa Tofauti.

17. Sayansi Ya Tabia.

18. Mbinu 8 Za Maandalizi Ya Kufaulu Mitihani Kwa


Kiwango Cha Juu.

19. Siri 12 Wanazotumia Wanafunzi Bora Ndani Ya


Chumba Cha Mitihani.

20. Maono.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 55


21. Mafanikio Ya Kifedha Kwa Wanandoa.

22. Kuyaishi Maono Yako.

23. Nguvu Ya Mwanamke.

24. Ishinde Tabia Ya Kughairisha Mambo.

25. Ishi Ndoto Yako.

26. Mbinu Za Kuongeza Kipato Chako.

27. Uzalendo Na Ujenzi Wa Nchi.

28. Pigania Maono Yako.

29. Mwanamke Na Biashara.

30. Vita Ya Mkombozi Wa Familia.

31. Kipaji, Jinsi Ya Kukigeuza Kuwa Pesa Na


Kukifanya Kidumu.

32. Jinsi Ya Kusimamia Na Kukuza Biashara Yako.

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 56


Kupata eBooks zangu Bofya hapa
>>> https://selar.co/m/joelnanauka

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 56


Kozi Za Joel Nanauka, Unaweza Kuzisoma Online.

1. Mbinu Za Kuuza Zaidi.

2. Jinsi Ya Kujenga Kipato Cha Uhakika Kwa Kujiajiri.

3. Jinsi Ya Kuondokana Na Madeni.

4. Money Formula

5. Kipaji, Jinsi Ya Kukigeuza Kuwa Pesa.

Kupata kozi hizi wasiliana nasi

WhatsApp: 0762 312 117

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 57


TEMBELEA MITANDAO YA KIJAMII YA
JOEL NANAUKA.

YouTube: Joel Nanauka (Utapata VIDEO nyingi za


kukufundisha mambo mbalimbali)

Instagram: JoelNanauka_ (Utapata mafunzo kila siku


yatakayokusaidia kupiga hatua katika maisha)

Facebook: Joel Nanauka (Utapata mafunzo kila siku


na pia shuhuda mbalimbali za watu walionufaika na
mafunzo)

Twitter: jnanauka

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 58


Unaweza kupata vitabu vingine vilivyoandikwa na
JOEL NANAUKA kutoka

1. Divine Destiny Bookstore Instagram


@DivineDestiny_Bookstore tunapatikana Bamaga.

Simu: 0762 312 171

2. TIMIZA MALENGO BOOKSHOP tunapatikana Njia


Panda Chuo Kikuu Ubungo, wasiliana nasi kwa
namba zifuatazo.

Instagram: @TimizaMalengo_Bookshop

Simu: 0745 252 670 | 0756 094 875

Nidhamu Ya Pesa | Joel Nanauka | 59

You might also like